Nenda kwa yaliyomo

Osama bin Laden

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Osama Bin Laden)
Osama bin Laden
Osama Bin Laden
Osama Bin Laden
Jina la kuzaliwa 'Osama bin Mohammed bin Awad bin Laden
Alizaliwa 10 Machi 1957
Alikufa 2 Mei 2011
Nchi Saudia
Kazi yake Gaidi

Osama bin Mohammed bin Awad bin Laden (kwa Kiarabu: أسامة بن محمد بن عوض بن لادن‎ ʾusāmah bin muḥammad bin ʿawaḍ bin lādin; 10 Machi 19572 Mei 2011) alikuwa mpiganaji na mwanzilishi na kiongozi wa kundi la kigaidi la Al Qaida mnamo 1988[1].

Osama bin Laden

Aliamini kwamba Waislamu wanapaswa kuua raia na wanajeshi wa Marekani na nchi washirika hadi wajiondoe katika kuunga mkono Israeli na kuondoa majeshi yao kutoka katika nchi za Kiislamu.[2][3]

Alipelekwa mahakamani katika mahakama ya shirikisho ya Marekani kwa kuhusika kwake katika mashambulio ya mabomu ya balozi za Marekani mwaka 1998 huko Dar es Salaam, Tanzania na Nairobi, Kenya, na alikuwa kwenye orodha ya FBI ya Marekani ya Watu Kumi Wanaotafutwa Zaidi.

Anatazamwa na watu wengi kama gaidi aliyesababisha vifo vya maelfu ya watu katika mashambulio ya kigaidi ya 7 Agosti 1998 katika Afrika ya Mashariki (Nairobi na Dar es Salaam) na hasa shambulio la 11 Septemba 2001 huko Marekani.

Kumbe wengine wanamwona kama mtetezi wa haki za Waislamu dhidi ya mashambulio ya Marekani akitumia mbinu za jihadi.

Aliuawa na wanajeshi wa Marekani tarehe 2 Mei 2011 nchini Pakistan alipokuwa amefichama.

Familia na kazi

[hariri | hariri chanzo]

Osama bin Laden alizaliwa katika familia tajiri ya Bin Laden wa Saudia. Baada ya masomo yake kwenye chuo kikuu, yasiyojulikana kama aliyamaliza, alifanya kazi katika kampuni za ujenzi za familia yake.

Afghanistan

[hariri | hariri chanzo]

Tangu uvamizi wa Umoja wa Kisovyeti katika Afghanistan mwaka 1979 alikusanya pesa kwa ajili ya mujahidin wa Afghanistan akawasaidia pia vijana Waarabu waliotaka kujiunga na mujahedin katika mapambano dhidi ya jeshi la Kisoveti na serikali ya Afghanistan.

Mwaka 1984 alihamia Pakistan kwa shabaha ya kuongoza wapiganaji wa kujitolea kutoka Uarabuni. Mwaka 1986 alichukua pia wanawake na watoto wake kutoka Saudia na kwa miaka kadhaa alikaa nao Pakistan. Mwenyewe alianza kushiriki katika mashumbulio dhidi ya jeshi la Kisovyeti pamoja na vikundi vidogo vya Waarabu.

Kuanzishwa kwa Al Qaida

[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 1988 jeshi la Kisovyeti lilianza kuondoka Afghanistan. Viongozi wa mujahedin Waarabu katika Afghanistan waliokuwa Bin Laden na Wamisri kama Aiman az-Zawahiri na Abdullah Azzam walishauriana namna ya kuendeleza jihadi zao. Walitofautiana kama kulenga serikali za nchi za Kiarabu zisizokuwa za kidini kama huko Misri au kuhamia Palestina au kupeleka jihadi yao kwenda jamhuri za Kisovyeti za Asia ya Kati kama Tajikistan au Kirgistan zilizokaliwa na Waislamu.

Mkutano huo ulifanyika katika kambi lililoitwa "al-qaida" kwa Kiarabu. [4]. Hilo lilikuwa baadaye jina la kundi lililoongozwa na bin Laden.

Sehemu ya mujahidin Waarabu walimfuata bin Ladin katika kushambulia jeshi la serikali ya Afghanistan iliyoendelea kujitetea hata baada ya kuondoka kwa Wasovyeti. Mwaka bin Laden alipotembelea tena Saudia akashauriana na serikali kuendelea namna gani. Alipopewa jibu heri arudi kwake akatii akarudi pamoja na kikosi chake.

Saudia 1989 - 1992 na Sudan hadi 1995

[hariri | hariri chanzo]

Baada ya kurudi Saudia aliishi Madina na Jiddah akaingia tena katika kampuni ya familia yake na kusimamia miradi ya ujenzi wa barabara. Wengi walimtazama kama shujaa aliyewajibika kwa kiasi kikubwa kufukuza Umoja wa Kisovyeti kutoka Afghanistan.

Mwaka 1990 serikali ya Saddam Hussein wa Irak ilivamia Kuwait. Serikali ya Saudia iliogopa mashambUlio mengine dhidi ya Saudia ikakubali kufika kwa wanajeshi wa Marekani nchini. Osama aliona hatua hiYO kama marufuku kwa sababu aliamini Uarabuni ni nchi takatifu kutokana na mahali patakatifu pa Kiislamu pa Makka na Madina akajitolea kukusanya mujahidin 100,000 kama ulinzi dhidi ya Saddam badala ya kuwaruhusu Wamarekani. Lakini serikali ilikataa.

Wanajeshi kadhaa wa Marekani waliendelea kukaa Saudia hata baada ya ushindi juu ya Irak katika vita. Hapo bin Laden alianza kupinga waziwazi siasa ya serikali yake. Kutokana na ugomvi huO aliamua kuhamia nchi ya Sudan alipotumia utajiri wake kuanzisha miradi, mashamba na makampuni lakini pia makambi kwa ajili ya vijana wenye itikadi kali ya Kiislamu waliomfuata na kuhamia Sudan. Alikaa karibu na viongozi wa kundi la Al-Jihad ya Misri waliowahi kushirikiana naye Afghanistan na kupambana dhidi ya serikali ya rais Hosni Mubarak.

Kukaa kwa Wamarekani katika Saudia na kuingilia kwa Marekani katika vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Somalia tangu Desemba 1992 kwa niaba ya Umoja wa Mataifa ilileta imani kati ya Waislamu wakali kuwa nchi za Magharibi wanaendesha upya vita ya misalaba.

Katika miaka iliyofuata yalitokea mashambulio mbalimbali dhidi ya wanajeshi na taasisi za Kimarekani yaliyoendeshwa na wanajihadi mbalimbali kama vile huko Yemen 1992 na shambulio la 1993 dhidi ya World Trade Center mjini New York. Haijulikani hadi leo kwa kiasi gani Osama na Al Qaida yalishiriki katika mipango hiyo lakini watendaji walikuwa watu wenye mawasiliano na Bin Laden. Pia alitoa pesa kwa vita ya harakati ya kijihadi ya Groupe Islamique Armee nchini Algeria na kuhubiri dhidi ya serikali ya Saudia. Hapo Saudia ilifuta uraia wake na kukamata mali yake nchini. Familia ya bin Laden ilitangaza ya kwamba walimfukuza katika ukoo.

Mwaka 1995 wanajihadi wa Al-Jihad ya Misri walijaribu kumwua rais Mubarak wa Misri kwenye mkutano wa Umoja wa Muungano wa Afrika mjini Addis Ababa. Hapo Umoja wa Mataifa ilidai Sudan kuwakabidhi kwa mahakama watendaji waliotoka huko na kutangaza hatua dhidi ya taifa hilo. Sudan ilijaribu kuepukana na kuadhibiwa na jumuiya ya kimataifa haikutaka kuonekana kama msaidzi wa ugaidi ikalazimisha wanajihadi wa kimataifa kuondoka. Tarehe 18 Mei 1996 Osama bin Laden alipelekwa tena Afghanistan.

Afghanistan 1996–2001

[hariri | hariri chanzo]

Afghanistan ilikuwa katika hali ya vita ya wenyewe kwa wenyewe na miezi michache baada ya kufika kwa Osama kundi la Taliban lilivamia mji mkuu wa Kabul na kutangaza Emirati ya Afghanistan likaendelea kutawala sehemu kubwa ya nchi.

Katika maeneo yaliyokuwa chini ya serikali ya Taliban Osama aliweza kuanzisha makambi mbalimbali alipopokea na kufunza wanajihadi kutoka nchi mbalimbali. Pamoja na Aiman az-Zawahiri alitoa tamko la fatwa tarehe 23 Februari 1998 waliposema: "Kuwaua Wamarekani na wanaoshikamana nao -kama ni wanajeshi au raia- ni wajibu wa kila Mwislamu mwenye uwezo wa kuyatekeleza katika nchi yoyote kwa kusudi la kuleta ukombozi wa msikiti wa al Aqsa na Masjid al-Haram (msikiti wa Makka) na kuwafukuza wanajeshi wao kutoka nchi zote za Uislamu. Kwa msaada wa Mungu tunamwita kila Mwislamu anayemwamini Mungu kutekeleza amri ya Mungu na kuwaua Wamarekani na kupora pesa zao kila mahali anapoikuta".

Mwaka uleule wa 1998 mabomu mawili yalipuliwa kwenye mashambulio ya kigaidi ya 7 Agosti 1998 katika Afrika ya Mashariki dhidi ya balozi za Marekani huko Nairobi na Dar es Salaam yaliyoua zaidi ya watu 300 na kuwajeruhi maelfu. Serikali ya Marekani ilijaribu kuwashawishi viongozi wa Taliban kuwakabidhi bin Laden lakini hadi 2001 badi hawakufikia mapatano.

Tarehe 12 Oktoba 2000 wanajihadi wa al Qaida walishambulia manowari USS Cole nchini Yemen. Tarehe 9 Septemba 2001 wapiganaji wa al Qaida walimwua mpinzani wa Taliban Ahmad Shah Massoud kwa bomu.

Tendo hilo lilifuatwa na shambulio la 11 Septemba 2001 katika Marekani lililoua takriban watu 3,000. Marekani ilidai tena Afghanistan imkabidhi bin Laden lakini viongozi wa Taliban walikataa wakadai kuonyeshwa uthibitisho. Rais George W. Bush wa Marekani alijibu kwa kushambulia Afganistan tarehe 7 Oktoba 2001; baada ya kutekwa kwa Kabul bin Laden alikimbia kwenye mapango ya milima ya Tora Bora na kutoka huko katika maeneo ya Pakistan kaskazini-mashariki ambako serikali ya taifa ilikuwa na athira ndogo.

Jitihada za Wamarekani kumkamata zilikuwa bila mafanikio. Osama bin Laden aliendelea kujificha nchini Pakistan, labda kwa msaada wa sehemu ya huduma ya usalama ya kijeshi ya nchi hiyo. Alitoa matangazo mbalimbali kwa njia ya kanda za video zilizosambazwa duniani kwa njia ya intaneti.

Aliuawa mjini Abbottabad, Pakistan, tarehe 2 Mei 2011 mnamo saa saba usiku [5][6][7] aliposhambuliwa na kikosi maalumu cha jeshi la Marekani.

  1. Michael Scheuer, Through Our Enemies' Eyes, p. 110
  2. "BIN LADEN'S FATWA". PBS. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo Oktoba 31, 2001. Iliwekwa mnamo Septemba 8, 2017.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  3. "Online NewsHour: Al Qaeda's 1998 Fatwa". PBS. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo Septemba 1, 2006. Iliwekwa mnamo 2006-08-21.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  4. القاعدة‎ al qaida inamaanisha "kambi" katika lugha ya Kiarabu
  5. Kutegemeana na kanda la wakati, saa 7 ni wakati wa Pakistan
  6. Miller, Greg. "CIA spied on bin Laden from safe house", May 5, 2011. Retrieved on May 6, 2011. Archived from the original on May 10, 2011. 
  7. Cooper, Helene. "Obama Announces Killing of Osama bin Laden", The New York Times, May 1, 2011. Retrieved on May 1, 2011. Archived from the original on May 2, 2011.