Nenda kwa yaliyomo

Mfumo wa mmeng'enyo wa chakula

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mfumo wa Mmeng'enyo wa Chakula wa Binadamu
Tafsiri: utumbo mwembamba (small intestine), utumbo mpana (large intestine), ini (liver), kongosho (pancrease), ulimi (tongue), tumbo (stomach), tezi za mate (salivary glands), umio (esophagus), puru (rectum), mkundu (anus)

Mfumo wa mmeng'enyo wa chakula (pia: mwanya wa chakula[1]) ni jumla ya viungo mwilini mwa binadamu na mamalia wengine vinavyofanya kazi ya kuingiza chakula mwilini, kukisagasaga, kukisafirisha ndani ya mwili, kukimeng'enya, kuondoa lishe ya mwili ndani yake, na kutoa mabaki nje ya mwili. Kwa hiyo mfumo wa mmeng'enyo wa chakula ni njia yote kuanzia mdomo hadi mkundu.

Magonjwa yake huchunguzwa na elimu ya gastro-enterolojia.

Kwa lugha nyingine unahusika na umeng'enyaji wa chakula mpaka kuwa katika hali inayoweza kusharabiwa na mwili. Ili chakula kiweze kutumika mwilini, ni lazima kivunjwevunjwe kiwe katika hali rahisi ya kuweza kusharabiwa. Kazi hiyo hufanywa na mfumo wa mmeng’enyo wa chakula. Mfumo wa mmeng’enyo wa chakula wa mwanadamu hufanana na ule wa sungura, panya au pimbi. Sehemu kuu zinazohusika katika umeng’enyaji huo ni kinywa, umio, mfuko wa tumbo, ini, mfuko wa nyongo, utumbo mwembamba, kongosho, utumbo mpana na puru.

Chakula kinaposafiri katika njia yake hufanyiwa mabadiliko ya kiumbo na ya kikemikali. Kila sehemu ya mfumo wa mmeng’enyo wa chakula ina kazi maalum. Chakula cha mnyama au binadamu huweza kuwa cha kabohaidreti/wanga, protini, mafuta au mchanganyiko wa viambato hivyo. Myeyuko wa makundi hayo ya vyakula hutokea katika sehemu mbalimbali za njia ya chakula kwa njia za kemikali.

Mmeng’enyo kinywani

[hariri | hariri chanzo]

Kinywa ni sehemu ya kwanza kupokea chakula. Chakula kinapokuwa mdomoni huvunjwavunjwa na kusagwa na meno au kwa lugha nyingine husagwa kimekanika. Mate husaidia kukilainisha. Ulimi husaidia kugeuzageuza chakula hicho na kukiviringisha kuwa tonge.

Meno huvunjavunja chakula kuwa vipande vidogovidogo wakati wa kutafuna na kusaga. Hivyo chakula huwa katika vipandevipande ambavyo huongeza eneo zaidi kwa shughuli za umeng’enyaji zinazofanywa na vimeng’enya vinavyopatikana katika njia ya chakula. Vilevile meno husaidia kufanya chakula kuwa rahisi kumezwa.

Mate ni mchanganyiko wa maji, uteute na kimeng’enya kinachofahamika kama salivary amylase au ptyalin. Kazi za mate katika umeng’enyaji ni kama ifuatavyo:

Ulimi huzungushazungusha chakula kiwe kama tonge. Kwa msaada wa ulimi, tonge hilo husukumwa kuelekea kwenye umio (kwa Kiingereza huitwa oesophagus). Chakula kinapoingia katika umio, huelekea kwenye mfuko wa tumbo. Vyakula rojorojo hupita kwa haraka zaidi kuliko vyakula vizito.

Mfuko wa tumbo

[hariri | hariri chanzo]

Chakula huhifadhiwa katika mfuko wa tumbo. Mfuko huo una uwezo wa kupanuka wakati unapopokea chakula na kusinyaa unapokuwa hauna chakula. Chakula huwa katika tumbo mwa muda wa saa tatu hadi nne. Muda huo hutegemea aina ya chakula. Chakula cha kabohaidreti, kwa mfano uji wa [mahindi]], huwa tumboni kwa muda usiozidi saa moja. Chakula cha protini kwa mfano nyama, huweza kukaa tumboni kwa muda wa saa moja au mbili.

Katika mfuko wa tumbo, kuta za tumbo zina tezi (gastric glands) zitoazo misusumo ya gastriki (gastric juice) ambayo huwa na asidi ya haidrokloriki, uteute na kimeng’enya. Vimeng’enya vinavyotolewa tumboni ni pepsinogen, prorennin, rennin.

Asidi ya haidrokloriki

[hariri | hariri chanzo]

Asidi ya haidrokloriki (HCl) husaidia kufanya mambo yafuatayo tumboni:

 • Husaidia kuweka mazingira ya asidi ili vimeng’enya vya tumbo viweze kufanya kazi. Vimeng’enya vya tumboni hufanya umeng’enyaji kwa ufanisi katika hali ya uasidi.
 • Huvunja sukari tata (complex sugar) kuwa sukari rahisi.
 • Huua bakteria waliomo katika chakula.
 • Huanzisha ufanyaji kazi wa vimeng’enyo vingine katika tumbo. Pepsinogen na prorennin hubadilishwa kutoka katika hali ya awali na kuwa pepsin na rennin kwa mpangilio uliotajwa; hali ambazo hasa ndizo hufanyazo umeng’enyaji.

Pepsin humeng’enya chakula cha protini na kuwa peptides. Pepsin hutolewa katika namna ya pepsinogen. Namna hii haiwezi kufanya mmeng’enyo mpaka itakapokutana na asidi; hivyo kuzuia kumeng’enya seli zinazoitoa katika tezi za tumbo.

Rennin hugandisha protini iliyo katika maziwa ili kimeng’enya cha pepsin kiweze kuivunja protini kwenda katika peptides. Kimeng’enya hiki pia hutolewa katika namna ya prorennin, ambacho huhitaji pia asidi ile kiweze kufanya kazi yake. Kimeng’enya hiki hupakitana sana katika matumbo ya mamalia wachanga walio katika kipindi cha kunyonya.

Uteute wa tumbo hulinda kuta za tumbo ili zisikwanguliwe na asidi ya haidrokloriki na pepsin. Bila uteute huu tumbo linaweza kujimeng’enya. Kuna uhusiano wa karibu sana kati ya uteute huu, asidi ya haidrokloriki na ugonjwa wa vidonda vya tumbo (ulcers).

Kazi za tumbo

[hariri | hariri chanzo]

Kwa ufupi kazi za tumbo ni kama ifuatavyo:

 • Hutumika kama sehemu ya kutunzia chakula kwa muda mfupi kabla ya kuendelea umeng’enywaji katika sehemu nyingine za mfumo wa chakula.
 • Umeng’enywaji wa chakula cha protini huanzia katika tumbo.
 • Kwa kutumia misuli yake, tumbo husaidia kuchanganya chakula na misusumo ya tumbo, hivyo kuboresha zoezi la umeng’enyaji tumboni.
 • Usharabiwaji wa maji, alkoholi na baadhi ya vitamini hutokea katika tumbo. Mfuko wa tumbo una misuli ambayo husinyaa na kutanuka mara nyingi, hivyo kwa muda wote chakula kinapokuwa kwenye mfuko huo huchanganywachanganywa. Kitendo hicho, pamoja na athari za misusumo iliyopo kwenye mfuko wa tumbo, husababisha kufanyika kwa tuitumbo (kwa Kiingereza huitwa chyme).

Utumbo mwembamba

[hariri | hariri chanzo]

Kutoka kwenye mfuko wa tumbo, chakula huelekea utumbo mwembamba. Utumbo mwembamba ni mrefu kuliko ogani nyingine yoyote ya njia ya chakula. Chakula huwa ndani ya utumbo mwembamba kwa muda mrefu kuliko sehemu nyingine za njia ya chakula. Katika utumbo mwembamba chakula hukutana na misusumo yenye vimeng’enya ambavyo hutoka kwenye kongosho na utumbo mwembamba. Vimeng’enya hivyo husaidia kuyeyusha chakula.

Utumbo mwembamba umegawanyika katika sehemu mbili, duodenum na ileum.

Duodenum

[hariri | hariri chanzo]
Tumbo (stomach), Kongosho (Pancrease) na Duodenum

Ini ni kubwa kuliko ogani nyingine za mwili wa binadamu. Ini huweka akiba ya chakula kama vile aina za wanga iitwayo glaikojeni, vitamini na chumvi za madini. Ini pia hutengeneza nyongo ambayo husaidia katika mmeng’enyo wa mafuta. Nyongo hufanya kazi zifuatazo:

 • Huvunjavunja mafuta (lipidi) na kuwa vipande vidogovidogo ambavyo huongeza nafasi kwa vimeng’enya vingine viweze kufanya kazi zao.
 • Huweka hali ya alkali ambayo ni mazingira mazuri kwa vimeng’enya vya utumbo mwembamba kufanya kazi.
 • Kuondoa asidi iliyo katika tuitumbo iliyoipata wakati chakula kilipo tumboni.

Kongosho

[hariri | hariri chanzo]

Misusumo inayotengenezwa na kongosho hufikia chakula kwa kutumia mfereji unaounganisha duodenum na kongosho. Misusumo ya kongosho huwa na vimeng’enya vifuatavyo:

 • Pancreatic amylase: hii huvunjavunja wanga/kabohaidreti iliyobaki kwenda katika maltose.
 • Pancreatic Lipase: humeng’enya vipande vidogovidogo vya mafuta na kuwa asidi ya shahamu na glaiserini (glycerol).
 • Trypsin: huvunja protini iliyobakia na kuwa peptides. Trypsin hutolewa katika namna ya trypsinogen.
 • Sodium Hydrogen Carbonate (NaHCO3): huweka hali ya alkali ambayo ni mazingira mazuri kwa vimeng’enya vya utumbo mwembamba kufanya kazi.

Hii ni sehemu ya pili ya utumbo mwembamba ambayo ni ndefu sana na imejikunjakunja sana ili iweze kutosha sehemu ya tumbo ambayo ingekuwa ndogo kama ungenyooka (inafikia karibu mita saba). Ileum hutoa misusumo yenye vimeng’enya vifuatavyo:

 • Erepsin (peptidase): humeng’enya peptides na kuwa asidi za amino.
 • Maltase: huvunja maltose na kuwa glucose.
 • Lipase: humeng’enya vipande vidogovidogo vya mafuta na kuwa asidi za shahamu na glaiserini (glycerol).
 • Sucrase: huvunja sucrose na kuwa glucose.

Mchakato wa umeng’enyaji humalizikia katika ileum. Ileum kwa ujumla ina kazi kuu mbili:

Kusharabiwa kwa chakula

[hariri | hariri chanzo]

Chakula kinapofikia hatua hizo huwa kiko tayari kusharabiwa na vinywelea vilivyo katika utumbo mwembamba viitwavyo vilasi. Vilasi hizo huchukua asidi za amino, sukari rahisi (glucose) na chumvi na kupeleka katika mishipa ya vena hadi kwenye ini. Katika ini sukari rahisi hubadilishwa kuwa glaikojeni na kuhifadhiwa. Asidi za amino za ziada hugeuzwa kuwa glaikojeni na yurea (kemikali ambayo baadaye huwa mkojo). Kutoka kwenye ini chakula kinachohitajiwa na mwili husafirishwa na damu hadi kwenye moyo. Damu hiyo husambaza chakula hicho katika mwili mzima kwa matumizi mbalimbali.

Sehemu kubwa ya chakula humeng’enywa na kusharabiwa katika utumbo mwembamba. Chakula kilichobaki huelekea kwenye utumbo mpana.

Utumbo mpana

[hariri | hariri chanzo]

Chakula kinachotoka katika utumbo mwembamba na kuingia utumbo mpana huwa ni kile ambacho hakikuweza kumeng’enywa au kimeng’enywa lakini hakikusharabiwa. Sehemu ndogo tu ya chakula kilichomeng’enywa husharabiwa na utumbo mpana. Sehemu kubwa ya maji iliyotokana na mmeng’enyo wa chakula husharabiwa na utumbo mpana. Sehemu iliyobaki ya chakula huelekea puru na kutolewa nje kupitia njia ya haja kubwa (mkundu) kama kinyesi.

Magonjwa ya mfumo wa mmeng'enyo wa chakula

[hariri | hariri chanzo]

Mfumo wa mmeng'enyo wa chakula hukumbwa na magonjwa tofauti ambayo yanaweza kumfanya mtu asile chakula fulani au akose kula chakula kabisa, akonde na hata pengine afe njaa. Magonjwa hayo ni kama uvimbe wa utumbo (constipation), fistula ya mkundu, saratani ya utumbo, madonda ya mkundu (perianal infections), bawasiri na colon polyps.

Kujikinga kutokana na magonjwa ya mfumo wa mmeng'enyo wa chakula

[hariri | hariri chanzo]

Magonjwa hayo yanaweza kuzuiwa kwa kula chakula chenye nyuzinyuzi, kuenda chooni wakati unaofaa pamoja na kuenda kufanyiwa skrini ili kukaguliwa usiende ukawa na saratani ya utumbo.

Hata baada ya kufanya hayo yote, huenda ukapata kwamba bado una shida za mfumo wa mmeng'enyo wa chakula. Hili likifanyika, wafaa umwone daktari anayekabiliana na magonjwa ya mfumo wa mmeng'enyo wa chakula aliyesomea somo la gastroenterolojia

 1. Mwanya wa chakula na Mwanya wa umeng'enyaji ni mapendekezo ya KyT

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
 • Mwaniki, J. M. (2008) Fundamentals of Biology Second Edition, Delah Educational Publishers, Dar es Salaam
 • Taasisi ya Ukuzaji Mitaala, Sayansi, Kitabu cha Nne, Eastern Africa Publications Limited
Makala hii kuhusu mambo ya anatomia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mfumo wa mmeng'enyo wa chakula kama matumizi yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.