Dwight D. Eisenhower

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Eisenhower kama Rais wa Marekani

Dwight David Eisenhower (14 Oktoba, 189028 Machi, 1969) alikuwa mwanajeshi na mwanasiasa kutoka nchi ya Marekani. Watu wengi walikuwa humwita Ike (tamka Aik). Wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia alikuwa jenerali mkuu aliyeongoza uvamizi wa Normandy tarehe 5 Juni, 1944. Kuanzia mwaka wa 1953 hadi 1961 alikuwa Rais wa 34 wa Marekani. Kaimu Rais wake alikuwa Richard Nixon.

[hariri] Maisha

Dwight Eisenhower alizaliwa tarehe 14 Oktoba, mwaka wa 1890, kama mtoto wa tatu wa David na Ida Eisenhower katika mji wa Denison, Texas. Watoto wote saba walikuwa wavulana, majina yao: Arthur, Edgar, Dwight, Roy, Paul (aliyefariki utotoni na dondakoo), Earl, na Milton. Kabla Dwight hajafikisha umri wa mwaka mmoja, wazazi wake walihamia mji wa Abilene, Kansas, ambapo alilelewa na kuhitimu shule. Baada ya kufanya kazi mbalimbali za mikono, alifaulu mtihani wa kuingia chuo cha kijeshi cha Westpoint ambapo alihitimu mwaka wa 1915.

Tarehe 1 Julai, 1916, alifunga ndoa na Mamie Geneva Doud. Mtoto wao wa kwanza alizaliwa tarehe 23 Septemba, 1917, jina lake Doud Dwight Eisenhower lakini aliitwa Icky na wote. Alifariki na homa ya vipele vyekundu tarehe 2 Januari, 1921, akiwa na miaka mitatu tu. Mtoto wa pili, John Sheldon Eisenhower, alizaliwa mwaka wa 1922.

Eisenhower alihamishwa kikazi mahali mbalimbali siyo Marekani tu lakini pia nje, k.m. Panama na Ufaransa. Mara nyingi alifanya kazi ya ofisi ingawa alipendelea kazi ya kijeshi yenyewe. Nafasi yake alifika wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Kuanzia mwaka wa 1942, Eisenhower alikuwa kamanda, kwanza upande wa Afrika Kaskazini, akiwa na makao makuu mjini Algiers, halafu aliongoza uvamizi wa Italia, na mwishoni alitayarisha uvamizi wa Normandy tarehe 5 Juni, 1944.

Baada ya vita alikuwa kamanda mkuu wa NATO. Watu wengi wa Chama cha Republican walimpendelea agombee urais mwaka wa 1952, yeye lakini hakutaka kuingia mambo ya siasa. Hata hivyo aliandikishwa na kuwa mgombea wa Repulican. Baada ya kumshinda Adlai Stevenson III, Eisenhower alikuwa Rais wa Marekani kwa awamo mbili hadi 1961. Wakati wa urais wake, vita ya Korea ilikomeshwa. Pia, siasa ya Marekani iliathiriwa na mawazo dhidi ya Wakomunisti yaliyotekelezwa na Joseph McCarthy.

Baada ya kustaafu, Eisenhower alikaa pamoja na mke wake katika mji wa Gettysburg, Pennsylvania. Tarehe 28 Machi, 1969, alifariki hospitalini baada ya kupatwa na shtuko la moyo.

[hariri] Marejeo

Pinkley, Virgil. 1979. Eisenhower Declassified. Old Tappan: Fleming Revell.

[hariri] Tazamia pia

Vifaa binafsi
Maeneo ya wiki

Vibadala
Vitendo
Urambazaji
Vifaa
Lugha zingine