Nenda kwa yaliyomo

Justino de Jacobis

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mt. Justino de Jacobis

Justino de Jacobis (San Fele, Potenza, Italia, 9 Oktoba 1800 - Eidale, Massawa, 31 Julai 1860) alikuwa mtawa wa Shirika la Misheni (Wavinsenti), halafu askofu na mmisionari nchini Ethiopia na Eritrea.

Anaheshimiwa na Kanisa Katoliki kama mtakatifu tangu tarehe 26 Oktoba 1975. Hata Wakristo wengine na Waislamu wanatembelea kaburi lake kwa heshima.[1]

Sikukuu yake ni tarehe 31 Julai[2][3].

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Akiwa mtoto wa saba wa Giovanni Battista de Jacobis na wa Maria Giuseppina Muccia, tarehe 17 Oktoba 1818 alijiunga na utawa huko Napoli akaweka nadhiri miaka miwili kamili baadaye.

Ingawa kwa unyenyekevu wake mkubwa alitaka kukataa, alipata upadrisho huko Brindisi tarehe 12 Juni 1824.

Kisha kufanya uchungaji huko Oria na Monopoli, alifanywa mkuu wa kanda katika shirika lake kwanza Lecce halafu Napoli. Huko alijitosa kuhudumia waliopatwa na kipindupindu mwaka 1836.

Akiwa huko alielezwa na Kardinali Franzoni juu ya haja ya umisionari nchini Ethiopia.

Mwaka 1839 alichaguliwa kuwa mkuu wa kitume nchini huko ili aanzishe misheni katoliki.

Kwa upole na wingi wa upendo wake, Justino alijitahidi kujifunza vizuri lugha za nchi, kuishi pamoja na wenyeji, akifuata utamaduni wao na mifano ya wamonaki wao.

Vilevile katika uinjilishaji alitumia mapokeo na liturujia ya Ethiopia, akiweka msingi wa Kanisa Katoliki la Waethiopia na wa Kanisa Katoliki la Waeritrea.

Baada ya kufanya kazi hiyo kwa mafanikio makubwa miaka minane, mwaka 1847 aliteuliwa kuwa askofu wa Nilopolis na makamu wa Papa kwa Uhabeshi, ila alikataa uaskofu hadi alipolazimika mwaka 1849.

Ingawa alipaswa kuvumilia njaa na kiu na kupata mapingamizi mengi hasa kutoka kwa Abuna Salama II, askofu mkuu wa Kanisa la Kiorthodoksi la Ethiopia (kufungwa, kufukuzwa n.k.), alifaulu kuanzisha misheni na shule nyingi hasa kwa lengo la kuandaa mapadri wenyeji[4].

Hatimaye askofu mkuu huyo alikiri kwamba hakuna mtu aliyewahi kushika vizuri maagizo na mashauri ya Injili kuliko Justino.

Kati ya watu 12,000 hivi aliowaongoa, mmojawapo ni mwenyeheri Ghebre Mikaeli.

Heshima baada ya kifo[hariri | hariri chanzo]

Kesi ya kumtangaza mwenye heri ilianza tarehe 13 Julai 1904, ikamalizika tarehe 25 Julai 1939 chini ya Papa Pius XII.

Alitangazwa na Papa Paulo VI kuwa mtakatifu tarehe 26 Oktoba 1975, akiwa wa kwanza kati ya wamisionari wa Afrika kusini kwa Sahara.

Mlolongo wa kitume[hariri | hariri chanzo]

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Tom Killion, Historical Dictionary of Eritrea, The Scarecrow Press, 1998, ISBN 0810834375
  2. Martyrologium Romanum
  3. https://catholicsaints.info/saint-giustino-de-jacobis/
  4. https://www.santiebeati.it/dettaglio/33850

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  • Mkusanyo wa maandishi yake - Giuseppe Guerra - Ed. Vincenziani (kwa Kiitalia).
  • Devin, A., (Traduzione inglese di Lady Elizabeth Herbert of Lea), Abyssinia and its Apostle, Burns and Oates, London, 1867
  • Antonio Furioli, L'eucaristia, epifania di dialogo e di comunione. Sua esemplarità in San Giustino de Jacobis in Rivista di ascetica e mistica, 75 (aprile-giugno 2006) 2, 213-228.
  • Antonio Furioli, Il frutto più prezioso dell'apostolato di San Giustino de Jacobis. Il Beato Gabra Mikā’ēl (1791-1855), martire per la fede in Abissinia in Rivista di ascetica e mistica, 75 (luglio-settembre 2006) 3, 385-403.
  • Antonio Furioli, Vangelo e testimonianza. L'esperienza di San Giustino de Jacobis in Abissinia (1839-1860), Milano, San Paolo, 2008.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Makala hii bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.