Mauaji ya kimbari ya Rwanda
Mauaji ya Kimbari ya Rwanda yalikuwa mauaji ya halaiki nchini Rwanda mnamo mwaka wa 1994 ambapo wananchi wa kundi la Watutsi pamoja na Wahutu waliotazamwa kuwa wapinzani wa serikali au mauaji waliuliwa na wanamgambo, polisi na wanajeshi wa serikali iliyosimamiwa na viongozi Wahutu.
Katika kipindi cha takriban siku 100, kuanzia kuuliwa kwa marais Juvenal Habyarimana wa Rwanda na Cyprien Ntaryamira wa Burundi tarehe 6 Aprili hadi katikati mwa mwezi Julai, walau watu 800,000 hadi milioni 1 waliuawa, au karibu asilimia 20 ya idadi ya watu nchini Rwanda wakati huo.
Historia ya awali
[hariri | hariri chanzo]Tangu uhuru wa Rwanda historia baina ya makundi mawili makuu ya Wahutu waliokuwa wengi na Watutsi waliokuwa kundi dogo zaidi ilikuwa ngumu. Rwanda iliingia katika ukoloni ikiwa ufalme chini ya wafalme Watutsi waliotawala wafugaji Watutsi na wakulima Wahutu. Wakoloni Wajerumani na halafu Wabelgiji waliendelea kuwatumia Watutsi wakitawala kupitia hao. Wakaongeza maeneo ya ziada chini ya mfumo wa Watutsi na hivyo kuimarisha mamlaka yao. Katika miaka ya 1950 Wahutu wa Rwanda walianza kudai haki za kisiasa, wakiungwa mkono na Kanisa Katoliki. Kukataa kwa tabaka la makabaila Watutsi kulisababisha uasi wa kwanza upande wa Wahutu ulioleta mauaji ya Watutsi mia kadhaa, na Watutsi lakhi mbili walikimbilia Uganda au Burundi.
Kabla ya uhuru Wabelgiji waliandaa uchaguzi wakaacha Rwanda kupata uhuru ikiwa jamhuri, tofauti na nchi jirani ya Burundi. Hapo idadi kubwa ya Wahutu walichagua Wahutu na vyama vyao walipata wabunge wengi sana.
Katika miaka ya kwanza baada ya uhuru wakimbizi Watutsi kutoka Uganda au Burundi walijaribu mara kadhaa kurudisha hali ya awali kwa silaha. Majaribio hayo yalishindikana yakasababisha tena mauaji ya Watutsi walioishi Rwanda, na wakimbizi wapya. Hadi mwaka 1964 takriban Watutsi lakhi tatu walikaa kama wakimbizi kwenye nchi jirani.
Wakati wa wimbi jipya la mauaji mnamo mwaka 1972 waziri Juvenal Habyarimana alipindua serikali akaunda chama kipya cha MRND[1] kilicholenga kupunguza uadui dhidi ya Watutsi. Baadaye utawala wake ulizidi kuwa na tabia za kidikteta na upinzani ulitokea upande mmoja kwa Watutsi wakali, upande mwingine kwa makundi yenye mwelekeo wa kidemokrasia, na wengine wao walikuwa tayari kushirikiana pia na Watutsi.
Utangulizi wa 1994
[hariri | hariri chanzo]Katika miaka ya 1980 kundi la wakimbizi katika Uganda wenye asili ya Rwanda, wengi wao wa kizazi cha pili, walijiunga na wanamgambo ya NRA chini ya Yoweri Museveni katika vita dhidi ya serikali ya Milton Obote. Idadi ya Wanyarwanda katika jeshi la NRA iliongezeka na wengi walipata maarifa ya vita na kupanda cheo katika jeshi la Uganda.
Baada ya ushindi wa Museveni mwaka 1986 Watutsi Wanyarwanda wengine walikuwa na vyeo vya juu katika jeshi la Uganda; Paul Kagame alikuwa mkuu wa tawi la upelelezi wa kijeshi la Uganda, Fred Rwigyema alikuwa jenerali na naibu waziri wa ulinzi. Mwaka 1987 waliunda kundi la RPF (Rwanda Patriotic Front) mjini Kampala.
Mwaka 1990 kundi la RPF Uganda walioongozwa na Rwigyema walivuka mpaka wa Rwanda wakashambulia jeshi la FRD (Forces rwandaises de defense). Rwigyema aliuawa na FRD wakisaidiwa na Ufaransa, Ubelgiji na Zaire walilazimisha wanaRPF kurudi Uganda. Kagame aliyesomea Marekani aliitwa akapewa uongozi wa RPF akaanza vita ya msituni kaskazini mwa Rwanda.
Hadi mwaka 1992 RPF ilishika sehemu ya Rwanda kaskazini na serikali ya Habyarimana ilipaswa kukubali majadiliano ya amani. Tokeo lake lilikuwa mapatano ya Arusha ya mwaka 1993 ambako serikali ya Habyarimana na RPF walipatana kuanzisha serikali ya umoja, kurudi kwa wakimbizi na kuunda jeshi jipya lililopangwa kuunganisha sehemu ya askari wa FRD na sehemu ya RPF. Habariyama alikuta upinzani mkali kutoka kwa wanasiasa Wahutu katika Rwanda akasitasita kutekeleza mapatano ya Arusha. Serikali za majirani, hasa Kenya na Tanzania, pamoja na Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa walisisitiza tena na tena utekelezaji.
Kwenye Oktoba 1993 Baraza la Usalama la UM liliamua kutuma wanajeshi 2400 kwa jina la United Nations Assistance Mission for Rwanda. Wawakilishi wa kwanza kutoka RPF walifika pia Kigali kwa maandalizi ya serikali mpya. Waliongozana na kikosi kidogo cha wanajeshi wa RPF waliopewa jengo kama kambi katika Kigali.
Hatimaye Habarimana alisafiri Dar es Salaam kwenye Juni 1994 akahudhuria mkutano kuhusu utekelezaji wa mapatano ya Arusha. Aliporudi tarehe 6 Juni ndege yake ilipigwa na kombora ilipokaribia uwanja wa ndege wa Kigali.
Mauaji ya 1994
[hariri | hariri chanzo]Kuuawa Habyarimana tarehe 6 Aprili 1994 kulikuwa chanzo cha mauaji ya kimbari nchini humo. Baada ya kifo cha rais kikatiba waziri mkuu Agathe Uwilingiyimana angechukua nafasi ya rais lakini Uwilingiyimana aliuawa na wanajeshi tarehe 7 Aprili kwa sababu alitazamiwa kuwa na siasa ya wastani, si kali. Waziri Theodore Sindikubwabo aliteuliwa na kamati ya kijeshi kuwa rais mpya akaapishwa tarehe 9 Aprili[2].
Kuhusiana na kuuawa Habyarimana, Wahutu wenye misimamo ya kufurutu mpaka walihusisha tukio la kutunguliwa ndege yake na wapinzani wa Kitutsi na kulitumia kama kisingizio cha kuanzishia mashambulio na mauaji makubwa na ya kutisha dhidi ya Watutsi na Wahutu wenye misimamo ya wastani.
Mauaji ya kimbari nchini Rwanda yaliendelea kwa muda wa siku 100 hadi hali ya mambo ilipodhibitiwa na vikosi vya waasi wa wakati huo wa RPF, wapiganaji wake wengi wakiwa ni Watutsi.
Inasemekana kuwa watu wapatao laki nane waliuawa, wengi wao wakiwa Watutsi, lakini wakiwemo pia Wahutu wenye misimamo ya wastani.
Huko nyuma Rais Paul Kagame wa Rwanda alituhumiwa na Jean-Lousi Bruguiere, mmoja wa majaji maarufu wa Ufaransa kuwa alishiriki katika mauaji ya halaiki ya wananchi wa nchi hiyo na vilevile uuaji wa Habiyarimana. Hatua hiyo iliipelekea serikali ya Kigali nayo kuwatuhumu viongozi wa Ufaransa kuwa walishiriki katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.
Kwa utaratibu huo Kamisheni Huru ya Kitaifa ambayo iliamuriwa na serikali ya Kigali ikusanye nyaraka na ushahidi unaothibitisha nafasi ya Paris katika mauaji ya Rwanda, ilitayarisha nyaraka zilizofichua jinsi Ufaransa ilivyoshiriki katika mauaji hayo, ambayo yalipewa jina la "Jinai za Watenda Jinai".
Kwa mujibu wa ripoti ya kamisheni hiyo, nduru za juu za kisiasa, za kidiplomasia na za kijeshi za Ufaransa ziliratibu na kutekeleza mauaji hayo ya kimbari. Vilevile ripoti hiyo ilisema kwamba, Paris ilishiriki katika kutoa mafunzo kwa wanajeshi na waasi wa Kihutu, kutoa silaha na suhula za kijeshi, kusaidia kwa siri mauaji, ubakaji na mateso katika ardhi ya Rwanda. Tuhuma hizo zilivuruga kabisa uhusiano kati ya Ufaransa na Rwanda.
Hata hivyo mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka 2009 viongozi wa nchi hizo mbili waliamua kuhuisha tena uhusiano wao na serikali ya Paris kuwapa majaji jukumu la kufuatilia faili la mauaji ya kimbari ya Rwanda.
Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, hamu ya nchi hizo mbili ya kutaka kuanzisha tena uhusiano wao wa kisiasa haiwezi kufuta shaka ya nafasi ya Ufaransa katika mauaji ya kimbari ya Rwanda. Ufaransa ambayo siku zote imekuwa ikisisitiza kuungwa mkono ngano ya mauaji ya kimbari ya Wayahudi katika Vita vya pili vya Dunia, hivi sasa inapaswa kutoa jibu kuhusiana na tuhuma zilizotolewa dhidi yake na Kamisheni ya Uchunguzi ya Rwanda.
Tanbihi
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Mouvement Révolutionaire National pour le Développement, yaani Harakati ya Kimapinduzi ya Kitaifa kwa Maendeleo
- ↑ SINDIKUBWABO, THEODORE, uk. 153f, makala katika Aimable Twagilimana: Historical Dictionary of Rwanda, Scarecrow Press 2007, ISBN 0810864266
Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Mauaji ya kimbari ya Rwanda kama enzi zake au matokeo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |