Pasaka ya Kikristo
Kwa matumizi tofauti ya jina hili angalia Pasaka, pia Pasaka ya Kiyahudi na Kipindi cha Pasaka
Mwaka wa liturujia |
---|
Magharibi |
Mashariki |
Pasaka ya Kikristo ni sikukuu ambayo Wakristo karibu wote hufanya kila mwaka ukumbusho wa kufufuka kwake Yesu Kristo siku ya tatu baada ya kusulubiwa, kufa na kuzikwa kwake.
Umuhimu wake
Inahesabiwa kuwa sikukuu muhimu kabisa katika madhehebu mengi ya Ukristo, kwa sababu ufufuko huo ndio msingi wa imani ya Kikristo. Mtume Paulo aliandika kwamba Kristo asingefufuka, imani hiyo ingekuwa haina maana, kwa kuwa asingeondolea dhambi za watu.
Pamoja na kifo cha Yesu, ndio kiini cha kanuni ya imani ya Wakristo wa kwanza kama alivyoipokea Paulo mwenyewe alipoongoka miaka sita baada ya matukio hayo. Katika Waraka wa kwanza kwa Wakorintho aliandika:
15:1 Basi, ndugu zangu, nawaarifu ile injili niliyowahubiri; ambayo ndiyo mliyoipokea, na katika hiyo mnasimama, 2 na kwa hiyo mnaokolewa; ikiwa mnayashika sana maneno niliyowahubiri isipokuwa mliamini bure. 3 Kwa maana naliwatolea ninyi hapo mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo maandiko; 4 na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo maandiko; 5 na ya kuwa alimtokea Kefa; tena na wale Thenashara; 6 baadaye aliwatokea ndugu zaidi ya mia tano pamoja; katika hao wengi wanaishi hata sasa, ila baadhi yao wamelala; 7 baadaye akamtokea Yakobo; tena na mitume wote; 8 na mwisho wa watu wote, alinitokea mimi, kama ni mtu aliyezaliwa si kwa wakati wake. 9 Maana mimi ni mdogo katika mitume, nisiyestahili kuitwa mitume, kwa sababu naliliudhi Kanisa la Mungu. 10 Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami. 11 Basi, kama ni mimi, kama ni wale, ndivyo tuhubirivyo, na ndivyo mlivyoamini.
12 Basi, ikiwa Kristo anahubiriwa ya kwamba amefufuka katika wafu, mbona baadhi yenu husema kwamba hakuna kiyama ya wafu? 13 Lakini kama hakuna kiyama ya wafu, Kristo naye hakufufuka; 14 tena kama Kristo hakufufuka, basi, kuhubiri kwetu ni bure na imani yenu ni bure. 15 Naam, na sisi tumeonekana kuwa mashahidi wa uongo wa Mungu; kwa maana tulimshuhudia Mungu ya kuwa alimfufua Kristo, ambaye hakumfufua, ikiwa wafu hawafufuliwi. 16 Maana kama wafu hawafufuliwi, Kristo naye hakufufuka. 17 Na kama Kristo hakufufuka, imani yenu ni bure; mngalimo katika dhambi zenu. 18 Na hapo wao nao waliolala katika Kristo wamepotea. 19Kama katika maisha haya tu tumemtumaini Kristo, sisi tu maskini kuliko watu wote.
20 Lakini sasa Kristo amefufuka katika wafu, limbuko lao waliolala. 21 Maana kwa kuwa mauti ililetwa na mtu, kadhalika na kiyama ya wafu ililetwa na mtu. 22 Kwa kuwa kama katika Adamu wote wanakufa, kadhalika na katika Kristo wote watahuishwa. 23 Lakini kila mmoja mahali pake; limbuko ni Kristo; baadaye walio wake Kristo, atakapokuja. 24 Hapo ndipo mwisho, atakapompa Mungu Baba ufalme wake; atakapobatilisha utawala wote, na mamlaka yote, na nguvu. 25 Maana sharti amiliki yeye, hata awaweke maadui wake wote chini ya miguu yake. 26 Adui wa mwisho atakayebatilishwa ni mauti. 27 Kwa kuwa, Alivitiisha vitu vyote chini ya miguu yake. Lakini atakaposema, Vyote vimetiishwa, ni dhahiri ya kuwa yeye aliyemtiishia vitu vyote hayumo. 28 Basi, vitu vyote vikiisha kutiishwa chini yake, ndipo Mwana mwenyewe naye atatiishwa chini yake yeye aliyemtiishia vitu vyote, ili kwamba Mungu awe yote katika wote.
Jina la Pasaka
Jina la "Pasaka" limetokana na sherehe ya Pasaka ya Kiyahudi linaloitwa "פסח" (tamka: pasakh) kwa lugha ya Kiebrania. Kinyume cha Kiingereza, ambacho kina maneno mawili, Passover na Easter, katika Kiswahili na lugha nyingine nyingi majina ya sherehe za Kikristo na Kiyahudi hazitofautiani.
Asili yake ni kwamba kusulibiwa na kufufuka kwa Yesu Kristo kumetokea wakati wa sikukuu ya Pasaka ya Kiyahudi mnamo Aprili ya mwaka 30 BK.
Wakristo wa kwanza, ambao wote walikuwa Wayahudi, walisheherekea sikukuu ya Kiyahudi pamoja na kumbukumbu ya ufufuko wa Yesu. Baadaye sherehe na pia tarehe zikawa tofauti, ingawa bila kwenda mbali sana. Badiliko kubwa zaidi lilikuwa lile la Wakristo kuadhimisha daima Pasaka siku ya Jumapili kwa kuwa ndiyo siku ya ufufuko, wakati Wayahudi wanadhimisha Pasaka kwa kuangalia tarehe, bila kujali ni siku ipi ya juma.
Tarehe ya Pasaka
Tarehe ya Pasaka inafuata kuonekana kwa mwezi angani, kwa hiyo sikukuu hiyo haina tarehe imara katika kalenda ya kawaida. Inapatikana katika Machi au Aprili. Pasaka haifuati mwezi pekee lakini tarehe yake imefungwa pia kwa sikusare (au ekwinoksi), kwa hiyo haiendelei kuzunguka mwaka wote kama tarehe za Kalenda ya Kiislamu.
Mtaguso wa kwanza wa Nisea mwaka 325 uliamua ya kwamba Pasaka itasheherekewa Jumapili ya kwanza baada ya mwezi mpevu wa kwanza baada ya 21 Machi (tarehe ya sikusare machipuo ambayo ni siku ya usawa wa mchana na usiku, hivyo mwanzo wa majira ya kuchipua kaskazini mwa dunia). Kwa kuwa mwezi mpevu baada ya 21 Machi inaweza kutokea kati ya 22 Machi na 19 Aprili, tarehe ya Pasaka, ambayo ni Jumapili inayofuata, hutokea kati ya 22 Machi na 25 Aprili.
Katika Ukristo kuna kalenda mbili zinazotumika, hivyo pia tarehe mbili za Pasaka. Kanisa la magharibi, yaani Wakatoliki wengi na Waprotestanti, hufuata Kalenda ya Gregori (ambayo imekuwa kalenda ya kawaida ya kimataifa), lakini Waorthodoksi wanaendelea kutumia kalenda iliyotangulia, yaani Kalenda ya Juliasi. Ndiyo maana mara nyingi Pasaka inaendelea kuadhimishwa katika Jumapili tofauti kati ya pande hizo mbili. Hata hivyo kuna majadiliano yenye lengo la kufikia makubaliano ili kuadhimisha Pasaka pamoja. Kwa sasa tofauti ya kalenda inaleta Kanisa la Mashariki kusheherekea Pasaka wakati mwingine hata katika mwezi wa Mei wa kalenda ya Gregori, ingawa kwao bado ni Aprili kufuatana na kalenda ya Juliasi.
Tanbihi
Viungo vya nje
Wikisource has original text related to this article: |
- Liturujia
- 50 Catholic Prayers for Easter Ilihifadhiwa 31 Machi 2012 kwenye Wayback Machine.
- Liturgical Resources for Easter
- Holy Pascha: The Resurrection of Our Lord (Orthodox icon and synaxarion)
- Mapokeo
- Liturgical Meaning of Holy Week (Greek Orthodox Archdiocese of Australia)
- Easter in the Armenian Orthodox Church Ilihifadhiwa 29 Januari 2006 kwenye Wayback Machine.
- Roman Catholic View of Easter (from the Catholic Encyclopedia)
- Easter in Belarus: In Pictures Ilihifadhiwa 4 Juni 2012 kwenye Wayback Machine. on the official website of the Republic of Belarus Ilihifadhiwa 15 Januari 2018 kwenye Wayback Machine.
- Polish Easter Traditions
- Hesabu
- A Perpetual Easter and Passover Calculator Julian and Gregorian Easter for any year plus other info
- Almanac—The Christian Year Julian or Gregorian Easter and associated festivals for any year
- Easter Dating Method for calculator
- Dates for Easter 1583–9999 Ilihifadhiwa 14 Oktoba 2007 kwenye Wayback Machine.
- Orthodox Paschal Calculator Julian Easter and associated festivals in Gregorian calendar 1583–4099
- About the Greek Easter and Greek Easter Calculator Orthodox Paschal calculator with technical discussion and full source code in javascript
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Pasaka ya Kikristo kama historia yake, matokeo au athari zake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |