Nenda kwa yaliyomo

Anjela wa Foligno

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Angela wa Foligno)
Angela akiwa na alama za Mateso ya Yesu.
Kanisa kuu la Mt. Felichano huko Foligno ambapo Angela alikutana na ndugu Arnaldo.
Anjela wa Foligno alivyochorwa na Francesco Mancini katika ukuta wa kuba ya kanisa kuu la Mt. Felichano, Foligno

Anjela wa Foligno (Foligno, 12484 Januari 1309) ni Mkristo wa Utawa wa Tatu wa Mt. Fransisko maarufu kwa vipaji vyake vya kiroho vilivyomfanya aheshimiwe na Kanisa Katoliki kama mtakatifu na msimamizi wa wanawake wajane.

Kwanza alitangazwa mwenye heri na Papa Inosenti XII mwaka 1693, halafu Papa Fransisko alipitisha utakatifu wake tarehe 9 Oktoba 2013.

Sikukuu yake huadhimishwa tarehe ya kifo chake[1].

Kutokana na umuhimu wa maandishi yake kwa teolojia, anaitwa tangu zamani Magistra Theologorum (kwa Kilatini, Mwalimu wa Wanateolojia) na anatarajiwa kutangazwa mwalimu wa Kanisa.

Anjela alizaliwa katika familia tajiri wa Foligno (mkoa wa Umbria, Italia), akaolewa mapema akafuata maisha ya anasa.

Anjela aliongoka alipoungama dhambi zake kwa ndugu yake Arnaldo, kasisi mtawa wa Ndugu Wadogo mwaka 1285 hivi.

Alipotambua dhambi zake kwa mara ya kwanza alishikwa na hofu kubwa kwa wazo la maangamizi ya milele aliyostahili, akalia machozi mengi, lakini kwa aibu hakuziungama, na hata hivyo akasogea meza ya Bwana: “Nikiwa na dhambi zangu niliupokea Mwili wa Yesu Kristo. Lakini usiku na mchana dhamiri yangu haikuacha kamwe kulalamika. Nikamuomba Mt. Fransisko anikutanishe na muungamishi wa kunifaa, ili aweze kunielewa, nami niweze kujifunua kwake… Nikaungama inavyotakiwa na kuondolewa dhambi. Sikuona upendo kabisa, ila uchungu, aibu na sikitiko. Nikadumu kufanya malipizi niliyopewa nikijitahidi kulipa haki, huku najikuta sina kabisa faraja, ila nimejaa uchungu. Halafu nikaanza kuzingatia huruma ya Mungu na kuifahamu hiyo iliyonitoa motoni na kunijalia neema ninayosimulia. Nikapata mwanga wake wa kwanza; uchungu na machozi vikazidi maradufu. Nikajiachia kufanya malipizi makali… Kwa mwanga huo ndani mwangu nikaona nina dhambi tu, nikatambua kwa hakika nimestahili moto wa milele… Faraja yangu pekee ilikuwa kulia machozi. Mwanga mpya ukanionyesha kwa undani ukuu wa dhambi zangu. Ndipo nilipoelewa kwamba, kwa kumchukiza Muumba nilivichukiza viumbe vyote pia. Kwa maombezi ya Bikira Maria na ya watakatifu wote nikaiitia huruma ya Mungu; nikijisikia mfu nikaomba uhai huku nimepiga magoti… Ghafla ikanitokea nijisikie kufikiwa na huruma ya viumbe vyote na watakatifu wote. Hapo nikapokea zawadi, yaani moto mkali wa upendo na uwezo wa kusali jinsi nisivyowahi kamwe… Nikajaliwa ujuzi mkubwa wa jinsi Yesu Kristo alivyokufa kwa dhambi zangu. Nikang’amua ukatili wa dhambi zangu, nikatambua kuwa aliyemsulubisha ni mimi mwenyewe. Ila nilikuwa sijapata kuelewa ukuu usio na mipaka wa faida ya msalaba…"

Baada ya kifo cha mume, watoto na mama yake, alijiunga na Wafransisko wa Utawa wa Tatu mwaka 1291 hivi, akifuata kwa bidii zote mifano ya toba ya Fransisko wa Asizi.

Mwenyewe aliendelea kusimulia kwamba, "Halafu Bwana, kwa wema wake, akanitokea mara nyingi, katika usingizi na katika kukesha, akiwa daima msalabani na kuniambia, Tazama, tazama madonda yangu! Alikuwa akihesabu mapigo ya mijeledi na kuendelea kuniambia, Ni kwa ajili yako, kwa ajili yako, kwa ajili yako… Nikawasihi bikira Maria na mtume Yohane waniombee nipate mateso ya Yesu Kristo, walau yale waliyojaliwa kushirikishwa. Wakanipatia fadhili hiyo, hata siku fulani Mt. Yohane akanishirikisha kiasi kwamba siku hiyo ikawa mojawapo kati ya zile za kutisha zaidi za maisha yangu… Mungu akaandika Baba Yetu moyoni mwangu kwa msisitizo mkubwa wa wema wake na wa unyonge wangu hata siwezi kutamka silabi moja”. Kwa majuto hayo Anjela alishika njia ya utakatifu.

Katika usiku wa roho aliandika, “Najiona sina jema wala adili lolote, nimejaa wingi wa vilema… rohoni mwangu naona kasoro tu… Ningependa kuwajulisha wengine kwa sauti kubwa uovu wangu… Mungu amejificha kwangu… Niwezeje kumtumainia?… Hata kama wenye hekima wote waliopo duniani na watakatifu wote wa mbinguni wangenijaza faraja zao, wasingenisaidia chochote kabla Mungu hajabadili undani wa roho yangu. Tabu hiyo ya ndani ni mbaya sana kuliko kifodini”.

Baada ya hapo, akikumbuka mateso ya Kristo, alitamani tabu hiyo iongezeke kwa kuwa inatakasa na kufunua vilindi vya mateso hayo. Siku chache baadaye, akiwa njiani alisikia kwa ndani maneno yafuatayo, “Binti yangu, nakupenda kuliko yeyote wa bonde hili… Fransisko alinipenda sana nikamtendea mengi; lakini mtu angenipenda kuliko Fransisko ningemtendea mema mengi zaidi… Nampenda upeo yule anayenipenda bila ya uongo… Hakuna anayeweza kujisingizia, kwa kuwa wote wanaweza kupenda; Mungu anaomba upendo tu, kwa kuwa mwenyewe anapenda bila ya uongo, naye ndiye upendo wa roho”. Yesu msulubiwa akimuonyesha kidogo mateso yake akaongeza, “Tazama vema: je, ndani mwangu unakuta chochote kisicho upendo?”

Mang'amuzi mengine aliyoshirikisha ni kama haya yafuatayo: “Siku moja roho yangu ilinyakuliwa, nikamuona Mungu katika uangavu mkubwa kuliko wowote niliowahi kujua… Nilimuona Mungu katika giza, na ni lazima liwe giza, kwa kuwa yuko juu mno kuliko roho, na lolote linaloweza kufikiriwa halilingani naye… Sioni kitu ila naona yote; hakika inapatikana katika giza. Kadiri giza lilivyo nene, wema unazidi yote. Ni fumbo lililofichika… Uweza, hekima na utashi wa Mungu, nilivyoviona vizuri ajabu siku nyingine, natambua ni kidogo kuliko hilo. Hilo ni kitu kizima, hivyo ni kama sehemu zake tu”. Maana yake, sasa sioni kitu maalumu, ila naona sifa zote za Mungu zimeunganika vizuri ajabu katika ukuu wake unaozidi akili yangu.

Kuhusu ekaristi aliandika: “Sina dhana tupu, bali hakika kabisa ya kwamba roho ingeona na kutazama kwa dhati kiasi fulani cha uangavu wa ndani wa sakramenti ya altare, ingewaka moto kabisa, kwa kuona upendo wa Mungu. Naona kwamba wanaotoa sadaka au kuihudhuria wanatakiwa kutafakari kwa dhati ukweli mkuu wa fumbo takatifu mno, ambalo tuzame ndani yake na kutulia tusigeuke”.

Inaaminiwa kuwa Ndugu Arnaldo ndiye aliyeandika kwa Kilatini "ukumbusho" wa yale aliyoshirikishwa na Anjela kuhusu mang'amuzi yake ya kiroho, ambayo yanahesabiwa na wataalamu kuwa ya juu kabisa, hasa kuhusu fumbo la Utatu.

Maandishi hayo yanaelekeza haya: hatua thelathini za roho hadi kufikia muungano wa dhati na Mungu, kupitia tafakuri ya mafumbo wa Yesu Kristo, Ekaristi, vishawishi na malipizi.

Ukumbusho huo ni sehemu ya kwanza ya Liber (kwa Kilatini, Kitabu), ambapo sehemu ya pili, inayoitwa Instructiones (Mafundisho), inakusanya hati mbalimbali zilizotungwa na watu tofauti wasiojulikana, pamoja na barua ambazo Anjela aliwaandikia wafuasi wake wengi.

Sala yake

[hariri | hariri chanzo]

Mungu wangu, unijalie kujua fumbo kuu linalotokana na moto wa upendo wako usiosemeka na wa Nafsi tatu za Utatu, yaani fumbo la umwilisho wako mtakatifu uliotaka kutekeleza kwa ajili yetu.

Ndio mwanzo wa wokovu wetu nao unatenda mambo mawili ndani mwetu: kutujaza upendo na kutuhakikishia ukombozi wetu.

Lo, upendo usioweza kueleweka kwa yeyote! Hakuna upendo mkuu kuliko huo: Mungu wangu amejifanya mtu anifanye niwe Mungu!

Lo, upendo la kupita kiasi: umejiharibu ili kunitengeneza wakati ulipotwaa mwili wetu.

Si kwamba wewe au umungu wako umekuja kupungukiwa kitu, ila kina cha umwilisho wako kinanitoa midomoni maneno yenye hisia kali!

Wewe, usiyeeleweka, umejifanya wa kueleweka; wewe usiyeumbwa umejifanya kiumbe; wewe usiyefikirika, umekuja kufikirika; wewe Roho tupu umekubali kuguswa na mikono ya watu!...

Ee Mkuu kabisa, uniwezeshe kuelewa zawadi hiyo ipitayo nyingine yoyote: malaika na watakatifu wote heri yao pekee ni kukuona, kukupenda na kukutazama!

Ee zawadi ya juu kuliko yoyote, kwa kuwa wewe ndiwe zawadi yenyewe, ndiwe Upendo!

Ee Wema mkuu, umekubali kujulikana kama Upendo, na unatufanya tuupende Upendo huo.

Wale wote watakaofika mbele yako watapata raha kadiri ya upendo waliokuwanao kwako.

Tazama pia

[hariri | hariri chanzo]
  1. Martyrologium Romanum: ex Decreto Sacrosancti oecumenici Concilii Vaticani II instauratum auctoritate Ioannis Pauli P.P. II promulgatum, Romae 2001, ISBN 8820972107
  • McGinn, Bernard (1998). The Flowering of Mysticism. ku. 143–144. {{cite book}}: Invalid |ref=harv (help)</ref>

Maandishi yake

[hariri | hariri chanzo]

Kitabu cha Mt. Angela kinaundwa na Memoriale na Instructiones.

  • A critical edition is Ludger Thier and Abele Calufetti, eds, Il libro della Beata Angela da Foligno, (Rome: Editiones Collegii S. Bonaventurae, 1985)
  • Angela of Foligno, Complete works, translated, with an introduction by Paul Lachance; preface by Romana Guarnieri, (New York: Paulist Press, 1993)
  • Angela of Foligno, Memorial, translated by John Cirignano, (Woodbridge: D.S. Brewer, 1999)

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
WikiMedia Commons
WikiMedia Commons