Biblia ya Kikristo
Biblia ya Kikristo ni mkusanyo wa maandiko matakatifu ya Ukristo. Maandiko hayo mbalimbali yanaitwa tangu zamani sana "vitabu" tu, inavyomaanishwa na neno la Kigiriki βιβλια, "biblia" ambalo ni wingi wa neno "biblos" yaani "kitabu".
Hutofautishwa na Tanakh ambayo ndiyo maandiko matakatifu ya dini ya Uyahudi na ambayo pengine inatajwa kwa jina lilelile la "Biblia", hasa katika matoleo ya Biblia ya Kiebrania. Vitabu vyake vimo katika sehemu ya kwanza ya Biblia ya Kikristo kwa jina la "Agano la Kale".
Biblia ya Kikristo hugawiwa sehemu mbili ambayo ni Agano la Kale na Agano Jipya. Agano la Kale lina maandiko yaliyoandikwa kabla ya Yesu Kristo na vitabu vya Agano Jipya viliandikwa baada yake.
Agano la Kale
Kimsingi vitabu vya Agano la Kale ni vilevile vya Biblia ya Kiebrania, ingawa madhehebu ya Kikristo hutofautiana kidogo katika hilo. Ni kwamba wakati wa kutokea kwa Ukristo palikuwa na tofauti ndani ya Uyahudi kuhusu vitabu vilivyohesabiwa kuwa maandiko matakatifu. Suala hilo liliondolewa kuanzia mwaka 80 BK wataalamu wa Wayahudi wa huko Jabneh (Jamnia) walipochukua msimamo mkali dhidi ya wafuasi wa Yesu.
Kwa wakati huo Wakristo walikuwa wamezoea tayari toleo la Kigiriki la maandiko matakatifu yaliyotafsiriwa katika karne ya 2 KK ambalo linajulikana kwa jina la Septuaginta na kuwa na vitabu kadhaa visivyokuwa vimetunzwa katika lugha asili ya Kiebrania wala ya Kiaramu, au vilivyoandikwa moja kwa moja katika lugha ya Kigiriki.
Hivyo Biblia ya Kikristo ilikuwa na vitabu 7 (viwili vya Wamakabayo, Yoshua bin Sira, Hekima, Tobiti, Yudith na Baruku, pamoja na sehemu za Esta na Danieli) visivyokubaliwa baadaye na Wayahudi.
Vitabu hivyo 7 vikaja kukataliwa na Martin Luther katika karne ya 16, halafu na Waprotestanti wengi, lakini vinazidi kutumiwa na Kanisa Katoliki na Waorthodoksi kwa jina la Deuterokanoni.
Agano Jipya
Kuna vitabu 27 vya Agano Jipya. Vinne vya kwanza ni Injili nne zinazoleta habari za maisha, matendo na maneno ya Yesu.
Vingine ni Matendo ya Mitume, Nyaraka za Mitume, hasa za Mtume Paulo, na Ufunuo wa Yohane.
Msimamo wa Kanisa Katoliki
Kanisa Katoliki linatambua Maandiko Matakatifu kati ya maandishi yote ya binadamu kwa njia ya Mapokeo, yaani kwa sababu yametumiwa na Kanisa tangu mwanzo kwa kulisha kwa hakika imani yake. Tunahitaji Mapokeo kwa kuwa Maandiko yenyewe hayataji orodha ya vitabu vyake vyote, Sanasana Yesu alividokeza baadhi akisema yanamzungumzia na kutimia ndani yake, “Ni lazima yatimizwe yote niliyoandikiwa katika Torati ya Musa, na katika Manabii, na Zaburi” (Lk 24:44). Halafu Barua ya Pili ya Mtume Petro ikalinganisha “na Maandiko mengine” nyaraka zote ambazo Paulo aliziandika “kwa hekima aliyopewa” (2Pet 3:15-16).
Sababu nyingine za Biblia kutojitosheleza ni kwamba mambo mengi muhimu hayakuandikwa, “Kuna mambo mengine mengi aliyoyafanya Yesu, ambayo yakiandikwa moja moja, nadhani hata ulimwengu usingetosha kwa vile vitabu vitakavyoandikwa” (Yoh 21:25). Tena barua ni nusu tu ya kuonana; hivyo Yesu hakuandika lolote, nao Mitume hawakupenda kuandika yote. “Kwa kuwa ninayo mambo mengi, sitaki kuyaandika kwa karatasi na wino; lakini nataraji kuja kwenu, na kusema nanyi mdomo kwa mdomo, ili furaha yetu iwe imetimizwa” (2Yoh 12). “Nalikuwa na mambo mengi ya kukuandikia, lakini sipendi kukuandikia kwa wino na kalamu. Lakini nataraji kukuona karibu, nasi tutasema mdomo kwa mdomo” (3Yoh 13-14). Hasa ibada haziwezi kufanyika kwa barua; k.mf. kuwekea mikono ili kumshirikisha Roho Mtakatifu. Paji la namna hiyo halipitii Maandiko, bali Mapokeo tu. Hatimaye Biblia ikipotoshwa haipingi, kwa kuwa si mtu hai anayeweza kujitetea.
Biblia iliandikwa kusudi tupate “kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini” tuwe “na uzima wa milele” (Yoh 20:31). “Tangu utoto umeyajua Maandiko Matakatifu, ambayo yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu. Kila Andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki” (2Tim 3:15-16). Si lengo lake kutufundisha historia, jiografia wala sayansi: kuhusu elimu hizo na kuhusu ufasaha wa lugha Biblia ilitegemea ujuzi na vipawa vya watu walioiandika.
Vitabu vya Biblia vinatofautiana kwa kuwa Mungu alijifunua hatua kwa hatua; hivyo vitabu 46 vilivyoandikwa kabla ya Yesu vinaitwa Agano la Kale na 27 vilivyomfuata vinaitwa Agano Jipya. “Kwa kule kusema, Agano jipya, amelifanya lile la kwanza kuwa kuukuu. Lakini kitu kianzacho kuwa kikuukuu na kuchakaa ki karibu na kutoweka” (Eb 8:13). Mungu “ndiye aliyetutosheleza kuwa wahudumu wa agano jipya; si wa andiko, bali wa roho; kwa maana andiko huua, bali roho huhuisha” (2Kor 3:6).
Pamoja na hayo, vitabu vyote vya Biblia vinahusiana kwa kuwa vinaangaziana na kuunda kitabu kimoja ambacho ni Neno la Mungu yuleyule, ingawa katika hatua tofauti: Agano la Kale ndiyo maandalizi na Agano Jipya ndio utimilifu wake. Yesu alisema, “Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua Torati au Manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza” (Math 5:17). Tunahitaji Agano la Kale ili tuelewe vizuri Agano Jipya katika maandalizi yake, na tunahitaji Agano Jipya ili tuelewe Agano la Kale lilivyotimilizwa na Yesu.
Haifai tushike neno lolote la Agano la Kale kama Wayahudi wasiozingatia jinsi Yesu alivyolitimiliza kwa maneno na matendo hata wakamshutumu kutenda kinyume: “Mtu huyo hakutoka kwa Mungu, kwa sababu haishiki sabato” (Yoh 9:16). Alipofafanua amri 10 za Mungu alikariri: “Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa… lakini mimi nawaambieni…” (Math 5:21,27,31,33,38,43). Alipouliziwa unajisi wa vyakula kadhaa, alisisitiza, “’Hivi hata ninyi hamna akili? Hamfahamu ya kwamba kila kitu kilicho nje ya mtu, kikimwingia, hakiwezi kumtia unajisi; kwa sababu hakimwingii moyoni, ila tumboni tu; kisha chatoka kwenda chooni?’ Kwa kusema hivi alivitakasa vyakula vyote” (Mk 7:18-19). “Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo” (Kol 2:16-17). Hakika, mwili ni mzito kuliko kivuli chake.
Yesu alitimiliza Agano la Kale kwa namna isiyotarajiwa hasa aliposulubiwa, akionekana na Wayahudi wenzake kama kwamba amelaaniwa: “Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa: ‘Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti’; ili kwamba baraka ya Ibrahimu iwafikilie Mataifa katika Yesu Kristo, tupate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani” (Gal 3:13-14).
Kati ya vitabu vya Biblia, vilivyo bora ni Injili 4 zilizoandikwa na Mathayo, Marko, Luka na Yohane. Ndio moyo wa Maandiko Matakatifu yote, kwa kuwa ndizo shuhuda kuu juu ya maisha na mafundisho ya Yesu. Yeye “amepata huduma iliyo bora zaidi, kwa kadiri alivyo mjumbe wa agano lililo bora, lililoamriwa juu ya ahadi zilizo bora. Maana kama lile la kwanza lingalikuwa halina upungufu, nafasi isingalitafutwa kwa lile la pili” (Eb 8:6-7).
Tuelewe Maandiko Matakatifu kwa kuzingatia hasa Mungu alitaka kusema nini kuhusu wokovu wetu kupitia waandishi wengi aliowaongoza kuyatunga kwa lugha na mitindo mbalimbali. Lakini ebu, “Yamo mambo ambayo ni vigumu kuelewa nayo; na mambo hayo watu wasio na elimu, wasio imara, huyapotoa, kama vile wayapotoavyo na Maandiko mengine, kwa uvunjifu wao wenyewe” (2Pet 3:16). Utitiri wa madhehebu yanayoshindana yakidai kushikilia Biblia tu unathibitisha uwekezano mkubwa wa kuipotosha kwa namna moja au nyingine. “Utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia walimu makundi makundi, kwa kuwa wana masikio ya utafiti; nao watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za uongo” (2Tim 4:3-4). Njia pekee ya kukwepa fujo hiyo ni kuelewa Maandiko ndani ya Kanisa, kadiri ya Mapokeo yake hai. “Lakini mtu yeyote akitaka kuleta fitina, sisi hatuna desturi kama hiyo, wala makanisa ya Mungu” (1Kor 11:16). Biblia nje ya Kanisa ni kama samaki nje ya maji.
Ufunuo wa Mungu unaweza kufafanuliwa rasmi na umoja wa Maaskofu tu, kwa kuwa ndio waandamizi wa Mitume 12 wa Yesu. “Au je, neno la Mungu lilitoka kwenu? Au kuwafikia ninyi peke yenu?” (1Kor 14:36). “Hakuna unabii katika Maandiko upatao kufasiriwa kama apendavyo mtu fulani tu. Maana unabii haukuletwa popote kwa mapenzi ya mwanadamu” (2Pet 1:20-21). Tunahitaji unyenyekevu wa Mwafrika ambaye mwinjilisti Filipo alimsikia “anasoma chuo cha nabii Isaya; akanena, ‘Je, yamekuelea haya unayosoma?’ Akasema, ”Nitawezaje kuelewa, mtu asiponiongoza?’ Akamsihi Filipo apande na kuketi pamoja naye” (Mdo 8:30-31).
Tazama pia
Viungo vya nje
- Biblia Takatifu w/audio (Kiswahili) Ilihifadhiwa 2 Mei 2012 kwenye Wayback Machine.
- Biblia ya Union Version (Kiswahili)
- Tafsiri mpya ya Biblica.com Ilihifadhiwa 10 Julai 2010 kwenye Wayback Machine.
Mwanzo * Kutoka * Walawi * Hesabu * Kumbukumbu * Yoshua * Waamuzi * Ruthu * Samueli I * Samueli II * Wafalme I * Wafalme II * Mambo ya Nyakati I * Mambo ya Nyakati II * Ezra * Nehemia * TobitiDK * YudithiDK * Esta * Wamakabayo IDK * Wamakabayo IIDK * Yobu * Zaburi * Methali * Mhubiri * Hekima DK * SiraDK * Wimbo Bora * Isaya * Yeremia * Maombolezo * BarukuDK * Ezekieli * Danieli * Hosea * Yoeli * Amosi * Obadia * Yona * Mika * Nahumu * Habakuki * Sefania * Hagai * Zekaria * Malaki
Alama ya DK inaonyesha vitabu vya deuterokanoni visivyopatikana katika matoleo yote ya Biblia.
Mathayo Marko Luka Yohane Matendo Waroma Wakorintho 1 Wakorintho 2 Wagalatia Waefeso Wafilipi Wakolosai Wathesalonike 1 Wathesalonike 2 Timotheo 1 Timotheo 2 Tito Filemoni Waebrania Yakobo Petro 1 Petro 2 Yohane 1 Yohane 2 Yohane 3 Yuda Ufunuo
Makala hii kuhusu mambo ya Biblia bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Biblia ya Kikristo kama historia yake au athari wake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |