Mwaka wa Kanisa
Mwaka wa liturujia |
---|
Magharibi |
Mashariki |
Mwaka wa Kanisa (pia: mwaka wa liturgia / liturujia) ni mpangilio wa maadhimisho au kalenda inayoratibu majira na sikukuu za Ukristo katika muda wa mwaka mmoja.
Kalenda hii inataja nafasi ya vipindi vya pekee kama vile Majilio (Adventi), Krismasi au Noeli, Kwaresima au Pasaka, pamoja na nafasi ya sikukuu mbalimbali.
Sikukuu kadhaa kama Krismasi zinafuata tarehe za kudumu za kalenda ya jua, lakini nyingine kama Pasaka tarehe zake zinazosogezwa katika kalenda ya kawaida, hasa kwa sababu zinafuata hesabu ya Jumapili, si tarehe katika mwezi fulani.
Mwendo wa vipindi vya liturujia unafanana na ule wa maisha ya binadamu, ambayo yana maadhimisho ya pekee na majira ya kukua na kukomaa kwa utulivu. Vivyo hivyo mwaka wa Kanisa una sikukuu na siku za kawaida, vipindi vya pekee na la.
Sehemu muhimu zaidi ya mwaka huo inategemea Pasaka na Krismasi, sherehe kuu mbili zinazoendesha muda mtakatifu wote, ingawa zimo sikukuu nyingine pia.
Mwaka wa Kanisa na madhehebu
[hariri | hariri chanzo]Si madhehebu yote ya Ukristo yanaangalia hesabu ya mwaka wa Kanisa kwa jumla, lakini karibu zote zinaadhimisha siku kubwa kama Krismasi, Ijumaa Kuu na Pasaka kufuatana na utaratibu uliopangwa na kueleweka.
Kimsingi kuna mahesabu mawili:
- mapokeo ya Ukristo wa magharibi kwa Kanisa Katoliki la Kilatini[1] na Waprotestanti wengi, kama vile Anglikana, Walutheri, Wapresbiteri, Wamoravian;
- mapokeo ya Ukristo wa mashariki kwa makanisa ya Waorthodoksi, Wakatoliki wa Mashariki na ya Waorthodoksi wa mashariki; makanisa ya kale ya mashariki pengine huwa na sikukuu na vipindi maalumu (kwa mfano Wakopti na Kanisa la Uhabeshi wanaozingatia hasa sherehe za Bikira Maria).
Tofauti mojawapo kati ya mapokeo ya magharibi na mashariki kimsingi ni matengenezo ya kalenda ya Juliasi kuwa kalenda ya Gregori kuanzia karne ya 16; Kanisa Katoliki na Waprotestanti wamepokea kalenda ya Papa Gregori lakini Waorthodoksi wanaendelea kutumia kalenda ya Juliasi iliyotangulia kuwepo.
Muundo wa mwaka wa Kanisa
[hariri | hariri chanzo]Muundo wa kalenda hii ya mwaka wa Kanisa unasimama juu ya sikukuu kubwa mbili za Krismasi na Pasaka na vipindi vya siku vinavyofuatana nazo.
Hesabu hii inaanza na Jumapili ya kwanza ya Majilio (Adventi) katika mapokeo ya magharibi ambayo ni hesabu ya kawaida kwa Wakristo wengi wa Afrika ya Mashariki. Mwisho wa mwaka wa Kanisa ni Jumamosi kabla ya Majilio. Jumapili inayotangulia katika madhehebu mbalimbali inasheherekewa kama sikukuu ya kutazama milele au kurudi kwake Yesu Kristo kama mfalme na hakimu.
Krismasi na kipindi chake vinategemea tarehe yake ya 25 Desemba (magharibi) au 6 Januari (mashariki). Jumapili ya nne (au ya sita) kabla ya Krismasi ni mwanzo cha kipindi cha kujitayarisha kwa sikukuu hiyo. Mwisho wa kipindi cha Krismasi ni moja ya Jumapili (au Jumatatu) baada ya Epifania.
Kipindi cha Pasaka kinabadilika tarehe kila mwaka kwa sababu Pasaka yenyewe inategemea hesabu ya Jumapili pamoja na kutazama jua na mwezi, yaani aina mbili tofauti za kalenda: ni Jumapili ya kwanza baada ya mwezi mpevu wa kwanza unaotokea baada ya sikusare ya 21 Machi. Ijumaa Kuu ambayo inaadhimisha ukumbusho wa kifo cha Yesu ni Ijumaa kabla ya Pasaka.
Siku arubaini kabla ya Pasaka ni kipindi cha Kwaresima kwa ajili ya maandalizi ya kumbukumbu hiyo ya kusulibiwa na kufufuka kwake. Lakini hesabu ya siku 40 kwa kawaida inaacha Jumapili za kipindi hiki. Ndiyo sababu Kwaresima inaanza kwenye Jumatano kabla ya Jumapili ya sita kabla ya Pasaka, isipokuwa huko Milano na parokia zinazofuata mapokeo yake nchini Italia na Uswisi.
Kipindi cha Pasaka kinakwisha kwenye Jumapili ya Pentekoste[2]; Pentekoste (maana ya neno ni "hamsini", kwa kuwa inatokea takriban siku 50 baada ya Jumapili ya Pasaka).
Vipindi vingine kati ya vipindi vya Krismasi na Pasaka ni majira bila tabia maalumu, lakini kuna sikukuu za kimadhehebu zinazoweza kutofautiana kati ya kanisa na kanisa.
Maana ya mwaka wa Kanisa
[hariri | hariri chanzo]Ufuatano wa sikukuu unatunza kumbukumbu ya matukio muhimu katika maisha ya Yesu jinsi yanavyosimuliwa katika Biblia ya Kikristo, na pengine hata ya matukio ya historia ya Kanisa, hasa kwa Waorthodoksi.
Wakati dunia inapozunguka kandokando ya jua hadi kurudi ilipokuwa, jumuia ya wafuasi wa Yesu Kristo inazunguka kandokando yake ili kuzidi kumfahamu kwa imani, kumuadhimisha kwa tumaini na kumfuata kwa upendo.
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ kama yanavyofuatwa Kenya na Tanzania; taz. Misale ya Waamini, toleo la mwaka 2021, uk. 6-9
- ↑ Makanisa mengine yanaendelea hesabu yake hadi Jumapili ya Utatu ambayo ni Jumapili baada ya Pentekoste
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- The Roman Catholic Church's liturgical calendar, from US Catholic Bishops Ilihifadhiwa 7 Februari 2016 kwenye Wayback Machine., or from O.S.V. publishing Ilihifadhiwa 13 Novemba 2013 kwenye Wayback Machine..
- Universalis — A liturgical calendar of the Catholic Church including the Liturgy of the Hours and the Mass readings.
- Greek Orthodox Calendar - Greek Orthodox Calendar & Online Chapel
- Russian Orthodox Calendar at Holy Trinity Russian Orthodox Church
- Lectionary Central - For the study and use of the traditional Western Eucharistic lectionary (Anglican).
- Liturgical Calendar — Basic liturgical calendar for the entire year with liturgical colours.
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Mwaka wa Kanisa kama historia yake, matokeo au athari zake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |