Odessa

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Majengo ya Odessa.
Ramani ya Odessa katika Ukraine.

Odessa [1] (kwa Kiukraine: Оде́са) ni jiji na bandari muhimu kusini magharibi mwa Ukraine. Ni makao makuu ya Mkoa wa Odessa. Jiji hilo liko kwenye mwambao wa Bahari Nyeusi.

Idadi ya wakazi ilihesabiwa kuwa 1,016,000 mwaka 2021[2].

Historia[hariri | hariri chanzo]

Ngazi kubwa mjini Odessa ilitumiwa kwa picha za filamu maarufu ya "Manowari Potemkin" ya Sergei Eisenstein.

Vyanzo[hariri | hariri chanzo]

Wagiriki wa Kale waliwahi kujenga hapa mji uliogunduliwa na wanaakiolojia.

Hakuna habari za uhakika zaidi hadi karne za kati, wakati mwambao wa kaskazini wa Bahari Nyeusi ulitawaliwa na Watartari, wasemaji wa lugha za Kiturki. Mtawala wao wa Krim alijenga hapa ngome na mji mnamo 1440 kwa jina la Hacibey. Tangu mwaka 1529 ngome na bandari hiyo ilikuwa sehemu ya Milki ya Osmani kwa jina la Khadjibey.

Katika vita ya Urusi dhidi ya Waosmani ya miaka 17871792 ilivamiwa na Warusi na kuwa sehemu ya Milki ya Urusi[3] .

Mji mpya ya Odessa[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 1794 malkia Katharina II wa Urusi aliamuru mji wa kisasa kujengwa penye ngome ya kale na kuufanya kitovu cha "Urusi Mpya", mkoa ulioanzishwa katika maeneo yaliyotwaliwa kutoka kwa Waosmani. Mji huo ulipangwa na kupanua kufuatana na ramani iliyoandaliwa na mhandisi Mholanzi Frans de Vollan[4].

Mwaka 1795 jina la Kiturki lilibadilishwa kuwa Odessa kwa kumbukumbu ya koloni la Wagiriki wa Kale katika eneo hili. Malkia Katharina alimteua mkabaila Mfaransa Duc de Richelieu, aliyewahi kukimbia mapinduzi ya Ufaransa, kuwa gavana wa Odessa. Huyu alisimamia ujenzi wa mji mpya na kuurembesha. Majengo mengi ya kipindi kile hufanana na usanifu wa nyumbaUfaransa na Italia.

Odessa ilikua haraka kwa sababu mwaka 1817 ilikuwa "bandari huru" ambako wafanyabiashara waliruhusiwa kuingiza bidhaa kutoka nje bila kulipa kodi ya forodha. Ilikuwa bandari muhimu ya Urusi kwenye bahari isiyo na baridi - tofauti na bandari za kaskazini ya Urusi- na kufaa kwa biashara ya kuuza nje nafaka zilizozalishwa kwa wingi kusini mwa Urusi.

Mwaka 1866 mji uliunganishwa na njia ya reli kwenda Kiev.

Katika karne ya 19 Odessa ilikuwa mji wa nne kwa ukubwa katika Milki ya Urusi, baada ya Moscow, Sankt Peterburg na Warsaw. [5]

Katika karne ya 19 Wayahudi wengi kutoka sehemu za Poland walihamia Odessa. Mnamo mwaka 1900 theluthi moja ya wakazi walikuwa Wayahudi. Sehemu ya Wakristo Waorthodoksi waliwachukia na kulikuwa mara kadhaa na mashambulio dhidi ya Wayahudi zilizoitwa pogromu.

Karne ya 20[hariri | hariri chanzo]

Mnamo mwaka 1905 Odessa iliona ghasia ya wanamaji wa manowari Potemkin dhidi ya serikali ya kifalme; ghasia hii ilifuatwa na pogromu kubwa dhidi ya Wayahudi wa mji. Sehemu ya Wayahudi hao walianza kuhama Odessa na wachache walitafuta makazi mapya huko Palestina[6] .

Baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, Odessa ilikuwa sehemu ya jamhuri mpya ya Ukraine katika Umoja wa Kisovyeti.

Kwenye Vita Kuu ya Pili ya Dunia, Odessa ilivamiwa na majeshi ya Ujerumani na Romania kwenye mwaka 1941. Katika miezi 6 ya utawala wa Wajerumani na Waromania, asilimia 80 ya Wayahudi wa Odessa waliuawa. Maadui walifukuzwa mjini katika Aprili 1944. Majengo mengi yaliharibika lakini serikali iliongoza matengenezo ya mji kufuatana na mfano wa awali katika miongo baada ya vita.

Mnamo 1991, baada ya kuporomoka kwa ukomunisti na Umoja wa Kisovyeti, Odessa ilikuwa mji wa Ukraine mpya iliyojitegemea.

Leo Odessa ni jiji la karibu watu milioni 1.1. Viwanda vya jiji ni pamoja na ujenzi wa meli, kusafisha mafuta, kemikali, utengenezaji wa madini na usindikaji wa chakula. Odessa pia ni msingi wa Jeshi la majini la Ukraine na bandari ya uvuvi. Inajulikana pia kwa soko lake kubwa la nje, Soko la Saba-Kilomita.

Uchumi[hariri | hariri chanzo]

Bandari ya Odessa ni bandari kuu ya Ukraine.
Arcadia ni mtaa wa majengo mapya na maduka mengi

Uchumi wa Odessa unatokana na nafasi yake kuwa bandari muhimu. Mawasiliano ya meli hayasumbuliwi na barafu. Iko karibu na midomo ya mito mikubwa kama Dnepr, the Bug, Dnestr na Danubi inayowezesha usafirishaji wa bidhaa kwenda nchi za bara.[7]

Wakati wa Umoja wa Kisovyeti, Odessa ilikuwa bandari iliyoshughulika mizigo mingi ya nchi. Bandari huwa na vitengo vya kupokea na kupakua mafuta na gesi, mizigo mikavu na abiria. Mwaka 2007 bandari ya Odessa ilishughulika tani 31,368,000 za mizigo.[8] [9]

Bandari hii ni pia nyumbani kwa wanamaji wa Ukraine.

Mawasiliano ya reli ni muhimu kwa usafirishaji kutoka au kwenda bandarini.

Takriban asilimia 5 za uzalishaji wote wa tasnia ya Ukraine unatokea hapa.

Utamaduni[hariri | hariri chanzo]

Lugha ya kwanza inayozungumzwa ni Kirusi pamoja na Kiukraine ambacho ni lugha rasmi nchini. Jiji ni mchanganyiko wa mataifa na makabila mengi, pamoja na Waukraine, Warusi, Wayahudi, Wagiriki, Wamoldova, Wabulgaria, Waarmenia na Waturuki.

Picha[hariri | hariri chanzo]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Resolution no. 55 of the Cabinet of Ministers of Ukraine, January 27, 2010 (ukr). zakon2.rada.gov.ua. Iliwekwa mnamo 2017-04-15.
  2. "Чисельність наявного населення України (Actual population of Ukraine)" (PDF) (in Ukrainian). State Statistics Service of Ukraine. Retrieved 11 July 2021.
  3. History of Odessa. Odessa Online. Jalada kutoka ya awali juu ya 2019-11-06. Iliwekwa mnamo May 1, 2006.
  4. About Odessa, tovuti ya Odessa Info, iliangaliwa Novemba 2019
  5. Herlihy, Patricia (1977). The Ethnic Composition of the City of Odessa in the Nineteenth Century. pp. p. 53.
  6. The Jewish Community of Odessa. The Museum of the Jewish People at Beit Hatfutsot. Jalada kutoka ya awali juu ya 2020-09-21. Iliwekwa mnamo 2019-11-23.
  7. Kravtsiv, Bohdan (2012). "Odesa". Internet Encyclopedia of Ukraine. Canadian Institute of Ukrainian Studies. http://www.encyclopediaofukraine.com/display.asp?linkpath=pages\O\D\Odesa.htm. Retrieved 4 November 2014. "Odesa is situated on a large, virtually ice-free bay on the Black Sea, near the mouths of the Danube River, the Dnister River, the Boh River, and the Dnieper River, which link it with the interior of the country.".
  8. Ассоциация портов Украины и всего Чёрного моря: члены kutoka [1], iliangaliwa 29 February 2012
  9. Ports of Ukraine. Jalada kutoka ya awali juu ya 9 November 2007.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

Kujisomea[hariri | hariri chanzo]

     . https://archive.org/details/sim_slavic-review_winter-2001_60_4/page/781.
     . PMID 18333319
      . https://archive.org/details/sim_journal-of-urban-history_2001-01_27_2/page/131.
     . https://archive.org/details/sim_slavic-review_winter-2001_60_4/page/781.
     . PMID 18333319
      . https://archive.org/details/sim_journal-of-urban-history_2001-01_27_2/page/131.
      . (paperback)
     . https://archive.org/details/sim_journal-of-social-history_winter-1994_28_2/page/435.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]