Vita ya wenyewe kwa wenyewe ya Hispania

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Manuel Azana, aliyekuwa rais wa Jamhuri ya Hispania.

Vita ya wenyewe kwa wenyewe ya Hispania ilitokea nchini huko hasa kuanzia tarehe 17 Julai 1936 hadi tarehe 1 Aprili 1939 kati ya watetezi wa serikali ya Jamhuri ya Hispania na wafuasi wa kiongozi wa kijeshi jenerali Francisco Franco na kusababisha vifo zaidi ya laki tano.

Pande mbili zilizopigana ziliungwa mkono na nchi za nje: Umoja wa Kisovyeti na Meksiko upande mmoja, Ureno, Ujerumani na Italia upande mwingine.

Hatimaye Franco alishinda akawa kiongozi na dikteta wa Hispania hadi kifo chake mwaka 1975.

Utangulizi wa vita[hariri | hariri chanzo]

Siasa ya Hispania ilikuwa katika hali ya vurugu tangu kuanzishwa kwa jamhuri ya pili mwaka 1931 iliyomaliza utawala wa mfalme Alfonso XIII. Sehemu kubwa ya wafanyakazi wa viwandani hawakuridhika na jamhuri, wakalenga mapinduzi ya kijamii.

Harakati kali ya upinzani dhidi ya nafasi kubwa ya Kanisa Katoliki katika taifa la Hispania ilisababisha mashambulio shidi ya makanisa na monasteri na kifodini cha Wakristo wengi, hasa mapadri na watawa.

Wafuasi wa mfalme aliyeondoka nchini, watetezi wa Kanisa Katoliki, wenye mashamba makubwa na chama kipya cha Falange walianza kuungana kupinga kwa jamhuri na katiba yake kwa jumla.

Baada ya majaribio ya vikosi vya wafanyakazi wasoshalisti, lakini pia wanajeshi wapenzi wa mfalme waliolenga wote kupindua serikali, uchaguzi wa mwaka 1936 haukuleta usuluhisho wa matata ya siasa. Vikundi viwili vikubwa vilivyoshindana vilikuwa "umoja wa wananchi" uliounganisha wasoshalisti, wakomunisti na vikundi vidogo dhidi ya "umoja wa taifa" uliounganisha wafuasi wa mfalme, Wakatoliki, chama cha wenye mashamba na Falange. Umoja wa wananchi ulipata kura chache kuliko wapinzani wake na sheria ya uchaguzi uliupa nafasi nyingi bungeni.

Franco kutwaa silaha[hariri | hariri chanzo]

Vurugu ziliendelea na baada ya mauaji ya kisiasa sehemu za jeshi chini ya jenerali Franco zilichukua silaha dhidi ya serikali ya jamhuri. Sehemu kubwa ya jeshi ilijiunga naye.

Serikali ya jamhuri ilikuwa na sehemu nyingine ya jeshi lakini viongozi wengi walikuwa upande wa upinzani. Kila upande ulitolea silaha kwa wanamgambo walioundwa na vyama mbalimbali vya kisiasa.

Watetezi wa jamhuri walipata usaidizi kutoka serikali za Umoja wa Kisovyeti na Meksiko na wapinzani walisaidiwa na serikali za Benito Mussolini nchini Italia na Adolf Hitler nchini Ujerumani. Marafiki wa jamhuri ya Hispania walikuja kutoka nchi nyingi na kushika silaha wakaitwa vikosi vya kimataifa ("international brigades").

Mahali pa Guernica.

Guernica kama mfano wa ukali wa vita[hariri | hariri chanzo]

Katika taswira ya "Guernica" mchoraji Pablo Picasso alionyesha ubaya wa vita.

Mapigano yalikuwa makali na watu wengi waliuawa ovyo.

Mwishowe jeshi la Franco lilishinda likisaidiwa na vikosi vya jeshi la Italia na Ujerumani.

Kati ya mapigano mengi lilitokea shambulio la ndege za kijeshi za Kijerumani dhidi ya mji wa Guernica, lililokuwa kati ya mashambulio ya kwanza ya idadi kubwa ya ndege dhidi ya mji wowote duniani.

Guernica iliharibika, na Pablo Picasso alichora taswira iliyopata kuwa maarufu.

Hispania ya Franco[hariri | hariri chanzo]

Baada ya ushindi wa Franco mwaka 1939 vyama vya upande wa jamhuri vilipigwa marufuku na vyama vyote vya upinzani vililazimishwa kuungana katika Falange chini ya uongozi wa Franco mwenyewe.