Nehemia

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Picha takatifu ya Nehemia.

Nehemia (kwa Kiebrania נְחֶמְיָה yaani: "Faraja ya Mungu" au: "Aliyefarijiwa na Mungu"), ni mtu wa Biblia, mhusika mkuu wa kitabu chenye jina lake.

Aliishi katika karne ya 5 KK.

Sehemu ya kwanza ya maisha yake[hariri | hariri chanzo]

Alikuwa mwana wa Hachaliah (Nehemia 1:1), na familia yake ilikuwa inaishi Yerusalemu (Nehemia 2:3) wakati ambapo mji huo ulikuwa chini ya dola la Waajemi.

Nehemia, kisha kuwa afisa wa Kiyahudi katika nyumba ya mfalme, alipandishwa cheo kuwa mnyweshaji mkuu wa mfalme Artashasta I katika ikulu la Shushan akafunga urafiki naye (Neh 1:11).

Wayahudi waliposikia kwamba mmojawao anaweza kusema na mfalme, walifika Uajemi ili wamwone. Nehemia aliposikia kwa ndugu yake Hanani na wengineo juu ya hali duni ya mji mkuu wa Yudea alisikitika sana, akafunga na kusali. Alijua kwamba matatizo ambayo yeye na watu wake waliyapata yalikuwa matokeo ya dhambi zao, na kwa moyo wa unyenyekevu na kukiri dhambi, aliweka mambo yote mbele ya Mungu na kuomba msaada wake (4-11).

Kwa muda wa miezi minne Nehemia aliomba kuhusu mambo hayo. Kwa hiyo alikuwa tayari kumweleza mfalme shida zake, nafasi ilipotokea ghafla.

Matokeo yake ni kwamba, mfalme aliona huzuni yake akamuuliza imetokana na nini. Nehemia akajieleza akaruhusiwa kwenda Yerusalemu kama tirshatha, yaani liwali, na kushughulikia ujenzi wa ngome wa mji na ustawi wa Wayahudi wote wa eneo hilo. Pia alipewa vifaa vilivyohitajika (2:1-8).

Nehemia alipokwenda Yerusalemu, hali na mazingira yalikuwa tofauti na wakati wa safari ya Ezra, naye aliona vizuri kupokea msaada wa mfalme, yaani kusindikizwa na kundi la askari (9; taz. Ezra 8:21-23). Maafisa wengine waliokuwa wametawala eneo la Yerusalemu hapo awali, walikasirika na kugeuka kuwa maadui wakali walipogundua kwamba eneo hilo liliwekwa chini ya liwali Nehemia. Licha ya kuwa Myahudi, alikuwa na mamlaka kutoka kwa mfalme wa Uajemi, na hivyo hawakuweza kumwingilia tena (10).

Kujenga upya kuta kubwa zilizobomolewa ilikuwa kazi ngumu sana, tena kubwa mno, hata wengine walisema haiwezekani. Kwa hiyo, kabla ya kutangaza madhumuni yake, Nehemia alichunguza mambo yote kwa siri, ili ajue vizuri kazi iliyotakiwa na vifaa vilivyohitajika (11-16). Ujuzi huo ambao Nehemia alijipatia, pamoja na maelezo yake ya jinsi Mungu alivyoongoza mambo yote mpaka alipotumwa Yerusalemu, yaliwaaminisha watu kwamba wakati umewadia wa kuanza kujenga ngome, wasiogope upinzani ambao utaendelea kuwepo (17-20).

Kazi ilipangwa vizuri. Vikundi mbalimbali vya watu vilipangwa kila mahali bega kwa bega kuzunguka mji wote, hata kuta zote ziiweza kujengwa wakati mmoja. Orodha ya wafanyakazi inaonyesha kwamba Wayahudi kutoka mbali na karibu walikuja kusaidia. Si waashi tu, bali pia makuhani, mafundi wa dhahabu, mafundi wa manukato, maafisa wa serikali, wafanya biashara na hata wanawake walisaidia kazi hiyo (3:1-16). Walawi walijenga karibu na nyumba ya kuhani mkuu (17-21). Makuhani na watu wengine walioishi Yerusalemu, kwa kawaida walipangiwa sehemu za karibu na nyumba zao, na watu waliotoka mbali walijenga sehemu zilizobaki (22-32).

Wayahudi walikuwa na kibali cha mfalme wa Uajemi kwa mradi wa kujenga kuta, kwa hiyo wapinzani wao ambao pia walikuwa chini ya mfalme huyo, waliogopa kuwashambulia hadharani. Hata hivyo waliwadhihaki na kufanya mzaha juu ya kazi yao, wakitumaini kwamba wataweza kuwachosha na kuwaachisha kazi ya ujenzi (4:1-5).

Lakini Wayahudi hawakukatishwa tamaa haraka wakaendelea na kazi yao (6). Kwa hiyo maadui walikusudia kuleta machafuko na kuvuruga akili za Wayahudi kwa kuleta mashambulio ya siri sehemu mbalimbali mjini. Wayahudi waliposikia makusudi hayo walizidisha maombi na kuongeza ulinzi wao (7-9). Wale walioishi vijijini walimletea Nehemia habari kuhusu shughuli za maadui (10-12), lakini Nehemia hakuogopa hatari. Aliwapa wafanyakazi silaha na kuwagawa katika makundi mawili. Wengine walipofanya kazi wenzao walilinda. Maarifa ya kivita yalifikiriwa ili kujihami kama maadui watashambulia ghafla (13-21). Watu wa nchini waliofanya kazi Yerusalemu waliombwa kulala mjini bila ya kurudi nyumbani, kwa kusudi la kuongeza ulinzi wa usiku (22-23).

Tatizo lingine lililomkabili Nehemia lilikuwa hali ya manung'uniko yaliyoongezeka polepole na kwa muda mrefu baina ya matajiri na maskini. Watu waliokuwa na shida ya fedha walikopa kwa matajiri ili waweze kununua chakula na kulipa kodi zao kwa serikali ya Uajemi. Matajiri wakaona hali hiyo kuwa ni nafasi ya kupata faida kwa kuwadai watu riba kubwa. Kisha maskini waliposhindwa kulipa, matajiri walichukua mashamba yao kuwa malipo ya deni, au wakachukua hata watoto wao na kuwafanya watumwa. Shida hiyo ilizidi katika mwaka wa njaa na wakati wa kazi ya kujenga kuta, kwa sababu wafanyakazi hawakuweza kujipatia mishahara ya kawaida. Maskini hawakuona njia yoyote ya kuondokana na hali hiyo, wakamsihi Nehemia awasaidie (5:1-5).

Nehemia alijua uchoyo na hila za matajiri, kwa sababu siku moja aliwaona wakiuza Wayahudi wawe watumwa wa wageni, nao walijua kwamba ilikuwa siasa ya Nehemia kuwanunua watumwa wale tena na kuwapa uhuru (6-8). Kwa hiyo aliamuru kwamba vitu au watu waliochukuliwa kuwa malipo ya madeni warudishwe na kupewa uhuru, na riba juu ya mikopo iondolewe kabisa (9-13).

Muda wote wa miaka 12 ya uliwali wake, Nehemia aliwapa watu kielelezo kizuri ili wakifuate. Yeye hakudai kitu chochote alichostahili kufuatana na cheo chake, asije akawatwisha watu mzigo zaidi. Aliwalisha wageni na wafanyakazi wake hata kutoka mfukoni mwake mwenyewe (14-19).

Maadui walipoona kuta zikikaribia kumalizika, waliona njia ya pekee ya kuzuia kazi hiyo ni kumwondoa Nehemia mwenyewe. Walijaribu kumwita katika vijiji vya mbali ili wakamwue huko, lakini Nehemia alitambua hila yao (6:1-4). Kisha wakaeneza fununu kwa njia ya barua wazi iliyosema kwamba Nehemia alipanga maasi dhidi ya Uajemi, lakini kazi yao ikawa bure (5-9).

Maadui wakafikiri maarifa mengine tena. Walijaribu kumsababisha Nehemia afanye mambo ambayo yataharibu sifa yake ya kuwa mtu asiyeogopa wapinzani naye avunje heshima ya hekalu. Mara nyingine tena wakashindwa (10-14). Hata wapelelezi na wasaliti ambao maadui walikuwa wamewaweka mjini Yerusalemu hawakuweza kumzuia Nehemia kumaliza kazi yake ya kujenga ukuta (15-19).

Wakati huo Yerusalemu ulizungukwa na kuta imara ulioweza kulinda mji. Hata hivyo, Nehemia alitaka kuongeza usalama. Mji ulikuwa haujapata wenyeji wengi, kwa hiyo tahadhari ilitakiwa. Ili kuzuia mashambulio ya ghafla ya alfajiri, Nehemia aliagiza milango ya mji isifunguliwe mpaka watu wote wawe macho na katika shughuli zao za kawaida za mchana. Pia aliweka ulinzi wa ngome yote uliopangwa kwa maarifa, ili watu wa kila nyumba walinde karibu na eneo lao (7:1-4).

Kisha Nehemia akaandika orodha kubwa ya watu wote walioishi Yerusalemu. Orodha hiyo ililinganishwa na ile ya kundi la kwanza la watu waliorudi kutoka uhamishoni pamoja na Zerubabeli karibu miaka 100 iliyopita (5-73; taz. Ezra 2:1-70, ambapo orodha hiyo imeandikwa).

Marekebisho ya Nehemia[hariri | hariri chanzo]

Kuta zilimalizika siku ya 25 ya mwezi wa sita (yaani muda wa ujenzi ulikuwa siku 52, taz.6:15). Sikukuu ya Israeli ya katikati ya mwaka iliadhimishwa katika mwezi wa saba (Law 23:24,27,34), na hiyo ilikuwa nafasi nzuri ya kuwakutanisha watu wote ili kusherehekea pia kumalizika kwa ujenzi wa kuta (taz.7:73; 8:1). (Wakati uleule wa mwaka ulikuwa umechaguliwa kwa kuweka wakfu madhabahu iliyojengwa upya zaidi ya miaka 90 ya nyuma; taz.Ezra 3:1-6).

Kufuatana na maombi ya watu, Ezra akisaidiwa na baadhi ya Walawi, alisoma Torati na kuieleza kwa watu waliokutanika. Inaonekana kwamba sheria hiyo ilikuwa haijasomwa kwa muda mrefu sana, kwa hiyo watu walisikiliza kwa uangalifu sana (8:1-8). Walipogundua jinsi maisha yao yalivyokuwa mbali na sheria hiyo, walijaa huzuni hata Nehemia aliogopa kwamba mambo aliyoyakusudia kuwa sikukuu ya furaha na karamu kubwa yatageuka kuwa wakati wa huzuni na maombolezo (9-12).

Siku ya pili yake viongozi wa Israeli walirudi tena ili wasikilize zaidi ya sheria ya Mungu (13). Matokeo ya mambo hayo yalikuwa sherehe kubwa ya taifa zima ya sikukuu ya Vibanda. Wakati wa sikukuu hiyo watu waliishi katika vibanda vya matawi ya miti na makuti, wakiwakumbuka mababu zao jinsi walivyoishi katika vibanda wakati wa safari yao ya jangwani walipotoka Misri (14-18; taz.Law 23:33-43).

Siku mbili baada ya kumaliza sikukuu ya Vibanda (iliyokuwa tangu siku ya 15 hadi ya 22 ya mwezi ule, taz.8:18; Law 23:34), watu walikutana tena kwa kusomewa sheria. Wakati huo baada ya kusomewa, ulifuata wakati wa kukiri dhambi na kumwabudu Mungu. Ibada hiyo iliongozwa na Walawi (9:1-5).

Ibada ilianza kwa kumtukuza Mungu mkuu aliye Mwumbaji, na kwa kumsifu kwa sababu ya kumchagua Ibrahimu na kufanya naye agano lake (6-8). Mungu siku zote alikuwa mwaminifu kwa watu wake wa Israeli, wakati wa shida zao huko Misri na hata katika safari kubwa ya jangwani (9-15). Hata walipomwasi, aliwasamehe na kuwaleta katika nchi ya ahadi yake (16-25). Wakaendelea kuasi, naye akaendelea kuwasamehe. Lakini waliendelea na ukaidi wao, hata mwisho, baada ya kushindwa na kunyanyaswa mara nyingi na maadui wao, walipelekwa kifungoni katika nchi za kigeni, kusudi Mungu aweze kuwanyenyekeza na kusababisha watubu (26-31). Ingawa wakati huo walikuwa wamerudi katika nchi yao, bado walikuwa chini ya utawala wa wageni. Walikubali kwamba mambo hayo yalikuwa adhabu ya haki kwa ajili ya dhambi zao, kwa sababu walikuwa wakiasi agano la Mungu (32-37).

Baada ya kukiri makosa yao, watu walitoa ahadi ya agano kuwa waaminifu kwa Mungu. Walithibitisha ahadi yao kwa kiapo kilichoandikwa na kutiliwa sahihi na viongozi wao kwa niaba yao (38). Nehemia alikuwa wa kwanza wa kutia sahihi (10:1), akifuatwa na makuhani (2-8), Walawi (9-13) na viongozi wa kiraia (14-27). Watu wote waliapishwa juu ya maandiko ya agano hilo kuwa waaminifu kwa sheria ya Mungu (28-29).

Mambo muhimu zaidi yaliyotajwa katika maandiko hayo yalihusu ndoa za mchanganyiko (30, taz.Kut 34:15-16); siku ya Sabato na mwaka wa Sabato (31, taz.Kut20:8-10;23:10-ll; Kum 15:1-2); kodi ya hekalu (32, taz.Kut 30:11-16); mahitaji kwa ajili ya hekalu na huduma zake (33-34); sadaka za malimbuko ya nafaka na wazaliwa wa kwanza wa wanyama (35-36, taz.Hes 18:13-18) na zaka (yaani utoaji wa sehemu ya kumi ya mapato, 37-39; taz.Hes 18:21-28).

Baada ya kusoma sheria, kusherehekea sikukuu ya Vibanda na kiapo cha watu kuhusu uaminifu wao kwa agano, kuta zilizinduliwa rasmi. Makuhani, Walawi, waimbaji na wenyeji wengine wenye heshima walishiriki katika sherehe hiyo (27-30). Watu walikutana sehemu moja karibu na kuta upande mmoja wa mji. Kisha wakagawanyika kuwa makundi mawili wakaanza kwenda kila upande kuzunguka kuta zote. Kundi moja liliongozwa na Ezra (31-37) na lingine liliongozwa na Nehemia (38-39). Makundi hayo mawili yakakutana tena upande mwingine wa mji karibu na hekalu watu walipounganika kwa kutoa sadaka na kumtukuza Mungu kwa furaha kubwa (40-43).

Hatimaye maafisa wakawekwa ili waangalie michango na matumizi ya fedha na vitu vingine ambavyo watu walivileta hekaluni. Waisraeli wote walitoa sehemu ya kumi ya mapato yao wakaiweka katika fungu hilo la jumla. Kutoka huko vitu vile vikagawiwa kwa Walawi waliowasaidia makuhani na kushughulika na nyimbo na muziki hekaluni. Walawi tena walitoa sehemu ya kumi ya mapato yao kuwa posho ya makuhani (44-47).

Masomo mengine ya sheria yaliwaonya watu kwamba walipaswa kutunza utakatifu wa hekalu. Wapagani au watu wa mataifa hawakuruhusiwa kuingia hekaluni (13:1-3).

Marekebisho ya Nehemia ya baadaye[hariri | hariri chanzo]

Baada ya miaka 12 ya kuwa liwali wa Yerusalemu, Nehemia alimrudia mfalme wa Uajemi kwa muda (taz. 5:14; 13:6). Wakati ule ambao Nehemia hakuwepo Yerusalemu, dini ya Wayahudi ilirudi nyuma, na maadui wao wa zamani, yaani San-balati na Tobia waliweza kupata nafasi ya ushawishi wao tena Yerusalemu. Kuhani mkuu, Eliashibu, alistahili kulaumiwa zaidi katika mambo hayo. Alimruhusu mtu wa familia ya kuhani mkuu kumwoa binti wa San-balati (taz. mstari 28), pia alimruhusu Tobia aishi katika chumba cha hekaluni. Jambo lile lilikuwa kinyume kabisa cha sheria ambayo Nehemia alijaribu kuitekeleza vizuri, kwa sababu Tobia alikuwa Mwamoni (taz. 4:3; 13:1). Nehemia aliporudi Yerusalemu alirekebisha mambo hayo mara moja (4-9).

Nehemia pia aligundua kwamba watu walikuwa wamevunja ahadi mojawapo ya maana sana ya agano waliyokuwa wametoa wakati wa kuweka wakfu kuta za mji. Hawakutoa zaka zao, na matokeo yake, Walawi walipaswa kuacha huduma yao hekaluni na kwenda mashambani kwao ili kutafuta riziki zao (10-14; taz. 10:35-39).

Pia watu walifanya kazi na biashara siku ya Sabato, na hivyo walivunja sheria nyingine ya ahadi ya agano (15-18; taz. 10:31). Kwa haraka Nehemia alikomesha mambo hayo. Kwa kufunga milango ya mji siku ya Sabato, aliwazuia watu waliotaka kuleta bidhaa zao mjini. Pia aliwazuia wasiuze nje ya malango au kungoja huko wakijiandaa kuuza mara baada ya kupita Sabato (19-22).

Siku za Ezra watu walikuwa wameapa kwamba watawaondoa wake zao wa kigeni, na kweli walifanya hivyo (Ezra 10:19,44). Wakati huo desturi hiyo mbaya ilienea tena, nayo ilitishia kuharibu dini ya Waisraeli. Kwa ushujaa ule uliokuwa tabia ya Nehemia, alirekebisha hali hiyo (23-29). Hakuna shaka lolote kwamba yeye, zaidi ya mtu yeyote, aliwasaidia watu wa wakati ule kutengeneza maisha yao katika msingi wa dini ya kweli kadiri ya sheria ya Mungu (30-31).

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Makala hii kuhusu mtu wa Biblia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Nehemia kama habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.