Nenda kwa yaliyomo

Virusi vya Corona

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Coronavirus)
Cross-sectional model of a coronavirus
Muonekano wa kimojawapo cha virusi vya Corona.

Virusi vya Corona (kwa Kiingereza: Coronavirus) ni kundi la virusi vinavyoweza kusababisha magonjwa kwa wanyama (mamalia na ndege) lakini pia kwa binadamu[1]. Inaaminiwa ni aina ya virusi vilivyohama kutoka kwa wanyama na kuathiri binadamu pia.

Virusi vya Corona vipo vya aina mbalimbali, zikiwemo 229E, NL63, OC43, HKU1 na SARS-Cov-2 [2][3].

Tabia za pamoja

Dalili za Corona
Dalili za ugonjwa wa Corona katika (kwa kiingereza)

Virusi vya corona huwa na uwezo wa kubadilikabadilika na aina nyingi za virusi hivyo husababisha magonjwa yasiyo hatari sana kwa binadamu. Kudhoofika kwa mwili kutokana na mashambulio ya virusi hivyo hufungua milango kwa bakteria wabaya kuvamia mwili wa binadamu na kusababisha maambukizi katika mfumo wa upumuaji kama vile mafua au homa ya mafua (influenza) ambayo kwa kawaida huisha baada ya siku kadhaa. Lakini pia kuna maambukizi ya hatari kama vile nimonia inayoweza kusababisha kifo. Hivyo inatakiwa watu wapunguze kutumia kwa ushirika vitu hatarishi kama vile vyenye ncha kali[4].

Hadi sasa hakuna chanjo wala dawa iliyogunduliwa na kuthibitishwa na mamlaka za afya kwa ajili ya kudhibiti virusi vya aina hiyo. Kwa hiyo kupona ugonjwa huo hutegemea mara kwa mara nguvu ya kinga mwilini ya mhusika. Hii inamaanisha virusi hivyo huleta hatari hasa kwa watu wenye kinga dhaifu ya mwili hali ambayo husababishwa na kuwa tayari na magonjwa mengine mwilini kama vile magonjwa ya moyo, presha na kisukari.

Aina hizo za virusi zina uwezo wa kubadilikabadilika, na kwa miaka ya nyuma kulikuwa na mabadiliko kadhaa yaliyosababisha vifo vya watu na kuenea haraka kwa virusi hivyo kimataifa, hivyo kusababisha hofu za epidemiki au hata pandemia.

SARS

SARS (Severe acute respiratory syndrome) ulikuwa ugonjwa sugu wa mfumo wa upumuaji uliosababishwa na virusi vya corona aina ya SARS-CoV. Uliripotiwa mara ya kwanza huko Asia mnamo Februari 2003 ukaendelea kusambaa katika miezi iliyofuata katika nchi zaidi ya 20 katika Amerika, Ulaya na Asia hadi kwisha. Ugonjwa ulianza kuonekana kwa homa juu ya 38, maumivu ya kichwa na kujisika dhaifu. Asilimia 10-20 za wagonjwa walihara. Wengi wa walioambukizwa waliendelea hata kupata nimonia. Kulikuwa na taarifa za watu 8,098 walioambukizwa, na 774 walifariki katika nchi 17[5], wengi wao nchini China. [6]

SARS haijatokea tena tangu mwaka 2004.

Covid-19 (2019 Novel Coronavirus SARS-Cov-2)

Kwa habari za undani zaidi kuhusu uenaji wa ugonjwa wa Covid-19 tazama hapa (Kiingereza).Kuhusu pandemia kwa Kiswahili tazama: Mlipuko wa virusi vya korona Wuhan 2019-20

Mwisho wa mwaka 2019 lilitokea badiliko jipya la virusi vya corona lililotambuliwa mara ya kwanza mjini Wuhan, China. [7] Serikali ya China inalaumiwa kwa kujaribu kuficha ugunduzi huo kwa maagizo yalitolewa tarehe 2 Januari 2020.

Aina hiyo ya virusi vya corona iliitwa mwanzoni 2019 Novel Coronavirus (2019-nCoV) na hatimaye ikapewa jina la SARS-Cov-2, na ugonjwa unaosababishwa nayo Covid-19 [8]. Usambazaji wake ulionekana kuanza kutokana na virusi vya wanyama vilivyofikia binadamu. Magonjwa ya aina hiyo huitwa zuonosia (zoonotic disease).

Wagonjwa walionyesha matatizo kwenye njia ya upumuo; wengine waliathiriwa kidogo tu, lakini wengine waligonjeka vibaya hadi kufa. Dalili zilizotambuliwa hadi mwisho wa Januari 2020 ni pamoja na homa, kukohoa na ugumu wa kuvuta pumzi. Inaonekana dalili za ugonjwa zinaweza kuanza takriban siku 2 hadi 14 baada ya kuambukizwa. Walio hatarini zaidi ni watu waliodhoofishwa na magonjwa mengine au wenye mfumo dhaifu wa kinga mwilini kwa sababu nyingine, kwa mfano umri mkubwa.

Hadi mwisho wa Januari 2020 takriban watu 10,000 waliambukizwa, idadi ya vifo ilikuwa mnamo 200. Virusi vilienea hadi nchi nyingine kwa njia ya abiria wa ndege za kimataifa. Wakazi wa Wuhan na miji mingine ya China yenye wagonjwa wamekataliwa kuondoka kwao baada ya hali ya karantini kutangazwa.[9].

Katikati ya Februari 2020 maswali mengi kuhusu virusi hivyo vilibaki bila jibu, lakini Shirika la Afya Duniani lilitoa tathmini kuwa[10]

  • zaidi ya asilimia 80 za wagonjwa huonekana kuwa na ugonjwa mwepesi, wanapona
  • kati ya asilimia za wagonjwa kuna maambukizi mazito yanayosababisha matatizo ya kupumua, hata nimonia, na asilimia 15 kudai walazwe hospitalini
  • takriban asilimia 5 huwa na magonjwa hatari
  • mnamo asilimia 2 hufa; hatari ya kifo inapatikana hasa kwa wazee, kuna mfano michache ya watoto. Baadaye imeonekana kwamba kiwango cha vifo si kubwa vile, labda kati ya % 0.5 hadi 1 lakini si rahisi kutaja kiwango kwa uhakika kwa sababu wengi walioambukizwa hawajulikani.
  • utafiti wa ziada bado unahitajika
  • kuna dalili kwamba virusi vya Covid-19 vinaweza kudumu hadi siku 8 kwenye uso wa kitu kilichoguswa na mgonjwa na bado kusababisha maambukizi

Uenezi wa Covid-19 nje ya China

Uenezi wa virusi vya SARS-Covid-19 duniani (ramani inasahihishwa kila siku)
Idadi ya watu waliothibitishwa kuwa na maambukizi
      zaidi ya 10,000       1,000–9,999       100–999       10–99       1–9 (Tarehe 16 Machi mtu wa kwanza alipatikana nchini Tanzania; tarehe 29 Aprili serikali yake iliacha kutoa takwimu)
Mlipuko wa Virusi vya Corona duniani hadi 2 Machi 2020

Katika Februari 2019 virusi viliendelea kuenea nje ya China, kupitia watu waliosafiri baina ya China na nchi nyingine. Tabia ya virusi kutosababisha ugonjwa mkali kwa wengi ilikuwa msingi kwa uenezaji usiotambuliwa mwanzoni hadi kufikia watu waliogonjeka vibaya. Milipuko ya kwanza ilionekana katika Iran[11], Korea Kusini[12] na Italia[13] ambako serikali zilitangaza hali ya karantini kwa maeneo kadhaa. Kufikia mwisho wa mwezi huo, wagonjwa wa nchi nyingine kwa pamoja walikuwa wamezidi wale wa China.

Katika Machi 2020 idadi ya maambukizi mapya ilipungua nchini China na Korea Kusini lakini iliongezeka Ulaya na kuanza kusambaa Marekani. Katika Ulaya Italia ilikuwa nchi iliyoathiriwa vibaya zaidi; serikali ilifunga shule zote pamoja na maduka yasiyo ya chakulas na dawa na kupiga marufuku mikusanyiko yote, ikiwemo ile ya ibada. Hatua kama hizo zilichukuliwa pia katika nchi nyingine. Katika Asia ya Magharibi nchi iliyoathiriwa vibaya zaidi ni Iran.

Kwa jumla si rahisi kupata picha kamili ya uenezi halisi wa virusi hivi. Ilhali dalili za ugonjwa zinafanana na mafua ya kawaida na kifua kikuu, inawezekana mara nyingi maambukizi hayakutambuliwa. Kwa sababu hiyo makadirio ya asilimia ya watu wanaokufa yanatofautiana kati ya nchi na nchi.

Tarehe 11 Machi 2020 Shirika la Afya Duniani ilitamka uenezi wa virusi umefikia ngazi ya pandemia, yaani epidemia (mlipuko) katika nchi nyingi za dunia[14].

Katikati ya mwezi Machi 2020 idadi ya wagonjwa iliongezeka sana katika nchi za Ulaya. Marekani ilizuia wasafiri kutoka Ulaya kuingia. Nchi mbalimbali, pamoja na Ujerumani, zilianza kufunga shule na kukataza mikutano yote yaliyolenga zaidi ya watu 100-500, kwa hiyo kufunga mechi za mpira wa miguu au michezo mingine, pamoja na hoteli na sinema. Kampuni mbalimbali ziliamuru wafanyakazi kukaa nyumbani na kutekeleza shughuli kupitia kompyuta pekee. Tarehe 14 Machi Denmark na Poland zilifunga mipaka kwa wote wasio raia wao, kwa kuamuru raia waliorudi wapaswe kukaa karantini wiki 2.

Kwa jumla serikali zilitangaza kwamba asilimia kubwa ya wananchi wataambukizwa zikiona changamoto kuchelewesha mchakato wa maambukizi ili wale wataokuwa wagonjwa sana wasijitokeze mara moja lakini polepole ili waweze kuhudumiwa hospitalini.

Kufikia tarehe 19 Machi nchi 170 zilikuwa na mgonjwa walau mmoja.

Tarehe 21 Machi Italia ilikuwa imezidi China kwa wingi wa vifo, kwa kuwa siku hiyo walifariki huko watu 796, kuliko siku yoyote ya China.

Hadi tarehe 23 Machi jumla ya waliothibitishwa kupatwa na virusi ilifikia 339,645 na vifo 14,717 kati nchi zaidi ya 40.

Hadi tarehe 13 Aprili walioambukizwa walifikia 1,850,000 na waliofariki dunia 114,000.

Hadi tarehe 2 Juni walioambukizwa walifikia 6,325,303 na waliofariki dunia 377,469.

Hadi tarehe 24 Oktoba walioambukizwa walifikia 42,613,522, wakiwemo wagonjwa 12,701,015 na waliopona 28,762,725; jumla ya waliofariki imefikia 1,149,782. Nchi zilizopatwa na maambukizi zaidi ya milioni moja zilikuwa: Marekani, India, Brazil, Urusi, Ufaransa, Argentina, Hispania na Kolombia. Nchi tatu za kwanza kati ya hizo zilipata kila moja vifo zaidi ya laki moja.

Afrika

Mwanzoni mwa Machi 2020 hakukuwa na taarifa ya maambukizi mengi ndani ya Afrika. Wataalamu walijadiliana kama hilo ni jambo linalotokana na kukosa vifaa vya kupima na kutambua ugonjwa, au kama kuna sababu ya ugonjwa kutoenea katika Afrika. Wagonjwa wengi waliotambuliwa kusini kwa Sahara ni wasafiri waliofika kutoka nchi za nje.

Hadi 12 Machi wagonjwa walithibitishwa hasa katika Afrika Kaskazini: Misri wagonjwa 67 (1 alifariki), Algeria 20 (0), Moroko 6 (1) na Tunisia 7 (0). Upande wa kusini wa Sahara taarifa zilipatikana hasa kutoka Afrika Kusini walipotambulia wagonjwa 17 (0), wengi wao watu waliorudi kutoka safari za Italia. Togo ilikuwa na mgonjwa 1 (0) aliyethibitishwa, Senegal 4 (0), Nigeria 2 (0), Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo 1 (0), Kamerun 2 (0), Burkina Faso 2 (0)[15]

Tarehe 15 Machi jioni mtu wa kwanza alithibitishwa Tanzania akiambukizwa; hadi tarehe 23 idadi ilifikia waambukizwa 12.[16] Wote waliambukizwa nje ya nchi wakagundulika baada ya kufika Tanzania.

Hadi tarehe 13 Aprili katika Afrika Bara nchi pekee isiyothibitisha maambukizi ilikuwa Lesotho, mbali ya Sahara Magharibi na visiwa mbalimbali, kama Komoro.

Kufikia tarehe 2 Juni walioambukizwa walifikia 152,442 na waliofariki dunia 4,344 katika nchi 54.

Ushauri wa kujikinga dhidi ya maambukizi

Maambukizi husambaa hasa kwa majimaji ya mwilini, kama matone madogo ya mate au chafya; mtu aliyeambukizwa atakuwa na virusi kwenye mikono yake akigusa pua au mdomo. Inawezekana mtu aliyeambukizwa asionyeshe dalili za ugonjwa bado lakini anaweza kupitisha virusi tayari.

Unashauriwa[17][18]:

  • epuka kuingia katika msongamano mkubwa wa watu maana wenye virusi hawaonekani kirahisi, na usiende karibu na mtu anayekohoa au anapiga chafya au ana homa. Kaa mbali na mtu mwingine walau meta moja
  • angalia wewe na watu walioko karibu na wewe wana tabia safi.
  • nawa mikono mara kwa mara kwa angalau sekunde 20 kwa maji na sabuni. Ukiwa nacho, tumia kitakasa mikono chenye alikoholi (si chini ya asilimia 60) kusafisha mikono. Ukisafisha mikono utaua virusi vinavyoweza kuwa katika mikono.
  • usiguse macho, pua na midomo kwa mikono kama hujanawa. Mikono inagusa vitu vingi na inaweza kuchukua virusi. Virusi vikiwa katika mikono, vinaweza kuhamia macho, pua na mdomo. Kutoka hapo, vinaweza kuingia mwilini na utakuwa mgonjwa.
  • epuka kuwa karibu sana na wagonjwa, tumia barakoa ya kinga ukimhudumia mgonjwa
  • kaa nyumbani ukiwa mgonjwa (ugonjwa wowote - maana kinga yako ni dhaifu katika hali hii)
  • tembea na karatasi za shashi (kama huna, hata karatasi ya choo / toilet paper) uitumie ukikohoa au kupiga chafya, halafu uitupe mahali pa takataka
  • safisha mara kwa mara vitu unavyovigusa (vikiwa pamoja na kikombe, meza, dawati, simu yako)[19]
  • ukikohoa au ukipiga chafya, funika mdomo na pua kwa kiko
  • ukiwa na homa, kikohozi, na ugumu wa kupumua, tafuta ushauri wa matatibu - lakini piga simu kabla ya kwenda
  • tafuta habari halisi juu ya virusi kutoka kliniki au mamlaka ya afya iliyo karibu na wewe, usikubali kudanganyika.

Tazama pia

Tanbihi

  1. "Coronavirus". WebMD (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2020-01-28.
  2. "Coronavirus | About | Symptoms and Diagnosis | CDC". www.cdc.gov (kwa American English). 2020-01-25. Iliwekwa mnamo 2020-01-28.
  3. "Coronavirus". www.who.int (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2020-03-09.
  4. "Ongezeko la baktria wasiosikia dawa". Iliwekwa mnamo 2020-03-09.
  5. Smith, Richard D (2006). "Responding to global infectious disease outbreaks: Lessons from SARS on the role of risk perception, communication and management". Social Science & Medicine. 63 (12): 3113–23. doi:10.1016/j.socscimed.2006.08.004. PMID 16978751.
  6. "Summary of probable SARS cases with onset of illness from 1 November 2002 to 31 July 2003". World Health Organization (WHO). Iliwekwa mnamo 31 Oktoba 2008.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  7. Julia Naftulin, Business Insider. "Wuhan Coronavirus Can Be Infectious Before People Show Symptoms, Official Claims". ScienceAlert (kwa Kiingereza (Uingereza)). Iliwekwa mnamo 2020-01-28. {{cite web}}: |author= has generic name (help)
  8. COVID-19: WHO renames deadly coronavirus, tovuti ya Al-Jazeera ya 11-2-2020
  9. 5 million people left Wuhan before China quarantined the city to contain the coronavirus outbreak, taarifa ya gazeti Business Insider USA, kupitia www.pulselive.co.ke, tarehe 27-01-2020
  10. Here's how long coronaviruses may linger on contaminated surfaces, according to science, tovuti ya CNN, tar 18-02-2020
  11. Turkey and Pakistan close borders with Iran ove Coronavirus deaths, gazeti la Guardian (UK) ya 23 Feb 2020
  12. Coronavirus: South Korea to test 200,000 sect members as pandemic fears hit markets, gazeti la Guardian (UK) ya 25 Feb 2020
  13. Coronavirus: Britons returning from northern Italy told to self-isolate,BBC ya 25 Feb 2020
  14. WHO characterizes COVID-19 as a pandemic, tovuti ya WHO, iliangaliwa 12 Machi 2020
  15. Confirmed Cases and Deaths by Country, Territory, or Conveyance, tovuti ya worldometers.com ya tar. 12.042020
  16. Coronavirus cases in Tanzania rises to Six
  17. "Tafsiri ya Ushauri 1 ya WHO wa Virusi Mpya ya Corona". https://github.com/isocrdsig/COVID-19. {{cite web}}: External link in |website= (help)
  18. "Tafsiri ya Ushauri 2 ya WHO wa Virusi Mpya ya Corona". https://github.com/isocrdsig/COVID-19. {{cite web}}: External link in |website= (help)
  19. About prevention and treatment, tovuti ya National Center for Immunization and Respiratory Diseases (NCIRD), Division of Viral Diseases, Marekani, iliangaliwa 30 Januari 2020

Viungo vya nje

Makala hii kuhusu mambo ya tiba bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Virusi vya Corona kama sababu yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.