Vuje
Vuje ni kata ya Wilaya ya Same katika Mkoa wa Kilimanjaro, Tanzania.
Wakati wa sensa iliyofanyika mwaka wa 2022, kata ilikuwa na wakazi wapatao 10,828 [1]. Wakati wa sensa iliyofanyika mwaka wa 2012, kata ilikuwa na wakazi wapatao 10,726[2] walioishi humo.
Wenyeji wa kata hiyo ni Wapare "Vaasu" japo kuna muingiliano wa makabila mengi kutoka Tanzania na hata raia kutoka nje ya Tanzania.
Jiografia na uchumi
[hariri | hariri chanzo]Kata ya Vuje Upande wa Kaskazini imepakana na Msitu wa Shengena, upande wa Magharibi imepakana na Kata ya Bombo mashariki imepakana na Kata ya Mbaga na kusini Kata ya Maore.
Magharibi mwa kata ya Vuje unatiririka mto mkubwa ambao chanzo chake ni msitu wa Chome (Shengena): mto huo ni Hingilili ambao unatengeneza maporomoko makubwa yanayojulikana kwa Kipare kama Ndurumo. Pia katika kata ya Vuje kuna mapango ambayo yana masalia ya binadamu wa kale ambayo yanaweza kutumika kama marejeo kwa wanafunzi kuthibitisha kuwa binadamu wa kale aliishi mapangoni.
Katika kata ya Vuje pia ni lango la kuingilia Msitu wa Chome ambako kunapatikana kilele cha Shengena 2462m juu ya usawa wa bahari ambacho ni kilele cha pili kwa urefu katika mkoa wa Kilimanjaro ambapo cha kwanza ni Mlima Kilimanjaro.
Misitu mingine midogo inayopatikana katika kata ya Vuje inayoweza kuvutia utalii wa mazingira ya asili ni Nkhanga, Mphombesela, Mbogweni na Kitala. Ukiwa juu ya kilele cha msitu wa Nkhanga asubuhi sana hali ya hewa ikiwa nzuri, unaona theluji ya mlima Kilimanjaro.
Misitu mingine maarufu inayopatikana sehemu inayojulikana kama Hemtema ni Msara wa kuvoka, Msara wa keri na Msara wa katatu. Majina hayo yanatokana na miti mingi inayopatikana kwenye hiyo misitu inajulikana kwa kipare kama Msara.
Pia kuna jiwe kubwa sana ambalo wakazi huliita "Bweteta" yaani "jiwe linalosema".
Kuna mandhari ya kuvutia ukiwa katika kata hiyo ukitazama uwanda wa chini ambapo unaweza kuona safu za milima ya Usambara na nchi ya Kenya na bonde zuri ambalo ni maarufu kwa kilimo cha mpunga.
Wakazi wa kata ya Vuje ni maarufu kwa kilimo cha tangawizi, ndizi, mahindi, maharagwe, kahawa na mbogamboga. Pia ni wafugaji wa ng'ombe wa maziwa, mbuzi, kondoo, nguruwe, kuku, bata, njiwa. Pia wenyeji wanajihusisha na ufugaji wa samaki kwenye mabwawa ambayo ni maarufu kwa jina la "madimbwi" au "ndiva"
Kwa kuwa kata ya Vuje ni sehemu yenye rutuba sana panapatikana aina nyingi za matunda kama maparachichi, mafenesi, mapera, stafeli, matungululu.
Watu na huduma
[hariri | hariri chanzo]Katika suala la kumcha Mwenyezi Mungu, kuna makanisa, misikiti na pia misitu midogomidogo ya asili ilitumika kipindi cha nyuma kama sehemu ya ibada na kufundishia vijana jandoni; na pia sehemu ya kufanyia matambiko ya kuomba mvua, kuondoa majanga yaliyoikumba jamii na hata kutoa shukrani kwa mizimu "nkoma"; misitu hiyo bado imebaki katika uasili wake.
Vuje pia kuna shule za msingi, sekondari na chuo cha ufundi Ntenga.
Ni katika kata hii ndipo kunapatikana sehemu yenye ukumbi mkubwa ambao hutumika kama sehemu ya starehe "disco"; ni maarufu kama "Vuje Social Hall".
Wenyeji wa kata ya Vuje wanaokumbukwa kwa kuleta maendeleo katika kata ni pamoja na:
- Mfumwa Mbwana Yateri alikuwa mtawala wa Gonja (chifu)
- Marehemu Ali Kadeghe - alikuwa mfanyabiashara, Muuza nyama ya ng'ombe, alilea mashehe waliokuwa wakieneza dini ya Uislamu, alihamasisha kujengwa kwa shule ya msingi "Msindo - Vuje" na pia alihamasisha sana kujenga Barbara ya Vuje.
- Marehemu Eliaza Samiji - mfanyabiashara maarufu, anatajwa kama mwanzilishi wa mji wa kibiashara kati ya kata ya Vuje na Bombo na maeneo ya jirani - "Kivukoni" ambapo mji huo panapatikana hospitali kubwa ya "Bombo Lutheran Hospital" na nyumba maarufu ya "Vuje Guest House". Kwa sasa Kivukoni ni "Shopping Centre" katika ukanda wa milimani.
Wasomi maarufu kutoka kata ya Vuje ni pamoja na:
- Profesa Ernesti Semu - mtaalamu wa udongo katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) - Morogoro
- Profesa A. H. Katani - kutoka Institute of Technology (DIT) -Dar es Salaam
- Elly Elikunda Elineema Mtango - balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huko Tokyo, Japan ambaye pia ameidhinishwa kwa Australia, New Zealand na Papua New Guinea. Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje Tanzania 19.12.1995 - 13.02.2000
- Hamphrey Mgonja - mtangazaji maarufu wa BBC - Swahili
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ https://www.nbs.go.tz
- ↑ "Sensa ya 2012, Kilimanjaro - Same DC" (PDF). Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2016-03-03. Iliwekwa mnamo 2016-05-21.
Kata za Wilaya ya Same - Mkoa wa Kilimanjaro - Tanzania | ||||
---|---|---|---|---|
Bangalala | Bendera | Bombo | Bwambo | Chome | Gavao Sawene | Hedaru | Kalemawe | Kihurio | Kirangare | Kisima | Kisiwani | Lugulu | Mabilioni | Makanya | Maore | Mhezi | Mpinji | Mshewa | Msindo | Mtii | Mwembe | Myamba | Ndungu | Njoro | Ruvu | Same Mjini | Stesheni | Suji | Tae | Vudee | Vuje | Vumari | Vunta
|