Nenda kwa yaliyomo

Upadri

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Padri wa Kanisa la Kiorthodoksi la Ethiopia.
Katika upadirisho, baada ya askofu, mapadri wote waliopo wanawawekea mikono mashemasi. Hapo tu inafuata sala ya kuwaweka wakfu.

Upadri ni daraja takatifu ya kati katika uongozi wa Kanisa Katoliki na madhehebu mengine kadhaa ya Ukristo.

Unatolewa na Askofu kwa kumwekea mtu mikono kichwani na kumuombea ili atoe vizuri huduma za kikuhani, hasa kwa kuhubiri rasmi Neno la Mungu, kuadhimisha Ekaristi na sakramenti nyingine na kuongoza jumuia za waamini.

Upadri unatolewa kwa namna ya kudumu, usiweze kurudiwa wala kufutwa.

Katika Agano Jipya

[hariri | hariri chanzo]

Shirika la kwanza la Kanisa la Yerusalemu lilikuwa na wasomi wengi sawa na lile la sinagogi la Uyahudi, lakini lilikuwa na Halmashauri ya wazee waliowekwa (πρεσβύτεροι, wazee)

Katika Matendo ya Mitume 11:30 na 15: 22 tunaona mfumo wa washirika wa uongozi huko Yerusalemu ingawa unaongozwa na Yakobo Mdogo, askofu wa kwanza wa mji huo. Katika Matendo 14: 23, Mtume Paulo anaweka wakubwa katika makanisa aliyoanzisha.

Maadili ya kipadri

[hariri | hariri chanzo]

Ikiwa bradha na sista wana wajibu wa pekee wa kulenga ukamilifu, zaidi tena anao padri, hata kama si mtawa. Utawa ni hali ya kulenga ukamilifu; maaskofu wako katika hali ya kutekeleza ukamilifu; ndiyo sababu inafaa wawe katika hatua ya muungano ya waliokamilika. Padri mwanajimbo anajiongezea stahili mpya akiingia utawani; kwa vyovyote anapaswa tayari alenge ukamilifu kutokana na sakramenti ya daraja na kazi zake takatifu. Wajibu huo maalumu ni mamoja na ule wa kutimiza kitakatifu majukumu mbalimbali ya kipadri. Kutokana na amri kuu anapaswa kuyatimiza vizuri zaidi na zaidi, kadiri upendo unavyostawi hadi kufa kwake. Upadirisho unadai, si tu hali ya neema inayotia utakatifu na sifa maalumu, bali mwanzo wa ukamilifu, maisha bora kuliko yanayotakiwa kwa kuingia utawani. Kwa kuwa padri anapaswa kuwaangaza wengine, inafaa awe katika hatua ya mwanga. Upadirisho unatia alama isiyofutika inayomshirikisha moja kwa moja ukuhani wa Kristo, na neema ya sakramenti inayomwezesha kutimiza kazi za kipadri inavyomfaa mtumishi wake. Hiyo neema ya sakramenti inatimiliza neema inayotia utakatifu na kumpa padri haki ya kupokea misaada inayohitajika atimize huduma yake kitakatifu zaidi na zaidi. Ni sehemu ya sura ya Kiroho ya padri, ambaye azidi kuelewa ukuu na masharti ya daraja yake. Kwa hakika upadirisho ni bora kuliko nadhiri za kitawa, na wajibu maalumu wa kulenga ukamilifu unaotokana nao ni mkubwa kuliko ule unaotokana na nadhiri.

“Umekuwa padri, umepakwa mafuta ili umtolee Mungu sadaka ya misa. Fanya sasa kwa bidii, kwa uaminifu, kila inapofaa. Uwe na mwenendo mzuri usio na hitilafu. Usidhani u huru kuliko watu wengine, bali umefungwa kifungo cha sheria, hata imekupasa kutafuta ukamilifu mkubwa zaidi. Ni lazima padri awe mtu aliyepambwa maadili yote, kusudi awape watu wengine mfano wa maisha mema. Mazoea yake siyo waliyozoea watu wa dunia, watu wa chini, bali yafuatana na malaika wa mbinguni; marafiki wake ndio watu watimilifu walioko duniani” (Kumfuasa Yesu Kristo IV,5:2). Kazi za padri, kuhusiana na Mwokozi aliyemo katika ekaristi na katika Mwili wake wa fumbo, zinatuonyesha kuliko upadirisho wenyewe wajibu wake wa pekee wa kulenga ukamilifu.

Padri anapoadhimisha misa anamwakilisha Kristo aliyejitoa kwa ajili ya watu wote. Anapaswa kuelewa ukuu wa kazi yake na kuzidi kuungana kwa dhati na kuhani mkuu ambaye ni kafara pia. Ni unafiki, au walau uzembe, kupanda altareni bila nia imara ya kupanda ngazi ya upendo. Mtumishi wa Kristo anapaswa aseme kila siku kitakatifu zaidi, “Huu ndio mwili wangu… Hiki ni kikombe cha damu yangu”. Kila siku zaidi komunyo yake iwe motomoto kwa utashi kuwa tayari kumtumikia Mungu, kwa sababu ekaristi inatakiwa kukuza upendo ndani mwetu, si kuutunza tu. “Kwa ukuu wa kazi ambayo padri altareni ni mtumishi wa Kristo, unadaiwa utakatifu wa dhati kuliko ule unaodaiwa na utawa” (Thoma wa Akwino). Hivyo, mambo yakilingana, tendo dhidi ya utakatifu ni dhambi kubwa zaidi likitendwa na padri kuliko likitendwa na bradha. “Padri mwenye kumtolea Mungu sadaka ya misa, humsifu Mungu, huwafurahisha malaika, huthibitisha Kanisa, husaidia walio hai, hutuliza marehemu, hupewa mwenyewe neema zote” (Kumfuasa Yesu Kristo IV,5:3).

Anapaswa pia kuadhimisha kwa makini na ibada halisi Sala ya Kanisa ambayo inatangulia na kufuata misa. Ni wimbo wa Bibi arusi wa Kristo kwa usiku na mchana, hivyo ni heshima kubwa kuhusika nao. Tusali hivyo tukizingatia nia kuu za Kanisa, kama vile kupatanisha ulimwengu kwa kueneza utawala wa Mungu.

Hatimaye padri ana wajibu wa pekee wa kulenga ukamilifu ili atimize vizuri kazi zake kwa ajili ya Mwili wa fumbo wa Kristo. “Hakuna kinachofaa zaidi kuongoza waamini kwenye ibada halisi kuliko mfano mwema wa padri. Macho ya watu yanamuelekea yeye, kama kioo cha ukamilifu wanaotakiwa kuiga. Kwa hiyo, basi, anatakiwa kupanga maisha yake, sura yake ya nje, mwenendo wake, matendo na maneno yake hivi kwamba adumishe daima uzito, utaratibu na tabia ya kidini anavyopaswa kuwa navyo” (Mtaguso wa Trento). Padri mwanajimbo halazimiki kuahidi ufukara, lakini anatakiwa kutoshikamana na vitu na kuwa radhi awape maskini; anatakiwa pia kumtii askofu wake na kuwa kama mtumishi wa waamini, bila kujali matatizo na pengine masingizio anayoweza akakabiliana nayo.

Haja ya ukamilifu huo ni wazi kuhusu mahubiri, maungamo na uongozi wa Kiroho. Ili mahubiri yawe hai na kuzaa matunda, ni lazima padri aseme “yaujazayo moyo wake” (Math 12:34) “kutokana na utimilifu wa sala ya kumiminiwa” (Thoma wa Akwino), yaani yatokane na imani hai yenye kupenya na kuonja fumbo la Kristo, thamani isiyo na kifani ya misa, ya neema inayotia utakatifu na ya uzima wa milele. Padri anapaswa kuhubiri kama mwokozi wa roho, akifanya kazi mfululizo kwa wokovu wa wengi. Asiwe amepokea upadri bure. Ni vilevile kuhusu huduma ya kitubio na uongozi wa Kiroho. Padri asipokuwa mwangavu na motomoto, huduma hiyo inaweza ikampotosha mwenyewe, badala ya kuokoa watu. Maisha yasipopanda, yanateremka; ili yasiteremke ni lazima yapande juu kama mwali wa moto. Hasa hapa ni kweli kwamba asiyesonga mbele, anarudi nyuma. Hatimaye, wanaweza wakamuelekea padri watu ambao Mungu anawadai zaidi; ni lazima awape msaada wa hakika kwa kufuata njia nyofu ya utakatifu; haifai waende mbali naye pasipo kupata chochote.

Antoni Chevrier aliwafundisha mapadri aliowalea wawe daima na pango, Kalivari na tabenakulo machoni mwao. Pango liwakumbushe ufukara; padri anapaswa kuwa fukara katika nyumba, mavazi na chakula. Anapaswa kuwa mnyenyekevu kwa Mungu na kwa watu. Kadiri alivyo hivyo anamtukuza Mungu na kumfaa jirani. Padri ni mtu asiye na kitu. Kalivari imkumbushe haja ya kujitoa sadaka, kujifisha kuhusu mwili wake, roho yake, matakwa yake, heshima yake, familia yake na ulimwengu. Anapaswa kujitoa sadaka kwa kimya, kazi, malipizi, mateso na kifo. Kadiri padri alivyokwishakufa hivyo ana uzima ndani mwake na kuwashirikisha wengine. “Padri ni msulubiwa. Kwa mfano wa Mwalimu anapaswa kujitoa kwa upendo mwili, roho, muda, mali, afya, uhai; anapaswa kueneza uhai kwa imani yake, mafundisho yake, maneno yake, sala zake, juhudi zake, mifano yake. Anapaswa kuwa mkate mtamu. Padri ni mtu wa kuliwa”. Tabenakulo imkumbushe upendo anaopaswa kuwa nao. Ndicho kipeo cha upadri ambacho kila mmoja awe nacho: “Nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo” (Yoh 13:15).

Padri anatakiwa kuwa “Kristo mwingine” kwa namna ya pekee. Yesu ni kuhani na kafara, naye padri hawezi kushiriki ukuhani wa Kristo asishiriki hali yake ya kuwa kafara kadiri alivyopangiwa na Mungu. Ndivyo walivyoelewa mapadri watakatifu, k.mf. Yohane Maria Vianney ambaye wakati wa kutolea mwili na damu takatifu ya Bwana alikuwa anatolea mateso yake yote kwa ajili ya waamini waliomuendea. Charles wa Foucauld, aliyeutia mhuri wa damu utume wake kati ya Waislamu, aliandika maneno yafuatayo katika daftari alilolichukua daima ndani ya mavazi yake, “Ishi kana kwamba leo ni siku yako ya kufia dini. Kadiri tunavyokosa vyote duniani, tunakikuta kitu bora zaidi ambacho dunia inaweza kutupatia, yaani msalaba”.

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]

Kanisa Katoliki

[hariri | hariri chanzo]

Makanisa ya Kiorthodoksi

[hariri | hariri chanzo]
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Upadri kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.