Mkoa wa Kigoma
Mkoa wa Kigoma |
|
Mahali pa Mkoa wa Kigoma katika Tanzania | |
Majiranukta: 4°53′S 29°40′E / 4.883°S 29.667°E | |
Nchi | Tanzania |
---|---|
Wilaya | 8 |
Makao makuu | Kigoma Ujiji |
Serikali | |
- Mkuu wa Mkoa | Rtd Commissioner Thobias Emiry Andengenye |
Eneo | |
- Jumla | 46,066 km² |
- Kavu | 37,037 km² |
- Maji | 8,029 km² |
Idadi ya wakazi (2022) | |
- Wakazi kwa ujumla | 2,470,967 |
Tovuti: kigoma.go.tz |
Mkoa wa Kigoma ni mmojawapo kati ya mikoa 31 ya Tanzania wenye postikodi namba 47000.
Umepakana na Burundi na Mkoa wa Kagera upande wa Kaskazini, mikoa ya Shinyanga na Tabora upande wa mashariki na Mkoa wa Rukwa upande wa kusini. Magharibi umepakana na Ziwa Tanganyika penye mpaka na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Jiografia
[hariri | hariri chanzo]Mkoa una eneo la km² 45,066 (sawa na 4.8% ya eneo lote la Tanzania) ikiwa km² 8,029 ndizo maji ya ndani (hasa Ziwa Tanganyika) na km² 37,037 ndizo nchi kavu.
Takriban robo ya eneo la mkoa wa Kigoma hutumika kwa kilimo na ufugaji, karibu nusu ni misitu.
Kwa ujumla eneo la mkoa ni tambarare ya juu inayoanza kwenye mita 800 juu ya UB karibu na Ziwa Tanganyika na kupanda hadi mita 1,750.
Mito mikubwa ndani ya mkoa wa Kigoma ni Malagarasi, Luiche, Ruchugi na Rugufu.
Hifadhi za wanyama na za kihistoria
[hariri | hariri chanzo]Kuna maeneo mawili yenye sokwe: ndipo Hifadhi ya Taifa ya Gombe (alikofanya utafiti wake mwanabiolojia Jane Goddall) na Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Mahale. Pia kuna Pori la Akiba la Moyowosi ambalo makao yake makuu yapo katika kijiji cha Kifura, Wilaya ya Kibondo.
Utawala
[hariri | hariri chanzo]Makao makuu ya mkoa ni Kigoma.
Mji wa Ujiji ulioko karibu na Kigoma mjini ndio mji wa kale zaidi katika Tanzania ya Magharibi; ndipo penye makumbusho ya David Livingstone.
Kuna wilaya nane ambazo ukubwa wa eneo na idadi ya wakazi katika sensa ya mwaka 2022 [1] ni kama ifuatavyo:
Wilaya au manispaa | Eneo km² | Wakazi kufuatana na sensa ya mwaka 2022 [2] | Kata | |
---|---|---|---|---|
1 | Buhigwe | 9,324 | 240,005 | 15 |
2 | Kakonko | 9,324 | 178,419 | 11 |
3 | Kasulu Mjini | 2,128 | 238,321 | 9 |
4 | Kasulu Vijijini | 7,196 | 537,767 | 19 |
5 | Kibondo | 16,058 | 362,922 | 13 |
6 | Kigoma Mjini | 93 | 232,388 | 19 |
7 | Kigoma Vijijini | 968 | 222,792 | 11 |
8 | Uvinza | 9,324 | 458,353 | 14 |
Jumla | 45,066 | 2,470,967 | 121 |
Wakazi
[hariri | hariri chanzo]Kadiri ya sensa ya mwaka 2022 wakazi walifikia kuwa 2,470,967 [3] kutoka 2.127.930 wakati wa sensa ya mwaka 2012.
Kabila kubwa ni Waha, likifuatwa na Wamanyema, Wabembe na Watongwe. Kuna pia Wavinza, Wanyamwezi, Wasukuma, Wafipa na watu wenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda na Burundi.
Idadi au msongamano wa watu katika maeneo ya mkoa huo imetegemea sana shughuli zinazofanyika kama vile kilimo na uvuvi pamoja na kupatikana kwa nzi aina ya ndorobo: penye ndorobo wengi huwa na watu wachache.
Uchumi na mawasiliano
[hariri | hariri chanzo]Mkoa wa Kigoma bado hauna maendeleo yanayolingana na mazingira yake. Hali ya barabara na mawasiliano mengine ni mbaya. Umbali hadi Dar es Salaam ni km 1316, hadi Mwanza 830, hadi Arusha 1204. Ipo barabara nzuri ya lami kuanzia wilaya ya Kaliua (mkoa wa Tabora) kupitia Uvinza, Malagarasi, Nguruka, Kaziramimba hadi Kigoma mjini, isipokuwa kipande cha kilomita 400 ni cha muramu ambayo nayo inapitika vizuri kama si kipindi cha mvua nyingi za uharibifu.
Usafiri muhimu ni reli kutoka Kigoma kwenda Dar es Salaam kupitia Tabora na Dodoma. Isipokuwa reli hii imeshazeeka kutokana na kujengwa zamani za Afrika ya Mashariki ya Kijerumani kabla ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Treni (gari moshi) zake huchelewachelewa kwa kuchukua muda mrefu. Wakati wa mvua inatokea ya kwamba mawasiliano yanavurugika.
Uwanja wa ndege wa Kigoma unashughulika na shirika la ndege la Tanzania lenye ndege nne zinazofanya safari kwa sasa nchi nzima na usafiri ni wa uhakika, pia yapo mashirika madogo yanyofanya shughuli zake kama auric air, nyingi zikiwa za kubeba watalii.Shukrani za kipekee zimwendee Rais wa nne(Mh Jakaya Mrisho Kikwete) wa Jamhuri ya Muungano aliepigana kiume kuufungua mkoa wa kigoma kwa njia ya mawasiliano ya barabara.
Takribani 85% ya wakazi wote hutegema kilimo, walio wengi kilimo cha kujitegemea tu, tena cha jembe la mkono.
Kuongezeka kwa wakimbizi kutoka nchi jirani na kukua kwa makambi kulikuwa tatizo kubwa.
Majimbo ya bunge
[hariri | hariri chanzo]Wakati wa uchaguzi mkuu wa Tanzania mwaka 2015 mkoa huu ulikuwa na majimbo ya uchaguzi yafuatayo:
- Buyungu : mbunge ni Bilago Samson (Chadema)
- Kasulu Mjini : mbunge ni Daniel Nsanzugwako (CCM)
- Kasulu Vijijini : mbunge ni Augustine (CCM)
- Kigoma Kaskazini : mbunge ni Peter Serukamba (CCM)
- Kigoma Kusini/Uvinza : mbunge ni Hasna Mwilima (CCM)
- Kigoma Mjini : mbunge ni Zitto Z. Kabwe (ACT-Wazalendo)
- Manyovu : mbunge ni Albert Ntabaliba (CCM)
- Muhambwe : mbunge ni Atashasta Justus Nditiye (CCM)
Tazama pia
[hariri | hariri chanzo]Marejeo
[hariri | hariri chanzo]Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- (Kiingereza) Sensa ya 2002 Kigoma Region Homepage for the 2002 Tanzania National Census*Serikali ya Tanzania Tanzanian Government Directory DatabaseIlihifadhiwa 15 Desemba 2003 kwenye Wayback Machine.
- (Kiingereza)Mkoa wa Kigoma - Taarifa ya kijamii na kiuchumi [1]
Arusha | Dar es Salaam | Dodoma | Geita | Iringa | Kagera | Katavi | Kigoma | Kilimanjaro | Lindi | Manyara | Mara | Mbeya | Morogoro | Mtwara | Mwanza | Njombe | Pemba Kaskazini | Pemba Kusini | Pwani | Rukwa | Ruvuma | Shinyanga | Simiyu | Singida | Songwe | Tabora | Tanga | Unguja Kaskazini | Unguja Kusini | Unguja Mjini Magharibi |
Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Kigoma bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Mkoa wa Kigoma kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. Tafadhali usiingize majina ya maafisa au viongozi wa sasa maana wanabadilika mno. |