Msenefu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Croton megalocarpus)
Msenefu
Msenefu ukichanua
Msenefu ukichanua
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Plantae (Mimea)
(bila tabaka): Angiospermae (Mimea inayotoa maua)
(bila tabaka): Eudicots (Mimea ambayo mche wao una majani mawili)
(bila tabaka): Rosids (Mimea kama mwaridi)
Oda: Malpighiales (Mimea kama mwenda-usiku)
Familia: Euphorbiaceae (Mimea iliyo mnasaba na mtongotongo)
Nusufamilia: Crotonoideae
Burmeist.
Jenasi: Croton
L.
Spishi: C. megalocarpus
Hutch.

Msenefu (Croton megalocarpus) ni mti wa nusufamilia Crotonoideae katika familia Euphorbiaceae. Ubao wake huitwa musine. Unatokea katika misitu minyevu, misitu kandokando ya mito na nyika yenye miti kwa mwinuko wa m 900-2100. Hupandwa sana kwenye mipaka ya mashamba. Msambao wa kijeografia ni Burundi, Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Malawi, Msumbiji, Rwanda, Somalia, Tanzania, Uganda na Zambia.

Mti huu unaweza kukua mpaka m 35 na kupata shina lenye kipenyo hadi sm 100. Uso wa gome una nyufa nyingi zinaelekea juu chini, unakwaruza na una rangi ya kahawiakijivu. Umbo la matawi na majani yote pamoja ni bapa na linaenea na matawi yamo katika matabaka. Majani yanafuatana na ni mazima; urefu wa kikonyo ni sm 2-8; ubapa una umbo la yai lakini mrefu, sm 7-14 x sm 3-7, kama karatasi nene au kama ngozi nyembamba, kijani juu na rangi ya fedha chini. Maua kijaninjano yamo katika vishada vinavyoning'inia vyenye urefu wa hadi sm 30. Maua yote ni ya kiume au kuna maua machache ya kike kwenye tako la kishada. Tunda ni kokwa ya mviringo au ya duaradufu yenye urefu wa sm 2.5-4.5 na rangi ya kahawiakijivu. Endokarpi ni nene na kama ubao. Kokwa inafunguka kwanzia ncha na ina mbegu 3.

Matumizi[hariri | hariri chanzo]

Ubao wa msenefu, inayojulikana kama 'musine', hutumika kwa ujenzi, sakafu, vigoda, vinu, mizinga ya nyuki, vinia na plaiwudi. Pia hutumika kama kuni na kwa uzalishaji wa makaa.

Maji ambayo ndani yake gome limechemshwa huchukuliwa kama dawa ya minyoo na kutibu kifaduro, kichomi, maumivu ya tumbo, homa na malalamiko ya tumbo yanayohusiana na shida ya kibofunyongo na wengu. Utomvu wa majani na vitawi vichanga hupakwa kwenye vidonda. Mbegu hutumika kama chakula cha kuku. Mbegu zinaweza pia kutumiwa ili kupatia sufu rangi ya manjano. Maua hutoa mbochi kwa nyuki-asali. Asali inayozalishwa ni nyeusi na ina ladha kali. Maganda ya kokwa hutumika kama matandazo katika bustani za mboga na kama sehemu ya michanganyiko ya vyungu vya mimea.

Mafuta yanaweza kusindikwa kutoka kwa mbegu na yanaweza kugeuzwa kuwa biodizeli. Kampuni huko Nanyuki, Kenya, ilijaribu kuuza biodizeli hii kwa jina la zamani la Ecofuels Kenya Ltd. (EFK). Hiyo ilibainika kutokuwa nzuri kiuchumi na jina la kampuni likabadilishwa kuwa EcoFix(K). Mafuta ya jozi sasa yanauzwa kwa madhumuni tofauti, kwa mfano kwa utengenezaji wa rangi. Keki ya mbegu ambayo hubaki baada ya usindikaji wa mafuta, hutumiwa kuzalisha malisho ya wanyama yenye protini nyingi. Viganda vya kokwa hubadilishwa kuwa mbolea.

Picha[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]