Nenda kwa yaliyomo

Kamusi za Kiswahili

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Kamusi ya Kiswahili)

Kamusi za Kiswahili ni zile zinazofafanua maana ya maneno ya lugha hiyo ya Afrika Mashariki ambayo inazidi kuenea hasa barani Afrika.

Kamusi hizo ni vyombo muhimu kwa kukuza na kuimarisha Kiswahili, ambacho kwa sasa ni lugha rasmi ya Jumuia ya Afrika Mashariki na mojawapo kati ya lugha za mawasiliano za Umoja wa Afrika.

Historia ya awali

Kamusi za lugha hiyo zilianza kupatikana katika karne ya 19 BK, kabla na wakati wa ukoloni wa Kizungu katika nchi za Afrika Mashariki. Hivyo watungaji wa kamusi za kwanza walikuwa Wazungu waliofahamu vizuri lugha za Kiingereza, Kifaransa, Kijerumani, n.k.

Waswahili wenyewe, watu wa pwani ya Afrika Mashariki na visiwa vya jirani (kama Unguja na Pemba), hawajulikani kuwa wametunga kamusi kabla ya wakati huo. Wasomi wao walijua kwa viwango tofauti Kiarabu, ambacho kilikuwa lugha kuu ya elimu kwenye mwambao wa Bahari Hindi mashariki mwa Afrika na pia lugha ya kidini katika Uislamu.

Vilevile hatuna habari kwamba Wareno waliofika Afrika ya Mashariki tangu mwaka 1500 hivi walitunga kamusi.

Utungaji wa Kamusi za Kiswahili ulianza kwa kukusanya orodha za maneno/msamiati wa Kiingereza-Kiswahili na Kifaransa-Kiswahili. Msamiati wa Kiswahili ulikusanywa ili kuwasaidia wageni hawa kuifahamu lugha ya Kiswahili na waweze kuwasiliana na wenyeji wao ambao ni Waswahili. Nakala za msamiati huo zilipelekwa Uingereza ili wageni wengine waliotaka kufika Afrika Mashariki wajifunze kabla hawajafika katika nchi hizo.

Mfano wa kwanza ni mkusanyo wa maneno uliyofanywa na nahodha Mwingereza T. Smee alipotembelea pwani kuanzia Somalia hadi Zanzibar kwenye mwaka 1811-1812; alikusanya istilahi 250 hivi za Kiingereza na maana yake kwa Kiswahili (alichoita "Souallie"), Kisomali na lugha ya Wagalla. Orodha hiyo ilichapishwa kwenye mwaka 1844[1]. Wengine wanaotajwa ni Henry Salt (1811-1813) na Browse Ross (1843). Msamiati uliokusanywa na watu hao unafikiriwa kuwa ni wa Kiswahili cha kaskazini mwa Mombasa na ulikuwa na maneno machache sana. Wakati huo mchungaji Krapf alikuwa ameshaanza kazi ya kutunga kamusi yake.

Ludwig Krapf

Kamusi ya kwanza inayojulikana ilitungwa mnamo 1848 na Ludwig Krapf huko Rabai Mpya / Mombasa (Kenya); ilikamilishwa na kutolewa kama "A Dictionary of the Suahili language, London 1882".[2] Kamusi inapatikana pia mtandaoni[3].

Tahajia ya maneno mara nyingi ni tofauti na kawaida ya leo kwa sababu usanifishaji wa lugha ulitokea tu miaka 40-50 baada ya kutolewa kwa kamusi yake; pia alikusanya maneno mengi huko Rabai / Mombasa kwa hiyo athira ya Kimvita ni kubwa. Pia kuna changamoto kutumia kamusi yake kwa sababu ilhali alitoa maana ya maneno ya Kiswahili kwa Kiingereza aliongeza maelezo juu ya matumizi na etimolojia kwa lugha ya Kilatini.

Alipoanza kazi aliamua kutotumia mwandiko wa Kiarabu uliokuwa njia ya kawaida ya kuandika Kiswahili akiona haulingani sana na lugha yenyewe, maana Kiarabu kina herufi kadhaa kwa sauti ambazo hazipatikani katika Kiswahili. Alitafakari angetumia herufi za Kiamhari (alichojua vizuri) lakini aliamua kuendelea kwa alfabeti ya Kilatini kwa sababu hakutaka kuwapa wanafunzi wa lugha tatizo la kupambana na alfabeti ya ziada.

Kamusi nyingine za kwanza

Wengine walioendelea kukusanya maneno na kutoa kamusi ni Askofu Edward Steere na mwanaisimu A.C. Madan. Wote wawili walifanya kazi Zanzibar wakiwa wamisionari wa Kanisa Anglikana.

Kamusi ya Kiswahili - Kijerumani ya kwanza ilitungwa mwaka 1890, wakati wa Afrika ya Mashariki ya Kijerumani, na Carl Gotthilf Büttner (Wörterbuch der Suaheli-Sprache, Berlin 1891) aliyetoa pia matini za Kiswahili kwa mwandiko wa Kiarabu. Kamusi pana zaidi ilitolewa mwaka 1911 na Carl Velten (Suaheli Wörterbuch, Berlin 1910).

Kamusi ya Kiswahili - Kifaransa ilitolewa na Charles Sacleux (Sacleux, Charles. 1939. Dictionnaire Swahili - Français. Travaux et Mémoires de l'Institut d'Ethnologie, Vols. 36/37. Paris: Institut d'Ethnologie, Université de Paris. Reprint 1959). Sacleux alikuwa padri katika misheni ya Kanisa Katoliki huko Bagamoyo. Kamusi hii imesifiwa kuwa ya pekee kwa jinsi iliyokusanya pia maneno ya lahaja za Kiswahili nje ya Kiunguja (Zanzibar) na Kimvita (Mombasa) na kwa upana wa maelezo yake kuhusu historia ya maneno.

Kiswahili sanifu

Hadi mwanzo wa karne ya 20 Kiswahili kilipatikana katika lahaja zake tu. Baada ya Vita Kuu ya Kwanza Uingereza ilitawala maeneo makuu ambako Kiswahili kilitumiwa. Hapo serikali ya kikoloni iliánzisha kamati kwa kusudi la kuunda Kiswahili sanifu kitakachotumiwa kote Afrika ya Mashariki. Kamusi mbili za "Inter-territorial Language (Swahili) committee to the East African Dependencies" zilitolewa mwaka 1939 na zimechapishwa upya mara nyingi. Mhariri mkuu wa kamati alikuwa katibu wake Frederick Johnson. Msingi wa kamusi hizi ulikuwa kazi ya Madan (taz. juu). Hivyo kamusi hizi hutajwa kama "Madan-Johnson".

Kiswahili tangu uhuru

Tangu kupatikana kwa uhuru wa nchi za Afrika ya Mashariki Kiswahili kiliendelea sana. Azimio la serikali ya Tanzania la kufanya Kiswahili kuwa lugha ya elimu katika shule za msingi lilianzisha masharti ya kutunga vitabu vya shule na kupanua msamiati wa Kiswahili. Orodha za maneno zilitungwa kwa ajili ya masomo mbalimbali.

Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (leo: TATAKI) katika Dar es Salaam ilianza kuandaa kamusi mbalimbali, hasa "Kamusi ya Kiswahili Sanifu" inayoeleza maana ya maneno kwa kutumia lugha yenyewe. Kamusi mbalimbali zilifuata.

Kamusi za maana zinazopatikana madukani

Vifupisho katika mabano si vya kawaida lakini vimeingizwa hapa kwa kusudi la kurahisisha marejeo katika makala za Wikipedia.

Kiswahili - Kiswahili

  • Kamusi ya Kiswahili Sanifu (KKS). Dar es Salaam, Tanzania: Oxford University Press. 1981, 2004, 2013. (imetungwa na TATAKI, awali TUKI)
  • Kamusi Kuu ya Kiswahili (KKK). Nairobi, Kenya; Kampala, Uganda; Dar es Salaam, Tanzania: Longhorn, 2015, ISBN 978 9987 02 098 4. (imetungwa na BAKITA)
  • Kamusi la Kiswahili Fasaha (KKF), (imetungwa na BAKIZA), Oxford 2010 - ISBN 978 019 5736182.
  • Kamusi ya Karne ya 21 (KK21). Nairobi, Kenya: Longhorn. 2011 - ISBN 978 9966 36 120 0.
  • Kamusi Teule ya Kiswahili (KTK). Nairobi, Kenya: East Africa Educational Publishers, 2014.
  • Bakhressa, Salim K., Kamusi ya Manaa na Matumizi (KMM). Nairobi, Kenya: Oxford University Press, 1992
  • Kiputiputi, Omari M. Kamusi Sanifu ya Kompyuta (KSK), Taasisi ya Taaluma za Kiswahili, toleo la kwanza 2011, ISBN 978 9987 531 12 7
  • Kamusi Sanifu ya Biolojia, Fizikia na Kemia / English-Swahili Dictionary of Biology, Physics and Chemistry - TUKI/UNESCO/SIDA, Dar es Salaam, 1990
  • Kamusi ya Tiba (KyT), TUKI, dar es Salaam 2003, ISBN 9976-911-65-3
  • Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha - TUKI/UNESCO/SIDA, Dar es Salaam, 1990, ISBN 9976 911 10 6
  • Massamba, D.P.B., Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha, TUKI, Dar es Salaam, 2004, ISBN 9976 911 73 4
  • Wamitila, K.W., Kamusi ya Tashbihi, Vitendawili, Milio na Milingano, Longhorn 2003, ISBN 9966 49 768 4
  • Wamitila, K.W., Kamusi ya Fasihi. Istilahi na Nadharia, Focus Books, Nairobi 2003, ISBN 9966 882 79 6
  • Mwansoko H.T.Z. - Tumbo-Masabo Z.N. - Sewangi S.S., Kamusi ya Historia - TUKI, Dar es Salaam, 2004 - ISBN 9976 911 75 0
  • Mkota, A., Kamusi ya Methali, Vide-Ruwa, Nairobi 2009
  • Arege, T. - Nyanje, M., Kamusi Fafanuzi ya Methali, Target Publications Ltd, Nairobi 2011, ISBN 9966 002 41 3
  • Tumbo-Masabo, Z.N. - Chuwa A.R., Kamusi ya Biashara na Uchumi, TUKI, Dar es Salaam, 1995, ISBN 9976 911 37 8
  • Mwita, A.M.A. - Mwansoko, H.J.M., Kamusi ya Tiba (TUKI) 2003
  • Mlingwa, C.O.F. - Kiango, J.G., Kamusi ya Ndege kwa Picha, TUKI 2006ù
  • Mdee T.S. - Kiango J.K., Kamusi ya Wanyama - TUKI 2008, ISBN 978 9987 442 263
  • Mkota, A. - Sakara, F., Kamusi ya Semi, Vide-Ruwa, Nairobi 2011
  • King'ei, K. - Ndalu, A., Kamusi ya Semi, EAEP Ltd, Nairobi, Kampala, Dar es Salaam, 1988-2007, ISBN 9966 46 898 6
  • Mohamed, H.A. - Mohamed, S.A., Kamusi ya Visawe, Swahili Dictionary of Synonims, EAEP, Nairobi, Kampala, Dar es Salaam, 1998
  • Nyenyembe, J. - Kamusi ya Ukristo, Mkuki na Nyoka, Dar es Salaam, 2016, ISBN 978-9987-753-17-8

Kiswahili - Kiingereza

  • Kamusi ya Kiswahili - Kiingereza (Swahili-English Dictionary KKK/SED) (imetungwa na Taasisi ya Taaluma za Kiswahili, toleo la pili Dar es Salaam 2014, ISBN 9976-911-44-0; online hapa [5])
  • Kamusi Awali ya Sayansi na Tekinolojia (KAST). Dar es Salaam, Tanzania: Ben & Co. Ltd., 1995.(imetungwa na TUKI)
  • Madan-Johnson, A Standard Swahili-English Dictionary (M-J SSE) (hutolewa na Oxford University Press, Nairobi & Dar es Salaam, 1939 na kuchapishwa upya mara nyingi)

Kiingereza - Kiswahili

  • English-Swahili Dictionary (Kamusi ya Kiingereza-Kiswahili KKK/ESD) (imetungwa na TUKI, third edition Dar es Salaam 2006, ISBN 9976-911-29-7; online hapa [6])
  • Madan-Johnson, A. Standard English-Swahili Dictionary (M-J SES) (Oxford University Press, Nairobi & Dar es Salaam, 1939 na kuchapishwa upya mara nyingi) online hapa
  • Snoxall R.A. - Mshindo H.B., Concise English-Swahili Dictionary / Kamusi ya Kiingereza-Kiswahili (Oxford University Press, Nairobi & Dar es Salaam, 1998 na kuchapishwa upya mara nyingi)
  • Kirkeby, Willy A. English Swahili Dictionary (Kamusi ya Kiingereza-Kiswahili) (Kirkeby Publishing Company, Dar es Salaam and Skedsmokorset, Norwei, 2002, ISBN 82-994573-2-7)
  • Mlacha, S.A.K., Kamusi ya Sheria Kiingereza-Kiswahili, TUKI 1999
  • Familia za Maamkio, English-Kiswahili Catholic Dictionary (a first English-Swahili dictionary of terms in use in the Catholic Church - with glosses in Latin and Italian) - Ndanda Mission Press, 2001, ISBN 9977 663 625 3
  • Kamusi sanifu ya Biolojia, Fizikia na Kemia (English-Swahili dictionary of Biology, Physics and Chemistry), David P.B. Massamba & alii, kutolewa na TUKI/UNESCO/SIDA,TUKI 1990, chapa ya tatu 2012, ISBN 9976 911 09 2
  • HJ.M. Mwansoko, ZNZ. Tumbo-Masabo, S.S. Sewangi Kamusi ya Historia, imetolewa na TUKI 2004, chapa la pili 2011, kurasa 37

Kiitalia - Kiswahili - Kiitalia

  • Pick, M. Vocabolario Kiswahili-Italiano Italiano-Kiswahili (Kamusi ya Kiswahili - Kiitalia - Kiswahili) (EMI, Bologna, 1978)

Kiswahili - Kijerumani

Kiswahili - Kifaransa - Kiingereza

M.A.J.E. CHIPA, Francais-Kiswahili-English / Misamiati ya msingi kwa wanaojifunza lugha Kifaransa-Kiswahili-Kiingereza - MAJEC-AJEJER, Dar es Salaam 2006, ISBN 9987 451 16 0

Kamusi zinazopatikana kwa njia ya intaneti

Marejeo

  1. Transactions of the Bombay Geographical Society, vol. VI, (from September 1841 to May 1844), uk. 51-56; online hapa kwa archive.org; tahajia yake ni ngumu, mfano "God - Moo,ungar", "Rain - Foo,ar"
  2. Linganisha utathmini wa kamusi ya Krapf katika Swahili Forum 16 Archived 9 Machi 2016 at the Wayback Machine. uliotolewa na G. Miehe na H. Fiersching
  3. A Dictionary of the Suahili Language by Rev. Dr. L. Krapf, London 1882, tovuti ya archive.org
  4. kwenye tovuti ya archive.org, ilitazamwa 21 Novemba 2015
  5. http://elimuyetu.co.tz/subjects/arts/eng-swa/index.html
  6. http://elimuyetu.co.tz/subjects/arts/eng-swa/index.html

Viungo vya nje