Kipindupindu
Kipindupindu (kwa Kilatini na Kiingereza cholera kutoka neno la Kigiriki χολέρα, kholera, lililotokana na χολή, kholē, nyongo) ni ugonjwa hatari unaosababishwa na bakteria hasa katika utumbo mwembamba. Bakteria hizo ambazo huitwa vibriocholerae huweza kusababisha kuhara sana na kutapika sana pamoja na homa kali.
Maambukizi hutokea hasa kupitia maji au vyakula vilivyochafuliwa na wadudu kama vile nzi. Wadudu hao huweza kuchafua vyakula endapo vyakula hivyo vitaachwa wazi bila kufunikwa na chombo chochote na kuvutia nzi hao kutua juu ya vyakula hivyo na kuacha bakteria zitakazosababisha ugonjwa wa kipindupindu kwa mtu atakayekula chakula kile.
Kiwango cha kuhara na kutapika kinaleta upungufu wa maji na uwiano wa chumvi mwilini. Baada ya dalili hizo kutokea kuna hatari ya kifo kwa asilimia 20 - 70 ya wagonjwa kama hawana tiba.
Tunaweza kujilinda na kipindupindu endapo tukajilinda na vitu vifuatavyo ambavyo ni kunywa maji safi na salama na kula chakula kisichopoa. Bila kusahau kusafisha maeneo yote yanayomzunguka kiumbe hai, hasa binadamu. Yatupasa kufanya usafi katika mikoa yetu yote, hasa majijini ambako kunashutumiwa sana kuwa machafu.
Ambukizo
Kipindupindu husababishwa na bakteria aina ya Vibrio cholerae zinazosababisha kuhara majimaji yenye rangi kama maji ya kupikia mchele. Bakteria hiyo ilitambuliwa mwaka 1854 na Filippo Pacini.
Robert Koch alifaulu mwaka 1883 kufuga bakteria kutokana na utumbo wa watu waliokufa kwa kipindupindu huko Misri.
Kipindupindu hutokea hasa katika nchi pasipo maji safi, hasa ambako maji ya kunywa na majimaji ya choo yanaweza kuchanganyikana. Bakteria ya vibrio cholerae hupatikana hasa katika mavi na maji ya choo na pia katika maji ya bahari, maziwa na mito kama maji machafu huingizwa katika magimba ya maji bila kusafishwa kwanza.
Vilevile samaki na vyakula vingine kutoka maji yenye bakteria vinachafuliwa na vinaweza kusababisha ambukizo. Vilevile vyakula vinavyooshwa kwa maji yaliyochafuliwa na bakteria ya kipindupindu.
Katika mazingira yenye maji ya bomba, yaliyopitia karakana ya kusafisha maji machafu, kipindupindu hutokea mara chache tu. Kujulikana kwa njia za kuambukizwa kulikuwa sababu ya kuanzishwa na kugharamiwa kwa teknolojia hizo katika nchi nyingi.
Matibabu
1. Mgonjwa hunyweshwa maji mengi, kwa sababu mwili wake hupoteza maji mengi anapougua maradhi haya.
2. Dawa zinazojulikana kufanya kazi ni kama cotrimoxazole, erythromycin, doxycycline, chloramphenicol, na furazolidone.[3] 3. Chanjo za kuzuia Kipindipindu hutolewa katika baadhi za nchi.[4]
Kuepukana na Kipindupindu
Kinga ni kama ifuatavyo:
- wakati wowote kunawa mikono kabla ya kutayarisha au kula chakula, kusafisha vyombo kama sahani, vikombe n.k.
- kunawa mikono kabisa kwa sabuni – kiganja, upande wa nyuma wa mkono, katikati ya vidole na kucha kwa sekunde. Baada ya haja na kabla ya kula.
- kuwa na akiba ya maji yaliyochemshwa pasipo na maji safi ya bomba
- kupika chakula vizuri maana halijoto juu ya 75 °C (hadi 85 mlimani) inaua bakteria;
- kumenya matunda yote
- kufunika chakula maana nzi wanapitisha bakteria kwa miguu yao
- maji ya choo yanayotokamana na wagonjwa wa kipindupindu yanapasa kupitia mashimo ya choo yaliyohifadhiwa vizuri ili kuzuia usambazaji wa bakteria
- vifaa vyote vinavyotumiwa na wagonjwa vinapaswa kuchemshwa kwa maji ya moto
- mikono inayoshika wagonjwa au nguo zao inapaswa kunaniwa kwa sabuni
- mashimo ya choo yanapaswa kutiwa dawa za kuua bakteria kwa kutumia klorini
- Tumia maji yaliyotibiwa pekee hasa ikiwa ya kunywa; yachemshe au utie matone 5 ya klorini kwa kila galoni 1 au utumie dawa ya kutakasa maji. Yaache maji yatulie kwa dakika 30 kabla ya kunywa.
- Tumia choo kila mara – usiende haja karibu au ndani ya chanzo cha maji.
Historia
Mnamo miaka 1816-1826 kulikuwa na janga la kwanza la kipindupindu mkoani Bengal, nchini India. Waingereza 10,000 na Wahindi walikufa.[5]
Janga la pili la kipindupindu lilikuwa mnamo 1829-1851 kilipoenea nchini Urusi, Hungaria, Ujerumani na Uingereza. Zaidi ya watu 55,000 walikufa katika Uingereza pekee.[6] Mwaka 1831, watu 150,000 walikufa kutokana na janga hili nchini Misri.[7]
Mwaka 1849, kipindupindu kilizuka tena kwa mara ya pili mjini Paris.[8] Mjini London watu 14,137 walikufa.
Miaka ya 1961-1970: kulikuwa na janga lingine la kipindupindu nchini Indonesia. Ilianzia Afrika Kaskazini na kuenea hadi nchi ya Italia. Katika miaka ya 1970, watu waliathirika kidogo nchini Ujapani.
Mnamo 1991-1994 kulikuwa na janga lingine huko Amerika Kusini, lililosababishwa na meli iliyomwaga maji machafu. Nchini Peru watu takriban 10,000 waliuawa.
Mwaka 2000, wagonjwa 14,000 waliripotiwa kuugua kipindupindu. Takriban 87% waliripotiwa kutoka bara la Afrika.[9]
Julai - Desemba 2007: ukame wa maji salama kwa ajili ya kunywa nchini Irak ulisababisha tena janga la kipindupindu.[10] Watu 22 walifariki.[11]
Mnamo Agosti 2007 jimboni Orissa, India, zaidi ya watu 2,000 walilazwa hospitalini.[12]
Machi - Aprili 2008: watu 2,490 walilazwa hospitalini nchini Vietnam kutokana na janga la kipindupindu.[13]
Waathirika maarufu
- George Bradshaw
- Nicolas Léonard Sadi Carnot
- Charles X wa Ufaransa
- Juan de Veramendi
- John Blake Dillon
- Alexandre Dumas mzee, mwandishi wa Kifaransa aliyeandika kitabu "The Three Musketeers"
- Mary Abigail Fillmore, mtoto wa rais wa Marekani Millard Fillmore
- James K. Polk, rais wa kumi na moja wa Marekani
- Pedro V, Mfalme wa Ureno
Tanbihi
- ↑
Favour Ndinyo Mulumia
Chrispus Ndinyo sifuma, Johnson praise Ndinyo patience tet
(editors 2023 (2004). Sherris Medical Microbiology (tol. la 4th). McGraw Hill. ku. 376–7. ISBN 0838585299.
{{cite book}}
:|author=
has generic name (help); line feed character in|author=
at position 22 (help)CS1 maint: numeric names: authors list (link) - ↑
Faruque SM; Nair GB (editors) (2099). Vibrio cholerae: Genomics and molecular biology. Caister Academic Press. ISBN 978-1-904455-33-2.
{{cite book}}
:|author=
has generic name (help); Check date values in:|year=
(help)CS1 maint: multiple names: authors list (link) - ↑ "Cholera treatment". Molson Medical Informatics. 2007. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2012-11-06. Iliwekwa mnamo 2008-01-03.
- ↑ "Is a vaccine available to prevent cholera?". CDC disease info: Cholera. Iliwekwa mnamo 2008-07-23.
- ↑ The 1832 Cholera Epidemic in New York State Ilihifadhiwa 13 Mei 2015 kwenye Wayback Machine., By G. William Beardslee.
- ↑ Asiatic Cholera Pandemic of 1826-37.
- ↑ Cholera Epidemic in Egypt (1947) Ilihifadhiwa 22 Novemba 2010 kwenye Wayback Machine..
- ↑ The Irish Famine.
- ↑ Disease fact sheet: Cholera Ilihifadhiwa 16 Julai 2011 kwenye Wayback Machine.. IRC International Water and Sanitation Centre.
- ↑ "U.N. reports cholera outbreak in northern Iraq", CNN. Retrieved on 2007-08-30.
- ↑ Cholera crisis hits Baghdad, The Observer, 2 Desemba 2007.
- ↑ Cholera death toll in India rises, BBC News.
- ↑ Cholera Country Profile: Vietnam. WHO.