Wernher von Braun

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Wernher von Braun mnamo 1960

Wernher Magnus Maximilian von Braun (23 Machi 1912 - 16 Juni 1977) [1] alikuwa mhandisi na mwanasayansi kutoka nchini Ujerumani . Alikuwa mbuni wa roketi kuanzia miaka ya 1930 hadi 1972. [2] Ametajwa kama mhandisi muhimu zaidi wa roketi katika karne ya 20. [3] Alifanya kazi kwa serikali na jeshi la Ujerumani wakati wa Vita vya Kidunia vya pili akajiunga pia na shirika la SS. Baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia alipelekwa Marekani kama mfungwa wa vita akaendelea kufanya kazi kwa jeshi la Marekani na NASA. Mnamo 1955 von Braun alipata kuwa raia wa Marekani.

Alikuwa mbuni mkuu wa roketi ya V-2, iliyokuwa roketi ya kwanza kuruka hadi anga-nje. [4] Baadaye alibuni roketi ya Saturn V iliyowapeleka wanaanga wa Apollo 11 hadi mwezini mnamo 1969. [1]

Maisha ya awali[hariri | hariri chanzo]

Von Braun alizaliwa Wirsitz (wakati ule: Ujerumani, tangu 1919/ 1945 Wyrzysk huko Poland) mnamo 23 Machi 1912. Baba yake alikuwa mtumishi wa serikali; mwaka 1915 familia ilihamia Berlin ambako baba aliendelea kuwa waziri wa kilimo katika Jamhuri ya Weimar.[5]

Wakati wa miaka ya kwanza ya shule, von Braun alihudhuria shule ya sekondari ya Kifaransa huko Berlin. [6] Katika umri wa miaka 13, alipata zawadi ya darubini ya kuangalilia nyota. Baadaye alitumia pesa yake ya mfukoni kununua kitabu Die Rakete zu den Planetenräumen (Roketi ya kusafiri hadi anga la sayari) cha Hermann Oberth, ambacho kiliweka msingi wa utafiti wa kisasa wa roketi. Mnamo 1930, alimaliza elimu yake ya sekondari akihitimu Abitur (Form VI ya Kijerumani).

Alianza kusoma katika Chuo Kikuu cha Ufundi cha Berlin mnamo 1930. Kuanzia 1931 aliendelea kusoma huko ETH Zurich, halafu alirudi Berlin. [5] Hapo aliendelea na somo la fizikia.

Braun pale Peenemünde mnamo 1941

Kazi ya kijeshi Ujerumani[hariri | hariri chanzo]

Pamoja na masomo yake ya fizikia, von Braun aliajiriwa kwenye taasisi ya uanahewa ya jeshi la Ujrumani mwisho wa 1932. Hapa alitakiwa kuchunguza na kutengeneza roketi. Alitunga tasnifu yake "Michango kuhusu changamoto ya roketi inayotumia fueli kiowevu" na kupokea shahada ya Uzamivu kutoka Chuo Kikuu cha Ufundi cha Berlin. [2]

Mwaka huohuo wa 1934 roketi yake ilifikia kimo cha mita 2200.

Katika miaka iliyofuata aliongoza timu iliyobuni injini ya roketi iliyotumiwa baadaye katika ndege Heinkel He 112. [7] Majaribio hayo yalifanywa katika kijiji kidogo cha Kummersdorf, karibu na Berlin. Mnamo 1936, von Braun na timu yake walitengeneza kizazi kijacho cha makombora kilichoitwa A-3. [8] Eneo la majaribio huko Kummersdorf lilikuwa dogo mno kwa roketi hii mpya. Pamoja na timu yake ya watu 90, taasisi ya von Braun ilihamishwa kwenda eneo kubwa la majaribio huko Peenemünde kwenye mwambao wa Bahari Baltiki kwenye mwaka 1937 na Braun alikuwa mkurugenzi wa kituo cha majaribio ya kijeshi- [5]

Roketi ya A4 (V-2) pale Peenemünde

Mwaka 1933 chama cha Hitler kilikuwa chama tawala katika Ujerumani na kuanzisha udikteta. Braun akiwa mwanafunzi alijiunga na kitengo cha shirika la Schutzstaffel - SS; inaonekana hakuwa mwanachama hai kwa miaka kadhaa. Baada ya kupata nafasi kama mkurugenzi wa Peenemünde, aliomba uanachama cha Chama cha NSDAP mwisho wa 1937. Mwaka 1940 aliomba kupokelewa tena katika SS. [1]

Kazi ya Peenemünde[hariri | hariri chanzo]

Von Braun alifanya kazi huko Peenemünde kati ya 1937 na 1945. Huko, alianza kutengeneza roketi mpya iitwayo A4 ("Aggregat 4"). Baada ya majaribio kadhaa, roketi ilipewa jina V-2. [9] "V" ni kwa neno la Kijerumani "Vergeltung", ambalo linamaanisha kulipiza kisasi. Hilo lilikuwa kombora la kwanza la masafa marefu iliyotumika vitani. [10] Iliweza kubeba bomu la baruti la tani moja hadi kilomita 80 juu kwenye anga, na kuifikisha mamia ya kilomita hadi shabaha yake. Mnamo 1943, Ujerumani ilianzisha utengenezaji wa roketi hiyo kwa kutumia maelfu ya wafungwa kutoka makambi ya KZ kama wafanyakazi wa kiwanda. [11] Maelfu ya roketi hizo zilirushwa hadi Antwerp na Uingereza, haswa London. Makombora zaidi ya 1700 V-2 yalifika Antwerp, na kuua zaidi ya watu 3,700. [12] Ila kwa jumla roketi hazikuwa na athira kubwa ya kijeshi maana hadi mwisho wa vita Braun alishindwa kubuni mfumo wa kulenga roketi hizo kwa umakini.

Kazi ya Marekani[hariri | hariri chanzo]

Von Braun mbele ya roketi

Miaka ya kwanza[hariri | hariri chanzo]

Von Braun pamoja na wahandisi na wanasayansi wengine 100 walikamatwa kwenye mwisho wa vita na kupelekwa Marekani.[13] Walianza kufanya kazi kwa Jeshi la Marekani huko Fort Bliss, Texas, ambapo waliwafundisha askari wa Marekani kuzindua roketi za V-2 zilizokamatwa.

Braun akawa raia wa Marekani mnamo 1955. Wakati wa miaka ya 1950, von Braun alijaribu kuanzisha mradi wa usafiri wa anga wa Marekani. Mradi huo ulianzishwa baada ya Umoja wa Kisovyeti kufaulu kurusha satelaiti Sputnik 1 kwenye mwaka 1957.

Von Braun alipewa nafasi ya kuendeleza mradi wa Marekani kutokana na uzoefu wake. Roketi ya Redstone iliweka satelaiti katika obiti mnamo 31 Januari 1958.

Huntsville na NASA[hariri | hariri chanzo]

Mnamo 1950 Von Braun alianza kufanya kazi huko Redstone Arsenal ya Jeshi katika Huntsville, Alabama, ambayo baadaye ilikuwa Kituo cha Anga cha NASA cha Marshall. [13] Huko, yeye na timu yake walitengeneza kombora la Redstone, iliyofanana na V-2. Mnamo 1959, Von Braun na Wajerumani wengine walihamishiwa NASA. Roketi yake ya mwisho iliyofaulu zaidi ilikuwa Saturn V, ambayo ilibeba wanaanga kwenda mwezi.

Lakini, baada ya kutua kwa Apollo 11 mwezini mnamo 1969, pesa kwa makisio kwa miradi ya angani ilipungua. Mnamo 1972, von Braun alistaafu kutoka NASA na akaenda kufanya kazi na kampuni ya Fairchild Industries, huko Maryland.

Von Braun mbele ya injini ya Saturn V

Miaka ya baadaye[hariri | hariri chanzo]

Mnamo 1972, von Braun aliondoka NASA. Alianza kufanya kazi katika sekta binafsi. Alistaafu kazi mnamo Januari 1977 kwa sababu alikuwa mgonjwa. Mwaka huohuo, alikufa katika umri 65 kwa kansa. [14]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

 1. 1.0 1.1 1.2 "Biography of Wernher von Braun in German" (kwa German). Deutsches Historisches Museum. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2014-08-17. Iliwekwa mnamo 2010-11-15.{{cite web}}: CS1 maint: unrecognized language (link)
 2. 2.0 2.1 "Biography of Wernher von Braun". NASA. Iliwekwa mnamo 2009-04-26.
 3. "From the SS to Citizenship to the Moon: von Braun's Odyssey" (PDF). The National Archives in the Regions. National Archives and Records Administration. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2012-01-08. Iliwekwa mnamo 2009-04-26.
 4. "Wernher von Braun, a biography" (kwa German). who's who.de. Iliwekwa mnamo 2009-04-24.{{cite web}}: CS1 maint: unrecognized language (link)
 5. 5.0 5.1 5.2 "Wernher von Braun (1912–1977)". urbin.de. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2007-10-14. Iliwekwa mnamo 2010-11-15.
 6. "Wernher von Braun (1912–1977)". urbin.de. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2007-10-14. Iliwekwa mnamo 2010-11-15."Wernher von Braun (1912–1977)". urbin.de. Archived from the original Archived 14 Oktoba 2007 at the Wayback Machine. on 2007-10-14. Retrieved 2010-11-15.
 7. Kunz, Martin (2008-06-16). "Der ewige Aufstieg des Raketen-Pioniers" (kwa German). Iliwekwa mnamo 2010-11-15.{{cite web}}: CS1 maint: unrecognized language (link)
 8. "A Brief History of Rocketry". NASA. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2009-01-07. Iliwekwa mnamo 2010-11-15. {{cite web}}: Unknown parameter |= ignored (help)
 9. "The V-2 (A4) Ballistic Missile Technology". Centennial Of Flight. NASA. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2012-02-08. Iliwekwa mnamo 2010-11-15.
 10. "V2ROCKET.COM - The A-4/V-2 Resource Site - The V-2 Rocket". v2rocket.com. Iliwekwa mnamo 16 Novemba 2010.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
 11. "V1 and V2 Rockets - GHN: IEEE Global History Network". ieeeghn.org. Iliwekwa mnamo 16 Novemba 2010.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
 12. "V2ROCKET.COM - Antwerp - City of Sudden Death". v2rocket.com. Iliwekwa mnamo 16 Novemba 2010.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
 13. 13.0 13.1 "Biography of Wernher von Braun". NASA. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2013-09-22. Iliwekwa mnamo 2010-11-15.
 14. Noble Wilford, John (1977-06-18). "Wernher von Braun, Rocket Pioneer, Dies; Wernher von Braun, Pioneer in Space Travel and Rocketry, Dies at 65". The New York Times. The New York Times Company. Iliwekwa mnamo 2010-11-15.