Nenda kwa yaliyomo

Maradhi ya zinaa

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Ugonjwa wa zinaa)
Ukimwi unavyoshambulia mwili.
Sehemu ya mfululizo wa makala kuhusu mapendo

Moyo katika mapokeo ya Ulaya
ni mchoro unaowakilisha mapendo.
Vipengele Msingi
Mapendo kadiri ya sayansi
Mapendo kadiri ya utamaduni
Upendo (fadhila)
Upendo safi
Kihistoria
Mapendo ya kiuchumba
Mapendo ya kidini
Aina za hisia
Mapendo ya kiashiki
Mapendo ya kitaamuli
Mapendo ya kifamilia
Mapendo ya kimahaba
Tazama pia
Mafungamano ya binadamu
Jinsia
Tendo la ndoa
Maradhi ya zinaa
Siku ya wapendanao

Maradhi ya zinaa ni namna ya kutaja magonjwa yanayosambazwa kwa njia ya vitendo vya kijinsia, mengine ya zamani (kisonono, kaswende n.k.), na mengine mapya (ukimwi n.k.).

Maradhi hayo yanaweza yakaambukizwa kwa njia nyingine pia, au kwa vitendo vya kijinsia vilivyo halali kwa wahusika, lakini yanaitwa “ya zinaa” kwa sababu yanaenezwa hasa kwa wingi wa vitendo hivyo vinavyofanyika nje ya ndoa kwa kujamiiana na watu mbalimbali.

Katika matokeo hayo pia tunaona kwamba uzinifu unamdhuru binadamu: hatuwezi kuchezea utakatifu wa uhai tusipate hasara katika roho, katika jamii na pengine hata katika mwili.

Wingi wa maradhi hayo na maambukizi yake

[hariri | hariri chanzo]
A map of the world where most of the land is colored green or yellow except for sub Saharan Africa which is colored red
Asilimia ya watu wenye umri wa miaka 15–49 walioambukizwa UKIMWI nchi kwa nchi (2011).[1]

     No data      <0.10      0.10–0.5      0.5–1

     1–5      5–15      15–50

Maradhi ya zinaa ni magonjwa ya maambukizi zaidi ya 25 ambayo kimsingi husambazwa kutoka mtu mmoja hadi mwingine kwa kujamiiana.

Magonjwa ya zinaa ni miongoni mwa maambukizi yanayofahamika sana na yaliyoleta madhara makubwa hasa katika nchi zinazoendelea ambazo nyingi ziko barani Afrika.

Marekani ina kiasi kikubwa cha maambukizi kuliko nchi nyingine zilizoendelea: kwa makisio nusu ya Wamarekani wote huambukizwa magonjwa ya zinaa kabla ya kufikia umri wa miaka 35.

Licha ya kuenea kwa magonjwa ya zinaa, uchunguzi unaonyesha kuwa watu wengi hawana ufahamu juu ya hatari za maambukizi ya magonjwa haya, madhara au kifo kabisa kinachoweza kusababishwa na matokeo ya kutotibu maambukizi.

Magonjwa ya zinaa kama kisonono au klamidia, yanaweza yasionyeshe dalili zozote. Watu wasiojua kuwa wameambukizwa huwa na hatari ya kuambukiza wapenzi wao, na wakati mwingine (kwa wanawake) watoto walio tumboni mwao.

Kama yataachwa bila kutibiwa, magonjwa hayo yanaweza kusababisha maumivu makali au kumuondolea mwanamke uwezo wa kupata mtoto.

Baadhi ya magonjwa ya zinaa yanaweza kutibiwa kwa dozi moja ya antibaotiki, lakini mengine kama Ukosefu wa Kinga Mwilini (UKIMWI) hayatibiki. Watu wenye magonjwa hayo hubakia na uwezo wa kuambukiza maisha yao yote.

Hatari kubwa zaidi ya kupata magonjwa ya zinaa ni kwa watu ambao huwa na wenzi wengi wa kimapenzi; hufanya ngono bila ya kutumia kondomu; na ambao huchangia sindano za kujidungia madawa katika miili yao.

Chunguzi zinaonyesha kuwa wenye umri kati ya miaka 16 na 24 wapo katika hatari kubwa zaidi ya kupata magonjwa ya zinaa kuliko watu wa makamo kwa sababu vijana wanaweza kuwa na wenzi wengi wa mapenzi kuliko kuwa na mahusiano ya muda mrefu na mwenzi mmoja. Zaidi, vijana wanaweza wakaona ugumu kuwaambia wenzi wao kuwa wameambukizwa magonjwa ya zinaa. Vijana pia wanaweza kuona aibu au kutokuwa na uwezo wa kutafuta matibabu ya magonjwa haya. Hii inamaamisha si tu kuwa wanaweza kuambukiza ugonjwa kwa vijana wenzao bali pia wana hatari kubwa ya kupata madhara yanayosababishwa na kutotibu ugonjwa kwa muda mrefu.

Maambukizi ya magonjwa ya zinaa

[hariri | hariri chanzo]

Magonjwa ya zinaa huambukizwa na wakala wa magonjwa – bakteria wadogowadogo, virusi, vidusia, fungi na protozoa wakaao katika sehemu vuguvugu na zenye unyevunyevu katika mwili kama vile sehemu za siri, mdomoni na kooni. Magonjwa mengi ya zinaa husambaa wakati wa kujamiiana (katika uke au mkunduni), lakini aina nyingine za kukutana kimapenzi kama kwa kutumia midomo (oral sex) zinaweza kusambaza magonjwa.

Magonjwa mengine ya zinaa yanaweza kusambazwa kwa njia nyingine zaidi ya kujamiiana. Magonjwa fulani ya zinaa yanayosababishwa na virusi kama UKIMWI yanaweza kuambukizwa kwa kukutana na damu iliyoathirika. Kwa mfano, magonjwa yanayosababishwa na virusi yanaweza kusafiri miongoni mwa watu wanaochangia sindano zilizo na maambukizi, na mtu anaweza kupata maambukizi kwa kupokea dawa iliyoambukizwa. Baadhi ya magonjwa ya zinaa huambukiza kwa kutoka kwa mama hadi kwa mtoto. Maambukizi yanaweza kutokea kabla ya kuzaliwa, wakati vijidudu vikifanikiwa kupita katika kondo la uzazi (placenta, ogani katika mji wa mimba wa mwanamke mjamzito ambayo huunganisha mfumo wa damu ya mama na wa mtoto) na kuingia katika mkondo wa damu wa mtoto. Maambukizi pia huweza kutokea wakati wa kujifungua, wakati mtoto anapopita katika njia ya uzazi au baada kujifungua, wakati mtoto anapotumia maziwa yaliambukizwa.

Magonjwa ya zinaa hayawezi kuambukizwa kwa kupeana mikono au kugusana, au kugusa nguo au katika viti vya chooni.

Magonjwa ya zinaa yanayofahamika

[hariri | hariri chanzo]

Kuna magonjwa ya zinaa mengi, haya ni baadhi yale yanayofahamika sana.

Klamidia

[hariri | hariri chanzo]
Makala kuu: Klamidia
Vijududu vinavyosababisha klamidia.

Klamidia ni ugonjwa wa kuambukiza ambao husababishwa na bakteria zinazoitwa na sayansi kama Chlamydia trachomatis.

Ugonjwa huo huwa hauonyeshi dalili za wazi kwa karibia asilimia 75 ya wanawake na asilimia 50 ya wanaume, hivyo maambukizi mengi hushindwa kufahamika mapema.

Kulingana na wakala wa afya wa Marekani Centers for Disease Control and Prevention ndiyo ya kwanza kati ya maradhi ya zinaa yanayoripotiwa zaidi nchini humo: wataalamu wamekisia kuwa karibia watu milioni tatu huambukizwa klamidia kila mwaka, lakini kulingana na CDC, ni maambukizi 660,000 tu ndiyo ambayo huripotiwa.

Watu ambao hawajafahamu kuwa wameambukizwa klamidia wanaweza wasitafute tiba na hivyo wakaendelea kufanya ngono, bila ya kujua kuwa wanaeneza ugonjwa.

Wakati dalili zinapoanza kujitokeza wanaume husikia maumivu wakati wa kukojoa au kutokwa usaha katika uume. Wanawake wanaweza kutokwa damu nje ya kipindi chao, maumivu wakati wa kukojoa, kutokwa usaha katika uke, au maumivu chini ya kitovu.

Kama utaachwa bila kutibiwa katika wanawake, klamidia inaweza kuleta madhara makubwa kwa afya ya binafsi na ya jamii. Klamidia huaribu tishu za uzazi za mwanamke na kusababisha uvimbe katika fupanyonga (pelvic inflammatory disease, PID). PID inaweza kusababisha mauvimu makali sana katika fupanyonga, utasa/ugumba au utata katika ujauzito ambao unaweza kusababisha kifo.

Watoto waliozaliwa na mama aliyembukizwa klamidia huwa na hatari ya kupata upofu au maambukizi katika mapafu.

Uchunguzi wa maambukizi ya klamidia hufanyika kwa kuchunguza fupanyonga na kiwango kidogo cha majimaji kutoka katika uke au uume ambayo huchunguzwa kwa uwepo wa Chlamydia trachomatis.

Uchunguzi mpya kama ule wa mkojo ili kufahamu uwepo wa bakteria wa klamidia umekuwa ukitumika pia ili kufanya uchunguzi rahisi zaidi wa watu ambao hawaonyeshi dalili za ugonjwa.

Klamidia inatibika kwa antibaotiki.

Kisonono

[hariri | hariri chanzo]
Makala kuu: Kisonono
Dalili ya ugonjwa katika ngozi.

Kisonono au Kisalisali ni maradhi ya zinaa ambayo husababishwa na bakteria zinazofahamika kisayansi kama Neisseria gonorrhoeae. Bakteria hizo hushambulia utandotelezi unaozunguka sehemu za siri.

Ingawa kwa makisio maambukizi 360,000 ya kisonono huripotiwa kila mwaka nchini Marekani, wataalamu wamekisia kuwa watu karibia 650,000 huambukizwa kwa mwaka. Kimataifa yanakadiriwa kuwa kati ya milioni 33 na 106 kwa mwaka. Wagonjwa ni 0.8% ya wanawake wote na 0.6% ya wanaume wote.

Kama ilivyo klamidia, kisonono nayo huwa haionyeshi dalili. Kisonono ikiwepo huwa na dalili kama zile za klamidia ambazo huhusisha mauvimu wakati wa kukojoa na kutokwa kwa maji yanayonuka au usaha katika uke au uume.

Kisonono huonekana kwa urahisi kwa wanaume ambao hutoa usaha kutoka katika mfereji wa mkojo (urethra). Huanza kidogo, lakini huongezeka na huwa mwingi na kusababisha kusikia haja ya kukojoa mara kwa mara huku kukiwa na maumivu.

Kisonono ikisambaa na kufikia tezi kibofu, mfereji wa mkojo huziba kwa kiasi fulani. Kwa wanawake maambuki hutokea katika urethra, uke au mlango wa uzazi (cervix). Ingawa mwasho unaotokana na majimaji katika uke unaweza kuwa mkubwa, mara nyingi dalili hizi huwa ni chache au hamna kabisa katika hatua za awali.

Kisonono isiyotibiwa inaweza kusababisha PID (Pelvic Infiammatory disease) kwa wanawake. Watoto wanaozaliwa na mama wenye kisonono huwa na hatari ya kuambukizwa wakati wa kuzaliwa; maambukizo haya yanaweza kusababisha magonjwa ya meno kwa wachanga.

Uchunguzi wa ugonjwa hufanywa kwa kuchungunza usaha kutoka katika uke au uume au mkojo kwa uwepo wa Neisseria gonorrhoeae.

Kisonono iliongezeka kwa kiasi kikubwa Marekani mnamo miaka ya 1970 na mwanzoni mwa miaka ya 1980, hadi kukaribia kufikia kiwango cha magonjwa ya mlipuko (epidemic proportions) kwa vijana wanaobalehe na watu wa umri wa kati.

Kisonono hutibiwa kwa antibiotiki kadhaa, ingawa maambukizi yamekuwa na ukinzani juu ya tiba ya baadhi ya madawa katika miongo ya nyuma. Moja kati ya mambo magumu katika kupambana na kisonono ni kutafuta mahusiano yote ya kimapenzi ya nyuma ya aliyeambukizwa ili kuweza kuzuia usambaaji zaidi wa ugonjwa.

Kaswende

[hariri | hariri chanzo]
Makala kuu: Kaswende
Mfano wa kichwa cha mtu mwenye kaswende katika hatua ya tatu.

Kaswende ni gonjwa tishio linalosababishwa na bakteria inayofahamika kama Treponema pallidum.

Katika hatua za mwanzo, vipele katika sehemu za uzazi huanza kujitokeza muda mfupi baada ya maambukizi ambavyo baadaye hupotea vyenyewe.

Kama ugonjwa hautatibiwa, maambukizi huendelea kwa miaka, yakishambulia mifupa, ubongo na moyo na kusababisha madhara mengine yanayotokana na matatizo katika mfumo wa fahamu kama vile homa ya uti wa mgongo na magonjwa ya moyo na kiharusi.

Kaswende wakati wa ujauzito unaweza kuwa hatari kubwa kwa kiumbe tumboni, kama vile kusababisha kutoumbika vizuri (deformity) na kifo.

Wanawake wengi wajawazito katika nchi zilizoendelea huchunguzwa kwa uwepo wa ugonjwa huu katika majuma ya kwanza ya mimba ili kutibu ugonjwa kabla kitoto hakijaathirika.

Siku hizi kaswende inaweza kutibika kwa urahisi kwa penicillin.

Malengelenge sehemu za siri

[hariri | hariri chanzo]

Ugonjwa wa malengelenge katika sehemu za siri husababishwa na maambukizi ya herpes simplex virus(HSV). Aina nyingi za malengelenge huwa ni kutokana na aina ya pili ya HSV (HSV type 2). hatahivyo, maambukizi kutokana na aina ya kwanza ya HSV (HSV type 1) nayo yapo. Malengelenge katika sehemu za siri husababisha vivimbe vinavyouma vinavyojirudia kila mara, ingawa mara nyingi ugonjwa huwa hauonyeshi dalili kwa muda mrefu. Nchini Marekani, mtu mmoja kati ya watano wenye umri wa zaidi ya miaka 12 ameathirika na HSV, na idadi kubwa ya hao waliambukizwa - karibia asilimia 90 - hawafahamu kuwa wana ugonjwa. Upimaji wa damu huweza kuonyesha uwepo wa maambukizi ya HSV, hata kama mtu bado hajaanza kuonyesha dalili. Dalili za HSV zinaweza kutibika kwa kutumia madawa ya yanayopambana na virusi kama vile acyclovir, lakini HSV hawawezi kutoka katika mwili - hawatibiki.

Makala kuu: Ukimwi

UKIMWI, Ukosefu wa Kinga Mwilini, ni matokea ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU) - Human immunodeficiency virus (HIV). UKIMWI ni ugonjwa wa zinaa hatari na usitibika ambao hushambulia mfumo wa kinga ya mwili na kumwacha mgonjwa akiwa hana hata uwezo wa kujikinga dhidi ya maambukizi madogo. Maambukizi ya VVU haimaanishi kuwa mtu ana UKIMWI. Baadhi ya watu na maambukizi ya VVU na wasionyeshe hali ya kuumwa ile inayotambulika kama UKIMWI kwa miaka kumi au zaidi. Watabibu hutumia neno UKIMWI pale mtu anapokuwa katika hatua za mwisho, zinazotishia uhai za maambukizi ya VVU.

UKIMWI uligunduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1981 miongoni mwa wanaume waliokuwa wanaingiliana (mashoga) na miongoni mwa watu waliokuwa wanajidunga sindano katika jiji la New York na California. Baadaye maambukizi mengine yaligundulika pia kusini mwa jangwa la Sahara barani Afrika. Kwa haraka UKIMWI ukawa ugonjwa wa mlipuko duniani kote ukiathiri karibia kila nchi. Mpaka mwaka 2002, ilikadiriwa kuwa watu wazima wapato milioni 38.6 na watoto milioni 3.2 duania kote wanaishi na VVU au UKIMWI. Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO, limekadiria kuwa kutoka mwaka 1981 mpaka mwisho wa mwaka 2002 watu karibia milioni 20 walikuwa wamekufa kutokana na UKIMWI. Kiasi cha hao milioni 4.5 walikuwa ni watoto wenye umri wa chini ya miaka 15.

Wakati VVU wanaweza kuenezwa kwa njia nyingine, kujamiiana ndiyo njia hasa ya maambukizi ya virusi hivi. Wanawake ambao wameathirika na virusi vya UKIMWI wanaweza kumwambukiza mtoto wakati wa ujauzito, kujifungua, au mara kadhaa wakati wa kuwanyonyesha. Njia mbadala ya kupunguza makali ya VVU ni pamoja na kutumia madawa yanayozuia kuzaliana kwa VVU (protease inhibitors), ambayo husaidia kwa kiasi kikubwa kurefu maisha.

Pamoja na kuenea kwa elimu juu ya ugonjwa huu, CDC wamekadiria kuna maambukizi mapya 40,000 kila mwaka Marekani na kuwa kwa ujumla kati ya Waamerika 800,000 hadi 900,000 wameambukizwa VVU.

Dutu za Sehemu za Siri

[hariri | hariri chanzo]

Dutu huota katika uume na katika eneo la kuzunguka uke na mkunduni. Husababishwa na kundi la virusi lifahamikalo kama human papillomavirus (HPV) ambao husambazwa wakati wa kujamiiana. CDC wamekadiria kuwa kuna maambukizi mapya ya dutu milioni 5.5 nchini Marekani kila mwaka. Dutu za sehemu za siri zinaweza kutibiwa na kuondolewa kwa upasuaji mdogo. Aina fulani ya HPV ambao husababisha maambukizi katika sehemu za siri wanaweza pia kusababisha kansa ya mlango wa uzazi (cervical cancer).

Trikomonasi

[hariri | hariri chanzo]

Trikomonasi husababishwa na maambukizi ya protozoa anayefahamika kisayansi kama Trichomonas vaginalis. Ugonjwa huu husababisha muwasho na karaha katika uke kwa wanawake na katika mfereji wa mkojo kwa wanaume. Trichomonasi huweza kutibiwa kwa urahisi na antibaotiki. CDC wamekadiria kuwa Waamerika milioni tano huambukizwa trikomonasi kila mwaka.

Kuzuia na kudhibiti maambukizi

[hariri | hariri chanzo]

Tofauti na magonjwa mengine hatari, hatua rahisi zinaweza kutumika kuzuia maambukizi ya magonjwa ya zinaa.

Hatua ambayo ni madhubuti kuliko zote ni kuepuka ngono kabisa. Bila ya kukutana kimwili hakuna uwezekano wa kupata maambukizi ya zinaa.

Kuwa na mwenzi mmoja tu katika ndoa na kwa wale wanaojiingiza katika mahusiano pia husaidia kupunguza hatari ya maambukizi.

Kondomu inakinga dhidi ya maambukizi hayo lakini si kinga kamili kwa asilimia mia moja. Kondomu huvaliwa kwenye uume au kwenye uke na huwa kama kizuizi kwa vijidudu vinavyosababisha magonjwa ya zinaa. Hata hivyo kondomu huwa haifuniki sehemu yote ya siri ambayo hukutana wakati wa kufanya ngono, na uwezekano wa kupata maambukizi ya zinaa bado upo, hasa malengelenge na dutu.

Uchunguzi wa awali na matibabu kamili huzuia madhara zaidi ya maambukizi ya zinaa; wakati huohuo huzuia uambukizaji kati ya mtu mmoja kwenda kwa mwingine. Hii ni muhimu sana kwa magonjwa ya zinaa ambayo huwa hayaonyeshi dalili, kwa sababu wale walioambukizwa huwa hawajui kuwa wana hatari ya kuwaambukiza wenzi wao.

Matibabu yote lazima yafuatwe hata kama matumizi ya awali ya dawa yalipelekea dalili zote kutoweka. Maambukizi yanaweza kuendelea bila ya kuwa na dalili na hivyo kupelekea aliyeambukizwa bila kujua kusambaza ugonjwa.

Mwenendo katika maambukizi ya zinaa

[hariri | hariri chanzo]

Wakati wowote katika historia, kushamiri na kuongezeka kwa magonjwa ya zinaa huakisi mabadiliko katika sayansi na jamii. Kwa mfano, katika nchi nyingi duniani, kuenea kwa magonjwa ya zinaa kuliongezeka wakati na baada ya vita vikuu vya pili (1939-1945), wakati wanajeshi walipokuwa kwa kipindi kirefu mbali na nyumbani kwao na kujihusisha katika ngono na watu tofauti ambao wengi wao walikuwa wana maambukizo ya zinaa. Wakati antibaotiki - penicillin, ilipopatikana miaka baadaye, nchi hizohizo zilishuhudia upunguaji wa maambukizi.

Hata hivyo kuanzia miaka ya 1950, huko Marekani kisonono kilianza kuenea kutokana na kuongezeka kwa tamaa za ngono. Vijidudu vya ugonjwa viliunda ukinzani dhidi ya penicillin, na mpaka miaka ya 1970 na 1980 ugonjwa ulifikia hatua ya kuwa ugonjwa wa mlipuko kwa vijana na watu wa umri wa kati.

Kuingia kwa VVU katika jamii ya binadamu kumepelekea janga la kimataifa la UKIMWI ambalo lilianza katika miaka ya 1980 na kuendelea hadi leo hii.

Majanga ya magonjwa ya zinaa yanaendelea, hata pamoja na utumiaji wa kondomu ambao umeongezeka tangu kuanza kwa UKIMWI. Maafisa wa afya wanaamini kuna mambo mengi yanayowezekana kuwa yanachangia kuongezeka kwa maambukizi ya magonjwa ya zinaa. Miongoni mwao ni mienendo ya tabia hatarishi. Katika miongo kadhaa iliyopita, umri ambao watu hufanya ngono kwa mara ya kwanza umepungua, wakati wastani wa wenzi wa kimapenzi ambao mtu hufanya nao ngono katika kipindi cha maisha yake umeongezeka. Kwa pamoja mienendo hii huongeza hatari ya kupata magonjwa ya zinaa.

Angalia Pia

[hariri | hariri chanzo]
  1. "AIDSinfo". UNAIDS. Iliwekwa mnamo 4 Machi 2013.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  1. Nevid, Jeffrey S.(1998). Choices: Sex in the Age of STDs, 2nd Edition. Allyn and Bacon
  2. Marr, Lisa, M.D. Sexually Transmitted Diseases: A Physician Tells You What You Need to Know. Johns Hopkins University Press, 1999.

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]