Heroini
Heroini (kwa jina la kitaalamu Diamasetilmorfini au Diamorfini) ni dawa inayotengenezwa kutokana na afyuni ambayo ni utomvu uliokauka wa ua la mpopi.
Heroini ni dawa ya tiba yenye uwezo mkubwa wa kutuliza maumivu na wakati huohuo ni dawa ya kulevya iliyo kali na ya hatari.
Pamoja na kokain ni kati ya madawa haramu yanayosambazwa sana duniani kwa kujali pesa kuliko binadamu anayepatwa na uraibu na hatimaye kufa.
Matumizi ya kiganga
[hariri | hariri chanzo]Kwa sababu hiyo matumizi ya kiganga hupatikana kwa masharti makali tu. Diamorfini (heroini) inatolewa hasa kwa wagonjwa wenye kansa kwenye ngazi za mwisho kabla ya kifo, wakati maumivu ni makali mno. Ikitumiwa kwa hali nyingine daktari anapaswa kuwa mwangalifu sana kutokana na hatari ya kuzoesha dawa.
Zamani dawa hiyo ilitumiwa bila maarifa ya kisasa, hivyo wagonjwa wengi walibaki katika hali ya kuzoeshwa na kutegemea dawa moja kwa moja baada ya kumaliza tiba.
Dawa ya kulevya
[hariri | hariri chanzo]Heroni inatafutwa sana kama dawa ya kulevya. Matumizi haya ni marufuku kote duniani lakini kuna biashara haramu ya kimataifa.
Chanzo chake ni nchi ambako mipopi inalimwa kwa wingi: ni nchi yenye serikali dhaifu na kiwango kikubwa cha rushwa. Nchi hizi ni hasa katika maeneo mawili:
- "Pembetatu ya dhahabu" ni maeneo ya porini mpakani wa Myanmar (Burma), Laos, Vietnam na Uthai.
- "Hilali ya dhahabu" ni eneo kati ya Afghanistani, Pakistani na Uajemi.
Nchi mbili zenye mashamba makubwa ya mpopi na mavuno makubwa ya afyuni ni Myanmar na Afghanistan; hapa na katika nchi jirani kuna maabara ambako heroini inatolewa katika afyuni bichi.
Biashara ni haramu lakini inazaa mabilioni ya pesa na uwezo wa kiuchumi wa vikundi vinavyoendesha biashara hii unazidi uwezo wa nchi ndogo na dhaifu. Nchini Afghanistan wanamgambo Waislamu wa Taliban wanatumia biashara hii kujipatia fedha inayowawezesha kuendeleza vita dhidi ya serikali na Marekani.
Umbo la heroini
[hariri | hariri chanzo]Heroini mara nyingi inapatikana kama unga mweupe au wenye rangi ya kahawia. Watu wanaivuta kama sigara au wanaichanganya na maji na kujidunga sindano. Heroini inayouzwa barabarani mara nyingi imechanganywa na vitu vingine kwa sababu kwa njia hiyo wateja wanadanganywa, na faida ya wauzaji huongezeka. Mchanganyiko huo ni pia hatari kwa sababu kwa njia hiyo uchafu unaingizwa mwilini kupitia mishipa ya damu.
Heroini kwa matumizi ya kiganga unatengenezwa rasmi katika maabara ya makampuni yanayohitaji kuwa na kumbukumbu kamili juu ya kila gramu ya dawa. Inauzwa katika hali ya majimaji kwa sababu hii ni njia ya kuitumia hospitalini.
Madhara ya heroini
[hariri | hariri chanzo]Hatari yake ni hasa uwezo wake mkubwa wa kuzoesha watu wanaoitegemea na wanapaswa kuzidi kuitumia. Watu waliozoea heroini wanapata matatizo makubwa ya kimwili na ya kiakili wakikosa heroini. Mwili unazoea heroini haraka, ukihitaji mapema kiwango kikubwa zaidi ili kuisikia.
Kwa kawaida hali ya kuihitaji inaanza baada ya matumizi ya siku chache.
Inaleta hatari za kimwili, za kiroho na za kijamii.
Watu wanakufa mara nyingi kwa sababu wanakosa kiasi wanachotumia na kama kiasi kinazidi pumzi au moyo husimamishwa. Kinazidi kunatokea mara nyingi kwa sababu heroini huuzwa kama mchanganyiko wa dawa yenyewe na dutu mbalimbali na asilimia ya dawa yenyewe ndani ya mchanganyiko unaouzwa kwa siri inabadilikabadilika. Ikitokea ya kwamba dawa safi sana inauzwa wateja wasiojua wanapata kiasi kikubwa mno.
Kwa jumla matumizi ya madawa kutokana na afyuni hupunguza njaa na hivyo watumiaji wa heroini hawali, wanapata miili dhaifu.
Matumizi ya sindano husababisha mara nyingi vidonda mwilini visivyopona kwa urahisi.
Katika mazingira ya matumizi ya siri watumiaji hushirikishana mara nyingi sindano. Hii inasaidia kuenea kwa magonjwa, hasa Ukimwi na hepatitis.
Hali ya ulevi wa mara kwa mara unaweza kuchanganya akili za watumiaji. Sawa na afyuni, matumizi ya mfululizo yanapunguza uwezo wa roho kuwaza na kufuatilia mipango.
Matatizo ya kijamii yanatokana hasa na mahitaji makubwa ya pesa kwa kujipatia heroini mara kwa mara. Watumiaji wa heroini mara nyingi wanashindwa kufanya kazi, kwa hiyo wanarudi nyuma kuombaomba, kuiba au kujiuza katika umalaya wa kike au kiume.
Matibabu kutokana na uraibu wa heroini
[hariri | hariri chanzo]Inawezekana kuwanasua walioko kwenye uraibu wa heroini kuiacha na kuwa hawaihitaji tena. Hata hivyo, idara ya Marekani inayopambana na utumizi wa madawa ya kulevya inaonyesha kwamba asilimia arubaini na nne hadi sitini ya wale walioacha heroini hujikuta katika mtego huohuo baada ya muda mfupi. Hali hiyo huitwa kwa Kiingereza "relapse". Hata hivyo haimanishi kwamba ufe moyo katika kuuacha uraibu huu. Kuna vituo ambako wenye uraibu huu husaidiwa kuanza upya na kuondoa sumu ya dawa hii.
Tanbihi
[hariri | hariri chanzo]Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- Taarifa kuhusu heroini kwenye tovuti ya DMOZ Ilihifadhiwa 2 Julai 2017 kwenye Wayback Machine.
- Taarifa kuhusu heroini
- Makala ya BBC kuhusu wakati heroini ilipokuwa halali
- Takwimu za vifo kutokana na matumizi ya heroini nchini Marekani
Makala hii kuhusu mambo ya kemia bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Heroini kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |