Nenda kwa yaliyomo

Virusi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Virus)
Virusi
Aina ya Rotavirus
Aina ya Rotavirus
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Virusi
Ngazi za chini

Makundi 7:

Virusi (kutoka Kilatini virus, yaani "sumu“; wakati mwingine pia umoja Kirusi) ni chembe ndogo sana iliyoundwa na maada jenetiki, kama ADN au ARN, katika koti la proteini.

Virusi vinahitaji msaada wa seli za viumbehai ili kutengeneza chembe nyingine za virusi.

Wakati mwingine huhesabiwa kati ya vidubini, lakini wataalamu wengi wanakanusha kwamba ni viumbehai kwa sababu haziwezi kuzaa vyenyewe pia havina metaboli. Si seli yenyewe, lakini vina sehemu za kiini cha seli.

Virusi vinaingia katika seli ya kiumbehai, kama bakteria, mmea au mnyama au binadamu, na kutumia seli hiihii kuzaa, yaani kujizidisha mara elfu kadhaa. Tendo hili linasababisha vurugu ndani ya seli za mwenyeji, inayoonekana kama hali ya ugonjwa.

Hadi sasa kuna aina za virusi zaidi ya 5000 zilizotambuliwa, lakini zinaweza kuwa mamilioni.

Takriban virusi vyote ni vidogo mara mia kuliko bakteria na huonekana tu tangu kupatikana kwa hadubini ya kielektroniki. Lakini mwaka 2014 virusi vikubwa sana, ukubwa wa bakteria ndogo, vimeelezwa: Pithovirus sibericus. Hivyo vinaambukiza amiba.

Muundo wa virusi una sehemu mbili pekee: uzi wa ADN au ARN halafu koti la proteini la kulinda uzi huo. Kwa kawaida ADN au ARN ya virusi ina jeni chache kwa kulinganisha na viumbehai, kama makumi kadhaa. Lakini virusi kama Pithovirus na Pandoravirus vina mamia ya jeni.

Ambukizo la virusi katika wanyama na watu husababisha itikio la kingamwili unaoelekea kuua virusi. Lakini mjibizo huu, unaoonekana mara nyingi kwa homa, unaweza kudhoofisha mwili na kuleta hali ngumu hadi kifo. Virusi hatari zaidi ni vile vinavyohama kutoka kwa mnyama kumwathiri binadamu; hivyo huitwa virusi vya zoonosia.

Ni vigumu kupata dawa za virusi kwa sababu virusi huishi ndani ya seli za mwili wa mwenyeji, hivyo kuna hatari ya dawa kusababisha hasara kwa seli zenyewe. Kuna virusi kadhaa ambavyo chanjo kimegunduliwa ingawa hakikingi asilima 100 maana virusi huwa na uwezo wa kubadilika haraka.

Kati ya magonjwa yanayosababishwa na virusi kuna influenza (homa ya mafua) na pia UKIMWI. Aina kadhaa za virusi zinaweza kusababisha saratani.

Si kila kirusi husababisha magonjwa kwa binadamu na wanyama tu, virusi vingine vina uwezo wa kuathiri bakteria, fangasi na hata mimea[1]. Binadamu wamekua wakijaribu kutumia virusi hivi hasa vinavyoasili bakteria viitwavyo bakteriofagi ili kujitibia magonjwa yanayosababishwa na bakteria[2].

Jinsi ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi

Unashauriwa:

  • kunawa mikono mara kwa mara kwa angalau sekunde 20 kwa maji na sabuni; ukiwa nacho, tumia kitakasa mikono chenye alikoholi (si chini ya asilimia 60).
  • kama chanjo ya virusi fulani hatari inapatikana pale ulipo, nenda kuipata
  • usiguse macho, pua na midomo kwa mikono kama hujanawa
  • epuka kuwa karibu sana na wagonjwa
  • wakati ugonjwa mkali wa virusi unazuru katika nchi ulipo, epuka kusalimu wengine kwa kushikana mikono
  • kaa nyumbani ukiwa mgonjwa (ugonjwa wowote - maana kinga yako ni dhaifu katika hali hii)
  • tembea na karatasi za shashi (kama huna, hata karatasi ya choo / toilet paper) uitumie ukikohoa au kupiga chafya, halafu uitupe mahali pa takataka
  • safisha mara kwa mara vitu unavyovigusa (vikiwa pamoja na kikombe, dawati, simu yako)[3]; kama unavyo, tumia dawa ya alikoholi (spirit – si konyagi!), lowesha karatasi nayo, futa, tupa

Picha

Tanbihi

  1. "Phage therapy (Bacteriophage therapy)". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2021-06-06. Iliwekwa mnamo 2021-06-06.
  2. "Phage Therapy: How It Works, Pros and Cons, Availability, and More". Healthline (kwa Kiingereza). 2019-01-14. Iliwekwa mnamo 2021-06-06.
  3. About prevention and treatment, tovuti ya National Center for Immunization and Respiratory Diseases (NCIRD), Division of Viral Diseases, Marekani, iliangaliwa 30 Januari 2020
Makala hii kuhusu mambo ya biolojia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Virusi kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.