Jiua
Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Kujiua ni tendo la mtu kumaliza maisha yake mwenyewe ama kwa kufanya kitu kinachoharibu uhai wake au kwa kuacha yale yanayohitajika kuuendeleza kama kula au kunywa.
Yaliyomo |
[hariri] Kutokea kwa kujiua
Shirika la Afya Duniani linakadiria ya kwamba duniani kote mtu anajiua kila baada ya sekunde 39 maana yake dunaini ni kama watu 800,000 kila mwaka. Pamoja na yale wanaofaulu kuna majaribio kila mwaka kati ya milioni 10 hadi 20. Kwa hiyo tendo la kujiua ni kati ya sababu muhimu za kifo cha watu.
Idadi ya wanaume wanaojiua kwa jumla inazidi idadi ya wanawake mara nne. Wazee hujiua kushinda vijana. [1]
[hariri] Sababu za kujiua
Kuna sababu mbalimbali kwa nini watu wanajiua kama vile
- hali mbaya ya wasiwasi, hofu, matatizo yanayomsababisha kuwa anataka kuepukana nayo mara moja
- ugonjwa wa akili
- maumivu makali
- kuona aibu kubwa pamoja na mawazo ya kiutamaduni yanayofundisha ni heri kufa kuliko kuishi na aibu
- kujisikia kuwa na wajibu wa kumaliza maisha kwa heshima ya taifa, ukoo, familia, dini au mengine
Waganga wa kisasa huona kujiua kama tatizo la afya ya kiroho; mara nyingi watu wanaojaribu kujiua hawataki kufa bali kuepukana na matatizo na kama wangeona njia ya kuachana na tatizo wasingejiua. Hivyo majaribio ya kujiua inaweza kuwa jaribio la kuwaonyesha watu wa mazingira ya kwamba kuna tatizo zito na kuomba msaada.
Watu wanaorudia majaribio ya kujiua mara nyingi wanafaulu hatimaye kama hali yao haibadiliki.
[hariri] Njia za kujiua
Njia ni nyingi na upendeleo hutegemea mazingira na utamaduni. [2]
- Watu wa Marekani hupendelea kujipigia risasi (52% wa wale waliojiua mwaka 2005); inaonekana sababu mkubwa ni ya kwamba kuna bunduki nyingi zinapatikana kirahisi
- Wajerumani hupendelea kujinyonga kwa kamba (50%), kujipigia risasi kunatokea mara chache (sheria kuhusu bunduki ni kali)
- Katika Ulaya ya Mashariki karibu wote wanaojiua hujinyonga kwa kamba
- kwenye nchi za wakulima wengi kama Asia, Amerika Kusini na pia Ureno wengi hutumia sumu mbalimbali hasa za kuua wadudu
- katika nchi ndogo ambako watu huishi hasa mjini kama Hong Kong au Luxemburg kuna asilimia kubwa wanaoruka kutoka majengo marefu.
Kwa jumla wanaume hutumia zaidi mbinu kali kama silaha au kujinyonga, wanawake njia ambazo ni pole zaidi kama kunywa sumu au kujizama kwenye maji.
[hariri] Kujiua na jamii
Katika mafundisho ya dini nyingi tendo la kujiua linatazamiwa kama dhambi au kosa. Katika Ulaya watu waliojiua hawakuzikwa makaburini pamoja na watu wengine lakini kando hadi karne ya 19. Nchi mbalimbali zilikuwa na sheria dhidi ya wale waliojiua na jaribio lilitazamiwa kama kosa la jinai.
Kuna pia jamii ambako hatua ile inaheshimiwa kama azimo la kila mtu.
Katika utamaduni wa Japani kujiua kulitazamiwa kama nafasi ya mkabaila kurudisha heshima yake kama ameshindwa au kuonekana na kosa kubwa.
Katika utamaduni wa Uhindi mjane alisifiwa kama alijiua baada ya kifo cha mume wake hasa kwa kujichoma pamoja na maiti ya marehemu.
Katika vita vilivyopita askari walisifiwa kama waliamua kujiua kwa kutumia miili yao kama silaha dhidi ya adui. Mfano mashuhuri ni marubani wa Kamikaze wa Japani waliojirusha pamoja na ndege zao dhidi ya meli za Marekani wakati wa vita kuu ya pili ya dunia. Wanamigambo wa Tamil Tiger nchini Sri Lanka walishambulia jeshi la serikali mara nyingi kwa mabomu hai yaani askari waliobeba bomu na kujilipusha karibu na maadui.
Mbinu huohuo unatumiwa pia katika dunia ya Kiislamu na wanamigambo na magaidi mbalimbali hasa katika nchi kama Palestina, Irak au Afghanistan. Ilitumiwa pia na magaidi kutoka Checheniya dhidi ya Warusi.
[hariri] Maelezo na vyanzo
- ↑ Taarifa ya WHO
- ↑ [http://www.who.int/bulletin/volumes/86/9/07-043489.pdf Methods of suicide: international suicide patterns derived from the WHO mortality database]