Pablo Picasso

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Pablo Picasso (1962).
Saini ya Pablo Picasso.
Saini ya Pablo Picasso.

Pablo Ruiz Picasso (25 Oktoba 1881 - 8 Aprili 1973) alikuwa mchoraji mashuhuri na pia mchongaji wa Hispania. Jina lake kamili ni Pablo Diego José Francisco de Paula Juan Nepomuceno María de los Remedios Cipriano de la Santísima Trinidad Clito Ruiz y Picasso.

Umuhimu wa Picasso[hariri | hariri chanzo]

Picasso anahesabiwa kati ya wasanii wakuu wa karne ya 20. Alibadilisha uzoefu jinsi ya kuona dunia katika utamaduni wa Kimagharibi wa Ulaya na Marekani. Mtindo wake wa uchoraji ulianza kutumia maumbo ya jiometri. Katika hatua hii aliathiriwa na sanaa ya Afrika.

Kipindi cha buluu: Picha ya Suzanne Bloch (1904)

Picasso hakuwa mchoraji wa kwanza wala mchoraji pekee aliyetumia mbinu mpya lakini alijulikana kushinda wote na ile "sanaa ya kisasa" ilitambulishwa mara nyingi kwa lugha ya "picha kama Picasso".

Mwanzo wa kazi[hariri | hariri chanzo]

Picasso alianza kuchora katika umri mdogo wa miaka saba akisaidiwa na baba yake aliyekuwa mwalimu wa sanaa. Akiwa na miaka 10 aliandikishwa kwenye chuo cha sanaa na mwaka 1895 alipokewa kwenye chuo kikuu cha sanaa huko Barcelona.

Alitembelea sana makumbusho yenye taswira na sanamu za wasanii waliotangulia. Alipenda kusafiri penye maonyesho makubwa kama Madrid au Paris.

Taswira zake za awali bado zililingana zaidi na picha jinsi zilivyokuwa kawaida. Mwanzoni alipenda rangi ya buluu na mfano wake ni picha ya Suzanne Bloch hapo chini.

Baada ya kuona sanaa ya Afrika: Mabinti wa Avignon (1910).

Athira ya Kiafrika na mtindo mpya[hariri | hariri chanzo]

Mjini Paris alikuta maonyesho ya sanaa ya Kiafrika iliyomwathiri sana. Hii inaonekana katika "Mabinti wa Avignon" (1910).

Baadaye aliendelea kuvunja maumbile ya kawaida na kuyajenga upya kwa kutumia maumbo ya kijiometri. Mtindo huo uliitwa "cubisme" kwa Kifaransa yaani "umchemraba" kutokana na mchemraba kama umbo la kijiometri linalotumiwa kujenga upya maumbile ya yale yanayoonyeshwa kwenye picha.

Ukubisti (uchembemraba): Picha ya Juan Gris (1912).

Picasso aliendelea kujaribu mitindo mipya-mipya. Kati ya taswira zake zilizopata kuwa maarufu sana kimataifa ilikuwa "Guernica" (1937) iliyonesha kikuli na maafa ya vita. Ilichorwa wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe ya Hispania baada ya shambulio la wanahewa Wajerumani dhidi ya mji mdogo wa Guernica.

Kwa jumla imekadiriwa ya kwamba Picasso aliumba kazi za sanaa zaidi ya 20,000 kama vile taswira, picha za mchapo na sanamu.

Maisha ya binafsi[hariri | hariri chanzo]

Picasso alioa mara mbili lakini alikuwa na wapenzi wengi. Alizaa watoto wanne na wake watatu.

"Guernica" (1937) imechorwa baada ya kuangamizwa kwa mji wa Guernica.

Baada ya kuhamia Paris alibaki huko akakataa kurudi Hispania kwa sababu alimchukia dikteta Francisco Franco. Wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia alikaa Paris chini ya utawala wa Wajerumani na wakati ule hakuweza kuonyesha kazi zake kwa sababu siasa ya Ujerumani ilichukia mtindo wake. Mwaka 1945 alijiunga na chama cha Kikomunisti abakabi Mkomunisti hata kama siasa ya Umoja wa Kisovyeti pia haikupenda mtindo wake.

Tangu mwaka 1961 aliishi katika Ufaransa ya Kusini alipoaga dunia mwaka 1973.

Makala hii kuhusu mtu huyo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Pablo Picasso kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.