Nenda kwa yaliyomo

Bronzi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Kichwa cha mfalme kilichotengenezwa kwa bronzi, Benin

Bronzi (pia: shaba nyeusi[1]) ni aloi ya metali. Kiasi kikubwa ndani yake ni shaba (70-90%) na metali nyingine ndani yake ni stani (takriban 10-30%).

Historia

[hariri | hariri chanzo]

Bronzi ilikuwa aloi ya kwanza inayojulikana kuwa ilitumiwa na binadamu katika historia yake. Mwisho wa zama za mawe watu walianza kutumia shaba kwa kutengeneza silaha na vifaa vingine. Lakini shaba peke yake ina hasara mbili: si ngumu sana, yaani umbo lake halidumu likitumiwa kwa kazi nzito au kwa mapigano; ukali wa kisu au shoka unapotea haraka. Hasara nyingine inafanya mmenyuko na oksijeni ya hewa au katika maji na uso wake hubadilika kuwa ganda la oksaidi.

Hapo watu waligundua ya kwamba tabia za shaba zinaboreshwa kwa kuiongezea kiasi cha stani. Walipata shaba kwa njia ya kupasha moto madini ya shaba hadi shaba kupatikana kwa hali ya kiowevu cha moto; kwa kuongeza kiasi cha stani katika hali hiyohiyo na kukoroga zote mbili aloi ya bronzi ilipatikana. Hii aloi ni ngumu zaidi kuliko shaba pekee na haina mmemenyuko wa haraka tena na oksijeni ya hewani.

Mahali pa kwanza ambako bronzi ilipatikana zamani za milenia ya 4 KK kulikuwa maeneo ya Uajemi, China, Mesopotamia na kwenye Balkani. Inaonekana ya kwamba bronzi iligunduliwa mara kadhaa mahali mbalimbali katika mazingira yenye shaba ambako watu walitangulia kutengeneza vifaa vya shaba tupu.

Kutoka vitovu vya kwanza ujuzi wa kutengeneza bronzi ulisambaa hadi maeneno mengine penye madini ya shaba, na biashara ya vifaa na silaha za bronzi ilianza kuunganisha mataifa na makabila ya mbali.

Baadaye nafasi ya bronzi ilichukuliwa na chuma kilichopatikana mahali pengi kwa gharama ndogo zaidi.

Matumizi leo

[hariri | hariri chanzo]

Siku hizi bronzi ina nafasi yake katika vifaa vya mapambo na pia katika sehemu za mashine, kwa mfano pale ambako vipande viwili vinagusana na kusugana.

  1. Bronzi ni msamiati wa KAST, pia ya BAKITA (Kamusi ya Istilahi za Sayansi na Tekinolojia 1992); Shaba nyeusi wa Tataki