Nenda kwa yaliyomo

Augustine Lyatonga Mrema

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Augustine Mrema)
Augustine Lyatonga Mrema
Mh. Mrema
Mh. Mrema
Mwenyekiti wa TLP
Tarehe ya kuzaliwa 1945
Mahali pa kuzaliwa Mkoa wa Kilimanjaro
Tarehe ya kifo 21 Agosti 2022
Chama Chama cha Wafanyakazi Tanzania
Dini Mkristo
Elimu yake Chuo Kikuu cha Cambridge, Chuo Kikuu cha Pacific
Digrii anazoshika Sayansi ya Jamii
Kazi Mwanasiasa


Augustine Lyatonga Mrema (31 Disemba 1945 - 21 Agosti 2022) alikuwa mwanasiasa nchini Tanzania aliyewahi kuwa waziri wa mambo ya ndani. Alianza kama mwanachama wa CCM akahamia baadaye upande wa upinzani.

Maisha ya mwanzo

Augustine Mrema alizaliwa mwaka 1945, huko mkoa wa Kilimanjaro Tanzania, katika kijiji cha Kilaracha kilichopo katika Wilaya ya Moshi vijijini akiwa mzaliwa wa pili katika familia ya watoto watano ya Lyatonga Mrema.

Elimu

Mwaka wa 1955 hadi 1963 alianza masomo yake ya darasani mpaka shule ya kati katika wilaya ya Moshi vijijini. Mwaka wa 1964 mpaka 1965 Mrema alijiunga na Chuo cha Ualimu cha Mtakatifu Patrick. Tangu mwaka 1966 Mrema alikuwa mwanachama mkubwa wa CCM.

Kazi na kujiendeleza kielimu

Baada ya kumaliza mafunzo yake ya ualimu na kupata kazi Mrema alianza kuchukua mafunzo yake ya sekondari ambapo mwaka wa 1968 alifanya mtihani wake wa kidato cha nne, wakati huo mitihani ikitoka Chuo Kikuu cha Cambridge cha nchini Uingereza.

Miaka 1970-1971 alijiunga kwenye mafunzo maalumu ya siasa na uongozi katika Chuo cha Kivukoni na miaka 1980 - 1981 alikwenda nchini Bulgaria ambako alifanikiwa kutunukiwa Diploma ya sayansi ya Ustawi wa jamii na Utawala.

Augustine Lyatonga Mrema baada ya hapo alifanya kazi mbalimbali za kijamii na kichama kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Pacific mwaka 2003 ambako alitunukiwa Shahada ya Sanaa katika Sayansi ya Jamii.

Mrema alianza kazi mwaka 1966-1969 kama mwalimu akifundisha shule mbalimbali za mkoa wa Kilimajaro, na mwaka 1972 na 1973 aliteuliwa kuwa mratibu wa elimu wa kata.

Mwaka 1974 na 1980 Augustine Lyatonga Mrema alichaguliwa kuwa mwalimu wa siasa katika wilaya mbalimbali kwa niaba ya Chama cha Mapinduzi.

Mwaka wa 1980 na 1982 Mrema alichaguliwa kuwa Mwalimu wa Chuo Kikuu cha Usalama wa Taifa na mwaka 1982 hadi 1984 aliteuliwa kuwa Kaimu mkuu wa Usalama wa Taifa kwa mkoa wa Dodoma, mwaka 1983 hadi 1984 aliteuliwa tena kuwa Katibu wa kikosi cha ulinzi na usalama makao makuu Dodoma.

Shughuli za kisiasa

Mwaka wa 1985 Mrema alirudi katika Jimbo lake na kugombea Ubunge huko alipata ushindi mkubwa tu, hata hivyo aliwekewa pingamizi na Mahakama Kuu ya Kilimanjaro na wakati kesi ikiendelea Mrema alipelekwa katika mkoa wa Shinyanga, Wilaya ya Kahama kuwa Afisa Usalama wa Taifa katika wilaya hiyo, hadi mwaka 1987 aliposhinda rufaa yake na kurejeshewa ubunge wake.

Aligombea ubunge kwa mara nyingine mwaka 1990 akafanikiwa kutetea jimbo lake tena safari hiyo kwa kishindo akarudi bungeni kwa mara ya pili.

Baadaye akateuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani kwa mwaka wa 1990 hadi 1994, na wakati huohuo mwaka 1993 hadi 1994 aliteuliwa pia kuwa Naibu Waziri Mkuu, cheo ambacho hata hivyo hakikuwepo kwenye Katiba ya nchi.

Mwaka 1994 alibadilishwa wizara hiyo na kuhamishiwa katika Wizara ya Kazi, Maendeleo ya Vijana na Michezo.

Baada ya kujiengua na chama tawala

Mrema alijiengua na CCM mwaka 1995 na kujiunga na Chama cha NCCR-Mageuzi ambako alikwenda kuwa Mwenyekiti wa Taifa na mgombea Urais kupitia chama hicho, akipata nafasi ya pili katika matokeo, ambayo hata hivyo yalikuwa na dosari, kama alivyokiri miaka ya baadaye Augustino Ramadhani aliyekuwa makamu mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa wakati huo.

Baadaye, kama Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), aligombea urais mara mbili, hiyo ilikuwa mwaka 2000 tena 2005 kwa mara ya tatu kupitia chama hicho cha TLP. Mwaka 2010 alifaulu kuchaguliwa kama mbunge wa Vunjo.[1] Mwaka 2015, ilhali aliendelea kuwa mwenyekiti wa TLP, alimkubali mgombea wa urais kutoka chama cha CCM, John Magufuli.

Rais Magufuli alimteua mwaka 2016 kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Parole ya Taifa.

Marejeo