Mobutu Sese Seko
Joseph-Désiré Mobutu aliyejiita baadaye Mobutu Sese Seko Kuku Ngbendu wa Zabanga (* Lisala, 14 Oktoba 1930 ; † Rabat, Moroko, 7 Septemba 1997) alikuwa rais na dikteta wa Zaire (Kongo-Kinshasa) kati ya miaka 1965 na 1997.
Utoto na jeshi la kikoloni
[hariri | hariri chanzo]Alizaliwa katika Kongo ya Belgiji mwaka 1930. Kijana, baada ya shule alijiunga na "Force Publique" yaani jeshi la kikoloni la Wabelgiji katika Kongo.
Hadi mwaka 1956 akafikia cheo cha staff sergent akaacha jeshi na kufanya kazi magazetini akishiriki katika siasa.
Kupanda ngazi
[hariri | hariri chanzo]Baada ya uhuru wa Kongo serikali ilimpa cheo cha kanali. Katika nafasi yake kama mkuu wa jeshi la Kongo alishirikiana na rais Joseph Kasavubu katika uasi dhidi ya waziri mkuu wa kwanza Patrice Lumumba aliyepinduliwa tarehe 14 Septemba 1960 na kuuawa baadaye.
Rais wa kijeshi
[hariri | hariri chanzo]Mwaka 1965 Mobutu aliamua kumpindua Kasavubu akachukua urais mwenyewe.
Mwaka 1970 alijirudisha ofisini kwa njia ya uchaguzi uliopangwa naye mwenyewe.
Mwaka 1969 alikandamiza upinzani wa wanafunzi wa chuo kikuu kwa nguvu ya kijeshi. Baada ya kuua wanafunzi wengi aliamuru 2000 wengine waingie katika jeshi ili wajifunze nidhamu.
Mapinduzi ya utamaduni wa Kiafrika
[hariri | hariri chanzo]Miaka 1970/1971 Mobutu alitangaza kile alichokiita "kampeni ya utamaduni wa Kiafrika". Alibadilisha jina la Kongo kuwa Zaire na raia wote waliagizwa kuacha majina yao ya Kikristo yenye asili ya Ulaya na kutumia majina ya asili ya Kiafrika. Suti za Kizungu zilipigwa marufuku na rais mwenyewe alianza kuvaa suti zilizoiga mfano wa Mao Tse Tung.
Mobutu alianza kujiita "Mobutu Sese Seko Kuku Ngbendu Wa Za Banga" yaani "Shujaa mwenye enzi asiyeshindikana".
Kiuchumi alitaifisha makampuni ya kimataifa mara nyingi kwa kuzikabidhi kwa ndugu na wenzake. Lakini hadi mwaka 1977 hali ya uchumi ulizorota kiasi cha kumlazimisha kuwaomba wageni warudi tena.
Rais mwizi
[hariri | hariri chanzo]Chini ya Mobutu nchi kubwa ya Kongo-Zaire ilirudi nyuma. Mobutu alijitajirisha kupita kiasi wakati nchi yake ilioza. Mwaka 1984 mali yake binafsi nje ya Kongo ilikadiriwa kuwa dolar za Marekani bilioni 4. Nchi kubwa za Magharibi, kama vile Marekani na Ufaransa, walimvumilia na kumsaidia kwa sababu alionekana kama mwanasiasa anayepambana na Ukomunisti na harakati za ukombozi, kwa mfano Angola.
Wakati wa kuporomoka kwa Umoja wa Kisovyeti nchi za magharibi hawakuona haja tena kumsaidia Mobutu. Tangu mwaka 1990 alipaswa kukubali vyama vya upinzani hata akijaribu kuendeleza udikteta wake.
Upinzani na mwisho
[hariri | hariri chanzo]Katika miaka 1996 na 1997 waasi walioongozwa na Laurent Kabila walienea katika mashariki ya Zaire kwa msaada wa nchi jirani Uganda na Rwanda. Mobutu alipaswa kumkubali mpinzani wake Etienne Tshisekedi kama waziri mkuu lakini jeshi la Kabila likaendelea kusonga mbele.
Tarehe 16 Mei 1997 wapinzani walitwaa uwanja wa ndege wa Lubumbashi na Mobutu aliyegonjeka alikimbia nchi. Alikufa nje ya nchi, huko Moroko tarehe 7 Septemba 1997. Kabila alikuwa ameshaingia tayari Kinshasa tangu tarehe 20 Mei 1997 na kuchukua utawala.