Nenda kwa yaliyomo

Bumbuli

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Kwemuae au Komeo ja Washai,)


Bumbuli
Bumbuli is located in Tanzania
Bumbuli
Bumbuli

Mahali pa mji wa Bumbuli katika Tanzania

Majiranukta: 4°52′0″S 38°28′0″E / 4.86667°S 38.46667°E / -4.86667; 38.46667
Nchi Tanzania
Mkoa Tanga
Wilaya Wilaya ya Bumbuli
Idadi ya wakazi
 - Wakazi kwa ujumla 9,917

Bumbuli ni kata ya Wilaya ya Bumbuli katika Mkoa wa Tanga, Tanzania.

Katika sensa ya mwaka 2022 wakazi walihesabiwa [1]. Kwa mujibu wa sensa iliyofanyika mwaka wa 2012, kata ina wakazi wapatao 10,159 waishio humo.

Wenyeji wa Bumbuli ni Wasambaa.

Bumbuli imezungukwa na milima kila upande, mji wenyewe wa Bumbuli upo chini ya mlima mkubwa unaoitwa Maduda ambao ni mshikano wa mwamba mkubwa ulioanzia sehemu inayoitwa Kungutana na kuendelea mpaka eneo la Mmanyai ambapo mwamba huo unaishia.

Kwa upande wa kaskazini mashariki upo mlima mkubwa unaoitwa Kizimba. Mlima huu huaminika sana kwa kuonyesha dalili za mvua kubwa mara wingu linapotanda juu yake.

Bumbuli mjini.

Kutokana na hali nzuri ya hewa ya eneo hili, wamisionari Wajerumani wa kwanza kufika milima ya Usambara walivutiwa sana na eneo hili na kujenga hospitali kubwa ambayo kwa sasa inamilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini Mashariki.

Historia

[hariri | hariri chanzo]
Bumbuli na milima ya Usambara mwaka 1906.

Bumbuli ni moja ya vijiji vya zamani sana katika nchi ya Tanzania.

Kiongozi wa jadi aliyekuwa anaongoza Bumbuli kabla ya uhuru alikuwa anaitwa Zumbe Daudi Sozi Kibanga. Moja ya sifa za kiongozi huyu ilikuwa kuleta mvua, tofauti na viongozi wa makabila mengine Zumbe Daudi Sozi Kibanga alikuwa haleti mvua kwa njia ya uganga au uchawi, la hasha. Zumbe Daudi alikuwa na kipawa cha kuomba (sala) kwa Mwenyezi Mungu na wananchi wakapata mvua.

Mahali alipokuwa anakaa Zumbe Daudi palikuwa panaitwa Kitaa. Kabla ya kuja wamisionari katika eneo hili kijiji kilikuwa kimoja kinachoitwa Kungutana. Kwemuane au Komeo ja washai kulikuwa eneo maalumu kwa ajili ya kuwahukumu kifo wachawi.

Baada ya kuja Wamisionari wa kwanza wa Kijerumani walivutiwa sana na eneo hili ndipo walipowashawishi wananchi kuhamia maeneo mengine ili waweze kujenga kanisa na shule katika eneo hilo la Kungutana.

Wananchi wa eneo hilo walihama eneo hilo na wengi walihamia kijiji kinachoitwa Bumbuli Kaya, mita 200 tu kutoka Kungutana na wengine walihamia eneo jipya linalojulikana kama Bumbuli Mission.

Wamisionari wa Kijerumani walijenga shule mbili na kanisa. Shule ya Maduda ambayo ilikuwa middle school kwa wakati huo, na nyingine inaitwa Shule ya Msingi Bumbuli na Kanisa la Kilutheri lipo mpaka leo.

Wajerumani hao waliendelea na kujenga hospitali kubwa sana katika eneo hilo na kwa sababu wamisionari hao wa Kijerumani walikuwa Walutheri, basi baada ya uhuru hospitali hiyo haikutaifishwa na serikali kama uliokuwa mfumo wa wakati huo wa kutaifisha mashirika binafsi, bali ilipewa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ili liendelee kuiendesha. Hospitali hiyo inaitwa Bumbuli hospitali.

Bumbuli Mission

Bumbuli kwa sasa ni Halmashauri na Bumbuli penyewe ndiyo makao makuu ya Halmashauri hiyo.

Bumbuli ina vijiji vifuatavyo: Mbokoi, Mazang'ombe Misaai, Maduda, Dule, Galambo, Kwanguruwe, Wena, Kitivo, Kiangwi, Mayo, Shembekeza, Ngulwi, Mahezangulu, Ngee, Muungui, Muangae, Kianga, Kwabosa na Mkoo.

Wenyeji wa Bumbuli ni wakulima. Shughuli yao kubwa ni kilimo: mazao makuu ya chakula ni mahindi, muhogo, maharage na viyuga. Mazao ya biashara ni chai, kahawa na iliki.

Bumbuli kuna viwanda viwili vya kusindika majani ya chai: viwanda hivyo ni Mponde Tea Factory na Helkulu Estate. Kiwanda kingine kilikuwa Balangai estate ambacho kimeshafungwa kwa kukosa usimamizi mzuri. Wananchi wa Bumbuli huuza chai yao katika viwanda hivyo na kujiongezea kipato chao.

Wasambaa wa Bumbuli ni wanajamii waliostaarabika na wasio na ubaguzi - utaratibu wao ni kwamba hawaongei Kisambaa akiwepo mtu asiyejua Kisambaa miongoni mwao.

Bumbuli pana mkusanyiko wa watu kutoka makabila mbalimbali, kutokana na kuwepo kwa chuo cha tiba ambacho kila mwaka wanafunzi wapya hufika kutoka sehemu mbalimbali za nchi. Wageni wanaofika Bumbuli au kwa ajili ya masomo au kwa ajili ya kufanya kazi katika hospitali na shule wanapata ushirikiano wa karibu sana kutoka kwa wenyeji.

Asili ya Wasambaa si wachoyo, hivyo jamii nyingi zilizofika kutoka mikoa mbalimbali wamejionea ukarimu wetu.

Utamaduni

[hariri | hariri chanzo]

Lugha za watu wa Bumbuli ni Kisambaa (Kishambala) na Kiswahili.

Chakula kikubwa cha Wasambaa ni ugali wa sembe, ugali wa muhogo maarufu kama bada, viyuga, magimbi, mhoro na ndizi.

Aina ya muziki inayovuma sana ni Mdumange. Ngoma ya Mdumange zamani ilikuwa na mvuto sana kutokana na msanii maarufu aliyejulikana kama Mawawa a.k.a. mzimu wa Shehondo aliyekuwa ana kikundi chake ambacho kilikuwa kikihamasisha sana muziki huo. Kijiji cha Bumbuli Kaya kiliendelea na ngoma hiyo baada ya msanii Mawawa kufariki. Hata hivyo kutokana na utandawazi na vijana wengi kukimbilia mijini ngoma hiyo inaonekana kufa.

Wakazi wa Bumbuli ni wachapakazi sana: mwezi Januari huwa wanaandaa mashamba yao, hivyo kipindi hicho ni kilimo tu, na mwezi wa tisa ni kuvuna.

Baada ya mavuno wakazi wa eneo hili hupumzika wakisubiria kwa hamu sikukuu za Krismasi ambazo zinasherehekewa kwa nguvu zote.

Baada ya kazi wasambaa wa Bumbuli huburudika na pombe yao ya asili wanayoipenda sana inayoitwa Boha au Mghuwa. Pombe hii ya asili hutengenezwa kutokana na zao la muwa. Miwa hukatwa na hukamuliwa kwenye mashine ya kiasili inayoitwa mkoroto au kwa jina la kiasili Mkooto.

Mashine ya Mkooto inayotengeneza pombe ya asili ya kisambaa ya Boha

Katika mji wa Bumbuli kuna vivutio vingi, cha kwanza kabisa utakachokutana nacho ni mwamba mkubwa mno ambao ni kama umeuinamia mji wa Bumbuli sehemu ya Bumbuli Mission. Mwamba huu umetengeneza mlima mkubwa unaoitwa Maduda. Juu ya mlima huu wa Maduda pale kileleni panaitwa Kwentui. Sehemu hii hutumiwa na Wakristo wa eneo la Bumbuli kama sehemu ya kuabudia wakati wa majira ya kupaa kwa Yesu Kristo. Watu wa Bumbuli hawasali kanisani kwa siku hiyo bali hupanda juu mlimani hadi hiyo sehemu inayoitwa Kwentui kwa ajili ya kuabudu wakikumbuka Kupaa kwa Yesu Kristo miaka 2000 iliyopita.

Kata za Wilaya ya Bumbuli - Mkoa wa Tanga - Tanzania

Baga | Bumbuli | Dule "B" | Funta | Kisiwani | Kwemkomole | Mahezangulu | Mamba | Mayo | Mbuzii | Mgwashi | Milingano | Mponde | Nkongoi | Soni | Tamota | Usambara | Vuga


Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Tanga bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Bumbuli kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
Tafadhali usiingize majina ya maafisa au viongozi wa sasa maana wanabadilika mno.