Vitabu vya hekima

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Miongoni mwa aina za vitabu vya Biblia vipo vile vinavyojulikana kama vitabu vya hekima.

Kati ya vitabu hivyo, Agano la Kale lina Methali , Kitabu cha Yobu, na Mhubiri, ingawa hata baadhi ya Zaburi na sehemu za vitabu vingine pia vinaweza kuhesabiwa kuwa ni maandiko ya hekima. Tena, kati ya Deuterokanoni, Kitabu cha Yoshua bin Sira na Kitabu cha Hekima ni vitabu vya hekima.

Upande wa Agano Jipya, ni hasa Waraka wa Yakobo ulioendeleza mtindo huo wa uandishi.

Maana ya vitabu hivyo[hariri | hariri chanzo]

Kadiri ya Biblia, Mungu alitumia aina mbalimbali za watu, kama vile wahubiri na walimu, ili kuwafundisha na kuwaongoza watu wake.

Alitumia makuhani ili katika kuendesha ibada wafundishe na kuangalia sheria yake (Law 10:8-11; Kum 33:10; Mal 2:7), na manabii ili walete ujumbe wa kufunulia makusudi yake na kuwageuza watu waache dhambi zao na kumtii Mungu (Eze 2:3-5; Amo 3:1, 7-8; Mik 3:8).

Pia alitumia walimu wa hekima. Watu hao wenye hekima walikuwa miongoni mwa walimu maalumu katika Israeli (Yer 18:18; Isa 29:14). Hawakujidai kuwa wamepata ufunuo wa pekee kutoka kwa Mungu, bali walieleza mambo ya maisha ya kila siku kama watu wenye imani, wakawafundisha wengine njia iliyo bora (Mhu 12:9-10).

Wenye hekima ni watu wanaopatikana katika makabila yote, hasa kati ya wazee wenye mang’amuzi mengi. Toka zamani watu wa namna hiyo walitegemewa kwa malezi ya vijana ili wajue jinsi ya kukabili vizuri maisha. Mbali na mithali na mafundisho yaliyotolewa kwa sauti, baada ya uandishi kubuniwa hata vitabu vya namna hiyo vilianza kutungwa katika lugha mbalimbali.

Waisraeli walifaidika na hekima ya nchi jirani zilizostaarabika zaidi, kwa namna ya pekee Mesopotamia na Misri. Hasa wakati wa amani na ustawi uliopatikana chini ya mfalme Solomoni, wenye hekima waliweza kujitokeza katika Israeli, kuanzia mwenyewe: ndiyo sababu aliendelea kuchukuliwa kama kielelezo cha hekima.

Maandiko ya Biblia yanayotokana na walimu wa hekima yanaonyesha kwamba watu hao waliweza kutazama mambo ya maisha kwa namna mbalimbali, hata mwalimu yuleyule aliweza kutafakari mambo muhimu akiangalia sehemu tofauti. Kwa mfano, mwandishi wa Mithali anakubali kwamba kanuni za kawaida si lazima zifae kwa kila jambo (Mit 26:4-5), ambapo waandishi wa Ayubu na Mhubiri wanatambua kwamba, ingawa kuna hali ya pekee au isiyo ya kawaida, kanuni za kawaida bado ni msingi wa mafundisho ya hekima (Ayu 28:20-28; Mhu 7:1-13).

Walimu wa hekima walikuwa wachaji wa Mungu waliotazama maisha pamoja na ugumu na furaha yote, ili wawasaidie watu wa Mungu watambue makusudi ya maisha waliyopewa na Mungu. Ingawa waliweza wakatambua maisha ya baada ya kufa (Ayu 19:26), lengo lao kuu lilikuwa kushughulika na mambo yanayowakabili watu katika maisha ya sasa.

Utunzi wa vitabu hivyo[hariri | hariri chanzo]

Pengine ni wakati wa kurudi toka uhamisho wa Babeli kwamba, baada ya muda mrefu wa mapokeo ya sauti, vilianza kuandikwa vitabu hivyo (Mithali, Ayubu) na vinginevyo (Wimbo Ulio Bora, Zaburi nyingi). Ingawa vinafanana na vile vya makabila ya jirani, vile vilivyomo katika Biblia vinafikiria maisha kwa mwanga wa imani katika Mungu aliye mmoja tu, hasa kwa kuzingatia uzima na kifo, uchungu, mwenendo, heri n.k.

Mithali ndicho kitabu cha kwanza cha aina hiyo, hivyo kinatuletea mawazo na maneno ya zamani zaidi na ya kwamba Mungu anamtuza mwadilifu na kumuadhibu mwovu hapa duniani.

Kitabu cha Ayubu kinakataa mtazamo huo kwa kuonyesha hali halisi, yaani kuwa duniani mara nyingi mwadilifu ndiye anayeteseka; hata hivyo binadamu hawezi kujua ni kwa nini: basi amuachie Mungu na kumuabudu katika fumbo lake linalozidi akili yetu (42:1-6).

Wimbo ulio Bora haumtaji Mungu wala dini: ulihusu mapenzi ya wachumba, lakini ukaja kufafanuliwa kama mapenzi ya Mungu na Israeli wanaotafutana ili kuungana kabisa.

Zaburi, ambazo zilitungwa na kurekebishwa polepole kwa muda unaokaribia miaka elfu, yaani muda ule wote uliotumika kutunga vitabu vingine vyote vya Agano la Kale, ndizo sala za kishairi au nyimbo ambazo katika hali ya sifa, ibada, shukrani na dua zinajumlisha Biblia nzima.

Halafu chini ya utawala wa Kiyunani, unabii ulipokuja kwisha (1Mak 9:27), badala yake yalitolewa maandiko ya kiapokaliptiko (hasa kitabu cha Danieli ambacho ni kama Kitabu cha Ufunuo cha Agano la Kale), hadithi (Kitabu cha Yona, Kitabu cha Tobiti, Kitabu cha Esta, Kitabu cha Yudith) na vitabu vingine vya hekima (Mhubiri, Yoshua bin Sira, Hekima). Humo tunaona maendeleo ya ufunuo, hasa kwa sababu Wayahudi wengi walianza kusadiki ufufuko wa wafu na mengineyo.

Mhubiri alisisitiza ubatili wa malimwengu yote (1:1-11) akimuunga mkono mwandishi wa Ayubu: mang’amuzi yanaonyesha matarajio ya kidunia hayana maana (8:10-17).

Yoshua bin Sira alikabili pia masuala hayo (15:11-16:23), akituelekeza tutafute jibu katika siku ya mwisho.

Kitabu cha Hekima kinakisiwa kuwa cha mwisho kuandikwa kabla ya Yesu kwa kuwa kilitungwa miaka 50 tu K.K. huko Misri katika lugha na utamaduni wa Kiyunani. Kina mpango mzuri sana na kutoa jibu wazi kuhusu suala la haki ya Mungu kwa waadilifu na waovu, kikifundisha uzima wa milele (2:23-3:10) hata kuliko kilivyowahi kufanya kitabu cha Danieli (12:1-4).

Kuelekea Agano Jipya[hariri | hariri chanzo]

Baada ya Torati kuzidi kuzingatiwa na Wayahudi, wataalamu wake pia walizidi kuheshimiwa kama watu wa Neno la Mungu, wanaoleta mwanga wake katika maisha ya jamii. Hekima, iliyotafutwa hasa chini ya Wagiriki, ilipotambulika kuwa inapatikana katika Torati, wataalamu hao wakaja kushika nafasi ya watu wa hekima kama vile hao walivyoziba pengo lililoachwa na manabii.

Wayahudi walizoea hali hiyo kiasi kwamba wakaona vigumu kumkubali Yesu ambaye hafafanui Torati kwa kufuata mapokeo ya wataalamu, bali kwa kujiamini kama manabii waliojiona wabebaji wa Neno la Mungu. Kadirio ya Ukristo ndiye Hekima ya milele ambaye ndani yake tunamjua Mungu, hivyo mwenendo wake na mafundisho yake haviwezi kuishia mambo yaliyozoeleka, kwa sababu kila mara ya Mungu yanapindua ya binadamu. La kufanya ni kujitahidi kufuata halafu kuelewa: ndiyo wongofu ambao Yesu aliudai pamoja na imani.

Waraka wa Yakobo[hariri | hariri chanzo]

Kitabu hicho ambacho labda kiliandikwa miaka ya 80 kina jina la Yakobo, lakini wataalamu hawapatani kuhusu huyo ni nani, aliandika wapi na lini.

Kwa hakika walengwa wa kitabu ni Wakristo wa Kiyahudi wenzake, lakini si barua halisi, bali ni mchanganyiko wa mawaidha yanayofuata mtindo wa vitabu vya hekima.

Lengo lake ni kuhakikisha Ukristo usiishie katika mawazo mazuri, bali imani ijitokeze katika matendo mema.

Lengo lingine ni kuwakuza mafukara na kuwakemea matajiri, kadiri ya mwelekeo wa Kanisa la Yerusalemu (Yak 1:1-2:26; 4:1-5:6).

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]