Laozi
Laozi (kwa Kichina 老子, Lǎo zi, pia Laotse, Lao-Tse au Lao-tzu) ni mmoja wa wanafalsafa mashuhuri wa China aliyeishi katika karne ya 6 KK. Laozi si jina bali cheo kama "mwalimu".
Anajulikana hasa kutokana na kitabu cha Tao te jing kinachotajwa kama kazi yake.
Anatazamwa kama mwanzilishi na mwalimu mkuu wa Utao ambao ni fundisho linalopatikana kama falsafa na pia kama dini. Katika matawi ya kidini ya Utao anatazamwa kama mungu mmojawapo.
Jina na maisha
Vyanzo
Hali halisi hakuna habari za kihistoria zenye uhakika juu ya Laozi lakini kuna masimulizi mengi juu yake.
Marejeo ya kwanza yapo katika maandiko ya mwanahistoria Sima Qian aliyeishi mnamo 145-86 KK na aliyekusanya hadithi tofautitofauti juu ya maisha ya Laozi. Kutokana na tofauti za hadithi hizo Sima Qian mwenyewe alisema hakuwa na uhakika kama Laozi aliishi kweli. Kuna wataalamu wanaodai ya kwamba ni habari za walimu mbalimbali zilizounganishwa kwa jina la "Laozi".
- Katika hadithi ya kwanza Laozi anasemekana aliishi wakati wa Konfusio (551-479 KK). Jina la familia lilikuwa Li (李 "plamu") na jina la kwanza lilikuwa Er (耳 "sikio") au Dan (聃 "sikio refu"). Alikuwa afisa katika kumbukumbu ya ikulu ya kifalme akaandika kitabu, halafu akaondoka kuelekea magharibi.
- Katika hadithi ya pili aliitwa Lao Laizi (老莱子 "mwalimu mzee") aliyeishi wakati wa Konfusio aliyeandika kitabu chenye sehemu 15.
- Katika hadithi ya tatu aliitwa Lao Dan (老聃 "Mzee sikio refu") aliyekuwa mwanahistoria mtaalamu wa nyota kwenye ikulu ya mtawala kabaila Xiàn (獻公) wa dola la Qin takriban miaka 150 baada ya Konfusio.[1][2]
Ushahidi wa kale wa kitabu chake Tao te jing unapatikana kwenye bao za mwanzi za karne ya 4 KK. Wanaakiolojia walikuta bao 800 zenye maandishi katika kaburi moja na sehemu za maandishi zinalingana na maneno ya Tao te Jing jinsi inavyojulikana kutokana na nakala za baadaye.[3] Kwa hiyo mafundisho ambayo baadaye yalijulikana chini ya jina la Laozi yamethibitishwa kwa zamani ile.
Sehemu muhimu ya mafundisho hayo ni wito wa kutambua "tao" ambayo ni kanuni au utaratibu wa msingi wa ulimwengu wote, pia chanzo cha kila kitu; Utao unalenga maisha yanayolingana na kanuni hii ya tao.
Hadithi ya Laozi
Hadithi juu ya maisha ya Laozi iliyosimuliwa mara nyingi katika karne zilizofuata ni hii:
Laozi alizaliwa katika wilaya ya Ku (苦縣 / 苦县 Kǔ Xiàn) ya dola la Chu katika jimbo la Henan ya leo. Jina lake likawa Li (李) Er (耳 ‚ sikio‘); aliitwa mara nyingi Boyang (伯陽 / 伯阳) au pia Lao Dan (老聃 ‚Mzee sikio refu‘).
Alifanya kazi ya mwandishi katika maktaba ya kumbukumbu ya nasaba ya Zhou. Alipoona hali ya milki kushuka chini na fujo kuenea aliondoka kwa kupanda nyati-maji.
Alipofika kwenye mipaka ya magharibi ya milki alipawa kuvuka milima na hapa mlinzi wa mpaka alimkaribisha kukaa kwake akamwomba kuandika hekima yake. Laozi aliandika hapa mafundisho ya Tao te jing. Baadaye aliendelea kuelekea magharibi akapotea asipatikane tena.
Masimulizi ya baadaye yalisisitiza ya kwamba aliendelea kufundisha nje ya China bila kutambuliwa.[4] Baada ya kufika kwa wahubiri wa Ubuddha nchini China ya kuwa ni Laozi aliyekuwa ama mwalimu wa Buddha au hata Buddha mwenyewe.
Leo hii mazingira ya kituo cha mpakani ni mahali muhimu kwa wafuasi wa Utao kuna mahekalu mbalimbali yanayotembelewa na wahiji wengi.
Katika masimulizi hayo Laozi alioa akawa na mwana aliyeitwa Zong na kuwa mwanajeshi. Wachina wengi wanaamini ya kwamba wako wa ukoo wa huyu Zong na hivyo ukoo wa Laozi mwenyewe. [5] [6]
Laozi kama nabii na mungu
Wakati wa karne ya 2 BK chini ya utawala wa nasaba ya Han wafuasi wa Utao walianza kujumuika katika shirika zilizosambaza mafundisho ya Tao te Jing na kumbukumbu ya Laozi. Sehemu ya shirika hizi zilifundisha Utao wa kidini yaani mbinu mbalimbali kuelekea maisha yaliyokamilika kulingana na fundisho la Tao.
Mwanzoni Laozi alihubiriwa kama nabii au mtume aliyeleta mwanga wa elimu ya tao kwa binadamu. Baadaye heshima aliyopewa ilimpandisha mbinguni kama mungu kati ya miungu iliyoabudiwa. Wengine walimwona kama tao yenyewe kwa maumbile ya kibinadamu.
Laozi kama mungu alifundishwa kuwa na makao kati ya nyota za Dubu Mkubwa (lat. Ursus Maior) kwenye kitovu cha ulimwengu. Kutoka huko anashuka na kupanda juu tena kama msuluhishi kati ya dunia na mbinguni. Anaweza kutumia umbo lolote ama kubwa sana au dogo kabisa. Anaunganisha ndani yake vinyume vyote jinsi inavyoonyeshwa katika alama ya yin-yang.
Athari za Laozi
Katika historia ya China kuna mifano mingi ya kwamba watu muhimu walimrejea Laozi wakiamua kutohudumia watawala na kuepukana na nafasi za heshima na utajiri.
Wataalamu wa nadharia ya siasa waliomrejea Laozi walikaza uvumilivu katika nafasi ya uongozi na upole katika shughuli za kuendesha serikali.
Watetezi wa uhuru wa mawazo walimtaja mara nyingi Laozi kama mtangulizi wao. Amelinganishwa na waandishi wa Ulaya wa karne ya 18 waliodai eti serikali inapaswa kuchukua nafasi ndogo katika jamii ikiwaachia watu wenyewe kugundua njia za kuboresha jamii na uchumi.[7][33]
Waanakisti kama Peter Kropotkin walimwona Laozi kama mtangulizi wa mafundisho yao pia.[8]
Nukuu
Kuna nukuu nyingi zinazoaminiwa kuwa za Laozi. Hata hivyo wataalamu wengi wanaoamini ya kwamba masimulizi juu yake yametungwa karne nyingi baadaye, pamoja na kuwa na mashaka kama kweli mtu huyu aliishi, hali halisi wanasita kukubali nukuu hizi. Kazi ya nukuu zinazopatikana katika jina lake ni kama zifuatazo: [9]
- Kuwa na maisha kunapita uwezo wa maneno ya kuieleza
- Kiongozi bora ni yule ambaye watu hawana habari nyingi juu yake; akimaliza kazi yake wengine watasema "ni sisi wenyewe tuliofanya yote"
- Ongoza milki kubwa kwa mkono wa upole jinsi unavyopika samaki wadogo
- Tatizo kubwa kabisa duniani ingepata suluhisho kirahisi wakati ilikuwa bado dogo na changa.
Marejeo
- ↑ Fowler, Jeaneane (2005), An Introduction To The Philosophy And Religion Of Taoism: Pathways To Immortality, Brighton: Sussex Academic Press, pp. 342, ISBN 1-84519-085-8
- ↑ Robinet, Isabelle (1997), Taoism: Growth of a Religion, Stanford: Stanford University Press, pp. 320, ISBN 0-8047-2839-9
- ↑ "Laozi". Stanford Encyclopedia of Philosophy by Stanford University. "In late 1993, the excavation of a tomb (identified as M1) in Guodian, Jingmen city, Hubei province, has yielded among other things some 800 bamboo slips, of which 730 are inscribed, containing over 13,000 Chinese characters. Some of these, amounting to about 2,000 characters, match the Laozi. The tomb...is dated around 300 B.C.E."
- ↑ Kohn, Livia; Lafargue, Michael, eds. (1998), Lao-Tzu and the Tao-Te-Ching, Albany: State University of New York Press, pp. 320, ISBN 0-7914-3599-7
- ↑ Kenneth Scott Latourette (1934). The Chinese: their history and culture, Volume 1 (2 ed.). Macmillan. p. 191. Retrieved 8 Februari 2012. "As a necessary foundation to this bureaucracy, T'ai Tsung maintained and reenforced the state schools and the public examinations. Although his family professed descent from Lao Tzu (for the latter's reputed patronymic was likewise Li)"
- ↑ Simpkins, Annellen M.; Simpkins, C. Alexander (1999), Simple Taoism: a guide to living in balance (3rd Printing ed.), Boston: Tuttle Publishing, pp. 192, ISBN 0-8048-3173-4
- ↑ Dorn, James A. (2008), Hamowy, Ronald, ed., The Encyclopedia of Libertarianism, SAGE, p. 282, ISBN 1-4129-6580-2, retrieved 12 Mei 2010
- ↑ Kropotkin, The historical development of anarchism http://dwardmac.pitzer.edu/anarchist_archives/kropotkin/britanniaanarchy.html
- ↑ Lao Tzu, 1944. The Way of Life, an American version by Witter Bynner. Capricorn Books, New York
Viungo vya nje
- Article by Bing YeYoung "The Shamanic Origins of Laozi and Confucius" Ilihifadhiwa 26 Juni 2013 kwenye Wayback Machine.
- True Tao Home Page: articles, stories focused on practical applications of Tao teachings.
- A reconstructed portrait of Laozi, based on historical sources, in a contemporary style.
- Lao Tzu Page Ilihifadhiwa 5 Februari 2005 kwenye Wayback Machine. that provides teachings on Laozi, his life and philosophical concepts.
- A collection of resources on Laozi by Patrick Jennings: Critical Thinkers: Lao Tse & Daoism.
- Stanford Encyclopedia of Philosophy entry
- 老子 Lǎozĭ 道德經 Dàodéjīng - 拼音 Pīnyīn + 王弼 WángBì + 馬王堆 Mǎwángduī + 郭店 Guōdiàn
- Works by Lao Zi katika Project Gutenberg