Ubalehe

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Ubaleghe)
Ndevu kwa kawaida zinaanza kuota wakati wa mtoto wa kiume kubalehe.

Ubalehe (pia: Ubaleghe[1]) ni jumla ya mabadiliko ya mwili na ya roho yanayomfanya mtoto kuwa kijana halafu mtu mzima.

Ufafanuzi[hariri | hariri chanzo]

Ingawa kila mtu ni mwanamume au mwanamke tangu atungwe (kadiri alivyo na kromosomu Y au la), kabla ya kubalehe tofauti hazionekani sana, isipokuwa katika viungo vya uzazi. Kumbe muda unafika wa watoto kuanza kukomaa kijinsia: ndipo tofauti zinapojitokeza wazi.

Kutoka utotoni kuingia utu uzima kuna mabadiliko ya haraka katika viungo, hisia na roho. Kama ilivyo kwa viumbe hai wote, ustawi huo unaweza ukawahi au kuchelewa, lakini kwa kawaida unatokea kati ya umri wa miaka 12 na 16. Wasichana wanawahi kuliko wavulana, na Wazungu kuliko Waafrika, lakini mabadiliko ni yaleyale, nayo yanafanyika hatua kwa hatua.

Katika hayo, mengine yanamfurahisha kijana, lakini mengine hayampendezi, anayonea aibu hata kuyafadhaikia hasa asipoyaelewa. Bila ya shaka anahitaji msaada wa walezi aweze kukabili hayo yote bila ya kuvurugika kiasi cha kupotoka.

Kwanza mvulana anajikuta akirefuka haraka na kupata misuli mikubwa; kifua kinapanuka. Papo hapo sauti yake inaanza kupasuka na kuwa nzito, ndevu zinaweza zikaota, na vilevile [[malaika sehemu za siri, kwapani na pengine kifuani. Hali ya ngozi inakuwa ikikwaruzakwaruza hasa usoni, na chunusi hujitokeza.

Katika hatua ya mbele mabadiliko yanahusu zaidi viungo vya uzazi vinavyokua na kuanza kazi ambayo kwa kawaida kwa mvulana itaendelea moja kwa moja, kumbe kwa msichana itakoma kati ya miaka 40 na 50.

Huyo vilevile anabadilika ili kujiandaa kuwa mama. Mwili unastawisha maziwa, ukubwa na uzuri wa umbo, malaika sehemu za siri na kwapani, mabadiliko ya rangi ya uso. Hatimaye “anavunja ungo”, yaani anaanza kutokwa na damu katika tumbo la uzazi. Kwa kawaida itatokea mara moja kwa mwezi, lakini itaweza ikawahi au kuchelewa kutokana na hali yake ya mwili na ya nafsi (shughuli nyingi, mahangaiko, uhamisho n.k.).

Sababu ya damu kutoka ni kwamba, kijiyai kilichokomaa na kutoka nje ya kifuko cha vijiyai kisipopata mbegu ya mwanamume baada ya siku moja kinaharibika harakaharaka; hapo ngozi nyembamba ya tumbo la uzazi, iliyotanuka kwa damu ili kupokea na kulisha mimba, inachanikachanika na kutoa damu. Kumbe mbegu ikikifikia kijiyai, mimba inapatikana na kujishikiza kwenye kuta za tumbo la uzazi ili iendelee kukua; hapo damu haitoki na mama anaweza kujihisi mja mzito.

Mabadiliko ya mwili yanaendana na mengine ya nafsi yanayofanya tabia iwe tofauti na ile ya awali. Hisia zinabadilika kadiri mwili unavyozidi kutengeneza chachu (homoni) zinazomfanya kijana aelekee namna ya baba au mama zake.

Mvulana anajikuta akivutiwa na uzuri wa wasichana, na kupenda kuwajua zaidi, kuongea nao n.k. Anapenda kuwagombeza na kuwaonea ili aonyeshe uwezo na nguvu alivyonavyo. Katika hatua hiyo anakuwa mvivu na mzito katika kutembea na mara nyingi hajali unadhifu. Kumbe msichana anazidi kupenda sifa na kujiremba.

Akili pia inapevuka na kumfanya kijana apende kuwa na maoni maalumu kuhusu mambo mbalimbali, hata kubishana na wengine. Pia apende mabadiliko, ujuzi mpya n.k. Ndiyo sababu kijana si mwepesi kupokea mashauri na maoni ya wakubwa, asije akajisikia tena mtoto huku akipenda kutambulika amekuwa mtu mzima. Kwa ajili hiyo anatamani kufanya yale wanayoyafanya wakubwa (kuvuta sigara, kurudi nyumbani usiku n.k.), kushirikiana na rika lake na hata kujiunga na makundi ya wanaomzidi katika shughuli zao (genge, timu n.k.) ingawa pengine hazifai (uhuni, bangi n.k.).

Hatimaye kuna mabadiliko upande wa roho: kati ya mawazo mengine, kijana anajitafutia msimamo mpya kuhusu maswali makuu ya maisha: anataka kuwa na falsafa na dini yake. Shida ni kwamba usahihi wa majibu unategemea sana uadilifu wa maisha: kijana akifuata anasa, akili inapofuka na imani inapotea.

Mabadiliko ya viungo vya uzazi[hariri | hariri chanzo]

Uume (mboo) wa mvulana unakua, lakini kwa kiasi tofauti kati ya mtu na mtu. Ni muhimu kila mmoja ajipokee alivyo hata katika kiungo hicho, bila ya kuhangaika wala kuona aibu kwa sababu, eti ni kidogo.

Kusimika kwa uume si jambo jipya kwa kuwa utotoni limeshatokea kawaida kutokana na kibofu kujaa mkojo. Ila sasa linaweza kutokea kwa sababu mpya, yaani jinsia.

Muundo wa uume ni misuli aina ya sifongo yenye neva nyingi. Kukiwa na msisimko damu inajaa nafasi zilizomo na kusababisha uume utanuke na kusimama imara na wima. Kusimika kunajitokeza na kupotea haraka kutegemeana na hali iliyopo. Hali hiyo inaweza kutokea bila ya mtu kutaka, kwa mfano usiku au pia mchana kati ya watu ikimfanya aone haya.

Upande wa maadili tusisababishe hali hiyo bila ya lengo jema, kama vile kumtibu mgonjwa, kutoa ushauri nasaha au kujielimisha kuhusu jinsia. Kwa hiyo tukwepe kwa kawaida yale yote yanayoweza kusisimua, kama vile mawazo, maneno, masomo, mitazamo na vitendo mbalimbali kuhusu jinsia. Mvulana anahitaji kujifunza nidhamu ya namna hiyo.

Mashauri mengine ni kutovaa kaptura wala suruali zinazobana, na kuficha kwa adabu hali hiyo ikitokea, lakini bila ya kuiogopa wala kudhani ni dhambi.

Mapumbu yanaanza kutengeneza mbegu za kibinadamu kwa wingi sana: hizo ni ndogondogo na zina umbo kama la viluwiluwi vya chura, yaani vina vichwa na mikia tu.

Vichwa ndivyo vinavyoleta viini vya urithi wa baba. Mikia kazi yake ni kusaidia tu kusukuma mbegu kwa kuogelea ndani ya tumbo la uzazi mpaka zikutane na kijiyai cha mama, halafu inapotea ndani ya kijiyai. Mbegu zikiwa tayari zinahifadhiwa kwanza katika kifuko cha akiba, karibu na kibofu, zikisubiri msisimko wa kijinsia ili zitoke kwa njia ya uume na kuanza mashindano ya kutafuta kijiyai, zikisaidiwa na majimaji ambayo yanaitwa shahawa na kutengenezwa ndani ya kifuko. Shahawa inafuata mshipa wa mkojo bila ya kuchanganyikana nao.

Shahawa inaweza ikatoka hata nje ya tumbo la uzazi la mke, lililo shabaha yake, kwa kuwa inalenga uzazi hasa. Inaweza ikatokea k.mf. kutokana na ndoto za usiku, bila ya mtu kukusudia; huyo anaweza akazinduka mara au kutambua asubuhi tu kilichotokea. Kwa vyovyote asihangaike kwa kuwa hilo ni jambo la kawaida lililopangwa na Mungu ili kumsaidia mwanamume asiye na mwenzi. Maana mbegu zake kadiri zinavyoongezeka katika kifuko cha akiba zinataka kutoka, hivyo zinamuelekeza kwenye matendo ya kijinsia. Basi, kwa ndoto hizo mbegu zinapungua bila ya dhambi, na vishawishi vinakosa ukali wake. Ni suala la kusubiri tu na kuwa na hakika kwamba havitadumu muda mrefu kwa nguvu ileile.

Upande wa wasichana pia, kuna siku zenye mvuto mkubwa wa kijinsia, kuhusiana na mabadiliko ya kila mwezi yanayoendana na kijiyai kukomaa; inatosha kusubiri nao utapungua mapema.

Mvulana anapotokwa na shahawa kwa mara ya kwanza ni dalili ya kuwa si mtoto tena, bali ana uwezo wa kuzaa: kwa hiyo awajibike kama mtu mzima kuhusu uwezo mpya aliojaliwa. Hasa azingatie kuwa uwezo wake huo bado ni mbichi: ingawa unaweza kusababisha mimba, mimba hiyo itaendelea kwa shida au kufa kabisa.

Ubichi wake ni mkubwa zaidi upande wa nafsi, kwa kuwa mvulana hajawa tayari kubeba mzigo wa familia mpya. Ndiyo sababu asichezee uwezo huo, bali ajiandae kuwa baba safi siku za mbele: ajipatie elimu au ufundi fulani, akomae kiutu na kutunza afya yake ya mwili na ya nafsi.

Msichana afanye vilevile aweze kuwa mama bora; kumbe akijiingiza mapema katika masuala ya ngono, anahatarisha heshima yake pamoja na afya, kwa kuambukizwa maradhi yanayoweza yakasababisha utasa au kwa kuzaa kwa shida kabla ya wakati wa kufaa.

Nini ifanywe na mtu aliye katika ubalehe[hariri | hariri chanzo]

  • Kutojiingiza kwenye masuala ya ngono
  • Kutoshirikiana na makundi maovu
  • Kuepuka kukaa sehemu za giza na kutokwenda sehemu nyingine hatarishi
  • Kuzingatia usafi wa mwili na mavazi na hasa yale ya ndani
  • Kupata elimu sahihi ya afya ya uzazi kutoka kwa wazazi au watu maalumu kama madaktari na wataalamu wengine wa masuala hayo na wa maadili, kulingana pia na dini ya mhusika.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Baleghe ni pendekezo la KyT