Misri ya Kale
Misri ya Kale ni ustaarabu uliokuwepo Afrika kaskazini, sambamba na mto Naili, kuanzia kwenye delta au mdomo wa Naili, toka kaskazini mwa Misri kwenda kusini hadi Jebel Barkal, kwenye maporomoko ya nne, wakati wa kupanuka kwake (Karne ya 15 KK).
Ustaarabu huo ulidumu kwa karibu milenia tatu, toka takribani mwaka 3200 KK hadi mwaka 30 KK nchi ilipovamiwa na Waroma na kuwa sehemu ya Dola la Roma. Historia ya kisiasa hutazamwa kuanza na Farao Menes mnamo 3200 KK na kwisha na uvamizi wa Wagiriki chini ya Aleksander Mkuu mnamo 332 KK. Kinachofuata kilikuwa kipindi cha Misri kama nchi ya kujitegemea chini ya mafarao Wagiriki (nasaba ya Ptolemaio) hadi kuvamiwa na Waroma na kuwa jimbo la Dola la Roma.
Uti wa mgongo wa Misri ya Kale ulikuwa mto Naili. Sehemu kubwa ya nchi hiyo ni jangwa lakini umwagiliaji wa mashamba kwa njia ya maji ya mto huo ulileta mazao mazuri yaliyolisha watu wengi.
Mahitaji ya kupanga na kutunza mifereji pamoja na mitambo ya umwagiliaji na kusimamia ugawaji wa maji yalisaidia kutokea kwa vyanzo vya hisabati na mwandiko. Mwandiko wa Misri ulikuwa hiroglifi zilizokuwa aina ya mwandishi wa picha.
Dini ya Misri ilitarajia maisha baada ya kifo ambayo yanapaswa kuandaliwa na watu wakati wa maisha haya.
Wafalme, walioitwa Mafarao, walijengewa makaburi makubwa sana na piramidi zao ni kati ya makaburi makubwa kabisa duniani.
Vipindi vya historia ya Misri ya Kale
[hariri | hariri chanzo]Historia ya Misri hugawiwa kufuatana na nasaba za wafalme wake ambao kwa jumla zilikuwa 31. Kuna ugawaji wa kimsingi kwa vipindi vikuu vitatu:
- Himaya ya Kale ya Misri (3200 KK - 2100 KK)
- Himaya ya Kati ya Misri (2100 KK - 1500 KK)
- Himaya Mpya ya Misri (1500 KK - 332 KK)
Siku hizi wanahistoria wamezoea ugawaji wa undani zaidi, ilhali miaka ya kuanza na kuishia mara nyingi hayana uhakika.
- Historia ya awali ya Misri: 4000 KK hivi
- Kipindi kabla ya maungano ya Kusini na Kaskazini: ca. 4000 KK – 3100 KK
- Kipindi cha nasaba za kwanza: 3100 KK– 2700 KK (nasaba 1 na 2)
- Himaya ya Kale: 2686 KK –2181 KK (nasaba ya 3 – 6)
- Kipindi cha kwanza cha mpito: 2216–2137 KK hivi (nasaba ya 7 - 11)
- Himaya ya Kati: 2137–1781 KK hivi (nasaba ya 11 - 12)
- Kipindi cha pili cha mpito: 1648–1550 KK hivi (nasaba ya 13 – 17)
- Himaya Mpya: 1550–1070 KK hivi (nasaba ya 18 – 20)
- Kipindi cha tatu cha mpito: 1070–664 KK hivi (nasaba ya 21 - 25)
- Kipindi cha mwisho: 664–332 KK hivi (nasaba ya 26 – 31)
- Kipindi cha Wagiriki: 332 KK - 395 n. Chr (nasaba ya Ptolemayo)
Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Misri ya Kale kama enzi zake au matokeo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |