Primata
Primata | ||||||||||
---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|
Nyani wa kawaida, kima wa Dunia ya Kale
| ||||||||||
Uainishaji wa kisayansi | ||||||||||
| ||||||||||
Ngazi za chini | ||||||||||
Nusuoda 2, oda za chini 4:
|
Primata ni jina la kitaalamu la kundi takriban spishi 400 za mamalia wanaojumlisha lemuri, nyani na sokwe wote pamoja na binadamu.
Wote huwa na mikono yenye vidole 5 na kucha na wanafanana na binadamu kwa namna fulani katika mengine kadhaa. Tofauti muhimu ni lugha.
Wanahesabiwa kuwa na vikundi au nusuoda 2:
- Haplorhini (wenye pua kavu) ni pamoja na nyani, sokwe na binadamu.
- Strepsirhini (wenye pua bichi) ni lemuri, komba na Aye-Aye.
Uenezi
[hariri | hariri chanzo]Binadamu pekee amesambaa kote duniani.
Primata wengine wanaishi hasa katika maeneo ya tropiki na nusutropiki ya Afrika na Asia. Barani Afrika wako kote na idadi kubwa ya spishi wako kusini kwa Sahara. Katika Amerika wako kati ya Meksiko na Arjentina ya kaskazini. Hawako Ulaya isipokuwa kundi moja huko Gibraltar (kusini mwa rasi ya Iberia) lakini inawezekana hao walipelekwa huko na binadamu. Vilevile hawako Asia ya Kaskazini na ya Kati, Australia na visiwa vya Pasifiki wala maeneo karibu na ncha za dunia.
Tabia
[hariri | hariri chanzo]Tabia zifuatazo zinapatikana
- mikono inafaa kwa kushika
- kucha ni bapa, ni kucha kali za kuchimba au za kujitetea; huwa na vifinyo kwenye vidole
- miguu ni muhimu zaidi kwa kutembea
- uwezo wa kunusa ni mkali sana, na hafifu zaidi kwa primates wanaofanya shughuli zao mchana
- macho ni makubwa na yote mawili yanatazama mbele, uwezo wa kuona ni wa juu
- wanazaa watoto wachache kila safari, mimba na kipindi cha kunyonyesha wadogo huchukua muda mrefu zaidi kuliko mamalia wengine wenye ukubwa sawa
- ubongo ni mkubwa kulingana na mamalia wengine
- meno ya magego si zaidi ya matatu, machonge mawili na magego madogo matatu
Ukubwa
[hariri | hariri chanzo]Wale wa nusuoda Strepsirhini kwa jumla ni wadogo kuliko Haplorhini.
Aina ndogo zaidi kati ya primata ni Lemuri-panya ya Berthe mwenye urefu wa sentimita 10 pekee na uzito wa gramu 38. Aina kubwa ni ngagi (gorilla) yenye kilogramu hadi 275,
Spishi kadhaa wana tofauti kubwa kati ya dume na jike; dume wa spishi hizo wanaweza kuwa na uzito mara mbili kuliko jike na pia kuonyesha rangi tofauti kama nyani wa Papio hamadryas.
Viungo vya mwili
[hariri | hariri chanzo]Primata wengi hukalia miti na viungo vyao vinalingana na maisha yao. Kwa spishi nyingi miguu ni mikubwa na yenye nguvu zaidi kuliko mikono, isipokuwa Giboni wa Asia Kusini-Mashariki na sokwe wakubwa wasio binadamu.
Katika spishi zinazotembea mtini kwa kuning’inia kwa mikono kidole gumba kimefifia.
Mkia ni muhimu kwa primata wengi wanaoishi mtini lakini spishi nyingine wana mkia mdogo au hawana. Nyani kadhaa wa Amerika wana mkia wa kushikilia usio na nywele upande wa chini wenye neva muhimu.
Manyoya
[hariri | hariri chanzo]Mwili wa primata wengi umefunikwa na nywele zenye rangi baina ya nyeupe, kijivu, kahawia hadi nyeusi. Viganja kwa kawaida havina nywele. Spishi kadhaa hazina nywele usoni. Binadamu ni spishi yenye nywele chache.
Makazi
[hariri | hariri chanzo]Inaaminiwa kuwa primata kiasili waliishi mtini na hadi leo wengine wana maisha yao mtini pekee ambao hawatembei ardhini. Wengine wanaishi chini na juu pia. Wanaotembea kwenye uso wa ardhi pekee ni wachache pamoja na binadamu.
Primata wanapatikana kwenye aina mbalimbali za misitu kama vile msitu wa mvua, mikoko na pia kwenye misitu ya mlimani hadi kimo cha mita 3000 juu ya UB.
Spishi nyingine zinaogopa maji lakini kuna pia aina zinazopenda maji zinajua hata kuogelea. Spishi kadhaa zimezoea mazingira ya binadamu zinazoishi kwenye vijiji na miji kama makaka wa Uhindi.
Kimsingi strepsirhini (wenye pua bichi) wanafanya shughuli zao wakati wa usiku na kulala mchana lakini haplorhini (wenye pua kavu) wanafanya shughuli zao machana na kulala usiku. Wale wanaofanya shughuli zao usiku kwa jumla ni wadogo zaidi na wana uwezo mzuri zaidi wa kunusu.
Sawa na mamalia wengine wale wanaokula hasa majani wanapumzika muda mrefu zaidi wakihitaji muda mrefu kumeng'enya chakula chao.
Viungo vya Nje
[hariri | hariri chanzo]- Primate Info Net
- Primates at Animal Diversity Web
- Primate Research Institute, Kyoto University
- High-Resolution Cytoarchitectural Primate Brain Atlases Archived 11 Oktoba 2019 at the Wayback Machine.
- EUPRIM-Net: European Primate Network
- PrimateImages: Natural History Collection
- Tree of Life web project Archived 26 Aprili 2011 at the Wayback Machine.