Nenda kwa yaliyomo

Ring'wani

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Ring'wani ni kata ya Wilaya ya Serengeti lakini pia kijiji katika wilaya ya Serengeti katika Mkoa wa Mara, Tanzania, yenye postikodi namba 31614.

Kata ya Ring'wani inaundwa na vijiji vya Remung'orori, Maghange, Masinki, Ring'wani Nyamitita na Kenyana ambacho ni kitovu na mhimili mkubwa kwa eneo la Ngoreme kwani ndicho kijiji kinachopakana na koo tata za kabila la Wakurya wanaojihusisha sana na uporaji wa mifugo wilayani Serengeti na hasa katika eneo la Ngoreme.

Katika sensa ya mwaka 2022 wakazi wa kata walihesabiwa kuwa 12,508 [1]. Kwa mujibu wa sensa iliyofanyika mwaka wa 2012, kata ilikuwa na wakazi wapatao 8,785 waishio humo.[2]'

Historia[hariri | hariri chanzo]

Historia ya watu na maeneo kama ilivyo jamii ya Ring'wani hujengwa na mafanikio au wasifu wa jamii husika hasa watu wake mashuhuri katika maisha ya kisisasa, kiuchumi, kitamaduni na kijamii, hasa kwa watu wale waliofanya mabadiliko chanya katika jamii.

Kijijini Kenyana ndiko alikoishi Nsaho Maro, mzee maarufu miongoni mwa waasisi wa TANU na baadaye Chama cha Mapinduzi (CCM). Mzee huyo alikuwa mstari wa mbele katika maendeleo ya Mkoa wa Mara, hasa Wilaya ya Serengeti na kijiji cha Kenyana kwa kuchangia ujenzi wa shule, zahanati, mahakama, na kituo cha polisi. Nia yake ilikuwa kuasisi kijiji cha kisasa chenye miundombinu yote muhimu. Nsaho alikuwa na ushawishi mkubwa katika jamii ya Ngoreme sambamba na wazee wenzake kutoka vijiji vingine vya Ngoreme kama James Baker (Bega) Ruge, Masiko Moghita, Maro Sosera, Hitler, Chacha Mangari, Mwita King'orori (Masase), James Makenge Ruge, Masosota Ighonga, Pius Maghoko Makongo, Maisori Tumbo, Herman, Petro Maswe, January Waisariro, Chacha Soghora, Wambura Bhwana, Nyambabhe, Renterenge, Maro Kyariga, Nyarukobha na baadaye kijana waliyemlea na kumwingiza katika siasa za Ngoreme, Faustine Maro Ruge. Wazee haO walihusika sana katika kuendeleza amani na mshikamano baina ya koo za Waikoma, Wangoreme, Wanyabasi, Wakira na koo nyingine za Kikurya.

Kijiji cha Ring'wani kilianza baada ya familia kadhaa za ukoo wa Ruge kuhamia katika eneo lao la asili tangu jadi, wakitokea pande za Roghoro na Majimoto walikokuwa Wakiishi uhamishoni tangu miaka ya 1940. Wazee wao walihama maeneo ya Ring'wani ya sasa wakati huo kutokana na mbung'o waliosababisha magonjwa ya mifugo na uvamizi wa mara kwa mara wa Wamasai.

Hizo familia za ukoo wa Ruge, wafugaji wakiongozwa na mfanyabiashara maarufu na mwanasiasa tajiri mfugaji James Makenge Ruge, aliyekuwa kiongozi wa ukoo huo, aliambatana na ndugu zake wakina Mahiti Chacha Bhayayi, Mtongori Mhoni, Ghiraita Ruge, Maro Muhoni na hakimu wa kwanza Mongoreme kuwahi kuhudumu katika mahakama ya mwanzo kwa kutumia lugha ya Kiswahili, Ferdinand Makore Ruge, na baadaye wakahamia William Moremi Ruge na mwanasiasa mashuhuri Kepteni Faustine Maro Ruge, mdogo wake James Makenge Ruge. Wazee wengine walihamia baadaye kama familia ya Nyaruchowa, Nyanduku, Kiroche, Nyamarasa, Ighonga,Temweni na wengineo.

Kijiji kilianzishwa rasmi mwaka 1977 baada ya kumeguka kutoka katika kijiji cha Ujamaa Kemgesi. Katika kijiji hicho ndiko asili ya ukoo wa Ruge unaofahamika kwa kuwa na wasomi wengi waliobobea katika nyanja mbalimbali.

Kijiji cha Ringwani, kisiasa kina sifa ya kutoa wanasiasa mashuhuri kwani kiliwahi kutoa mwenyekiti wa CCM wa wilaya ya Serengeti 1982-1992 na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa Kepteni Faustine Maro Ruge ambaye pia aliwahi kuwa Diwani wa Kata ya Ring'wani kati ya miaka 2000 na 2005. Yeye alichangia sana maendeleo ya kielimu wilayani Serengeti kwani ndiye mwasisi wa ujenzi shule zasSekondari za kwanza wilayani humo yaani, shule za sekondari Ngoreme, Serengeti, Issenye Nyabhehore, na Kambarage, ambazo alihakikisha zinajengwa kwa nguvu ya wananchi na kusajiliwa kinyume cha sera ya serikali wakati huo.

Baadaye kijiji hicho kilimpata mbunge wa jimbo la Serengeti Dr. Deogratias Mwita kuanzia mwaka 1991 mpaka 2000, ambaye alifikia kuwa Naibu Waziri wa Serikali za mitaa katika serikali ya awamu ya tatu ya Rais Benjamin Mkapa na baadaye Mkuu wa Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro. Yeye alifanikiwa kukomesha wizi sugu wa mifugo kwa kudumisha urafiki maalum wa kimila baina ya Wangoreme na koo za Wakurya wilayani Serengeti sambamba na rafiki yake Ruge. Mwita anafahamika kwa umahiri wake wa kutumia lugha ya Kengoreme jukwaani.

Wilayani Serengeti Kijiji cha Ring'wani kinafahamika kwa kutoa wanasiasa mahiri hata katika medani ya taifa: Kapteni Faustine Maro Ruge na aliyekuwa rafiki yake mkubwa, Dr. Deogratias Mwita, wote ni wenyeji wa kijiji hicho. Ruge ndiye aliyemwingiza kwenye siasa Deogratias Mwita, na baadaye inasemekana ugomvi baina yao ulisababisha kuanguka na kufutika kabisa kisiasa kwa Dr. Mwita aliyejaribu mara kadhaa kurudi kwenye ulingo wa siasa bila mafanikio. Ruge ni mwanajeshi mstaafu wa JWTZ akiwa amewahi kuwa kamanda mwandamizi na mkuu wa vikosi mbalimbali nchini. Tanzania ikiwa moja ya nchi za mstari wa mbele Ruge alipata fursa ya kushiriki kikamilifu katika harakati za ukombozi wa bara la Afrika akihusika katika kufundisha wapigania uhuru hasa wa FRELIMO na ZANU PF na hata kushiriki na kuongoza harakati za siri za kijeshi na mapambano katika mataifa mbalimbali yakiwamo Msumbiji, Angola, Afrika Kusini, Komoro, Shelisheli, Namibia, Zimbabwe na Uganda aliposhiriki kwa nguvu katika harakati za kumwondoa madarakani dikteta wa nchi hiyo Idd Amin Dada, ambapo pia alibaki katika kazi maalumu ya kuilinda nchi hiyo hadi mwaka 1982. Ruge ametunukiwa medani mbalimbali za utumishi uliotukuka ikiwamo nishani ya vita (Medal for Victory in Uganda), Nishani ya Kagera, Nishani ya Zimbabwe, Nishani ya Ujasiri na nyingine kadhaa. Ruge ni mmoja kati ya askari wawili wa kwanza wakati wa vita vya Kagera walioshuhudia na kuthibitisha kuwa daraja la Kagera limevunjwa na askari wa Idd Amin. Ruge ndiye kamanda aliyeongoza zoezi la kufungua vyumba vya mateso vya dikteta huyo na kuachilia huru wafungwa wengi wa kisiasa mara baada ya kuiokomboa Uganda. Ruge alipewa kazi maalum ya kulinda kituo cha kurushia matangazo cha Radio Uganda. Baadaye alirudishwa Entebbe kwa kazi ya kulinda ikulu ya nchi hiyo na kuhakikisha usalama wa marais Godfrey Lukongwa Binaisa, Yusuf KirondeLule na Paulo Muwanga. Baadaye tena yeye na wenzake walisimamia uchaguzi ambao ulifanyika mwaka 1980, wa kwanza baada ya kumwondoa madarakani Idd Amin; uchaguzi huo ulikuwa na ushindani mkali kati ya Paul Ssemogerere na Sir Milton Obote. Uchaguzi huo uligubikwa na utata uliopelekea machafuko baada ya Obote, aliyekuwa rafiki mkubwa wa Julius Nyerere, kutangazwa mshindi. Machafuko hayo yalisababisha vifo vingi vya askari wa Tanzania hali iliyopelekea Ruge kupewa kazi maalum ya kutuliza na kukomesha maasi hayo katika jiji la Kampala na Entebbe.  

Ruge, akiwa ameanza siasa tangu mwaka 1982 ambapo wanajeshi walikuwa wanaruhusiwa kushiriki siasa, anafahamika kwa umahiri wake wa kuzungumza jukwaani na ushawishi mkubwa katika siasa za wilaya hiyo, anaheshimika kwa kuasisi na kusimamia ujenzi wa shule ya msingi Kemalambo iliyoko kijijini kwake Ring'wani, na ujenzi wa shule za Sekondari Serengeti, Kambarage Nyerere na Ngoreme, aliasisi pia ujenzi wa shule za sekondari Nyabehore na Isenye ambazo baadae zilikabidhiwa kwa taasisi za kidini kutokana na uwezo mdogo wa Serikali na wananchi wakati huo (kwa vipindi tofauti alikuwa mwenyekiti wa bodi za shule hizo). Kitendo cha ujenzi wa shule hizo kwa wakati mmoja mwanzoni na katikati ya miaka ya 1980 kilimsababishia maswali mengi kutoka kwa Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyeamini zaidi katika uboreshaji wa Shule za Misingi wakati huo. Nyerere akiwa Mwenyekiti wa CCM Taifa alimshauri Ruge kujikita zaidi katika katika elimu ya msingi kwani ndiyo elimu iliyopatikana kwa wengi vijijini lakini Ruge aliamini katika maendeleo ya mapema katika jamii yake endapo vijana wangesoma elimu ya juu kwanza.

Baadaye, wageni walizidi kuhamia kwa ajili ya uchimbaji mdogomdogo wa madini ya dhahabu katika eneo la Kemalambo kwani pia kijiji cha Ringwani kimekuwa eneo linalovutia kwa kuwa njiapanda ya kijiji kikubwa cha Kemgesi na njiapanda ya kijiji cha Maburi na pia kijiji hicho kimepitiwa na barabara ya mkoa kutoka Musoma kwenda Mugumu hadi Arusha.

Kwa siku za karibuni Ring'wani kuna vuguvugu la wananchi kujiletea maendeleo, mfano katika ujenzi wa zahanati kwa kutumia nguvu zao wenyewe, kwani licha ya kuwa na wanasiasa mashuhuri hakukuwahi kuwa na kituo cha afya, kwa sababu kijiji hicho kina matatizo makubwa ya misuguano baina ya koo za Waireghe na Wabhwiro ambayo imekwamisha baadhi ya maamuzi muhimu ya maendeleo kwa miaka mingi. Uharibifu wa misitu na uchomaji hovyo wa majani Ring'wani ni vitendo viliyopelekea uharibifu wa vyanzo asili vya maji na ukame uliokithiri.

Katika kijiji hicho ndiko anakotoka mwanasiasa machachari wa mrengo wa upinzani (CHADEMA) na Mbunge Dr. Catherine Ruge akitokea katika ukoo wa kisiasa na wasomi; ni binti wa hakimu Ferdinand Makore Ruge, na mwanafunzi wa kisiasa wa Kapteni Ruge (mwana CCM na baba yake mdogo) na inasadikiwa anafuata nyayo zake.

Katika kijiji hicho ndipo zinapopatikana familia za wazee wa zamani kama Wichoka Masancha, Chacha Masabhi, Mahemba Changure, Machota Witocho, Nyabhunya, Ndeghe Temweni, mwanasiasa mkongwe Cleophas Maighe Mohogo, Chacha Soghora, Maro Ghesimba, Maro Monyi, George Mato, Ghesusu, King’orori na Mghaya Keghuku.

Kijiji cha Ring’wani kina historia ya kuwa na familia za mifugo mingi na pia wafugaji mahiri waliowahi kutokea wakiongozwa na Nyamarasa Masiko Nyangogho aliyekadiriwa kuwa na idadi ya ng’ombe wapatao 14,000 mpaka wakati wa kifo chake, pia waliwahi kuwapo matajiri wa mifugo kama Masosota Ighonga na nduguye Edward Ghaghuri Ighonga, Nyanduku Maheri “Tip Tip" Masiko Moghita na Chacha Nyaruchowa.

Matajiri hao wa mifugo James Makenge Ruge, Edward Ghaghuri Ighonga, Nyamarasa Masiko na Masosota Ighonga wanakumbukwa kwa busara na moyo wao wa kutoa misaada katika jamii, hasa wakati wa shida kama njaa, ugonjwa, misiba, ada za shule na hata mahari kwa ajili ya vijana waliopungukiwa. Wakati fulani baraka hii ya mifugo mingi ilisaidia sana kwani asilimia kubwa ya vijana waliochipukia maisha na zile familia duni kwa miaka mingi zilitegemea mifugo ya matajiri hao kwani karibu asilimia 20 ya kaya katika kijiji cha Ring’wani na vijiji vingine vya jirani zilikuwa na ng’ombe wa Nyamarasa wakiwatumia kwa maziwa na kilimo.

Kijiji cha Ring’wani kina sifa ya kutoa wasomi wengi pia, kwani waliwahi kuwapo wasomi kama Dr. Caroly Maro Nyanduku, mtaalamu na daktari aliyebobea katika kilimo, mtaalamu wa uhasibu Genchwere Makenge Ruge, Mongoreme wa kwanza kuwa Certified Public Accountant, mwanasheria wa siku nyingi Flavian Makore Ruge, mtaalamu wa mazao ya maziwa Richard Makenge Ruge, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi Dr. Genchwere Makenge Ruge, Dr. Magori Makenge Ruge, Bwana Kilimo Dr. Genchwere Makenge Ruge, Dr. Nicodemus Masosota Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bunda na mtaalamu wa ramani za ujenzi Kabhori Chacha Matara.

Pia katika kijiji hiki ndipo anapotokea kamanda mwandamizi wa Tume ya Taifa ya Kupambana na Kuzuia Rushwa nchini, James Ghenchwere Maro Ruge, kuna wasomi wengine kama Mwalimu Sangi Makenge Ruge ambae anatambulika kwa jina la Matare - yeye amekuwa Mkufunzi wa vyuo mbalimbali nchini, Afisa Elimu Taaluma Sec wilaya na Mshauri wa Baraza la Mitihani NECTA kwa miaka 9, Bigeso Makenge Ruge pamoja ma kuwa mjasiriamali hodari lakini pia amefanya kazi katika sekta ya afya binafsi kwa takribani miaka nane sasa ambapo ni mshauri wa maswali ya uendeshaji wa biashara katika sekta ya afya binafsi Tanzania, Ruge Makore Ruge,  Matara Kabhori, Nyamase Masosota, Sangi Makenge Ruge, Ruge Maro Mhoni, Sangi Maro Mhoni, Dr. Stephen Maro Muhoni na nduguye Vedastus Maro Mhoni, aliwahi kuwepo Nyanchoghu Masosota na nduguye Nyamase Masosota, wapo wasomi Sabhai Nicholaus, Mantoye Mahende Nyanduku, Mtaalamu wa Sayansi ya Uchunguzi Maalum Manyere Maro Ruge na nduguye mwanasiasa hodari Mhasibu Mapinduzi Maro Ruge na wengineo wengi, wanawake pia hawako nyuma  katika shule wakiongozwa na mwanasiasa msomi Dr. Catherine Nyakaho Makore Ruge (CPA) (Mbunge), pia wapo vijana wasomi na wataalamu wa uhasibu kama Mhasibu Sangi Maro Ruge (CPA) Afisa Mapato Denis Maro Ruge (CPA)

Wapo pia wanasheria mahiri akiwamo Sabhai Chrispin Nyanduku na wakili Pius Maro Ruge, mtaalamu wa Sheria za Kimatifa na mwanaharakati wa Haki za Binadamu, na nduguye Mwanasheria chipukizi Ferdinand Makore Ruge.

Kijiji hiki pia kina wakimbiaji mahiri wakiongozwa na Motibha “Rotwewe” Nyanduku, Daudi Mahende Nyanduku n.k

Pia kijiji hiki kina wasanii na wachekeshaji mahiri kama Kirabhari Nyamhanga Mataratora ambaye hivi sasa ni mchungaji mwenye kanisa lake, Ghiteghe Matoka na Saghaswe Motibha.

Pia kijiji hiki kina historia ya mafundi waliowahi kufahamika kwa ujenzi wa nyumba za jadi na za kisasa wakiongozwa na Rohuro Masiko, Nyamarori Machoghu, Mzee Matoka na wengineo; vipaji hivi vimerithiwa na vijana wao ambao waliviendeleza kama alivyokuwa mfanyabiashara fundi Nyambeta Nyamarori na vijana wa Rohuro kama Maro na Sarighoko.

Kijiji hiki pia kina watu wanaofahamika na wenye busara, mfano Abas Mresi, Bhoke Nyaruchowa, Simoni, Mwita Marata, Gerald Nyaghesore Nyanduku, Rhobi Masosota Ighonga, Maro Daudi Mahende, Ghati Nesi, Msaghu Masosota n.k.

Pia wapo wafanyabiashara kama Sabhai Wakori, Saquid Nyamhanga Msaghu, na tajiri chipukizi Moniko Chacha Maighe anayetoa huduma ya biashara kwa kiasi kikubwa kijijini hapo.

Pia kijiji hiki kimebarikiwa wanajeshi wa ngazi za juu na askari kama Luteni Kanali Meritus Masese Machota, na Makepteni Machoke Mahemba Chacha Soghora, Faustine Maro Ruge, Nicholaus Ighonga, John Machoghu, John Abas Mresi, Sabhai Nicholaus na wengine wengi.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

Kata za Wilaya ya Serengeti - Mkoa wa Mara - Tanzania

Busawe | Geitasamo | Ikoma | Issenye | Kebanchabancha | Kenyamonta | Kisaka | Kisangura | Kyambahi | Machochwe | Magange | Majimoto | Manchira | Matare | Mbalibali | Morotonga | Mosongo | Mugumu | Nagusi | Natta | Nyamatare | Nyambureti | Nyamoko | Nyansurura | Rigicha | Ring'wani | Rung'abure | Sedeco | Stendi Kuu | Uwanja wa Ndege


Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Mara bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Ring'wani kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.

Usiingize majina ya viongozi au maafisa wa sasa maana wanabadilika haraka mno.