Kitabu cha Mormoni
Kitabu cha Mormoni ni mwandiko wa kidini wa jumuiya ya Wamormoni walioitwa kufuatana na kitabu hiki. Wenyewe huamini kuwa ni kitabu kitakatifu chenye neno la Mungu. Jina la Mormoni lamtaja nabii na kiongozi wa kidini anayetambulishwa mle kama mhariri wa kitabu. Kitabu cha Mormoni kikatolewa mwaka 1830 na Mwamerika Joseph Smith, Kijana aliyedai kuwa alitafsiri kitabu kutoka kwa mabamba ya dhahabu aliyopewa na malaika wa Mungu.
Historia ndani ya Kitabu cha Mormoni [hariri]
Kufuatana na taarifa za Kitabu watu walihamia kutoka nchi za Biblia mara tatu kwenda Amerika.
Kundi la kwanza walikuwa Wajared walioondoka Mesopotamia baada ya kukwama kwa mnara wa Babeli.
Mnamo mwaka 600 KK kundi la Wayahudi walioongozwa na nabii Lehi waliondoka Yerusalemu kabla ya mji kuangamizwa na Babeli wakajenga jahazi kubwa na kufika katika nchi mpya. Baada ya kifo cha Lehi wafuasi wa wanawe Nephi na Laman walianza kugombana na kuwa makabila mawili maadui.
Wanephi walikutana baadaye na wafuasi wa Mulek aliyekuwa mwana wa mfalme Zedekiya wa Yuda waliokimbia wakati wa anguko la Yerusalemu wa 587 KK.
Kitabu cha Mormoni chaenedelea kueleza jinsi Yesu aliwatembelea Wanephi baada ya ufufuo wake na kuwapa mafundisho ya hotuba ya mlimani pamoja na chakula cha Bwana.
Wanephi na Walaman waliungana baadaye kwa karne kadhaa na kuishi kwa amani lakini amani hii ikavurugika na Wanephi waliangamizwa kabisa katika vita kali. Kabla ya mwisho wa taifa Mormoni mnamo mwaka 400 BK alipokea maagizo ya Mungu kukusanya habari zote na kuziandika kwa mabamba ya dhahabu yaliyofichwa mahali alipoyakuta Joseph Smith.
Historia au riwaya? [hariri]
Nje ya Wamormoni habari hizi hutazamiwa kuwa si ya kihistoria. Wataalamu wasio Wamormoni huamini ya kwamba Joseph Smith alitunga mwenyewe taarifa hizi pamoja na hadithi ya mabamba ya dhahabu. Smith mwenyewe alieleza ya kwamba alirudisha mabamba ya maandiko kwa malaika huyu baada ya kuyatafsiri.
Hadi leo Kitabu cha Mormoni kimetafsiriwa katika lugha 72 za dunia.