Uhindi ya Kiingereza
Uhindi ya Kiingereza ni kipindi cha historia ambapo nchi za Bara Hindi ama zilitawaliwa na Uingereza moja kwa moja ama zilikuwa chini ya usimamizi wa Uingereza kama nchi lindwa.
Utawala huo ulienea juu ya nchi za leo za Uhindi, Pakistan, Bangladesh, Nepal na kwa muda pia juu ya Burma (Myanmar).
Utawala wa Kiingereza ulikuwa na vipindi viwili:
Utawala wa Kampuni ya Kiingereza kwa Uhindi wa Mashariki (British East India Company)
[hariri | hariri chanzo]Tarehe 31 Desemba 1600 malkia Elizabeth I alitoa hati ya ulinzi wa kifalme kwa biashara kati ya Uingereza na "Uhindi wa Mashariki".
Kampuni iliyopokea hati hii ilikuwa kundi la wafanyabiashara na matajiri wa London waliovutwa na utajiri wa nchi za mashariki na hasa na faida kubwa mikononi mwa wafanyabiashara Wareno na Waholanzi waliotangulia katika biashara kati ya Ulaya na nchi za Asia ya Kusini.
Kampuni ilishindana kibiashara na kivita na wafanyabiashara wa Ureno, wa Uholanzi na wa Ufaransa. Iliweza kununua au kuvamia vituo vya biashara na kujenga maboma yake kuanzia mwaka 1644 huko Bombay, Madras na penginepo.
Mwaka 1717 kampuni ilipata kibali cha mtawala wa Moghul cha kusamehewa kodi kwa biashara katika Ubengali.
Tangu mwaka 1680 kampuni ilianzisha jeshi lake la maaskari Wahindi na kuwa mshiriki katika siasa ya Uhindi.
Kati ya miaka 1756 na 1763 Uingereza pamoja na mataifa mengine ya Ulaya ilishiriki katika Vita ya miaka saba iliyokuwa vita ya kwanza ya kimabara. Waingereza walipigana pamoja na Prussia dhidi ya Austria, Ufaransa, Urusi na Uswidi. Jeshi la kampuni liliendesha vita hii dhidi ya maeneo ya Ufaransa katika Uhindi. Wafaransa walishindwa wakabaki na vituo vidogo tu katika miji kama Pondicherry na Mahe lakini kampuni iliongeza maeneo yake katika Uhindi.
Baada ya mwaka 1757 Kampuni ya Kiingereza ilikuwa enzi muhimu, iliweza kushindana hata na nguvu ya Moghul. Ilianza kutawala sehemu kubwa za Uhindi wa Kusini pamoja na Ubengali.
Kampuni ilitumia mbinu mbili:
- mikataba na madola ya watawala wa Kihindi waliokubali kupokea mabalozi wa kampuni kwao waliokuwa kama washauri wakuu wa Maharaja au Nawab wa eneo; siasa ya nje na mambo ya jeshi ziliwekwa chini ya kampuni
- uvamizi na utawala wa moja kwa moja, maeneo yale yalikuwa mali ya kampuni.
Mafaniko makubwa ya kampuni yalisababisha mgogoro huko Uingereza na sheria mbalimbali za bunge la Uingereza zililenga kuongeza athira ya serikali ya Uingereza juu ya shughuli za kampuni.
Katika karne ya 19 kampuni ikawa mtawala juu ya sehemu kubwa za Uhindi, ama kwa njia ya mikataba na watawala wa kienyeji au kwa utawala wa moja kwa moja. Kampuni ilianza kubadilisha uso wa India kujenga reli na kuanzisha mawasiliano wa kisiasa kwa huduma ya posta na pia simu za telegrafi.
Mwaka 1857 ilitokea uasi wa wanajeshi Wahindi wa jeshi la kampuni uliosababisha na mkasi wa mabadiliko na dharau ya viongozi Waingereza kwa utamaduni wa wenyeji. Utawala wa kampuni ulianza kuporomoka; uliokolewa tu kwa kupeleka Uhindi wanajeshi kutoka Uingereza. Uasi ulikomeshwa kwa mabavu.
Lakini kuingilia kati kwa serikali ya Uingereza kulikuwa mwisho wa utawala wa kampuni. Mwaka 1858 serikali ya London ilichukua madaraka yote ya kampuni ikafanya Uhindi kuwa koloni la taji la Uingereza.
Utawala wa kiserikali kati ya 1858 hadi 1947
[hariri | hariri chanzo]Kuanzia mwaka 1858 Uhindi ilitawaliwa kama koloni la Uingereza. Kaisari wa mwisho wa Moghul Bahadur Shah Zafar II aliondolewa nchini. Malkia Viktoria wa Uingereza alichukua cheo chake akaitwa "Kaisari wa Uhindi" (kwa Kiingereza: "Empress of India"; kwa Kihindi: "Padishah-e-Hind") akamwachia utawala gavana wake aliyepewa cheo cha "makamu wa mfalme" (Vice-Roy).
Muundo wa utawala uliendelea: Maeneo ya kampuni yalikuwa makoloni ya Uingereza. Maeneo ya watawala Wahindi yalibaki yalivyo lakini kila Maharaja au Nawab alipaswa kula kiapo cha utii kwa malkia kama Kaisari au malkia mkuu wa Uhindi na kumkubali mshauri Mwingereza katika jumba lake kama mwakilishi wa Uingereza.
Mwisho wa karne ya 19 harakati za kutafuta uhuru zilianza upya. Mwaka 1885 chama cha INC (Indian National Congress) iliundwa na Wahindu na Waislamu pamoja waliodai uhuru. Mwaka 1906 viongozi Waislamu walitoka katika INC na kuunda "Shirikisho la Waislamu".
Mwaka 1917 Uingereza ulitamka ya kwamba ulitaka kuelekea polepole hali ya kujitawala kwa Wahindi. Viongozi wa wenyeji hawakuridhika na mkasi wa mabadiliko. Chini ya uongozi wa Mahatma Ghandi mwendo wa kupigania uhuru bila mabavu ulipata nguvu. Ghandi alipigania hasa umoja wa Wahindu na Waislamu lakini alipingwa na viongozi wakali wa pande zote mbili.
Baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia Waingereza walikubali kujiondoa katika Uhindi. Swali kubwa lilikuwa kama nchi itabaki kama nchi moja au kama maeneo ya Waislamu yatajitenga.
Tarehe 14/15 Agosti 1947 utawala wa Uingereza ulikwisha. Bara Hindi iligawanywa katika nchi mbili za Uhindi na Pakistan. Mgawanyo ulikuja na vita na kumwaga kwa damu nyingi.
Tarehe 30 Januari 1948 Ghandi mwenyewe aliuawa na Hindu mkali aliyemchukia kwa sababu alitaka usawa wa Waislamu na Wahindu.