Manda (Ludewa)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search

Kwa matumizi tofauti ya jina hili angalia hapa Manda

Mbuyu mkubwa karibu na bandari ya Manda.
Mji Mdogo na Kata ya Manda
Nchi Tanzania
Mkoa Mkoa wa Njombe
Wilaya Ludewa
Idadi ya wakazi
 - 4,304 (2,012)

Mji ndogo wa Manda upo wiilaya ya Ludewa katika Mkoa wa Njombe, Tanzania. Wakati wa sensa iliyofanyika mwaka wa 2012, kata ilikuwa na wakazi wapatao 4,304 [1] walioishi humo. Kwa sasa wameongezeka sana. Msimbo wa posta ni 59423.

Historia[hariri | hariri chanzo]

Zamani za Afrika ya Mashariki ya Kijerumani ilijulikana kwa jina la Wiedhafen [2] ikawa kitovu cha biashara kwenye sehemu ya Kijerumani ya ufuko wa Ziwa Nyassa kabla ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia.

Manda ilianzishwa kwenye mwezi wa Mei mwaka 1897 na kuwa ofisi ndogo ya Mkoa wa Langenburg (DOA). Baadaye ofisi ndogo ya serikali ilifungwa, Wiedhafen na eneo lake lilihamishwa kwenda Mkoa wa Songea. Wajerumani walichagua mahali pa Wiedhafen-Manda kwa sababu ilifikiwa na njia ya misafara kati ya Kilwa na Ziwa Nyassa na kuwa na bandari asilia. Kulikuwa na kituo cha posta ya Kijerumani. [3]

Mazingira[hariri | hariri chanzo]

Mji mdogo wa Manda upo kwenye mwambao wa Ziwa Nyasa karibu na mdomo wa mto Ruhuhu mpaka Lupingu. Manda ina vivutio vingi sana, ikiwemo ufukwe maridhawa wa Ziwa Nyasa, aina mbalimbali za samaki kama Mbasa, Ngumbu, Mbelele, Mawoma na milima ya Livingstone. Ukiwa juu ya milima ya Livingstone utaona Ziwa Nyasa vizuri sana na nchi ya Malawi ambayo zamani ilikuwa inaitwa Nyasaland.

Mto Ruhuhu ndio mto mkubwa unaoingiza maji katika Ziwa Nyasa, si kwa upande wa Tanzania tu, bali hata Malawi. Tanzania inaona madai ya nchi ya Malawi kwamba Ziwa Nyasa lote ni mali yake hayana msingi kabisa. Ardhi kubwa karibu ya Mto Ruhuhu na kandokando mwa Ziwa Nyasa kuanzia Mbamba Bay mpaka Kyela imeliwa na maji ya Ziwa Nyasa. Leo Wamanda wengi wahamia milimani kutokana na ardhi yake kubwa kuliwa na maji ya Ziwa Nyasa.

Pia kuna Kanisa la Mt Thomaso na bandari ya kale ya Manda-Wiedhafen. Hapo kwenye mbuyu mkubwa kuna kibao cha heshima ya Mdachi aliyejitolea kupigana vita upande wa Wajerumani, lakini alifia Ruanda, wilaya ya Mbinga.

Watu[hariri | hariri chanzo]

Vijiji maarufu vya Manda ni pamoja na Igalu, Ilela (Ilela ilihama kutoka ziwani; zamani hiyo sehemu ilikuwa ndio Ngelenge), Luilo, Mbongo, Masasi, Ngelenge (Ngelenge zamani ilikuwa inatiwa Kulondoni; kwa sasa Ngelenge inaunganisha vijiji vya zamani vya Kuliwolelo, Kuntudu, Kupanda, Kutakanini na Kulondini), Nsungu, Kipingo, Lihanguli[4].

Wenyeji wa Manda ni kabila la Wamanda na lugha yao ya asili ni Kimanda. Lugha hiyo hufanana sana na lugha ya Kingoni na ina maneno mengi ya Kiingereza. Wamanda wanapatikana katika wilaya za Ludewa, Mbinga na Nyasa kuanzia Lituhi, Ndongosi na kata za jirani upande wa wilaya ya Nyasa.

Wamanda wa Ndongosi wengi wao walihamia Ndongosi wakitokea Lituhi na vijiji vya karibu kama KuNkaya, KuMangori etc. kutokana na kiongozi mmoja wa serikali kuundanganya uongozi wa juu wa serikali kwa manufaa yake kwa kudai ati, Lituhi yote ipo majini.

Vyakula vya asili vya wakazi wa Manda ni ugali wa muhogo na samaki.

Ngoma za asili za wakazi wa Manda ni Mganda, Kihoda na Ligambusi.

Wamanda wamepata elimu sana kutokana na misingi ya misheni za Anglikana na Katoliki, maana shule zote zilikuwa za misheni. Kwa hiyo Wamanda wengi ni Wakristo wa Anglikana na Katoliki. Leo kati ya Wamanda kuna maprofesa na madaktari na wanasiasa maarufu kama hayati Horace Kolimba mwanasheria kitaaluma (Kati ya wanafunzi wa kwanza walianza kusoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pale Mnazi Mmoja - leo Chuo wa Watu Wazima (Institute of Adult Education) - aliyekuwa katibu mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambaye aliweka misingi imara ya chama, Profesa Chrispini Haule ambaye alikuwa Waziri Mdogo wa Wizara ya Fedha na Mipango, Daktari Aleck Chaponda na chama chake cha siasa, mwimbaji maarufu John Komba kutokana na misingi hiyo.

Kuna Wamanda wengi nje ya Tanzania kama wataalamu wa mashirika mbalimbali, yakiwa pamoja na ya Umoja wa Mataifa na mashirika ya utafiti.

Manda kuna madini mengi sana.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Sensa ya 2012, Njombe - Ludewa DC
  2. ling. Makala Wiedhafen katika Koloniallexikon ya 1920; "Wiedhafen" ilikuwa kiasili jina la bandari ndogo nchini Ujerumani pale ambako mto Wied unaingia katika mto Rhein.
  3. Linganisha Rudolf Pfitzner, Deutsches Kolonial-Handbuch, Band I, Berlin 1901, uk. 339 (online hapa kwenye archive.org)
  4. 2002 Population and Housing Census General Report (en). Government of Tanzania. Jalada kutoka ya awali juu ya 2003-12-17. Iliwekwa mnamo 2008-08-21.
Flag of Tanzania.svg Kata za Wilaya ya Ludewa - Mkoa wa Njombe - Tanzania Flag of Tanzania.svg

Ibumi | Iwela | Kilondo | Lifuma | Luana | Ludende | Ludewa | Lugarawa | Luilo | Lumbila | Lupanga | Lupingu | Madilu | Madope | Makonde (Ludewa) | Manda (Ludewa) | Masasi (Ludewa) | Mavanga | Mawengi | Milo | Mkongobaki | Mlangali (Ludewa) | Mundindi | Nkomang'ombe | Ruhuhu


Flag-map of Tanzania.svg Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Njombe bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Manda (Ludewa) kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
Tafadhali usiingize majina ya maafisa au viongozi wa sasa maana wanabadilika mno.