Mlipuko wa virusi vya corona 2019-20

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search
Mlipuko wa Virusi vya Korona duniani
Komesha Kuenea kwa Viini

Mlipuko wa Virusi vya Korona (kwa Kiingereza: Coronavirus) ulibainika rasmi tarehe za katikati za mwezi Desemba mwaka 2019 katika mji wa Wuhan huko China ya kati. Ulikuwa kikundi cha watu wenye nimonia bila chanzo kinachoeleweka. Ulibanika baadaye kama aina mpya ya virusi vya korona.[1][2][3][4]

Tarehe 20 Januari 2020 Waziri Mkuu wa Uchina Li Keqiang alitoa wito wa kutia juhudi katika kukomesha na kudhibiti janga la nimonia lililosababishwa na virusi vya korona.[5] Kufikia tarehe 23 Machi, 2020, kesi 337,000 zimethibitishwa,[6]

Kufikia tarehe 5 Februari 2020, vifo 493 vilitokana na virusi hivyo tangu kifo cha kwanza kilichothibitishwa Januari 9, na watu 990 waliopona. [7] Kifo cha kwanza nje ya Uchina kiliripotiwa tarehe 1 Februari nchini Ufilipino, kilikuwa ni kifo cha mwanamume wa Kichina mwenye umri wa miaka 44.

Kumekuwa na majaribio ambayo yameonyesha kesi zaidi ya 6000 zilizothibitishwa nchini Uchina, ambazo baadhi zao ni za wafanyakazi wa huduma ya afya.[8]

Katikati ya Februari 2020 maswali mengi kuhusu virusi hivi vilibaki bila jibu, lakini Shirika la Afya Duniani lilitoa tathmini kuwa[9]

 • zaidi ya asilimia 80 za wagonjwa huonekana kuwa na ugonjwa mwepesi, wanapona
 • kati ya asilimia za wagonjwa kuna maambukizi mazito yanayosababisha matatizo ya kupumua, hata nimonia, na asilimia 15 kudai walazwe hospitalini
 • takriban asilimia 5 huwa na magonjwa hatari
 • mnamo asilimia 2 hufa; hatari ya kifo inapatikana hasa kwa wazee, kuna mfano michache ya watoto. Baadaye imeonekana kwamba kiwango cha vifo si kubwa vile, labda kati ya % 0.5 hadi 1 lakini si rahisi kutaja kiwango kwa uhakika kwa sababu wengi walioambukizwa hawajulikani.
 • utafiti wa ziada bado unahitajika
 • kuna dalili kwamba virusi vya Covid-19 vinaweza kudumu hadi siku 8 kwenye uso wa kitu kilichoguswa na mgonjwa na bado kusababisha maambukizi

Kufikia tarehe 11 Julai 2020, zaidi ya watu milioni 12.5 walithibitishwa kupatwa na COVID‑19 katika nchi na maeneo 188 duniani kote. Kati yao waliokufa ni zaidi ya 560,000 na waliopona ni zaidi ya milioni 6.89.

Uenezi wa Covid-19 nje ya China[hariri | hariri chanzo]

Uenezi wa virusi vya SARS-Covid-19 duniani (ramani inasahihishwa kila siku)
Idadi ya watu waliothibitishwa kuwa na maambukizi
      zaidi ya 10,000       1,000–9,999       100–999       10–99       1–9 (Tarehe 16 Machi mtu wa kwanza alipatikana nchini Tanzania)
Mlipuko wa Virusi vya Corona duniani hadi 2 Machi 2020.

Hadi mwisho wa Januari 2020 takriban watu 10,000 waliambukizwa, idadi ya vifo ilikuwa mnamo 200. Virusi vilienea hadi nchi nyingine kwa njia ya abiria wa ndege za kimataifa. Wakazi wa Wuhan na miji mingine ya China yenye wagonjwa wamekataliwa kuondoka kwao baada ya hali ya karantini kutangazwa.[10].

Maambukizi ya kwanza ya ndani ya virusi hivi nje ya Uchina yalitokea Vietnam kati ya wanafamilia,[11] wakati maambukizi ya kwanza ya ndani ambayo hayakuhusisha familia yalitokea Ujerumani, tarehe 22 Januari, wakati mwanamume mmoja wa Kijerumani alipata ugonjwa huo kutoka kwa mgeni wa China kwenye kikao cha biashara.[12]

Kesi nyingine zilizothibitishwa mapema ziliripotiwa huko Thailand, Korea Kusini, Japani, Taiwani, Makau, Hong Kong, Marekani (Everett, Washington na Chicago),[8] Singapore, [13] Vietnam, Ufaransa[14], Italia na Nepali.

Katika Februari 2019 virusi viliendelea kuenea nje ya China, kupitia watu waliosafiri baina ya China na nchi nyingine. Tabia ya virusi kutosababisha ugonjwa mkali kwa wengi ilikuwa msingi kwa uenezaji usiotambuliwa mwanzoni hadi kufikia watu waliogonjeka vibaya. Milipuko ya kwanza ilionekana katika Iran[15], Korea Kusini[16] na Italia[17] ambako serikali zilitangaza hali ya karantini kwa maeneo kadhaa. Kufikia mwisho wa mwezi huo, wagonjwa wa nchi nyingine kwa pamoja walikuwa wamezidi wale wa China.

Katika Machi 2020 idadi ya maambukizi mapya ilipungua nchini China na Korea Kusini lakini iliongezeka Ulaya na kuanza kusambaa Marekani. Katika Ulaya Italia ilikuwa nchi iliyoathiriwa vibaya zaidi; serikali ilifunga shule zote pamoja na maduka yasiyo ya chakulas na dawa na kupiga marufuku mikusanyiko yote, ikiwemo ile ya ibada. Hatua kama hizo zilichukuliwa pia katika nchi nyingine. Katika Asia ya Magharibi nchi iliyoathiriwa vibaya zaidi ni Iran.

Kwa jumla si rahisi kupata picha kamili ya uenezi halisi wa virusi hivi. Ilhali dalili za ugonjwa zinafanana na mafua ya kawaida na kifua kikuu, inawezekana mara nyingi maambukizi hayakutambuliwa. Kwa sababu hiyo makadirio ya asilimia ya watu wanaokufa yanatofautiana kati ya nchi na nchi.

Tarehe 11 Machi 2020 Shirika la Afya Duniani ilitamka uenezi wa virusi umefikia ngazi ya pandemia, yaani epidemia (mlipuko) katika nchi nyingi za dunia[18].

Katikati ya mwezi Machi 2020 idadi ya wagonjwa iliongezeka sana katika nchi za Ulaya. Marekani ilizuia wasafiri kutoka Ulaya kuingia. Nchi mbalimbali, pamoja na Ujerumani, zilianza kufunga shule na kukataza mikutano yote yaliyolenga zaidi ya watu 100-500, kwa hiyo kufunga mechi za mpira wa miguu au michezo mingine, pamoja na hoteli na sinema. Kampuni mbalimbali ziliamuru wafanyakazi kukaa nyumbani na kutekeleza shughuli kupitia kompyuta pekee. Tarehe 14 Machi Denmark na Poland zilifunga mipaka kwa wote wasio raia wao, kwa kuamuru raia waliorudi wapaswe kukaa karantini wiki 2.

Kwa jumla serikali zilitangaza kwamba asilimia kubwa ya wananchi wataambukizwa zikiona changamoto kuchelewesha mchakato wa maambukizi ili wale wataokuwa wagonjwa sana wasijitokeze mara moja lakini polepole ili waweze kuhudumiwa hospitalini.

Kufikia tarehe 19 Machi nchi 170 zilikuwa na mgonjwa walau mmoja.

Tarehe 21 Machi Italia ilikuwa imezidi China kwa wingi wa vifo, kwa kuwa siku hiyo walifariki huko watu 793, kuliko siku yoyote ya China.

Kufikia tarehe 23 Machi jumla ya waliothibitishwa kupatwa na virusi ilifikia 339,645 na vifo 14,717 kati nchi zaidi ya 40.

Takwimu za tarehe 27 Machi zinaonyesha waliopatwa kwa hakika ni walau 536,000 na kati yao walau 24,100 wamekufa kwa ugonjwa huo. Idadi kubwa ya walioambukizwa nchi kwa nchi imekuwa ile ya Marekani.

Kufikia tarehe 13 Aprili walioambukizwa walifikia 1,850,000 na waliofariki dunia 114,000.

Kufikia tarehe 2 Juni walioambukizwa walifikia 6,325,303 na waliofariki dunia 377,469.

Hadi tarehe 11 Juni walioambukizwa walifikia kuwa zaidi ya 7,360,000 na waliofariki dunia 416,000.

Afrika[hariri | hariri chanzo]

Mwanzoni mwa Machi 2020 hakukuwa na taarifa ya maambukizi mengi ndani ya Afrika. Wataalamu walijadiliana kama hilo ni jambo linalotokana na kukosa vifaa vya kupima na kutambua ugonjwa, au kama kuna sababu ya ugonjwa kutoenea katika Afrika. Wagonjwa wengi waliotambuliwa kusini kwa Sahara ni wasafiri waliofika kutoka nchi za nje.

Hadi 12 Machi wagonjwa walithibitishwa hasa katika Afrika Kaskazini: Misri wagonjwa 67 (1 alifariki), Algeria 20 (0), Moroko 6 (1) na Tunisia 7 (0). Upande wa kusini wa Sahara taarifa zilipatikana hasa kutoka Afrika Kusini walipotambulia wagonjwa 17 (0), wengi wao watu waliorudi kutoka safari za Italia. Togo ilikuwa na mgonjwa 1 (0) aliyethibitishwa, Senegal 4 (0), Nigeria 2 (0), Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo 1 (0), Kamerun 2 (0), Burkina Faso 2 (0)[19]

Tarehe 15 Machi jioni mtu wa kwanza alithibitishwa Tanzania ameambukizwa; msafiri aliyeleta virusi vya ugonjwa huo ni mwananchi aliyefika Arusha kutoka Ubelgiji na ambaye baadaye alipona. Hadi tarehe 30 idadi rasmi ilifikia waambukizwa 19.[20] Wengi waliambukizwa nje ya nchi wakagundulika baada ya kufika Tanzania. Tarehe 31 Machi 2020 Mtanzania wa kwanza alifariki huko Dar es Salaam. Waliobaki na virusi ni watu 17 kwa mujibu wa Waziri wa Afya[21].

Kenya kulikuwa na maambukizi 31 na kifo cha kwanza.

Hadi tarehe 13 Aprili katika Afrika Bara nchi pekee isiyothibitisha maambukizi ilikuwa Lesotho, mbali ya Sahara Magharibi na visiwa mbalimbali, kama Komoro.

Kufikia tarehe 2 Juni walioambukizwa walifikia 152,442 na waliofariki dunia 4,344 katika nchi 54.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

 1. Hui, David S.; Azhar, Esam EI; Madani, Tariq A.; Ntoumi, Francine; Kock, Richard; Dar, Osman; Ippolito, Giuseppe; Mchugh, Timothy D. et al. (14 January 2020). "The continuing epidemic threat of novel coronaviruses to global health – the latest novel coronavirus outbreak in Wuhan, China" (in English). International Journal of Infectious Diseases 91: 264–266. doi:10.1016/j.ijid.2020.01.009 . ISSN 1201-9712 . https://www.ijidonline.com/article/S1201-9712(20)30011-4/pdf.
 2. Undiagnosed pneumonia - China (HU) (01): wildlife sales, market closed, RFI Archive Number: 20200102.6866757. International Society for Infectious Diseases. Iliwekwa mnamo 13 January 2020.
 3. Cohen, Jon; Normile, Dennis (17 January 2020). "New SARS-like virus in China triggers alarm" (in en). Science 367 (6475): 234–235. doi:10.1126/science.367.6475.234 . ISSN 0036-8075 . PMID 31949058 . https://science.sciencemag.org/content/367/6475/234. Retrieved 17 January 2020.
 4. Parry, Jane (20 January 2020). "China coronavirus: cases surge as official admits human to human transmission". British Medical Journal 368. doi:10.1136/bmj.m236 . ISSN 1756-1833 . https://www.bmj.com/content/368/bmj.m236.
 5. Chinese premier stresses curbing viral pneumonia epidemic. Xinhua News Agency (21 January 2020).
 6. Deutsche Welle (www.dw.com). Hali ilivyo kuhusu Corona duniani | DW | 23.03.2020 (sw-TZ). DW.COM. Iliwekwa mnamo 2020-03-23.
 7. Qin, Amy. "China Reports First Death From New Virus", The New York Times, 10 January 2020. 
 8. 8.0 8.1 Field, Field. "Nine dead as Chinese coronavirus spreads, despite efforts to contain it", The Washington Post, 22 January 2020. 
 9. Here's how long coronaviruses may linger on contaminated surfaces, according to science, tovuti ya CNN, tar 18-02-2020
 10. 5 million people left Wuhan before China quarantined the city to contain the coronavirus outbreak, taarifa ya gazeti Business Insider USA, kupitia www.pulselive.co.ke, tarehe 27-01-2020
 11. China coronavirus: 'family cluster' in Vietnam fuels concerns over human transmission (29 January 2020).
 12. Germany confirms human transmission of coronavirus. Deutsche Welle (28 January 2020).
 13. Singapore confirms first case of Wuhan virus; second case likely (23 January 2020). Iliwekwa mnamo 23 January 2020.
 14. France confirms two cases of deadly coronavirus (en) (2020-01-24).
 15. Turkey and Pakistan close borders with Iran ove Coronavirus deaths, gazeti la Guardian (UK) ya 23 Feb 2020
 16. Coronavirus: South Korea to test 200,000 sect members as pandemic fears hit markets, gazeti la Guardian (UK) ya 25 Feb 2020
 17. Coronavirus: Britons returning from northern Italy told to self-isolate,BBC ya 25 Feb 2020
 18. WHO characterizes COVID-19 as a pandemic, tovuti ya WHO, iliangaliwa 12 Machi 2020
 19. Confirmed Cases and Deaths by Country, Territory, or Conveyance, tovuti ya worldometers.com ya tar. 12.042020
 20. Coronavirus cases in Tanzania rises to Six
 21. https://www.mwananchi.co.tz/habari/kitaifa/Ndugu-wa-Mtanzania-aliyekufa-kwa-corona-azungumza/1597296-5509666-cpgxwl/index.html