Viti maalum vya wanawake
Viti maalum vya wanawake ni nafasi bungeni zinazotolewa kwa utaratibu unaopatikana katika nchi mbalimbali na unaolenga kuongeza idadi ya wanawake na athira yao katika bunge na mabaraza na kwa njia hiyo katika siasa ya nchi hizo kwa jumla.
Kuna nchi nyingi za dunia zilizochukua hatua za kuongeza nafasi za wanawake serikalini kulingana na mkataba kuhusu ufutaji wa ubaguzi wote wa wanawake (Convention on the Elimination of All Forms of Discrimination Against Women) uliosainiwa na mataifa 189 tangu kuanzishwa mwaka 1981 na kuimarishwa na azimio la Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa mwaka 2011. [1].
Nchi zinazotumia utaratibu wa viti maalumu vya wanawake katika bunge zao
[hariri | hariri chanzo]Kati ya hatua hizo ni utaratibu wa kisheria wa kutenga sehemu ya viti vya bunge za kitaifa kwa wanawake pekee. Mnamo mwaka 2013 utaratibu huo ulitumiwa katika nchi 36, hasa za Afrika na Asia Kusini.
Katika Amerika ni nchi ya Haiti.
Katika Afrika ni nchi za Algeria, Burundi, Djibouti, Eritrea, Eswatini, Guinea, Kenya, Lesotho, Libya, Mauritania, Morocco, Niger, Rwanda, Sierra Leone, Somalia, Sudan Kusini, Sudan, Tanzania, Uganda na Zimbabwe.
Katika Asia ni nchi za Afghanistan, Bangladesh, China, India, Iraq, Jordan,Palestina, Saudi Arabia, Pakistan, Philippines, Samoa, Taiwan, Timor-Leste na Vanuatu.
Mifumo mbalimbali
[hariri | hariri chanzo]Nchi nyingi hutenga idadi ya viti vya wabunge kwa ajili ya wanawake wanaochaguliwa kwa namna za pekee. Mara nyingi wananchi hupiga kura mara mbili, kwanza kwa wawakilishi wao kwa jumla halafu kura ya pili kwa ajili ya wanawake pekee.
Kuna pia nchi ambazo zimeanzisha majimbo ya uchaguzi kwa ajili ya wagombea wanawake pekee.
Nchi chache hutumia mfumo kama Tanzania ambako takriban theluthi 1 ya viti kwenye bunge ni viti maalumu ya wanawake wanaoingia baada ya kutajwa na vyama vya kisiasa lakini bila kupigiwa kura.[2]
Tanbihi
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Resolution adopted by the General Assembly on 19 December 2011 - 66/130 Women and political participation, Tovuti ya Umoja wa Mataifa undocs.org, iliangaliwa Mei 2017
- ↑ "Fungu 66, 1b ya Katiba ya Tanzania" (PDF). Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2017-05-16. Iliwekwa mnamo 2017-05-15.
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- Tovuti ya quotaproject.org Ilihifadhiwa 14 Machi 2017 kwenye Wayback Machine. (mradi wa International IDEA, Inter-Parliamentary Union na Chuo Kikuu cha Stockholm)
- Atlas of Electoral Gender Quotas Ilihifadhiwa 23 Aprili 2017 kwenye Wayback Machine.