Nenda kwa yaliyomo

Sfinksi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Sfinksi kubwa mashuhuri inapatikana katika eneo la Piramidi za Giza.

Sfinksi (kwa Kiingereza sphinx) ni kiumbe cha visasili katika tamaduni za Misri ya Kale, Ugiriki wa Kale na Mesopotamia. Inajulikana pia katika visasili na sanaa za Asia ya Kusini na Kusini-mashariki.

Inaunganisha mwili wa simba na kichwa cha binadamu.

Kisasili cha sfinksi za Mashariki ya Kati kwa kiasi kikubwa kimesahauliwa. Ni pekee kuhusu sfinksi ya Ugiriki ya kwamba hadithi kadhaa zimehifadhiwa.

Sfinksi katika visasili vya Ugiriki ya Kale

[hariri | hariri chanzo]

Wagiriki wa Kale walisimulia ya kwamba Sfinksi ilikaa nje ya geti la mji wa Thebi ikamwuliza kitendawili kila mtu aliyepita. Kibali cha kuingia mjini kilitolewa kwake aliyejua jibu pekee. Aliyeshindwa kujibu aliuawa na kuliwa naye.

Huyu Sfinksi iliaminiwa kuwa ilitumwa na mungu Hera (au Ares kufuatana na mapokeo tofauti) kutoka kwake Ethiopia. Kwa hiyo Wagiriki walikumbuka ya kwamba kiasili habari za Sfinksi zilifika Ugiriki kutoka Afrika.

Kitendawili kilikuwa hiki: "Kiumbe gani kina sauti moja lakini inapatikana kwa miguu minne, halafu miguu miwili, halafu miguu mitatu?"

Katika kisasili cha Wagiriki ni Oedipus aliyeweza kujibu kwa usahihi: "Ni binadamu. Akiwa mtoto mchanga anatambaa kwa kutumia mikono na miguu, akiwa mtu mzima anatembea kwa miguu yake miwili, akiwa mzee anatumia fimbo."[1]

Kulikuwa na hadithi yenye kitendawili tofauti: "Kuna wakinadada wawili. Wa kwanza anamzaa wa pili, halafu wa pili anamzaa wa kwanza. Hao ni nani?" Jibu sahihi lilikuwa "Mchana na usiku", maana kwa lugha ya Kigiriki maneno kwa Usiku na mchana yote kisarufi ni ya kike.

Safu ya sfinksi mbele ya hekalu la Karnak, Misri.

Sfinksi katika sanaa ya Misri ya Kale

[hariri | hariri chanzo]

Sfinksi zinaonekana mara nyingi katika sanaa ya Misri ya Kale. Mashuhuri hasa ni Sfinksi Kubwa katika eneo la Piramidi za Giza karibu na jiji la Kairo. Kichwa chake kinaaminiwa kuonyesha uso wa Farao Khufra.

Sanamu za Sfinksi ziliwekwa mbele ya piramidi na mahekalu kama walinzi na wote waliotaka kuingia hapo walipaswa kupita kwa. Kuna mifano kadhaa ya makundi ya sfinksi yanayosimama upande wa kulia na kushoto wa njia inayoelekea geti la hekalu.

Kulikuwa pia na sfinksi zilipewa kichwa cha mnyama aliyekuwa nembo wa mungu fulani kwa mfano kondoo (nembo ya mungu Amun) au ndege wa kipanga (nembo ya mungu Horus).

Sfinksi katika sanaa ya Ulaya

[hariri | hariri chanzo]

Wakati wa Zama za mwamko (Renaissance) katika Ulaya wasanii walivutwa na habari za Misri ya Kale wakaanza kuchonga sanamu za Sfinksi kama mapambo wa nyumba za kifalme au nyanya za miji.

Wasanii wa Ulaya walitumia Sfinksi kama alama ya milele na kitendawili. Wachoraji walionyesha Sfinksi kama wa kike. Hii imetokana na lugha ya Kigiriki ambako Sfinksi ina jinsi ya kike kisarufi .

Sfinksi katika Asia ya Kusini na Kusini-Magharibi

[hariri | hariri chanzo]
Sfinksi ya Uthai "Manussiha"

Viumbe vya kufanana na Sfinksi vinapatikana pia katika visasili na sanaa ya tamaduni za Asia Kusini na Asia Kusini-Magharibi.[2] Kwa lugha mbalimbali wanajulikana kama ''purushamriga'' (Kisanskrit mtu-mnyama), ''purushamirugam'' (Kitamil mtu-mnyama) , ''nara-simha'' (Kisanskrit mtu-simba) au ''manusiha'' (Kipali mtu-simba).

Sanamu za kwanza zinazounganisha tabia za mtu na simba zimepatikana tangu karne ya 1 KK[3]

Hata katika mapokeo ya Uhindi Sfinksi anasimama mara nyingi karibu na geti la hekalu, inaaminiwa kuondoa maovu kutoka waumini wakiingia hekaluni.

Katika mapokeo ya Wabuddha wa Sri Lanka narasimha ni mlinzi wa upande wa kaskazini wa hekalu unaotazamiwa kuwa mtakatifu zaidi.

Picha za sfinksi

[hariri | hariri chanzo]
  1. [http://people.hsc.edu/drjclassics/texts/Oedipus/sphinx.shtm The Sphinx and Oedipus Rex by Janice Siegel]
  2. Deekshitar, Raja. "Discovering the Anthropomorphic Lion in Indian Art." in ''Marg. A Magazine of the Arts''. 55/4, 2004, p.34-41; [http://www.sphinxofindia.rajadeekshithar.com Sphinx of India]
  3. The sphinx in early Indian art, by Raja Deekshiktar; anajadili hapa swali kama kulikuwa na athira ya Kigiriki kwenye sanamu na labda kisasili ya sfinksi katika Uhindi
  • Clay, Jenny Strauss, Hesiod's Cosmos, Cambridge University Press, 2003. ISBN 978-0-521-82392-0.
  • Stewart, Desmond. Pyramids and the Sphinx. [S.l.]: Newsweek, U.S., 72. Print.
  • Kallich, Martin. "Oepidus and the Sphinx." Oepidus: Myth and Drama. N.p.: Western, 1968. N. pag. Print.

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Wikimedia Commons ina media kuhusu: