Nenda kwa yaliyomo

Ngozi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Skin)

Kwa maana nyingine ya neno hili linganisha ngozi (maana)

Ngozi ya mkono wa binadamu.

Ngozi ni ganda la nje linalofunika mwili wa mnyama au binadamu. Aina mbalimbali huwa na aina za ngozi tofautitofauti kulingana na mazingira wanapoishi na ukoo wa spishi mbalimbali.

Ni wanyama wa nusufaili ya vetebrata pekee wenye ngozi; wengine kama konokono, kaa au wadudu huwa na kiunzi nje, si ngozi. Mamalia wote walio sehemu ya vetebrata huwa na nywele angalau chache kwenye ngozi yao.

Ngozi ikiondolewa mwilini na kushughulikiwa kwa kuikausha na kutia dawa mbalimbali inaweza kutunzwa na kutumiwa kwa kutengeneza viatu, mavazi n.k.

Kazi za ngozi

[hariri | hariri chanzo]
  1. Kazi ya kwanza ya ngozi ni kukinga sehemu za mwili dhidi ya athira za nje, hasa dhidi ya vijidudu na michakati zinazoweza kusababisha ugonjwa.
  2. Ngozi inatunza unyevu au kiwango cha maji mwilini, hivyo ni kinga dhidi ya kukauka.
  3. Ngozi ni kinga dhidi ya maji ya nje ambayo ingeyeyusha kemikali za seli na kuzitoa nje ya mwili.
  4. Ngozi ina uwezo wa kutawala halijoto ya mwili ama kwa kutoa joto la ziada kwenda nje au kuitunza ndani ya mwili. Ngozi ikijikaza inatunza joto, ikilegea inapanua eneo la uso wake na kupunguza joto la ndani ya mwili.
  5. Ngozi huwa na neva nyingi, hivyo ni kiungo muhimu kwa kutambua dunia kwa kuhisi baridi, joto, kuguswa, tetemeko n.k.
  6. Ngozi inasaidia kupumua yaani kupeleka oksijeni kwenye seli; kwa mwanadamu seli za ngozi yenyewe zinapata oksijeni kutoka nje moja kwa moja; kuna wanyama kadhaa ambao hawana mapafu wanapata mahitaji yote ya oksijeni kupitia ngozi yao.
  7. Uzuri na mawasilianoː ngozi za binadamu huweza kuonyesha hali ya mtu kiafya, kihisia, n.k.
  8. Ngozi hutumika pia kuchukua vitamini D toka kwenye mwanga wa jua ili kutumiwa na mwili wa binadamu.
  9. Ngozi husafisha mwili kwa kutoa jasho. Licha ya kuratibu kiwango cha joto mwilini, jasho huwa linabeba uchafu kama vile urea, ingawa kiwango chake ni kidogo ukilinganisha na mkojo.
  10. Ngozi huwa kama mlinzi muhimu ambaye anazuia virutubishi muhimu visitoke nje ya mwili.

Muundo wa ngozi ya mamalia

[hariri | hariri chanzo]

Katika ngozi ya mamalia kuna sehemu mbili:

  • ngozi ya nje inayoitwa kwa lugha ya kitaalamu epidemisi (epidermis). Ina unene wa milimita 0.03 hadi 0.05 lakini imaweza kufikia unene wa milimita kadhaa chini ya miguu na kwenye makofi ya mikono. Haifikiwi na mishipa ya damu. Hii ngozi ya nje hasa ina kazi ya kukinga mwili.

Ndani yake kuna kanda mbalimbali; sehemu ya chini ni kanda la kizazi ambako seli mpya zinazalishwa; jinsi zinavyosukumwa kuelekea nje zinakauka na mwishoni zifikia nje kabisa zinatoka kama mba.

  • ngozi ya ndani (demisi au dermis). Ni nene zaidi na hii ni sehemu inayoweza kukaushwa na kutumiwa kama ngozi kwa ajili ya viatu na kutengeneza vifaa kama mfuko au ng'oma.

Kanda za ngozi ya ndani zina hasa kazi ya kulisha na kushika epidemisi. Ndani yake kuna mishipa mingi ya damu na mishipa fahamu (neva). Ndani yake kuna pia tezi za jasho na tezi za mafuta. Kuna pia seli za musuli kwa ajili ya kukaza au kulegeza ngozi.

Rangi za ngozi

[hariri | hariri chanzo]

Rangi tofauti za ngozi zinategemea uwezo wa seli maalumu katika kanda la kizazi la epidemisi kutengeneza kiasi kikubwa au kidogo cha melanini.

Melanini ni kemikali inayokaa ndani ya epidemisi yenye kazi ya kuzuia au angalau kupunguza athira za mnururisho wa jua. Mnururisho huo unaweza kuwa wa hatari kama jua ni kali na kuchoma seli, hasa kusababisha kansa.

Sehemu mbalimbali za mwili zinaweza kushika viwango tofautitofauti za melanini: ngozi ya makofi kwa kawaida ina melanini kidogo tu.

Uwezo wa kutengeneza melanini unarithiwa. Hivyo watu "weusi" huzaliwa na kiwango kikubwa cha melanini ya kudumu kwenye ngozi. Watu "weupe" wana kiwango kidogo.

Katika mazingira yenye jua kidogo rangi nyeupe ina faida ya kwamba ngozi inahitaji nuru ya jua kwa kutengeneza vitamini D. Hapo mtu "mweusi" katika mazingira yenye jua kidogo anaweza kupata uhaba wa vitamini hiyo.

Kinyume chake wingi wa nuru inaongeza hatari ya kushika kansa ya ngozi. Watu wa Australia waliotoka katika koo za Wazungu wa Ulaya ilhali wanaishi katika nchi ya tropiki yenye jua kali wana kiwango kikubwa cha kansa ya ngozi.

Tabia hizo zimesababisha ya kwamba mara nyingi watu katika nchi za jua kali ni "weusi" zaidi, lakini watu kwenye nchi za jua kidogo ni "weupe" zaidi, maana tofauti za rangi ya ngozi zinasababisha faida au hasara za kiafya kulingana na mazingira.

Pale ambako hali ya jua ni ya katikati watu wa kila rangi wanaweza kuishi bila matata, lakini wakizaa pamoja kwa kawaida urithi wa ngozi nyeusi zaidi hushinda juu ya urithi wa rangi nyeupe.

Bidhaa mbalimbali hutumiwa na binadamu ili kuweza kutunza ngozi. Moja ya bidhaa maarufu ni zile zinazotunza ngozi kwa kuzuia ukali wa mionzi mikali ya jua (kwa Kiingerezaː sunscreen na sunblock). Bidhaa hizo mara nyingi hutumia Titani dioksaidi na oksaidi ya zinki ni mbili ya viungo muhimu katika jua.

Chakula pia ni muhimu kwa utunzaji wa ngozi.

Vitamini A, inayojulikana pia kama retinoidi, hufaidisha ngozi kwa kuimarisha katalini, kupunguza viwango vya uzalishaji wa sebumi vinavyochangia kuwepo kwa chunusi mwilini.

Vitamini D husaidia ukuaji wa seli, kuimarisha kinga na kusaidia ngozi kutozeeka kwa haraka.

Vitamini C husaidia mwili kutopata kansa na pia ngozi kutengeneza vitamini E.

Vitamini E hutoa ulinzi dhidi ya mionzi mikali ya jua yenye madhara.

Masomo kadhaa ya sayansi yalithibitisha kuwa mabadiliko katika hali ya lishe ya msingi huathiri hali ya ngozi.

Vyakula ambavyo husaidia ngozi ni kama vile matunda na mboga za njano, na za kijani, na machungwa; bidhaa za maziwa zisizo na mafuta; vyakula vya nafaka nzima; samaki; karanga.

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Makala hii kuhusu mambo ya anatomia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Ngozi kama matumizi yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.