Nenda kwa yaliyomo

Dumuzi mkubwa

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Prostephanus truncatus)
Dumuzi mkubwa
(Prostephanus truncatus)
Dumuzi mkubwa juu ya punje za mahindi
Dumuzi mkubwa juu ya punje za mahindi
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Arthropoda (Wanyama wenye miguu yenye viungo)
Nusufaila: Hexapoda (Wanyama wenye miguu sita)
Ngeli: Insecta (Wadudu)
Ngeli ya chini: Pterygota (Wadudu wenye mabawa)
Oda: Coleoptera (Wadudu wenye mabawa magumu)
Nusuoda: Polyphaga
Familia ya juu: Bostrichoidea
Familia: Bostrichidae
Nusufamilia: Dinoderinae
Jenasi: Prostephanus
Lesne, 1898
Spishi: P. truncatus
Horn, 1878

Dumuzi mkubwa (pia scania au Osama (Kenya); kisayansi Prostephanus truncatus) ni spishi ndogo ya mbawakawa ya familia Bostrichidae katika oda Coleoptera ambaye ni msumbufu wa hatari kwa sababu anaharibu nafaka zinazohifadhiwa maghalani. Spishi nyingine ya familia hii ni dumuzi mdogo (Rhyzopertha dominica) ambaye ni 67% ya saizi ya dumuzi mkubwa, lakini ni msumbufu mbaya vilevile.

Dumuzi mkubwa ana urefu wa mm 3-4.5 kulinganisha na urefu wa mm 2-3 katika dumuzi mdogo. Mpevu ana umbo la mcheduara la kawaida la Bostrichidae na ncha ya nyuma inayoonekana kama imekatwa. Kichwa kimefichwa kutoka juu chini ya pronoto. Uso wa mwili una vijishimo na chembe nyingi ndogo ndogo kama sugu (vinundu). Vipapasio vina pingili 10 na vina kirungu chenye pingili tatu, ambazo ile ya mwisho ni pana sawa au zaidi kuliko pingili zilizotangulia. 'Shina' la kipapasio ni jembamba na limefunikwa kwa nywele ndefu[1][2].

Mabuu ni weupe na wororo na wamefunikwa kwa nywele habahaba. Pande zao ni sambamba, yaani hazipunguzi. Miguu ni mifupi na kidonge cha kichwa ni kidogo kulinganisha na saizi ya mwili[2].

Katika hali nzuri ya unyevuanga wa 80%, 32°C na chakula kinachopatikana, dumuzi mkubwa anakamilisha mzunguko wa maisha ndani ya siku 27. Ni msumbufu wa hatari wa nafaka zilizokauka, haswa mahindi, na mahogo yaliyokauka katika sehemu nyingi za Afrika na mabara mengine.

Dumuzi mkubwa ni wa asili katika sehemu za tropiki za Amerika ya Kusini, Amerika ya Kati na kusini kabisa mwa Marekani kama msumbufu muhimi, lakini kwa mahali, wa mahindi yaliyohifadhiwa shambani. Aliwasilishwa nchini Tanzania, labda mwishoni mwa miaka ya 1970, na amekuwa msumbufu mbaya wa mahindi na mahogo yaliyohifadhiwa katika sehemu hiyo ya Afrika ya Mashariki. Tangu hapo amesambaa hadi Kenya, Burundi, Rwanda, Malawi, Zambia, Msumbiji, Namibia na Afrika Kusini, na hakika yumo katika nchi nyingine kadhaa za eneo hilo lakini hajaripotiwa. Alipatikana huko Afrika ya Magharibi kwanza katika Togo mnamo 1984, ambapo labda aliwasilishwa kupitia uingizaji wa nafaka kutoka Amerika ya Kaskazini. Tangu hapo amesambaa mpaka Benin, Nijeria, Ghana, Nijeri na Burkina Faso. Mlipuko tofauti ulitokea Gini.

Dumuzi mkubwa anaweza kuvamia maeneo yote ya Afrika ya kitropiki na ya kinusutropiki ambapo muhindi na muhogo inakuzwa, na ni mfano wa pekee wa hivi karibuni wa msumbufu mbaya wa mavuno yanayohifadhiwa anayevamia kwa kiwango cha kikanda au bara zima. Anabaki kuwa tishio la karantini kwa maeneo mengine katika Dunia ya Kale ambapo muhindi unakuzwa.

Mwenendo

[hariri | hariri chanzo]

Dumuzi mkubwa ni msumbufu wa hatari wa mahindi na viazi vikavu vya muhogo zinazohifadhiwa, na atashambulia mahindi shambani kabla ya uvuno. Majaribio ja kukuza spishi hiyo kwenye kunde, maharagwe, kakao, buni na mchele usiokobolewa katika maabara hayakufanikiwa, ingawa ukuaji unawezekana kwenye aina nyororo za ngano na ulaji wa wapevu unaweza kuharibu bidhaa hizi nyingine.

Dumuzi mkubwa hutenda kama msumbufu wa kawaida wa mahindi yaliyohifadhiwa shambani. Punje nzima hushambuliwa kwenye mabunzi kabla na baada ya kuvuna. Pia ni msumbufu wa mahogo yaliyohifadhiwa shambani, haswa chipsi za muhogo. Wapevu hutoboa vyakula vingi na vitu vingine vikiwemo kuni, mwanzi, plastiki na sabuni. Idadi kubwa za dumuzi wakubwa hutokea katika mazingira ya asilia na wamerekodiwa juu ya spishi kadhaa za miti huko Amerika ya Kati[3][4] na Afrika[5][6][7] katika visa vingine wakioanishwa na mbawakawa vipapasio-virefu wanaotoa miviringo ya gome kutoka vitawi[8].

Uvamizi wa mahindi unaweza kuanza kwenye mazao yaliyokomaa shambani, k.m. wakati unyevu umekuwa sawa na au chini ya 18%. Kupunguza uzito hadi 40% kumerekodiwa katika mabunzi yaliyohifadhiwa kwa muda wa miezi 6[9]. Nchini Tanzania madhara ya hadi 34% yameonekana baada ya kuhifadhi mahindi kwa muda wa miezi 3 shambani, na dhara la wastani ni 8.7%[10]. Dumuzi mkubwa ni msumbufu anayeharibu zaidi kuliko wadudu wengine wa kuhifadhi, pamoja na kidungadunga wa mchele (Sitophilus oryzae), kidungadunga wa mahindi (S. zeamais) na nondo wa nafaka (Sitotroga cerealella), katika hali sawa. Madhara yanayosababishwa na dumuzi mkubwa kwenye viazi vikavu vya muhogo yanaweza kuwa makubwa sana. Wapevu wanaotoboa viazi hivyo huvipunguza kwa urahisi kuwa vumbi na dhara la 70% limerekodiwa baada ya miezi 4 tu ya kuhifadhi shambani[11]. Dumuzi mkubwa yuko Afrika ya Magharibi, ya Mashariki na ya Kusini.

Kugundua na kufuatilia

[hariri | hariri chanzo]

Kabla ya kuanzisha hatua za kudhibiti dumuzi mkubwa, ni muhimu kwanza kujua ikiwa msumbufu huyo yupo katika eneo. Hii inaweza kufanywa kwa kutumia mitego ambayo ina feromoni ya madume ya kukusanyika. Mitego hii inapaswa kuwekwa angalau m 100 kutoka kwenye mashamba ya mahindi au maghala yaliyo na mahindi au mahogo yaliyokaushwa ili kuepusha kuvutia mbawakawa kwenye chanzo cha chakula chao[12]. Kwa ufuatiliaji wa muda mrefu, mitego iliyotengenezwa kwa mbawakawa wa Japani ("Popillia japonica") na iliyo na feromoni ya dumuzi mkubwa hutumiwa siku hizi kwa mafanikio katika Afrika ya Magharibi na ya Mashariki.

Aina sugu na usafi

[hariri | hariri chanzo]

Mbinu bora ya kudhibiti itakuwa matumizi ya aina sugu za mahindi, ingawa nyingi bado hazijapatikana na kazi nyingi bado inahitajika kufanywa.

Ni muhimu sana kutumia maghala yaliyo rahisi kusafishwa. Ni wazi kwamba hatua zozote za maisha za dumuzi mkubwa zitaanza vamizi mpya.

Dawa za aina ya pareto, kama permethrin na deltamethrin, hufanya kazi vizuri dhidi ya dumuzi mkubwa lakini hazina ufanisi sana dhidi ya wasumbufu wengine wa uhifadhi. Kwa hivyo, dawa hizi mara nyingi huchanganywa na vifundiro vya organofosfati, kama pirimiphos na fenitrothion[13]. Maghala makubwa yanaweza kufukizwa kwa fosfini.

Mbawakawa mbuai Teretrius nigrescens ametolewa Afrika ya Magharibi na ya Mashariki[14]. Ingawa kwa kweli amepunguza idadi ya dumuzi mkubwa, akiwa mbuai hafanyi kazi vizuri kama vile vidusia[15]. Kwa hivyo, milipuko ya dumuzi mkubwa bado hufanyika mara kwa mara inayohitaji hatua za udhibiti. T. nigrescens hakujilowea kwa urahisi nchini Tanzania kwa sababu isiyojulikana.

Jitihada zimefanywa kudhibiti dumuzi mkubwa katika maghala kwa kuvu Beauveria bassiana. Walakini, kuvu haziwezi kufikia mabuu ndani ya punje na wapevu huweza kutaga mayai kabla ya kuuawa na kuvu.

  1. [1] Dumuzi mkubwa kwenye EAFRINET
  2. 2.0 2.1 2.2 [2] Dumuzi mkubwa kwenye CABI
  3. Rees, D.P., Rodriguez, R. & Herrera, F.L. (1990) Observations on the ecology of Teretriosoma nigrescens Lewis (Col. Histeridae) and its prey Prostephanus truncatus (Col.: Bostrichidae). Tropical Science, 30: 153-165.
  4. Ramirez-Martinez, M., Alba-Avila, A. de & Ramirez-Zurbia, R. (1994) Discovery of the larger grain borer in a tropical deciduous forest in Mexico. Journal of Applied Entomology, 118(4/5): 354-360.
  5. Nang'ayo, F.L.O., Hill, M.G., Chandi, E.A., Chiro, C.T., Nzeve, D.N. & Obiero, J. (1993) The natural environment as a reservoir for the larger grain borer Prostephanus truncatus (Horn) (Coleoptera: Bostrichidae) in Kenya. African Crop Science Journal, 1(1): 39-47.
  6. Nang'ayo, F.L.O., Hill, M.G. & Wright, D.J. (2002) Potential hosts of Prostephanus truncatus (Coleoptera: Bostrichidae) among native and agroforestry trees in Kenya. Bulletin of Entomological Research, 92(6): 499-506.
  7. Nansen C., Meikle, W.G., Tigar, B., Harding, S. & Tchabi, A. (2004) Nonagricultural hosts of Prostephanus truncatus (Horn) (Coleoptera: Bostrichidae). Annals of the Entomological Society of America, 97(3): 481-491.
  8. Borgemeister, C., Goergen, G., Tchabi, A., Awande, S., Markham, R.H. & Scholz, D. (1998) Exploitation of a woody host plant and cerambycid-associated volatiles as host-finding cues by the larger grain borer (Coleoptera: Bostrichidae). Annals of the Entomological Society of America, 91(5): 741-747.
  9. Giles, P.H. & Leon, O. (1975) Infestation problems in farm-stored maize in Nicaragua. In: Proceedings of the 1st International Working Conference on Stored Products Entomology, Savannah, Georgia, USA, 1974: 68-76.
  10. Hodges, R.J., Dunstan, W.R., Magazini, I. & Golob, P. (1983) An outbreak of Prostephanus truncatus (Horn) (Coleoptera: Bostrichidae) in East Africa. Protection Ecology, 5(2): 183-194.
  11. Hodges, R.J., Meik, J. & Denton, H. (1985) Infestation of dried cassava (Manihot esculenta Crantz) by Prostephanus truncatus (Horn) (Coleoptera: Bostrichidae). Journal of Stored Products Research, 21(2):73-77.
  12. Hodges, R.J. & Pike, V. (1995) How to use pheromone traps to monitor the Larger Grain Borer (Prostephanus truncatus). Chatham Maritime, Kent, UK: Natural Resources Institute.
  13. Golob, P. & Hanks, C. (1990) Protection of farm stored maize against infestation by Prostephanus truncatus (Horn) and Sitophilus species in Tanzania. Journal of Stored Products Research 26(4): 187-198.
  14. Borgemeister, C., Holst, N. & Hodges, R.J. (2003) Biological control and other pest management options for larger grain borer Prostephanus truncatus. In: Neuenschwander, P., Boregemeister, C. & Langewald, J. (eds.) Biological Control in IPM Systems in Africa. Wallingford, UK: CABI Publishing, 311-328.
  15. Holst, N., Meikle, W.G. & Markham, R.H. (2000) Grain injury models for Prostephanus truncatus (Coleoptera: Bostrichidae) and Sitophilus zeamais (Coleoptera: Curculionidae) in rural maize stores in West Africa. Journal of Economic Entomology 93(4): 1338-1346.