Benito Mussolini

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Mussolini pamoja na Hitler mwaka 1940 wakitembelea Yugoslavia
Mussolini akihotubia wafuasi wake

Benito Amilcare Andrea Mussolini (29 Julai 1883 - 28 Aprili 1945) alitawala Italia kidikteta kati ya 1922 hadi 1943.

Mwanasiasa wa Kisoshialisti[hariri | hariri chanzo]

Alisoma ualimu lakini alijiunga na siasa na kuwa mwanachama wa chama cha kijamaa (soshialisti) cha Italia. Akawa mhariri mkuu wa gazeti la chama. Wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia alidai ya kwamba Italia ijiunge na vita dhidi ya Ujerumani akafukuzwa katika chama kilichopinga vita. Mussolini akawa mwanajeshi.

Mwanzo wa ufashisti[hariri | hariri chanzo]

Baada ya vita akatunga itikadi yake ya "ufashisti" akaunda harakati ya "Fasci di Combattimento" (Muungano ya mapambano). Wafuasi wake mara nyingi waliwahi kuwa wanajeshi wasioridhika na matokeo ya vita na siasa ya nchi. Mussolini aliwavalisha sare nyeusi na kuwapanga katika vikosi kwa utaratibu wa kijeshi. Idadi yao iliendelea kukua haraka hadi kufikia 200,000 mwaka 1922. "Mashati nyeusi" walishambulia Wakomunisti na Wasoshialisti na kuvunja migomo ya wafanyakazi wakipokea pesa kutoka wenye viwanda au mashamba makubwa.

Kwenye uchaguzi mkuu mwaka 1921 Wafashisti walipata wabunge 34. Mussolini alibadilisha "fasci" kuwa chama cha kifashisti cha kitaifa (PNF). Wakati huohuo "mashati nyeusi" waliendela kupigana na wafanyakazi na wa soshialisti kwenye barabara za Italia.

Kiongozi wa serikali[hariri | hariri chanzo]

Hali ya vurugo ilisababisha kuanguka au kujiuzulu kwa serikali kadhaa. Mfalme Vittorio Emanuele III alioogopa vita ya ndani akampatia Mussolini wito wa kuanzisha serikali mpya. 31 Oktoba 1922 Mussolini alikuwa waziri mkuu wa Italia na kiongozi wa serikali.

Tangu mwaka 1924 aliimarisha utawala wake. Kwa sheria maalumu alibadilisha utaratibu wa uchaguzi akajipatia wabunge wengi. Sheria zilizofuata zilipiga marufuku vyama vya upinzani. Wanahabari wote walipaswa kuwa wanachama wa chama cha kifashisti. Hadi 1928 udikteta wa chama kimoja ulisimama imara.

Siasa ya nje[hariri | hariri chanzo]

Dikteta Mjerumani Adolf Hitler alikuwa amevutwa na siasa ya Mussolini akamwiga katika mengi. Lakini Mussolini hakumpenda Hitler hasa itikadi yake ya kimbari. Alikuwa na wasiwasi kuhusu mipango ya Hitler dhidi ya Austria. Mwaka 1934 alituma wanajeshi mpakani na Austria alipoogopa uvamizi wa Wajerumani katika nchi ya jirani.

Katika siasa ya nje Mussolini alikuwa na ndoto la kujenga upya Dola la Roma la Kale. Mwaka 1935 alishambulia Ethiopia akitaka kujipatia koloni mpya na pia kulipiza kisasi cha ushindi wa Ethiopia dhidi ya Italia katika vita ya Adua mwaka 1896. Italia ikafukuzwa katika Shirikisho la Madola lakini ilifauli kutawala Ethiopia yote.

Katika Vita ya wenyewe kwa wenyewe ya Hispania tangu 1936 Mussolini alichukua upande wa jenerali Francisco Franco. Kufukuzwa katika Shirikisho la Madola na msaada kwa Franco kulisababisha hali ya karibu zaidi na Hitler. 25 Oktoba 1936 Mussolini na Hitler walitia sahihi mkataba wa ushirikiano kati ya Italia na Ujerumani.

Benito Mussolini, Claretta Petacci na wengine walionyeshwa mbele ya watu baada ya kuuawa.

Vita Kuu ya Pili ya Dunia[hariri | hariri chanzo]

Albania[hariri | hariri chanzo]

Katika Aprili 1939 - kabla ya mwanzo wa Vita Kuu - Italia ilivamia Albania. Jeshi la Italia ilipata matatizo makubwa kushinda nchi hii ndogo. Hivyo Mussolini alitulia mwanzoni alipomwona Hitler kushambulia Poland katika Septemba 1939. Alikaa kimya pia Hitler alipovamia Ufaransa. Mwishoni tu, siku chache kabla ya ushindi wa Ujerumani kukamilika, Mussolini aliamua kuingia katika vita akateka sehemu ndogo ya Ufaransa ya kusini.

Ugiriki[hariri | hariri chanzo]

28 Oktoba 1940 Mussolini aliamrisha jeshi lake kushambulia Ugiriki. Lakini Wagiriki walijitetea kwa nguvu Waingereza wakawasaidia. Jeshi la Wagiriki liliingia katika Albania. Hitler alipaswa kuingilia kati na kutuma wanajeshi Wajerumani Ugiriki waliofaulu kuwashinda Wagiriki na Waingereza nchini.

Afrika[hariri | hariri chanzo]

Mussolini alikuwa na matumaini ya kwamba ingekuwa rahisi kuvamia na kuteka koloni za Uingereza katika Afrika. Alipanga kuwashambulia Waingereza kutoka koloni zake za Libya, Ethiopia na Somalia akilenga Misri, Somaliland ya Uingereza na Kenya. Lakini mipango hii ilishindikana.

Mwisho[hariri | hariri chanzo]

Wakati huohuo Uingereza ilizamisha manowari nyingi za Kiitalia. Mwaka 1943 Waingereza na Waamerika -waliowahi kuteka Afrika ya Kaskazini- walivamia Italia ya kusini.

Mussolini aliangushwa na halmashauri ya chama chake pamoja na mfalme akatupwa katika jela. Wajerumani walimwokoa gerezani lakini hakuweza kutawala Italia tena. Alikuwa na eno ndogo katika Italia ya Kaskazini.

Katika siku za mwisho wa vita kuu Mussolini alijaribu kujiokoa mbele ya jeshi la Waamerika waliokaribia kwa kukimbia Uswisi. 27 Aprili 1945 Mussolini pamoja na wasaidizi wake na mpenzi wake Clara Petacci walikamatwa na wanamgambo Waitalia wakomunisti waliomwua siku iliyofuata tar. 28.Aprili.