Homa ya mafua

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Influenza)
Jump to navigation Jump to search

Homa ya mafua ni ugonjwa wa kuambukiza unaojulikana pia kwa jina lenye asili ya Kiitalia influenza (yaani "athari") na kwa kifupi chake "flu". Kwa Kiswahili unaitwa pia kaputula au Homa ya kaptura kwa sababu uliingia Afrika Mashariki pamoja na kaptura.[1]

Dalili zake zinafanana katika mengi na mafua ya kawaida lakini ni kali zaidi. Homa ya mafua inasababishwa na virusi ya influenza aina A au B, mara chache pia aina C.

Homa ya mafua inaathiri kila mwaka asilimia 10 hadi 20 za watu wote duniani.

Dalili[hariri | hariri chanzo]

Dalili za homa ya mafua ni pamoja na kikohozi, maumivu shingoni, maumivu ya misuli, maumivu ya kichwa na homa. Wakati mwingine, lakini si kwa kawaida, kunatokea pia kutapika na kuhara.

Homa ya mafua inaweza kudhoofisha mwili na kufungua hivyo mlango kwa magonjwa mengine kama vile kifua kikuu. Hii ni sababu ya kwamba homa ya mafua inaweza kuwa hatari kwa watoto na wazee hasa na kusababisha ugonjwa mkali hadi kifo.

Ambukizo[hariri | hariri chanzo]

Virusi inaingia mwilini kupitia ngozi kamasi za pua, mdomo na jicho. Kwa hiyo inapitishwa kirahisi wakati mgonjwa anakohoa au kupiga chafya. Katika tendo hili matone madogo ya kamasi yenye virusi yanatoka mdomoni au puani na kuelea hewani kwa muda mfupi. Mtu mwingine anayepigwa na matone yale madogo yasiyoonekana kwa macho anaweza kupokea matone kadhaa wakati wa kupumua na kuambukizwa kwa njia hii.

Kinga[hariri | hariri chanzo]

Kuvaa gubizi ya kitambaa juu ya mdomo na pua inapunguza hatari maana matone mengi yanashikwa na kitambaa wakati wa kukohoa na kinyume mtu asiyeambukizwa analindwa kwa njia hiyo pia.

Kunawa mikono mara kwa mara hupunguza hatari ya maambukizi kwa kuwa virusi hufanywa tuli kwa sabuni.[2] Kuvaa kinyago cha upasuaji pia ni muhimu.[2]

Uchanjaji dhidi ya influenza ya kila mwaka imependekezwa na Shirika la Afya Duniani kwa walio katika hatari sana. Chanjo hii husaidia dhidi ya aina tatu au nne za influenza.[3] Kwa kawaida hustahimilika vyema. Chango iliyotengenezwa ili kutumika kwa mwaka mmoja huenda isitumike katika mwaka ufuatao, kwa kuwa virusi hubadilika haraka.

Vitamini D inasaidia kuimarisha kinga asilia ya mwilini dhidi ya maambukizo.

Tiba[hariri | hariri chanzo]

Hakuna tiba ya homa ya mafua isipokuwa kupumzika na kuepukana na kazi zote na kusubiri hadi kinga ya mwili imepambana na virusi. Kuna madawa yanayoweza kupunguza dalili kama homa au maumivu.

Siku hizi kuna pia madawa ya antiviral yanayopunguza ukali wa ugonjwa yenyewe bila kuitibu moja kwa moja. Madawa yale yatumiwe tu baada ya kumwona daktari atakayeamua kama yanafaa au yanaweza kuwa hatari kwa mgonjwa.

Tatizo ni hasa ya kwamba virusi ya homa ya mafua inabadilika haraka; hii ni sababu ya kwamba watu wengine huambukizwa upya mwaka baada ya mwaka. Hali ya hatari inatokea hasahasa wakati aina ya virusi ya influenza inahamia kutoka wanyama kumwathiri binadamu. Hii inatokea kila baada ya miaka kadhaa na kusababisha vifo.

Dawa za kupambana na virusi kama vile kizuio cha neuraminidase oseltamivir miongoni mwa zingine zimetumika kutibu influenza.[3] Manufaa yake kwa walio na afya bora hayaonekani kuwa zaidi ya hatari zake.[4] Hakuna manufaa yaliyopatikana kwa wale walio na matatizo mengine ya kiafya.[4][5]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Ndivyo inavyosema kamusi ya Johnson. Zile za baadaye zinahusianisha kaputula na kuharisha.
  2. 2.0 2.1 Jefferson T, Del Mar CB, Dooley L, et al. (2011). "Physical interventions to interrupt or reduce the spread of respiratory viruses". Cochrane Database Syst Rev (7): CD006207. doi:10.1002/14651858.CD006207.pub4 . PMID 21735402 .
  3. 3.0 3.1 Influenza (Seasonal) Fact sheet N°211 (March 2014). Iliwekwa mnamo 25 November 2014.
  4. 4.0 4.1 Michiels, B; Van Puyenbroeck, K; Verhoeven, V; Vermeire, E; Coenen, S (2013). "The value of neuraminidase inhibitors for the prevention and treatment of seasonal influenza: a systematic review of systematic reviews.". PLoS ONE 8 (4): e60348. doi:10.1371/journal.pone.0060348 . PMC 3614893 . PMID 23565231 .
  5. Ebell, MH; Call, M; Shinholser, J (April 2013). "Effectiveness of oseltamivir in adults: a meta-analysis of published and unpublished clinical trials.". Family practice 30 (2): 125–33. doi:10.1093/fampra/cms059 . PMID 22997224 .
Rod of Asclepius2.svg Makala hii kuhusu mambo ya tiba bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Homa ya mafua kama sababu yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.