Nimattullah Kassab Al-Hardini

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mt. Nimattulah akisali.

Nimatullah Kassab Al-Hardini, O.L.M., (1808 - 14 Desemba 1858) alikuwa mmonaki padri na msomi wa Kanisa la Wamaroni nchini Lebanoni.

Papa Yohane Paulo II alimtangaza mwenye heri tarehe 10 Mei 1998 na mtakatifu tarehe 16 Mei 2004. [1]

Sikukuu yake huadhimishwa kila mwaka siku ya kifo chake[2].

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Utoto na ujana[hariri | hariri chanzo]

Jina lake la awali lilikuwa Youssef Kassab, mtoto mmojawapo kati ya saba wa Joji Kassab na Mariam Raad, binti wa padri wa Kimaroni. Alizaliwa mwaka 1808 katika kijiji cha Hardine, kaskazini mwa Lebanoni[3]

Akiwa mtoto, Youssef alisoma katika shule iliyoendeshwa na wamonaki wa Utawa wa Kimaroni wa Lebanoni karibu na monasteri ya Mt. Antoni huko Houb.

Alipomaliza masomo yake mwaka 1822, alijiunga na monasteri ya Mt. Antoni huko Qozhaya, akianza unovisi mnamo Novemba 1828 kwa jina la Nimatullah.[3]

Mmonaki[hariri | hariri chanzo]

Nimatullah alichaguliwa na abati kujifunza kujaladia vitabu. Hata hivyo alitumia muda mwingi katika sala, akikesha pengine usiku karibu na ekaristi.[1]

Aliweka nadhiri zake tarehe 14 Novemba 1830, akatumwa kwenye monasteri ya Watakatifu Sipriani na Justina huko Kfifan, wilaya ya Batroun, ili aendelee na masomo kwa ajili ya Upadrisho, aliopewa sikukuu ya Noeli 1833.

Akiwa padri, abati alimpangia kufundisha katika seminari ya shirika na kulea waseminari,[1] mmojawapo akiwa Charbel Makhlouf, ambaye pia sasa anaheshimiwa kama mtakatifu.

Nimatullah alitumia maisha yake yote kusali na kuhudumia shirika. Sehemu kubwa ya miaka 1845-1858 alikuwa katika halmashauri kuu, na kufikia cheo cha Makamu wa Abati mkuu kwa kuteuliwa na Ukulu mtakatifu, huko akiendelea na majukumu yake seminarini. Hata hivyo alikataa kuwa Abati mkuu.

Kwake mwenyewe alikuwa mkali, lakini kwa wengine alikuwa kielelezo cha subira na uvumilivu, kiasi kwamba alishutumiwa kuwa mpole mno. Yeye alikubali hata hilo kama sehemu ya toba ya kimonaki.

Kwa sababu hiyo, ndugu yake wa damu, aliyekuwa ameacha monasteri na kwenda kuishi kama mkaapweke, alimshauri yeye naye ajitafutie hali ya upweke, lakini Nimatullah alikataa, akisema maisha ya kijumuia ndiyo changamoto halisi ya mmonaki.[1]

Kifo[hariri | hariri chanzo]

Nimatullah alianza kuugua wakati wa baridi wa mwaka 1858, akafa baada ya wiki mbili za homa kali tarehe 14 Desemba.

Mwaka 1864, kaburi lake lilifunguliwa ili kumzika upya, kumbe wamonaki walishangaa kukuta mwili wake haujaoza. Basi, kutokana na sifa ya utakatifu aliyokuwanayo akiwa hai, mwili wake ulionyeshwa hadharani mpaka mwaka 1927, ulipohamishiwa kikanisa fulani.[3]

Miujiza[hariri | hariri chanzo]

Nimattulah Kassab anasadikiwa kutabiri mambo na kutenda miujiza mingi enzi ya uhai wake kutokana na maadili yake ya hali ya juu.

Heshima baada ya kifo[hariri | hariri chanzo]

Kesi ya kumtangaza mtakatifu ilianza rasmi tarehe 7 Septemba 1978.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Makala hii bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.