Nenda kwa yaliyomo

Heinrich IV wa Ujerumani

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Kaizari Heinrich IV akiwa amevaa mapambo ya kifalme.
Kanisa kuu la Speyer (Ujerumani) lililojengwa kwa amri wa Heinrich IV.

Heinrich IV (kwa Kiing. Henry IV ; 1050 - 1106) alikuwa Mfalme wa Ujerumani kuanzia mwaka 1056 na Kaizari wa Roma kuanzia mwaka 1084, hadi alipolazimishwa kujiuzulu madarakani mnamo 1105[1].

Alikuwa mtawala wa tatu wa nasaba ya Wasali na mmoja wa watu muhimu zaidi wa karne ya 11.

Utawala wake unajulikana kwa Fitina ya Usimikaji wa Maaskofu na Upapa na vita kadhaa ya wenyewe kwa wenyewe dhidi ya wagombea wa ufalme wake nchini Italia na Ujerumani.

Mandharinyuma

[hariri | hariri chanzo]

Heinrich IV alikuwa mfalme wa tatu wa nasaba ya Wasali waliotawala Ujerumani kutoka mwaka 1024 hadi 1125. Wafalme hao wa Ujerumani katika karne ya 11 walitawala pia Italia. Vilevile waliweza kupokea cheo cha Kaizari wa Dola Takatifu la Roma. Cheo hicho kilitolewa na Papa, hivyo mfalme Mjerumani alipaswa kufanya safari ya kwenda Roma. Wafalme hao waliamini kwamba cheo cha Kaizari kiliwafanya kuwa wakuu wa Wakristo wote na pia kusimamia uchaguzi wa Papa mpya. Imani hiyo iliwaingiza mara kwa mara katika fitina za ndani za Italia, maana Roma yenyewe ilikuwa mikononi mwa makundi ya makabaila waliotumia ushawishi wao kupelekea wagombea kwa nafasi ya Papa mbele. Matokeo ya fitina zao yalikuwa uchaguzi wa Mapapa tofauti kwa wakati mmoja; mwaka 1045 uliona Mapapa watatu: Benedikto IX, Silvester III na Gregori VI.

Ili kumaliza mgawanyiko, mfalme Heinrich III (baba wa Heinrich IV) alivuka [[milima] ya Alpi kwenda Italia akaitia sinodi ya kanisa huko Sutri mnamo 20 Desemba 1046. Sinodi iliwandoa mapapa wote watatu na kumchagua askofu Mjerumani, Suidger wa Bamberg, ambaye alichukua jina la kipapa Klementi II.

Heinrich IV alirithi imani ya baba yake kuwa mfalme aliyebarikiwa kwa mafuta matakatifu ni mlinzi wa Kanisa lote, ilhali Mapapa waliona umuhimu kutetea madaraka yao juu ya Kanisa lote.

Ugomvi ulikuwa wa lazima katika suala la kuteua na kusimika maaskofu waliokuwa pia maafisa wa utawala katika ufalme. Wafalme walitaka kuteua maaskofu waliosimama upande wao, ilhali Mapapa walisisitiza askofu kuwa cheo cha kidini, kwa hiyo walidai haki ya kuwateua na kuwasimika.

Heinrich alikuwa mtoto wa kwanza wa Mfalme Heinrich III na mke wake wa pili Agnes de Poitou. Wakati Henry III alipokufa ghafla mnamo 1056, Heinrich IV alikuwa na umri wa miaka sita akatangazwa kuwa mfalme bila shida. Mamake malkia Agnes alishika utawala kwa niaba yake na Papa Viktor II aliyekuwa Mjerumani aliteuliwa kama mshauri wake.

Alipotimiza umri wa miaka 15, Heinrich alikuwa mtu mzima. Aliona wakati alipokuwa mfalme mtoto, wakubwa wengine walinyanganya mali ya kifalme, hivyo alijitahidi kutawala tena yale yote yaliyowahi kuwa mali ya baba yake. Hatua alizochukua, zilisababisha upinzani kutoka kwa makabila mbalimbali katika Ujerumani, hasa wa Wasaksoni. Katika vita za ndani baina ya miaka 1073 hadi 1075 aliwashinda Wasaksoni.

Fitina ya Usimikaji wa Maaskofu

[hariri | hariri chanzo]

Hatimaye alijikuta katika mapambano na Papa Gregori VII. Papa huyo alichaguliwa mnamo 1073. Wakati huohuo mfalme aliwahi kumsimika askofu mmoja nchini Ujerumani kufuatana na uzoefu jinsi walivyokuwa nao huko Ujerumani. Papa aliona haki yake ya kuteua maaskofu iliingiliwa, akatafuta na kupata tamko la wakubwa wa Kanisa huko Italia, kuwa washauri wa mfalme watengwe na Kanisa.

Mfalme alikasirika akaita maaskofu wa Ujerumani waliamua Papa huyo asiwe Papa tena. [2] Wakati Gregori aliposikia hayo alimtenga Heinrich IV na Kanisa, alitangaza kuwa hakuwa mfalme tena akafuta viapo ambavyo watu walikuwa wamemwapia mfalme.

Kutengwa kwa mfalme kulisababisha hisia kali huko Ujerumani na Italia. Babu wa mfalme Henry III aliwahi kuwaondoa mamlakani Mapapa watatu, lakini wakati Henry IV alipojaribu kuiga mfano huo, hakuungwa mkono na watu.

Kwenda Canossa

[hariri | hariri chanzo]

Hali ikawa mbaya sana kwa mfalme. Papa alimtenga mfalme katika Kanisa. Alipiga marufuku askofu au padre yeyote kumruhusu katika ibada au kumhudumia kwa namna yoyote. Ilibainika kuwa ilibidi apate msamaha kutoka kwa Papa. Mwanzoni alijaribu kufanya hivyo kwa kutuma balozi. Baada ya Papa kumkataa balozi huyo, mfalme alikwenda Italia mwenyewe.

Alimkuta Papa huko Canossa akapiga magoti mbele ya ngome ya Papa na kuomba msamaha. Kwa kuonyesha unyenyekevu vile alimfanya Papa kumsamehe na kumrudisha katika jumuiya ya Kanisa.

Kutengwa mara ya pili kwa Heinrich IV

[hariri | hariri chanzo]

Wakubwa huko Ujerumani waliwahi kutumia nafasi ya kutengwa kwa mfalme kanisani ili kumtangaza mfalme mpinzani. Papa aliamua kumuunga mkono huyo mfalme wa upinzani akamtenga Heinrich upya mwaka 1080.

Lakini baada ya miezi michache yule mfalme mpinzani alifariki dunia, hivyo Heinrich alianza kupigania upya kuwa mfalme.

Mnamo 1081 alianzisha vita dhidi ya Papa Gregori VII nchini Italia. Aliitisha mkutano wa maaskofu waliomwunga mkono na mkutano huo ulitangaza kufukuzwa kwa Papa Gregori wakamchagau Antipapa. Jeshi la mfalme Heinrich liliingia Roma mnamo mwaka 1084, kumtangaza papa mpya aliyeweka taji la ukaizari kwenye kichwa cha mfalme.

Hatimaye mfalme alipaswa kuondoka Roma tena, Papa Gregori aliaga dunia uhamishoni na maaskofu wa upande wake walimchagua Papa mpya. Kwa muda Kanisa Katoliki lilikuwa na Mapapa wawili.

Mapigano juu ya madaraka

[hariri | hariri chanzo]

Kutokana na ugomvi wake na Kanisa mfalme alidhoofishwa na wapinzani wake katika Ujerumani na Italia walimshambulia mara kwa mara, na makundi ya maaskofu yalikutana na kutangaza tena na tena kuwa mfalme si Mkristo halali anayetengwa katika Kanisa, Hata hivyo, sehemu kubwa ya maaskofu wa Ujerumani walisimama upande wake wakamtetea.

Katika hali hiyo mfalme alifaulu kutimiza utawala wa miaka hamsini.

Mwishoni mtoto wake aliasi na kumlazimisha Heinrich IV kujiuzulu. Mwanawe alipanda kiti cha kifalme kwenye mwaka 1104 kwa jina la Heinrich V.

Bertha alikuwa mke wa kwanza wa Heinrich IV alikufa mnamo 27 Desemba 1087. Alizikwa katika Kanisa Kuu la Speyer.

  1. Schutz, Herbert (2010). The Medieval Empire in Central Europe: Dynastic Continuity in the Post-Carolingian Frankish Realm, 900-1300. Cambridge Scholars Publishing. ISBN 978-1-4438-1966-4., uk. 113
  2. "Nakala iliyohifadhiwa". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2014-11-12. Iliwekwa mnamo 2021-10-21.
  • Brooke, Z.N. (1968). "Germany under Henry IV and Henry V". Katika Tanner, J.R.; Previte-Orton, C.W.; Brooke, Z.N. (whr.). The Cambridge Medieval History. Juz. la Volume V. Cambridge University Press. {{cite book}}: |volume= has extra text (help); Invalid |ref=harv (help)
  • Brooke, Z.N. (1968). "Gregory VII and the first Contest between Empire and Papacy". Katika Tanner, J.R.; Previte-Orton, C.W.; Brooke, Z.N. (whr.). The Cambridge Medieval History. Juz. la Volume V. Cambridge University Press. {{cite book}}: |volume= has extra text (help); Invalid |ref=harv (help)
  • TJH McCarthy: Nyaraka za Shindano la Uwekezaji: Frutolf wa Michelsberg na waendelezaji wake (Manchester, 2014).
  • Gerd Althoff (Mh.): Heinrich IV. (Ostfildern, 2009) (Vorträge und Forschungen; 69).
  • Gerd Althoff: Heinrich IV. (Darmstadt, 2006)
  • Hati iliyotolewa na Henry kwa askofu wa Bamberg, 17.8.1057 . Picha zilizochukuliwa kutoka kwa makusanyo ya Lichtbildarchiv älterer Originalurkunden Ilihifadhiwa 10 Desemba 2008 kwenye Wayback Machine. katika Chuo Kikuu cha Marburg ikionyesha muhuri wa mfalme.
  • Whitney, J.P. (1968). "The Reform of the Church". Katika Tanner, J.R.; Previte-Orton, C.W.; Brooke, Z.N. (whr.). The Cambridge Medieval History. Juz. la Volume V. Cambridge University Press. {{cite book}}: |volume= has extra text (help); Invalid |ref=harv (help)
  • Robinson, I.S. (2000). Henry IV of Germany 1056-1106.

Viungo vya Nje

[hariri | hariri chanzo]
WikiMedia Commons
WikiMedia Commons
Makala hii kuhusu Kaizari fulani wa Ujerumani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Heinrich IV wa Ujerumani kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.