Nenda kwa yaliyomo

Afrika ya Mashariki ya Kiingereza

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka British East Africa)
Stempu ya posta ya anna 2 1/2, mwaka 1896.

Afrika ya Mashariki ya Kiingereza (kwa Kiingereza British East Africa Protectorate) lilikuwa jina la eneo la Kenya lililowekwa chini ya utawala wa ulinzi wa Uingereza kuanzia mwaka 1895 hadi 1920 BK kama mtangulizi wa koloni la Kiingereza la Kenya.

Historia

[hariri | hariri chanzo]

Wakati wa mashindano ya kugawa Afrika kati ya madola ya Ulaya, Kampuni ya Kifalme ya Kiingereza kwa Afrika ya Mashariki ilianza shughuli zake katika eneo hili kwa kibali cha sultani wa Zanzibar kuanzia mwaka 1888.

Kampuni hiyo ilitakiwa kuwa na mamlaka juu ya eneo hili kwa kusudi la kufanya biashara, lakini uwezo wake haukutosha kutimiza shughuli, hasa maandalizi ya kujenga reli ya Uganda kati ya Mombasa na Kampala.

Baada ya kuazimia kujenga reli, Uingereza iliona haja ya kulinda eneo la reli hiyo: ndipo ikatangaza eneo lote kati ya Mombasa na Uganda kuwa chini ya ulinzi wake kuanzia tarehe 1 Julai 1895. Huo ndio mwanzo wa Afrika ya Mashariki ya Kiingereza ambaye baadaye iliitwa Kenya.

Eneo hilo baadaye lilipanuliwa zaidi hadi kukutana na maeneo yaliyokuwa chini ya utawala wa Italia (Somalia) na Ethiopia upande wa Kaskazini, utawala wa ushirikiano wa Misri na Uingereza (Sudan). Upande wa kusini mpaka ulifuata mapatano na Afrika ya Mashariki ya Kijerumani.

Mpaka na eneo chini ya utawala wa ulinzi wa Uganda ulisahihishwa mwaka 1905; hadi wakati ule sehemu kubwa ya eneo la Kenya ya Magharibi ya leo ilihesabiwa kuwa upande wa Uganda.

Baada ya vita kuu ya kwanza hali ya eneo ilibadilishwa kuwa koloni la Kenya kuanzia 1920.


Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Afrika ya Mashariki ya Kiingereza kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.