Kimondo
Kimondo ni kiolwa kidogo cha angani kinachozunguka Jua katika anga-nje. Kikiingia katika angahewa la Dunia kinaonekana kama mwali wa moto angani.
Majina na ukubwa
Kimsingi hakuna tofauti kati ya kimondo na asteroidi: ni suala la ukubwa tu. Violwa vidogo kuanzia ukubwa wa punje ya mchanga hadi kufikia kipenyo cha mita kadhaa huitwa vimondo. Vikubwa zaidi huitwa asteroidi. Hivyo kimondo ni kidogo kuliko asteoridi na kikubwa kushinda vumbi la anga-nje.
Katika lugha nyingi kuna majina tofauti kutaja hali mbalimbali za vimondo.
- Kimondo-anga (kwa Kiingereza meteoroid) ni kimondo wakati kipo kwenye anga-nje; ni vipande vya mwamba au metali vinavyopatikana katika anga-nje, kwa kawaida kutokana na kuvunjika kwa asteroidi au nyotamkia (kometi).
- Kimondo (ing. meteor) ni hali ya kimondo-anga kinapopita kwenye angahewa ya Dunia pamoja na mwangaza unaoonekana, hasa kwenye anga la usiku. Wakati kinapopita katika angahewa ya Dunia, kinawaka kutokana na joto la msuguano na molekuli za hewa; kinaonekana kama mstari mfupi wa nuru. Waswahili wa Kale waliita hali hii "kinga cha shetani" kufuatana na sura 67,5 ya Kurani[1][2].
- Kimondo-nchi (ing. meteorite) ni mabaki ya kimondo-anga yaliyofika kwenye uso wa ardhi kama mawe bila kuungua kabisa hewani.
Kugonga angahewa ya Dunia
Obiti (ing.orbit) ya kimondo inaweza kuingiliana na njia ya Dunia au sayari nyingine. Kimondo kikikaribia kiolwa cha angani kikubwa zaidi kinavutwa na graviti yake.
Kikikaribia Dunia yetu kinaingia katika angahewa na kuanguka chini kwa kasi kubwa sana. Njiani kinapashwa moto kutokana na msuguano wa hewa dhidi yake. Kiasi cha joto kinatosha kuchoma kabisa kimondo kidogo hewani. Hii inaonekana na macho matupu kama mstari wa moto angani unaowaka kwa sekunde 1-2. Hii ni hali ya kimondo inayoitwa pia "meteori". Waswahili wa Kale waliita "Vinga vya sheitani" walieleza miali hiyo ya moto angani kuwa malaika angani wanaozuia mashetani kupanda juu kwa kuwarushia vipande vya kuni vilivyowaka.[3]
Kama kimondo ni kikubwa zaidi, ni sehemu zake za nje tu zinazochomwa, na kiini kinaanguka kwenye uso wa Dunia. Mara nyingi kimondo kinapasuka hewani na kumwaga vipande vyake.
Kati ya vimondo kumi vikubwa kabisa duniani ambavyo mabaki yake yanaonekana, kimojawapo ni Kimondo cha Mbozi nchini Tanzania. Cha kwanza kabisa kinapatikana Namibia kikiwa na urefu wa mita 2.7.
Mvua ya vimondo
Vipande vya vimondo-anga mara nyingi hupatikana kwenye anga-nje na kuonekana kama wingu lililotawanyika sana. Wakati Dunia linapopita eneo la wingu la aina hiyo vipande vidogo vya vimondo-anga huingia katika angahewa kwa kasi kubwa na kuungua. Mvua ya vimondo huonekana kama kuongezeka kwa mianga ya vimondo angani kwa kipindi cha siku kadhaa, ilhali idadi kubwa ya vimondo huwaka kwa siku chache tu.
Mvua ya vimondo kwa kawaida unasababishwa na mabaki ya nyotamkia. Wingu la vipande hivyo linazunguka Jua kwenye obiti inayokutana na obiti ya Dunia, kwa hiyo kuna mawingu ya namna hiyo yanayorudi kila mwaka. Vipande vya wingu husogea angani kwa pamoja; vikigusana na angahewa la Dunia mianga yake inaonekana kutokea katika sehemu fulani ya anga. Hivyo mvua ya vimondo hupewa jina kutokana na eneo la kundinyota ambako inaonekana, kama vile Perseidi na Leonidi. Perseidi huwa na jina la Perseus (Farisi) ikionekana kila mwaka mnamo 12 Agosti na Leonidi huitwa hivyo kutokana na Leo (Simba ikionekana mnamo 17 Novemba.
Hatari za vimondo
Kimondo, kama ni kiolwa cha kukaribia Dunia, ni hatari kwa vyombo vya angani kwa sababu ya kasi yake kubwa. Hata punje ndogo yaweza kusababisha uharibifu mwingi.
Duniani kuna hatari fulani lakini hali halisi si kubwa ingawa vimondo vinaingia kila saa katika angahewa. Lakini theluthi mbili za uso wa Dunia ni bahari na sehemu kubwa ya nchi kavu haina watu. Katika miaka yote ya karne ya 20 kuna taarifa 21 pekee za nyumba kugongwa na kimondo.
Katika karne ya 20 kuna taarifa zifuatazo kuhusu watu walioathiriwa na vimondo:
- 5 Septemba 1907 Weng-li, China - familia yote kufa
- 30 Juni 1908 mlipuko mkubwa ulitokea juu ya eneo la Tunguska, Urusi, uliosababishwa na kimondo mkubwa au hata asteroidi. Inaaminiwa wavindaji kadhaa waliuawa.
- 28 Aprili 1927 Aba, Japan - binti kujeruhiwa
- 8 Desemba 1929 Zvezvan, Yugoslavia - kimondo kugonga kwenye arusi, mmoja kufa
- 16 Mei 1946 Santa Ana, Meksiko - nyumba kuharibiwa, watu 28 kujeruhiwa
- 30 Novemba 1946 Colford, Ufalme wa Muungano - simu kuharibiwa, mvulana kujeruhiwa
- 28 Novemba 1954 Sylacauga, Alabama, USA - kimondo cha kilogramu nne kugonga nyumba, mama kujeruhiwa
- 14 Agosti 1992 Mbale, Uganda - vimondo 48 kuanguka, mvulana kujeruhiwa
- 13 Februari 2013 - kimondo kikubwa (au: asteroidi ndogo) kilkipasuka juu ya mji wa Chelyabinsk, Urusi. Watu wengi walijeruhiwa na vioo vya nyumba vilivyopasuka.
Hatari ni kubwa kweli kama asteroidi inagonga Dunia, kwa kuwa pigo la asteroidi linaachisha nishati sawa na mabomu ya nyuklia. Mgongano na asteroidi kubwa yenye kipenyo cha km 180 unaaminiwa uliangamiza dinosauri na kusababisha vifo vya viumbehai wengi duniani miaka milioni 65 iliyopita.
Tazama pia
Tanbihi
- ↑ Surat Al-Mulk (The Sovereignty) - سورة الملك, tovuti ya quran.com
- ↑ Qur'ani Tukufu, tarjuma ya Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani, tovuti ya International Islamic University Malaysia
- ↑ Sacleux, Dictionnaire Swahili - Français uk. 384: "Vinga vya shetani, étoiles filantes, que les Musulmans pensent être les tisons enflammés, dont se servent les anges pour chasser les démons, qui tentent de s'approcher du ciel pour voir ce qui s'y passe."
Viungo vya Nje
- Meteor Shower Calendar 2020, tovuti hii inaruhusu kuchagua mvua wa vimondo fulani na kuangalia tarehe zake na mahali ambako utaonekana; kuanzia mwaka 2012 n.k. utabadilisha tu namba ya mwaka katika URL
- Kimondo cha Mbozi (Kijerumani) Archived 28 Septemba 2007 at the Wayback Machine.
- Ujurasa mzuri juu ya vimondo kutoka Kanada Archived 15 Septemba 2007 at the Wayback Machine.
- Hatari za vimondo
- Matokeo ya migongano na vimondo Archived 7 Septemba 2006 at the Wayback Machine.
Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Kimondo kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |