Chipsi
Mandhari
Chipsi (kutoka Kiingereza: "chips"; pia: vibendo, viepe) ni vipande vyembamba vya chakula vilivyokaangwa katika mafuta. Kwa kawaida huongezewa chumvi na mayai au kitoweo kingine.
Aina
[hariri | hariri chanzo]Chipsi zinajulikana hasa kama chipsi za viazi, tena kwa namna mbili tofauti:
- Chipsi moto (pia: vibanzi, kwa Kiingereza: fries (Marekani), chips (Uingereza), pommes frites (Kifaransa na penginepo)) ni vipande vya kiazi ambavyo mara nyingi vinalingana na ukubwa wa kidole kidogo na vinakaangwa katika mafuta. Baada ya kukaanga ziwe kaukau upande wa nje lakini laini upande wa ndani. Baada ya kupoa si tena tamu sana. Chipsi za aina hiyo huliwa zikiwa moto pamoja na nyama, kuku, samaki au peke yake, kwa kawaida pamoja na sosi ya nyanya au pilipili. Chipsi mayai ni chipsi zinazokorogwa pamoja na mayai na kukaangwa tena.
- Chipsi baridi (kwa Kiingereza: potato chips, crisps) ni vipande bapa na vyembamba sana vya chipsi ambavyo vinakaangwa katika mafuta hadi kukauka kabisa. Chipsi hizo huliwa mara nyingi peke yake. Vinauzwa madukani katika mfuko na kuliwa kama chakula baridi. Chipsi baridi hutengenezwa pia kwa kutumia ndizi, mizizi mingine yenye wanga au nafaka mbalimbali.
- Chipsi za tortilla: pamoja na chipsi baridi za viazi kuna chipsi za tortilla zilizoenea kimataifa zikiandaliwa kwa unga wa mahindi. Mara nyingi hutengenezwa kiwandani na kuuzwa kwa wingi kupitia maduka. Kuna watu wanaozipika nyumbani.
Chipsi na afya
[hariri | hariri chanzo]Chipsi za kila aina ni chakula kinachopendwa lakini kina pia madhara ya kiafya. Chipsi mara nyingi zina kiwango kikubwa cha mafuta na hivyo zinachangia kutokea kwa unene wa kupindukia. Pia zinatayarishwa na chumvi na mlaji anapita haraka kiasi cha chumvi kinacholingana na afya (gramu 6/siku kwa mtu mzima).
Kama chipsi zimekaangwa katika mafuta yasiyo mapya au kwa joto kubwa mno kuna kemikali zinazoweza kusababisha kansa.
Angalia pia
[hariri | hariri chanzo]Makala hii kuhusu mambo ya utamaduni bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Chipsi kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |